Wednesday, October 21, 2015

Utunzi wa kazi za Fasihi Simulizi

Kazi za fasihi simulizi hazikutokea tu, zilitungwa. Mtu fulani alikaa na akatunga kazi fulani ambayo inajulikana katika jamii. Katika mada hii utajifunza kanuni mbalimbli zinazohusika na utunzi wa kazi za fasihi simulizi. Pia utapata fursa ya kujifunza jinsi ya kutunga kazi mbalimbali za fasihi simulizi kama vile ngonjera, methali , nahau, vitendawili na kazi nyingine. Utajifunza pia kanuni zinazoongoza utunzi wa kila kazi ya fasihi simulizi.
Kanuni za utunzi wa kazi za fasihi simulizi
Mtunzi lazima awe na jambo linalomgusa au kumkera. Kwa mfano, mtunzi ameona masichana mrembo na amempenda, kaona ajali barabarani au kaona jamii yake inazidi kuhatarisha mazingira kwa kuchoma misitu ovyo. Katuka hatua ya pili mtunzi hana budi kulitoa jambo hadharani. Hivyo hatua ya mwisho mtunzi ni lazima awe makini kuamua kutumia lugha gani na umbo gani katika kufikisha ujumbe.
Kwa kawaida mtunzi katika fasihi hutegemea nguzo mbili muhimu yaani fani na maudhui. Mtunzi wa nyimbo mathalani katika jamii iliyokumbwa na vita, atakuwa na kazi moja yaani kuwahamasisha wanajeshi walio katika mstari wa mbele kumshinda adui. Hapo fanani anaweza kutoa jumbe mbalimbali kutokana na wazo hilo. Fanani huyo pia atapaswa kupanua ujumbe kwa kuongeza mawazo madogomadogo ambayo kwa pamoja yataukamilisha ujumbe huo. Hatimaye atayapanga mawazo hayo kuwa katika mpangilio wa beti na kuzipa mahadhi.
Utunzi wa ngonjera
Ngonjera ni aina ya igizo linalotungwa kwa kufuata kanuni za ushairi wa kimapokeo. Kama ilivyo katika mashairi ya kimapokeo, ngonjera katika fani yake zina vina na mizani pamoja na kituo kama mashairi.
Unapotunga ngonjera, ieleweke kwamba ngonjera ni mazungumzo au majibizano ya kishairi kuhusu mada fulani ambapo jibu, utatuzi na suluhisho hupatikana mwishoni mwa ngonjera.
Kanuni za kutunga ngonjera
  1. Kuteu mada, kwa mfano, ukosefu wa kazi, usawa wa kijinsia n.k
  2. Kuweka dhamira – wazo kuu la mtunzi ni kama vile kutatua tatizo, kufafanua jambo, kuondoa utata wa jambo n.k
  3. Kuteua maudhui – ni muhimu mtunzi achague hoja ambazo wahusika watatoa ili kuchangia suluhisho kuhusu mada. Hoja hizo ni lazima ziweze kufahamisha au kufurahisha wasikilizaji.
Kama ilivyo katika utunzi wa mashairi, kwa ujumla mtunzi wa ngonjera anapaswa kutumia fani zifuatazo.
  1. Mtindo wa mashairi wa kimapokeo.
  2. Muundo wa mashairi ya kimapokeo wenye mizani, vina, vipande, mishororo na beti. Kila ubeti yapasa uwe na jambo moja.
  3. Kuteua mandhari kutegemeana na mada.
  4. Wahusika wawili au zaidi au makundi mawili au zaidi. Kundi linaweza kuwa la raia au watawala. Kwa kawaida, mhusika au kundi la wahusika husema jambo moja katika ubeti mmoja au zaidi na mhusika au kundi linguine la wahusika hujibu au kuendeleza. Maswali pia yaweza kutokea pande zote. Kwa kawaida, mhusika au upande mmoja huwa na ujuzi wa mambo zaidi ya upande mwingine. Wahusika katika ngonjera hujibizana kwa madaha. Madaha hayo ndiyo huwavutia watazamaji.
  5. Matumizi ya lugha ya kishairi. Hii hujumuisha lugha ya mkato, maneno mateule, lugha ya picha na matumizi ya methali, misemo na tamathali za semi.
Utunzi wa maigizo
Maigizo ni tendo la kuiga sura, tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine yaani kuiga jinsi walivyoumbwa, wanavyotembea, wanavyovaa, wanavyosema n.k
Kanuni na hatua za kutunga maigizo
  1. Kuchagua wazo, tendo, visa au tukio la kuigizwa
    Ni lazima jambo hilo liwe na uzito, umuhimu au athari fulani katika jamii. Matukio hubainika kutokana na utafiti. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile matumizi mabaya ya simu za mkononi, mitindo ya mavazi, madhara ya uganga wa kienyeji, madhara ya UKIMWI n.k.
  2. Kuchagua muktadha au mahali pa kutendeka kwa jambo
    Muktadha waweza kuwa ofisini, shuleni, kijijini, mjini, barabarani, kwenye daladala n.k
  3. Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa
    Hapa mtunzi anaweza kutumia fumbo, vichekesho, historia, tanzia n.k. Inashauriwa mtunzi kuchanganya mbinu ili kuongeza mvuto.
  4. Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo
    Maudhui hujikita katika migogoro au mivutano. Suluhisho la mivutano hupatikana pale migogoro inapofikia kilele. Kwa mfano jamabazi sugu anapokamatwa.
  5. Kuweka mpangilio wa maonyesho
    Maonyesho hujumuisha vitendo na hoja zinazokamilisha sehemu inayobeba aina moja au zaidi ya maudhui. Sehemu kadhaa nazo hukaa zikajenga kitendo ambacho hubeba jambo mojawapo muhimu. Katika migawanyo hii yapasa mtunzi atunge kauli na vitendo vinavyoandamana navyo.
  6. Kubuni wahusika na kuweka aina au idadi yao kulingana na matukio
    Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika wanaohitilafiana. Kwa mfano wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi n.k. Mtunzi akishawateua anaweza kuwatungia kauli na zamu za matendo katika sehemu mbalimbali.
  7. Ni muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua maleba yao.
    Uamuzi huu yapasa ufanywe kwa kuzingatia mazingira. Kwa mfano siku hizi sio lazima wahusika wazee kuvaa ngozi, kutumia mkongojo na kuvuta mtemba.
  8. Urefu wa maigizo ni suala la kuamliwa kutegemea tukio
  9. Kutunga maelezo kuhusu mandhari
    Maumbile ya wahusika na vitendo vyao, ni muhimu kuelezwa katika mabano.
  10. Kuandika maigizo na kuhariri
    Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo inayovutia, yenye kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleza maadili kwa mnato.
Utunzi wa majigambo
Majigambo ya jadi ni maghani ya kujisifu yanayofanywa na mwanamume kuthibitisha udume wake au wa nasaba yake mbele ya umma, hasa kwa kudokeza kifani baadhi ya matendo ya kishujaa aliyoyafanya katika jamii yake kwa malengo maalumu.
Nduni anuai za majigambo ya jadi ni pamoja na hizi zifuatazo:-
  • ni fani ya wanaume,
  • ni fani ya kujisifia au kusifia nasaba ya mjigambaji,
  • mambo yanayorejelewa au kugusiwa si lazima yawe ya kweli,
  • fani hii hughanwa badala ya kuimbwa,
  • hutungwa papo kwa papo kutegemeana na muktadha,
  • dhima zake hufungamana na muktadha tawala,
  • hutendwa kwa sauti ya juu sana,
Miktadha ya ujigambaji
Miktadha ya majigambo ni pamoja na jandoni, harusini (kuoa), vitani, kushinda jambo gumu kama mnyama mkali, mchezo, kesi mahakamani, masomo ya kijadi, katika shughuli za uwindaji, kwenye mazishi hasa ya mashujaa, katika ikulu za watawala wa jadi, na kadhalika.
Kanuni za utunzi wa majigambo
  1. Kuteua tendo la kutungia majigambo
    Hapa linaweza kuwa tendo lolote katika maisha ya kila siku. Mara nyingi majigambo huwa ni juu ya tendo fulani la kishujaa ambalo linamtofautisha mtu mmoja na mwingine.
  2. Maudhui
Kimsingi maudhui ya majigambo huwa ni kuonesha umahiri wa mjigambaji au umuhimu wake. Hata hivyo mambo muhimu ya kutaja katika majigambo ni pamoja na haya yafuaatayo:
  • Jina la mjigamabaji, laweza kuwa la kubuni au lakabu, mfano, mwamba wa kaskazini, dudu baya n.k
  • Asili ya mjigambaji; hii huwa ni kabila, ukoo, jamii, kijiji n.k
  • Matendo – mjigambaji ni lazima aeleze tendo au msururu wa matendo aliyoyatenda.
  • Matokeo ya matendo – aghalabu mjigambaji hueleza matokeo ya matendo yake ambayo huwa ushindi na fahari kwake, lakini pia hutaja madhara au hasara aliyoisababisha kwa washindani wake.
  • Matumaini – mwisho mjigamabaji hutoa kauli kuonyesha matumaini ya kuendelea na ushujaa siku za usoni.
      c. Fani 
Mbinu anazoweza kutumia mtunzi wa majigambo ni pamoja na:
  • Mtindo wa kuficha jambo au taswira nzito. Kwa mfano badala ya kujisifu jinsi alivyowaokoa majeruhi katika ajali ya daladala anaweza kusimulia jinsi alivyowaokoa watu waliopata ajali baharini.
  • Muundo – kwa kawaida majigambo huwa na muundo wa kishairi lakini wenye mwanzo mwendelezo na mwisho.
     d. Wahusika
Wahusika wanaotajwa ni mjigambaji mwenyewe na wengine alioangaliana nao katika matukio fulani.
      e. Matumizi ya lugha
Lugha itumiwayo ni ya kishairi inayoambatana na misemo, nahau, methali, taswira, tamathali za semi, na ishara ainaaina, aidha mjigambaji hutumia nafsi ya kwanza kujirejelea na nafsi nyingine kurejelea wahusika wengine. Matumizi ya vivumishi, vitenzi, vielezi, na vihisishi hukithiri ili kuonyesha uhalisia na mguso wa vitendo.
      f. Mandhari
Yapasa mtunzi aeleze mazingira yanamotokea matendo. Mazingira yaweza kuwa msitu, mtaa, ukumbi, darasa, uwanja n.k.
Utunzi wa hadithi
Kanuni za utunzi wa ngano
Ngano ni tungo za kubuni zinazosimulia mambo kwa lugha ya nathari. Ngano hudai kutungwa kwa kuzingatia kanuni zifuatazo:
  1. Dhamira 
    Inabidi kuweka dhamira ambayo ni wazo kuu au fungu kuu. Wazo kuu huweza  kujitokeza kama onyo, himizo, ushauri, tahadhari n.k
  2. Wazo 
    Ni lazima kubuni fikra au mawazo akilini na kuwasilisha funzo kuu kwa namna ya kufurahisha au kuhuzunisha.
  3. Maudhui
    Inabidi kutafuta maudhui au ujumbe wa kupitisha na unaobebwa na hadithi. kwa kawaida huwa ni maadili, yaani mafundisho juu ya mwenendo mwema katika jamii.
  4. Fani
    Hujumuisha mbinu za kusukia ngano. Baadhi ya mbinu hizo ni kama:
  5. Umbo- huhitaji kuwa na sehemu nne:

  • Kichwa – kiwe kifupi na cha kuvutia, mfano: Kisa cha chongo watatu.
  • Mwanzo – ngano huwa na mwanzo maalum, kama vile hapo zamani za kale…..
  • Mwendelezo – ndiyo sehemu ya matukio
  • Mwisho – ngano humalizika kwa namna maalumu. Aghalabu mtunzi husema: Basi chongo wale walipata uwezo wa kutumia macho yote, wakaoa na wakaishi raha mustarehe.
 f. Muundo au msuko
Ngano yapasa kuwa na loti au mpangilio wa matukio rahisi kuanzia mwanzo hadi mwisho. Matukio muhimu yanayokamilisha hadithi hayana budi kupangwa katika mtiririko mzuri na unaohitilafiana. Aidha masimulizi yatolewe kwa kusisimua ili kuwatia wasomaji au wasikilizaji hamu ya kutaka kujua litakalotokea.
  1. Kujenga mazingira ya wakati na mahali yatakapotendeka matukio mbalimbali.
  2. Matumizi ya lugha – mtunzi atumie lugha rahisi na ya kinathari lakini ya kuvutia na iliyojaa vito, kama vile methali, misemo, tamathali za semi na lugha ya picha.
  3. Wahusika – ngano huhitaji matumizi ya wahusika wa aina nyingi, kama vile wanadamu, wanyama, ndege, mimea, vitu, miungu, mazimwi na mizuka. Ni muhimu wahusika watumike kikamilifu kukuza kisa au visa na kupitisha ujumbe. Hii ndio maana huhitaji kupewa ujumbe na maumbile mwafaka.
  4. Kutumia mbinu nyingine – mbinu hizi ni pamoja na mafumbo, nyimbo, mashairi, vichekesho na kuishirikisha hadhira. Mbinu hii huipa ngano uhai.
Utunzi wa visasili
Visasili ni visa vya kubuni vinavyoeleza asili ya watu na mambo mengine katika maisha. Mara nyingi visasili huhusishwa na imani ya kidini. Kanuni zinazoongoza utunzi wa visasili ni pamoja na hizi zifuatazo:
  1. Dhamira ya kuelezea asili ya jambo
  2. Kuteua jambo la kutungia kisasili
Visasili havisimuliwi kulingana na ukweli wa kihistoria wala kisayansi bali hutungwa kulingana na imani za watu wanaohusika. Kwa hiyo kuna haja ya mtunzi kufanya uchunguzi na utafiti wa kutosha. Mambo ya kutungia visasili ni kama vile asili ya wanyama na mimea, mwanzo wa maumbile ya nchi kama vile maziwa, mito, maziwa, bahari na mabonde na asili ya binadamu kama vile kabila, ukoo na tabia. Pia huhusu asili ya matukio kama kifo, uzazi, wizi, ujambazi na mengineyo.
  1. Maudhui
Maudhui ya visasili hujumuisha jina la kinachohusika, mahali kinapotokea, mazingira, michakato, matukio au visa, utamaduni, awamu mbalimbali za matukio, mabadiliko, sababu za matukio, sababu za mabadiliko na hali ya sasa.
     2. Fani
Vipengele vinavyohusika hapa ni:
  1. Umbo – huwa na sehemu kama za ngano
  2. Muundo – huwa ni ploti rahisi
  3. Muktadha – ni muhimu mtunzi ajenge muktadha wa umbali kimasafa na kiwakati. Huwezekana kwa kusema: Hapo zamani za kale katika nchi ya mbali.
  4. Wahusika huwa ni mtu, jamii, kitu au miungu
  5. Matumizi ya lugha – lugha ya kutungia visasili huwa ya mantiki na inayoelezea na inayoelezea maumbile na mazingira kikamilifu. Inahitaji matumizi ya nomino za pekee kutambulisha watu, vitu na maeneo. Pia hutegemea matumizi ya vitenzi, vielezi, na matumizi kutoa picha ya mguso wa mambo na huhusika kwa visa. Matumizi ya methali, misemo na tamathali za semi hunogesha masimulizi.
  6. Mbinu nyingine kama miujiza, uganga, nyimbo na majigambo hutumika kuvipa visasili mvuto.
Utunzi wa tarihi
Tarihi ni hadithi zinazosimulia kuhusu matukio ya kihistoria. Ili kutunga tarihi ipasavyo tunahitaji kuzingatia mambo yafuatayo:
  1. Dhamira
    Ni vema kuweka dhamira ya kutunga tarihi. Hii huweza kuwajuza wanajamii, kuelimisha, kuburudisha au kuwapa watu kujitambulisha.
  2. Aina
    Inapasa kuamua aina ya tarihi ya kutunga. Tarihi yaweza kuihusu nchi, asasi, mji, kijiji, kitu au mtu fulani.
  3. Maudhui
Ni lazima kupanga maudhui. Maudhui ya tarihi hutokana na kujibu maswali yafuatayo:
  1. Nini au nani anahusika? Inabidi kutaja jina, maumbile yake na sifa nyingine.
  2. Kulitokea nini? Maelezo kuhusu matukio na matendo muhimu.
  3. Yalitokea lini? Muktadha wa wakati
  4. Yalitokea wapi? Muktadha wa mahali
  5. Yalimhusu nani? Waathiriwa
  6. Kwa sababu gani?
  7. Matendo yalikuwa na athari gani?
Mambo yanayosimuliwa hujengwa kwenye matukio ya kihistoria lakini fantasia huweza kuingizwa kwenye usimulizi. Mifano ya tarihi za aina hii ni zile zinazohusu watu kama Kinjekitile, Shaka, Sundiata na Fumo Liyongo.
      4. Fani
Mtunzi wa tarihi hana budi kutumia mbinu zifuatazo:
  1. Umbo – tarihi huwa na sehemu nne kama ngano, yaani utangulizi, mwanzo, mwendelezo na mwisho.
  2. Tarihi inahitaji kuwa na mtiririko rahisi na ploti yenye matukio yanayohitilafiana lakini yenye mvuto. Mambo yateuliwayo ni yale yenye umuhimu tu.
  3. Mandhairi
  4. Wahusika – katika tarihi yoyote huwa kuna shujaa anayeitwa jagina. Shujaa huyu anapambana na wapinzani wanaoitwa majahili. Mshindi katika mapambano daima huwa jagina. Tarihi pia inajumuisha wahusika wengine wanaojenga masimulizi.
  5. Matumizi ya lugha – lugha ya tarihi huwa ni ya kupiga chuku na kunasa imani za watu.
  6. Mbinu nyingine – katika utungaji wa tarihi mbinu zinazotumika katika ngano baadhi hutumika. Aidha, hutumika mbinu za kuingiza maajabu katika masimulizi. Mfano ni wa mtu mmoja kuangamiza jeshi zima la maadui bila kuguswa na silaha zao kali, lakini baadae akafa kwa kudungwa kitovu kwa mwiba.
 5. Kichwa
Baadhi ya vichwa vya tarihi huwa na anwani kama “Tarihi ya Kilwa” au jina la jagina kama vile Fumo Liyongo, Mandela au Tip Tippu.
Utunzi wa methali (Semi)
Kanuni za utunzi wa methali
  1. Kuweka madhumuni ya methali
    Lengo kuu la methali ni kumfundisha binadamu kuhusu maisha yake na kujenga uhusianao bora na viumbe wengine. Ili kutimiz haya ni lazima methali itekeleze yafuatayo: kufurahisha, kukosoa, kuadilisha, kukejeli, kusisitiza, kuhimiza, kufariji na kuelimisha.
  2. Kuchagua maudhui
Methali hubeba mambo yafuatayo:
  • Fikra au wazo zito. Mfano: Akili ni mali
  • Matukio ambayo huelezwa kwa muhtasari. Mfano, atafutaye hachoki, akichoka keshapata.
  • Maadili na mafundisho. Mfano, mwana mtukana nina, kuzimuni enda akiona.
  • Maana- methali huwa na maana zinazofungamana na vipengele mabalimbali vya maisha, kama vile Mungu, binadamu na viungo vyake, tabia za watu, matendo ya watu, tabia za wanyama na kadhalika. Ni muhimu kujua vipengele vyote katika methali humlenga binadamu.
     c. Fani
  • Methali zina msuko au mpangilio maalumu wa maneno machache lakini yaliyoteuliwa kwa uangalifu. Mfano; Hewala si mtumwa; Ndugu wakigombana chukua jembe ukalime, wakipatana chukua kapu ukavune.
  • Methali nyingi huwa na muundo wa mashairi ambapo hutokeza mistari, vipande, mizani, vina na takriri. Mfano: haraka haraka haina baraka; Duma hukamata, sungura hupata.
  • Kila methali hutaja wahusika ambao huweza kuwa binadamu. Mfano: Mungu si Athumani; Shukrani ya punda ni mateke.
  • Methali hutumia lugha zenye sifa mbalimbali kama vile:
  • Lugha ya kimafumbo. Mfano: Jembe la kuku mguu
  • Lugha ya kishairi. Mfano: Ajuae mengi hasemi mengi.
  • Lugha ya mifano. Mfano: Akili ni nywele kila mtu ana zake.
  • Lugha ya picha. Mfano: Akikalia kigoda mtii
  • Methali pia hutumia mbinu nyingine kama vile:
  • Takriri – Bandubandu huisha gogo.
  • Mchezo wa maneno – Mpigwa nje uenda kwao mpigwa kwao huenda api?
  • Kuficha maana
  • Mazingira – Ni muhimu kuchunguza na kuchagua mazingira mahususi ya kujenga methali. Mazingira yaweza kuwa ya furaha, huzuni, vita au kikazi. Mfano: Mgagaa na upwa hali wali mkavu; Mtaka cha uvunguni sharti ainame.
Utunzi wa nahau
Nahau zina sifa zifuatazo:
  1. Ni vifungu vya maneno ya kawaida lakini hubeba maana tofauti kabisa na maana halisi ya maneno yanayotumika. Mfano:
  • Joseph amevaa miwani (amelewa)
  • Mali ya mfanyabiashara italindwa maana anadaiwa kope si zake. (ana madeni mengi)
     b. Ni kauli zinazotumia picha ambayo huleta maana iliyofichika. Mfano:
  • Hakimu amechelewesha kesi yake kwa sababu hajazunguka mbuyu. (Hajatoa rushwa)
    c. Nahau hutumia lugha ya mkato yenye maneno machache. Mfano: asi ukapera (oa); bei ya kuruka (bei ya juu); bwaga mtwae (ovyo ovyo).
    d. Hutoa ujumbe mzito wa kimafumbo. Mfano: Ingawa ulikosa, rudi kwa wazee wako uwashike miguu(uwaombe radhi).
Miundo ya nahau
  • Kitenzi na nomino. Mfano: kuiva macho (kasirika sana); peleka ubani (toa mchango kwa waliofiwa)
  • Nomino na nomino. Mfano: Dunia kazi (ulimwengu unahitaji bidii).
  • Nomino na kivumishi. Mfano: Debe tupu (mtu asiyejua lolote)
  • Kitenzi na kielezi. Mfano: enda kinyume (haribika)
  • Nomino, kihusishi na nomino. Mfano: denge la mbuzi (mbuzi dume); jeraha la moyo (machungu)
  • Kitenzi na kitenzi. Mfano: pata potea (bahati na sibu)
  • Kitenzi, kiunganishi na nomino. Mfano: cheza na moto (fanya jambo hatari)
Utunzi wa vitendawili na mafumbo
Kanuni za utungaji wa vitendawili na mafumbo ni pamoja na hizi zifuatazo:
  1. Madhumuni
Maana na muundo wa vitendawili hutegemea lengo lenyewe la kitendawili kama ni kuelimisha, kunoa udadisi, kuchemsha bongo, kuimarisha tabia ya uchunguzi, kuburudisha au kukuza uwezo wa kuhusianisha mambo. Mfano:
  • Kuelimisha – macho ya babu yapo hapa lakini yanaona Uchina (Darubini)
  • Kuburudisha – kisimani mwa Bi Mpaji kuna jini mnywa maji (kandili)
  • Kuhusianisha – Gogo la kwetu limelala nyasini (chatu)
  • Kuchemsha bongo – watoto wangu daima hufukuzana lakini hawakamatani (magurudumu)
      b. Maudhui
  • Ujumbe kulingana na maisha. Mfano: chumba changu ni kikubwa lakini nalala peke yangu (kaburi)
  • Mawazo na dhana fulani. Mfano: Huja na kuondoka kwa njia mbili za ajabu (Kuzaliwa na kufariki kwa binadamu)
  • Matendo na matukio mbalimbali. Mfano: hawapandi wala hawatafuti chakula lakini wanakula na wanashiba (mdomo na tumbo)
       c. Fani
  • Muundo
Vitendawili ni mazungumzo ya watu wawili yaani mtegaji na mteguaji yenye sehemu zifuatazo:
  • Kianzio au kiingizi. Mfano:
Mtegaji: kitendawili!
Mteguaji: tega!
  • Maelezo, swali au kauli ya fumbo. Mfano: Mtegaji: cheka uchekwe.
  • Jibu. Mtegwaji: mwenye pengo
  • Hoja ya mtegaji. Mfano, Mtegaji: umepata
  • Kutoa tuzo au kudai fidia
  • Kutoa mji
  • Kukubali mji
  • Kukubali kauli
  • Jibu
  • Uteuzi wa maneno
Vitendawili huundwa kwa maneno machache na hudai majibu mafupi. Mfano: Adui mpenzi (moto). Maneno hutumiwa kueleza hali mbalimbali kama vile: umbile la kitu – nyumba yangu haina mlango wala dirisha (yai), Tabia au sifa ya kitu au jambo – kila siku hupita njia hiyohiyo lakini arudipo hatumwoni (jua), matendo na matukio – hulia huku akiunganisha (cherehani)
  • Wahusika
Maelezo, maswali na kauli za vitendawili daima huhusu watu, wanyama, wadudu, ndege na vitu mbalimbali vinavyopatikana katika mazingira ya mwanadamu.
  • Mazingira

No comments:

Post a Comment