Kazi za fasihi andishi ni sanaa, yaani zinahitaji ubunifu wa mwandishi ili ziwe katika mwonekanao huo wa kisanaa. Fasihi andishi hutumia lugha na wala sio lugha tu bali lugha ya kisanaa, kama tulivyokwishaona katika mada zilizotangulia kwamba lugha ni kipengele muhimu sana katika fasihi. Ili kazi ya kifasihi ya msanii husika iwe nzuri na ya kuvutia, masanii hana budi kuwa na ubunifu wa hali ya juu katika kutumia lugha.
Msanii awe na uwezo wa kupangilia maneno, kuteua maneno katika hali ya ujumi lakini pia yakiwa yamebeba ujumbe unaoigusa hadhira yake. Kwa maana hii mwandshi wa kazi za kifasihi, iwe riwaya au tamthilia ni lazima azingatie sana lugha, kwani lugha ndio nyenzo kuu ya usanaa wa fasihi kwa ujumla.
Kuna hatua kadhaa za kuzingatia wakati wa kuandika kazi ya kisanaa, hatua hizo ni kama zifuatazo:
Kuwa na kisa/wazo unalotaka kuliandikia
Katika jamii kuna mambo mengi sana yanayotendeka, msanii anaweza kupata wazo la kiubunifu kutokana na mambo hayo yanayotendeka katika jamii. Kama tujuavyo fasihi andishi kazi yake ni kuonesha yale yanayotendeka katika jamii, kwa hiyo msanii anaweza kutumia fursa hiyo ili kuweka wazi mambo yanayoendelea katika jamii. Kwa mfano mwandishi naweza kutunga kazi ya kibunifu kuhusu, ufisadi, umasikini, mapenzi, ndoa, maisha yake mwenyewe, ushirikina, jambo lolote analoliamini katika maisha (falsafa yake)
Kwa hiyo hatua ya kwanza kwa msanii kabala ya kuandika ni kuelewa vizuri jambo analotaka kuandikia. Pia katika hatua hii msanii anaweza kubuni jina la hadithi yake, pia hii inaweza kumsaidia katika upangaji wa visa na matukio ya hadithi yake.
Kuchagua umbo la kazi ya fasihi
Msanii akishapata wazo la kuandika, sasa inambidi achague jinsi atakavyoliwasilisha wazo lake hilo. Yaani anaweza kuchagua endapo aandike hadithi fupi, riwaya au tamthiliya, au ushairi au utenzi. Sasa uchaguzi wa umbo la kazi ya fasihi unategemeana na uwezo wa msanii katika tanzu hizo, kuna mwingine anapenda tamthiliya lakini kuandika riwaya hawezi, kuna mwingine anaona kuandika ushairi ni rahisi na kuna mwingine hawezi. Kwa hiyo ubunifu wa msanii utadhihirika katika utanzu ule anaoumudu vizuri zaidi.
Kubaini hadhira
Mwandishi kujua yule anayemwandikia ni suala la msingi sana. Hadhira ipo ya watu wa aina mbalimbali, watoto, watu wazima, wasomi, wenye elimu ndogo, wakulima, wanasiasa n.k. Sasa mwandishi akishabaini hadhira anayoindikia itamsaidia kuteua lugha ya kuandikia, kwa mfano kama ni watoto, hatutegemei mwandishi kutumia lugha ngumu, misemo na nahau nyingi.
Kubuni wahusika na mandhari
Mwandshi baada ya kujua kazi yake inahusu nini sasa inambidi abuni wahusika wa hadithi yake. Wahusika wanaweza kuwa ni watu, wanyama, mimea, mazimwi, malaika n.k. Pia ni lazima abaini mazingira ambamo visa vyote vya hadithi na matukio yatakapofanyika. Mandhari yanaweza kuwa baharini, kijijini, mjini, mbinguni, kuzimu n.k
Kupanga msuko wa visa na matukio
Msuko wa visa na matukio ni muhimu sana katika usimulizi wa hadithi. Sasa kama mwandishi amaeamua kuwasilisha kazi yake kwa njia ama ya hadithi fupi au riwaya au tamthiliya ni vema ajue namna visa na matukio vitakavyopangwa. Katika kufanya hivi maswali yafuatayo ni muongozo mzuri katika kupangilia ploti.
- Hadithi yangu itaanzaje?
- Mgogoro utaanzaje? Ni kati ya nani na nani?
- Je, kilele cha mgogoro ni nini? Je, ni mhusika mkuu kubakwa na kuambukizwa VVU?
- Hadithi yangu inaishaje? Je mhusika mkuu ashindwe? Atorokee nje ya nchi? Afungwe? Abadilike? Au maadui ndio wafungwe au wafe? Au wabadilike?
Kuanza kuandika
Sasa baada ya kupitia hatua hizo zote, mwandishi sasa anaweza kuanza kuandika. Mchakato wa kuandika hua ni mrefu na mwandishi anaweza kujikuta anafuta mara nyingi kile alichokiandika, hii ni kutokana na kwamba mambo mengi ya kuandika huwa yanakuja wakati mwandishi ameanza kuandika kazi husika. Hata hvyo sio vibaya kufanya hivi, hii pia inasaidi kuwa na zao bora la fasihi.
Utungaji wa hadithi
Hadithi ni masimulizi ya kubuni yaliyoandikwa kinathari inaweza kuwa na wahusika wengi, matukio mengi na mandhari mapana (inategemena na aina ya hadithi, iwapo ni hadithi fupi wahusika wake huwa ni wachache na pia matukio ni machache, mandhari yake pia ni finyu). Kuna aina zifuatazo za hadithi kulingana na kigezo cha urefu au maudhui. Kwa kigezo cha urefu kuna Hadithi Fupi na Riwaya.Kutokana na maudhui kuna Riwaya Dhati na Riwaya Pendwa.
Riwaya dhati ni zile zinazozungumzia masuala muhimu ya kijamii, kama vile uonevu wa tabaka la chini, rushwa, uongozi mbovu n.k
Riwaya pendwa ni hadithi zenye lengo la kuburudisha, kutokana na usimuliaji wake uliojaa taharuki na fantasia. Mambo yanayosimuliwa katika riwaya hizi ni yale yanayogusa hisia za watu kwa urahisi kama vile mapenzi, mauaji, ujasusi n.k.
Mikondo ya uandishi wa hadithi
Mkondo wa hadithi ni mwelekeo ambao mwandishi anaufuata katika utunzi wa kazi yake. Mikondo ya utunzi wa hadithi ni pamoja na hii ifuatayo:
- Mkondo wa kiwasifu; mkondo huu huhusisha hadithi zote zinazosimulia maisha ya watu. Ni riwaya ambayo inasimulia maisha ya mtu toka alipozaliwa hadi wakati huo.
- Mkondo wa kitawasifu; hadithi zinazofuata mkundo huu ni zile zinazosimulia maisha ya mtu binafsi yaani mwandishi mwenyewe. Kwa mfano riwaya ya “maisha yangu baada ya Miaka hamsini”. (S.Robert)
- Mkondo wa kihistoria; hadithi katika mkondo huu zinahusu matukio ya kweli ya kihistoria yaliyotokea. Kwa mfano riwaya ya “Uhuru wa Watumwa”
- Mkondo wa kipelelezi; hizi ni hadithi zinazozungumzia upelelezi wa uhalifu fulani kama vile ujambazi, wizi, rushwa, mauaji n.k.
- Mkondo wa kimapenzi; katika mkondo huu zinaingia riwaya zote zinazozungumzia masuala ya mapenzi.
Utungaji wa hadithi fupi
Kama tulivyokwisha ona hapo nyuma sifa za hadithi fupi, basi katika utungaji wake mambo yafuatayo ni sharti yazingatiwe:
- Hadithi fupi inakuwa na mhusika mkuu mmoja ambaye anajitokeza sana kuliko wahusika wengine.
- Idadi ya wahusika ni ndogo ukilinganisha na wahusika wa kwenye riwaya.
- Mandhari ya hadithi fupi si mapana kama ilivyo katika riwaya
- Hadithi fupi inakuwa inaongelea dhamira kuu moja tu ambayo inaonekana toka mwanzo hadi mwisho wa hadithi.
Utungaji wa tamthiliya
Tamthiliya ni kazi ya fasihi iliyoandikwa kwa lengo la kuonyeshwa jukwaani, ambapo wahusika huzungumza na kutenda vitendo mbalimbali. Tamthiliya huigiza maisha ya kila siku.
Kwa kuwa tamthiliya imeandikwa kwa lengo la kuigizwa huwa imeandikwa na maelezo ya jukwaani, maelezo yanayoonesha nini kifanywe na nani na kwa namna gani. Tamthilya hugawanywa katika maonyesho kama ambavyo riwaya inavyogawanywa katika sura.
Aina za tamthiliya
- Tanzia; ni aina ya tamthiliya ambapo mhusika mkuu/shujaa anapata anguko kubwa au kifo ambacho huwafanya hadhira kuwa na huzuni.
- Ramsa ni tamthilia ambayo hulenga kufundisha kwa njia ya kuchekesha ili kuleta ujumbe mzito.
- Vichekesho/Futuhi ni aina ya tamthiliya ambayo lengo lake kuu ni kuchekesha kwa kutumia mbinu ya kutia chumvi mambo, kudhihaki na kukejeli.
Mbinu za utungaji wa tamthiliya.
Katika utunzi wa tamthiliya kuna mambo kadhaa ya kuzingatia, mambo hayo ni kama yafuatayo:
- Chagua jambo unalotaka kuandikia
- Panga namna msuko wa visa na matukioa utakavyokuwa
- Buni wahusika wako kulingana na kile unachotaka kukiandika
- Chagua mandhari yanayofaa kulingana na visa vyako
- Tumia mtindo wa majibizano kati ya wahusika
- Gawa tamthiliya katika maonyesho
- Weka maelekezo ya jukwaa. Haya huelezea kile kinachotendeka kwa wakati ule. Maelezo ya jukwa huwa katika maandishi ya italiki.
- chanzo shule direct
hongera baba yao wengine yaliishia darasani tu
ReplyDeleteshukran
ReplyDelete