Wednesday, October 21, 2015

Matumizi ya Lugha katika Miktadha Mbalimbali

Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi.
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika.
Dhima ya matumizi ya lugha
Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii inayohusika.
Mambo ya kuzingatia katika matumizi ya lugha
        1. Mada inayozungumziwa
Mada za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii, kwa mafano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k. Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara, faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.
       2. Muktadha wa mazungumzo
Mazungumzo yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa mfano kuna miktadha ya kidini, kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu, kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza kufanyika mjini, kijijini, ugenini, shuleni, dukani, hotelini n.k
       3. Malengo ya mazungumzo hayo
Malengo ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya lugha. Kwa mfano, lengo linaweza kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia moyo n.k. Sasa jinsi lugha itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti na itakavyotumika katika kutia moyo au kukejeli.
        4. Uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji
Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi, marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi, mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili yatategemea uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia mambo haya manne, itawafanya wazungumzaji wawe makini katika uteuzi wa maneno, miundo, mifano na kina cha ufafanuzi wa maelezo au habari inayozungumzwa.

REJESTA
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika.

AINA ZA REJESTA
  1. Rejesta za Mitaani
    Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke)n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka wa wazungumzaji wenyewe.
  2. Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali) 
    Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
    Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
         - Maofisini au mahali popote pa kazi
         - Mahakamani
         - Hotelini
         - Hospitalini
         - Msikitini
          - Kanisanin.k
(a)        Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
  1.  Nani wali kuku?
     B: Mimi
  1. Chai moja wapi?
     B:   Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”: ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
(b)        Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitizausahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi: Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi:Sijui.
Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.
          iii. Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
       - Vijana wenye rika moja,
       - Wazee wenyewe,
       - Wanawake wenyewe,
       - Wanaume wenyewe,
       - Mwalimu na mwanafunzi,
       - Meneja na wafanyakazi wake,
      - Mtu na mpenzi wake, n.k.
(c)        Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
Mfano:
'Basi,  Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana’
‘Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga’
‘Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa noma kila mzamiaji’
Alikuwa mnoko kishenzi’
‘Akatema mkwara mbuzi, nikajibu kwa mkwaradume....akabloo mimi ndani’.
Maana ya Maneno
Wikiendi – Mwisho wa wiki.
Kibaridi –tulivu.
Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa.
Zinga la Mnuso –sherehe kubwa.
Saiti –sehemu.
Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni.
Noma – Hatari.
Mnoko kishenzi – kinaa sana
Mkwala mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.
Dhima za rejesta
Utambulisho wa kijamii
Katika kipengele cha utambulisho wa kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha miongoni mwa watumiaji wake au kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii husika. Pia katika utambaulisho wa kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu hutambulika katika jamii kulingana na namna anavyoongea kulingana na hadhi, tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza kusababisha mshikamano au mwachano katika mazungumzo. Kwa mfano jamii itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo anaoutumia, au ni mtu wa mtaani kulingana na lugha anayotumia.
Rejesta, ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hii ni kutokana na kwamba, madhumuni makuu ya mawasiliano katika biashara ni kuwavutia wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma wanazouziwa ni za kiwango cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha ya biashara (rejesta), kwa kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au huduma, huwa na sentensi au vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu” pia huwa na lugha ya kupumbaza na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia rejesta inasaidia sana kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika masuala mbalimbali ya kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii. Mfano hospitalini “mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni “kata nusu” na maeneo mengine.
Baadhi ya rejesta hutumika kupunguza idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe mafupi na yanayoeleweka kwa urahisi mfano rejesta za hotelini kama vile:- Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja: hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa.
Pia katika kutolea elimu ya dini kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa katika kujenga maadili.
Vilevile rejesta ina nafasi ya kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza hapa na pale hupenda kutumia maneno tofautitofauti ili kufanya mazungumzo yawe ya kuvutia. Mfano mazungumzo miongoni mwa vijana: 
Kijana 1: Niaje? Nakuona umechili
Kijana 2: mzuka jembe. Kama kawa… kama dawa!
MISIMU
Misimu ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. misimu inayodumu huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya lugha ya jamii hiyo.
Chanzo cha misimu
  • Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii husika katika nyakati mbalimbali.
  • Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia zoa juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano, njaa, mafuriko, vita n.k.
   Aina za misimu:
  1. Misimu ya pekee
    Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.
  2. Misimu ya kitarafa
    Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya au tarafa.
  3. Misimu zagao
    Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.
   Sifa za misimu:
  • Huzuka na kutoweka  kufuatana na mabadiliko ya jamii.
  • Ni lugha isiyo sanifu.
  • Ina chuki.
  • Ni lugha ya mafumbo.
  • Ina maana nyingi.
   Dhima ya misimu:
  • Hutumika kupamba lugha.
  • Hutumika kukuza lugha.
  • Hutumika kutunza historia ya jamii fulani.
  • Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji.
  • Hufurahisha na kuchekesha.
TUNGO TATA
Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni tungo ambayo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja.
Mfano:
  1. Patience amemwandikia Lilian barua
    Sentensi huweza kuwa na maana kuwa Patience ameandika barua kwenda kwa Lilian au Patience ameandika barua kwa niaba ya Lilian
  2. Umefanikiwa kununua mbuzi?
    Sentensi hii huweza kumaanisha ununuzi wa mbuzi mnyama au mbuzi kifaa cha kukunia nazi.
  3. Alimkuta amelala kwenye nyumba ya wageni
    Sentensi hii huweza kumaanisha, nyumba ya mtu lakini inatumika kwa ajili ya wageni kwa malipo au ni nyumba inayomilikiwa na watu ambao ni wageni katika eneo lile.
  4. Attu ametumwa na Aritamba
    Sentensi hii inaweza kueleweka kumaanisha, Aritamba amemtuma Attu au Attu na Aritamba wametumwa wote kwa pamoja.
Sababu za utata
Utata katika tungo hutokea kwa sababu zifuatazo:
  1. Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzikata n.k.
  2. Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta Nyammy na rafiki yake, Mazala vs Tulimkuta Nyammy na rafiki yake Mazala. Katika sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti, sentensi ya kwanza inamaana kulikuwa na watu wawili Nyammy na rafiki yake aitwaye Mazala na sentensi ya pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa na watu wawili Nyammy na mtu mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala
  3. Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya maneno hayo.
  4. Utamkaji wa maneno
    Wakati mwingine utata unaweza kujitokeza katika matamshi tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani. Kwa mfano; Mimina wewe, katika maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe, na hivyo kuondoa utata.
  5. Mjengo wa maneno
    Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia. Chanzo cha utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-. Kiambishi hiki kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa kutumia chombo fulani.., au mahali fulani.
Mfano:
  • Alimpigia ukorofi wake (kwa sababu ya)
  • Alimpigia kiatu (kifaa)
  • Alimpigia ndani (mahali)
Lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
Lugha ya mazungumzo
Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.
Faida ya lugha ya mazungumzo
  1. Mzungumzaji anaweza kukaa ana kwa ana na msikilizaji, hivyo hukuza uhusiano.
  2. Mzungumzaji anaweza kutumia ishara za mwili katika kusisitiza maelezo yake.
  3. Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kuuliza au kuulizwa maswali.
  4. Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake kwa kulia, kupaza sauti, kupunguza sauti, kuonyesha furaha huzuni au hasira.
  5. Mzungumzaji anaweza kuuliza maswali, kuona hisia za mzungumzaji kwa kusikiliza lugha zinazotolewa na kuangalia ishara za mwili zinazotumika.
  6. Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kufuta usemi wake, kuongezea jambo au kutoa maelezo ya ziada.
  7. Mzungumzaji anaweza kubadilisha lugha yake kulingana na mazingira aliyomo.
  8. Mzungumzaji anao uhuru wa kutumia lugha ya mitaani, misimu kulingana na muktadha.
Matatizo ya lugha ya mazungumzo
  1. Maelezo lazima yahifadhiwe kichwani, hivyo kama mtu hana kumbukumbu, taarifa zilizotolewa hupotea na kusahaulika.
  2. Mtumiaji wa lugha ya mazungumzo anaweza kurudiarudia vipengele fulani na hivyo kuichosha hadhira.
  3. Ujumbe unaweza usieleweka kama unatolewa kwenye kelele nyingi
Lugha ya maandishi
Hii ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Lugha ya maandishi huzihusiha pande mbili, mwandishi na msomaji. Lugha ya maandishi sharti iwe fasaha ili msomaji anaposoma maandishi hayo, apate kuelewa kila kitu, yaani asibaki akijiuliza maswali.
Lugha ya maandhi huambatana na alama za uakifishaaji, hii husaidia maandishi kusomeka vizuri na kueleweka kwa urahisi.
Ubora wa lugha ya maandishi
  1. Lugha ya maandishi huwawezesha watu walio mbali kuwasiliana.
  2. Lugha ya maandishi hustawisha sarufi ya lugha na misingi yake, kwa sababu mwandishi anahakikisha kwamba anazingatia vizuri kanuni za kisarufi ili msomaji wake aweze kumwelewa.
  3. Ili kuhakikisha maelezo yake yanaeleweka mwandishi analazimika kuandika kwa uwazi na kwa kuzingatia kanuni na miiko yote ya uandishi.
Udhaifu wa lugha ya maandishi
  1. Lugha hii hutumiwa na wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
  2. Lugha ya maandishi haina msisimko uletwao na lafudhi na matamshi.
  3. Msomaji hukosa vidokezo vingi ambavyo katika lugha ya mazungumzo huchangia katika mawasiliano.
  4. Lugha ya maandshi inamnyima mwandishi nafasi ya kupima welewa wa msomaji kwa kuwa hamwoni.
Dhima ya lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
Lugha ya mazungumzo na lugha ya maandshi zote zina umuhimu wa pekee katika maisha ya kila siku kwa sababu ndizo zinzaowezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali.
Umuhimu wa lugha ya maandshi pia hutokana na dhima yake kwa watu. Maandishi yanaweza kuhifadhiwa na kusambazwa kwa watu wengi hata walio mbali. Maandishi yanahifadhi kumbukumbu na kwa muda mrefu. Kwa hali hii, watu wa vizazi vingine wanaweza kusoma na kujua mambo yaliyofanyika karne nyingi zilizopita.
Tofauti kati ya lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
  1. Lugha ya mazungumzo huwezesha mawasiliano ya ana kwa ana lakini lugha ya maandishi haiwezeshi mawasiliano ya ana kwa ana.
  2. Lugha ya mazungumzo haihitaji maandalizi wakati lugha ya maandishi huhitaji maandalizi. Mwandishi atalazimika kupata muda wa kuandika pamoja na kuandaa vifaa kama vile kalamu, karatasi n.k
  3. Lugha ya mazungumzo hailazimiki kuzingatia kanuni za kisarufi, lakini lugha ya maandshi hutakiwa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Tofauti nyingine kati ya lugha ya maandishi na lugha ya mazungumzo huweza kuonyeshwa katika jedwali lifuatalo.
Kipengele
Mazungumzo
Maandishi
Muktadha
  1. Wahusika huonana
  2. Viungo vya mwili hutumika
  3. Maandalizi na matumizi hufanyika wakati mmoja
Wahusika hawaonani
Viungo vya mwili havitumiki
Maandalizi hufanyika kabla ya matumizi
Mada
Hazina uzito mkubwa
Huelekea kuwa na uzito mkubwa.
Mpangilio wa mada na mawazo
Hautabiriki. Unaelekea kutokuwa na mtiririko.
Hutabirika. Huelekea kuwa na mtiririko.
Mjadala wa mada
Hauelekei kuwa na kina. Hazichujwi kwa uaangalifu.
Unaelekea kuwa na kina. Huchujwa.

No comments:

Post a Comment