Showing posts with label ELIMU YA DINI. Show all posts
Showing posts with label ELIMU YA DINI. Show all posts

Thursday, October 15, 2015

Amali Za Kutenda Na Mambo Ya Kujiepusha Nayo Katika Mwezi Mtukufu Wa Muharram

AlhamduliLLaah. Inapasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kutupa umri hadi kutufikisha katika mwezi mtukufu wa Muharram ambao ni mwezi wa mwanzo kuanzia mwaka mpya wa Kiislamu.  Ni fursa nyingine kwetu kutenda mema yatakayotuchumia thawabu nyingi kuliko miezi mingine. Mema ambayo hatuna budi kuyatenda kwa ajili ya kujenga Aakhirah yetu kabla ya siku hii kufika. Siku ambayo hakuna mmoja wetu yeyote atakayeweza kuikwepa. Basi hebu kila mmoja wetu ajiulize: "Nimetanguliza nini kwa ajili ya siku hiyo?" Siku ambayo safari yake ni ndefu mno. Mahmaa tutakavyobeba zawadi huko hazitoshi wala hatuna hakika nazo kama zitapendekezeka au zitakuwa na thamani huko tuendako ambako kuna makazi ya milele tusiyokuwa na hakika nayo; ima moto au Pepo.  


Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):


(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ))

((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah,, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Allaah, Hakika Allaah, Anazo khabari ya mnayoyatenda)) [Al-Hashr: 18]



Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):


(( إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم ))

((Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah, tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo)) [At-Tawbah: 36]


Miezi minne hiyo imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:




  عَنْ أَبَى بَكْرَة أَنَّ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - قَالَ فِي حَجَّة الْوَدَاع : (( إِنَّ الزَّمَان قَدْ اِسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْم خَلَقَ اللَّه السَّمَوَات وَالْأَرْض السَّنَة اِثْنَا عَشَر شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَة حُرُم : ثَلَاث مُتَوَالِيَات ذُو الْقَعْدَة وَذُو الْحِجَّة وَالْمُحَرَّم وَرَجَب مُضَر الَّذِي بَيْن جُمَادَى وَشَعْبَان))      صَحِيح الْبُخَارِيّ



Kutoka kwa Abu Bakrah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa wa sallam) amesema alipokuwa katika Hijjah ya kuaga (Hijjah wa mwisho): ((Mgawanyo wa nyakati umerudi kama ulivyo (wakati) Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili, minne ambayo ni mitukufu; mitatu inafuatana pamoja (nayo ni) Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram, na (wa nne ni) Rajab wa (kabila la) Mudhwar ambao upo baina ya Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy]  


Katika miezi yote kumi na mbili Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameichagua hii minne na Ameifanya kuwa ni mitukufu na kusisitiza kuitakasa, na kwamba dhambi zitakazofanyika humo ni zaidi na hali kadhalika thawabu za vitendo vyema zinakuwa maradufu na zaidi. [Atw-Twabariy 14: 238]


Ni sawa kama Anavyoonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kufanya maasi katika sehemu tukufu Alipotaja Masjidul-Haraam (Msikiti Mtukufu Makkah):


((إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاء الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ))

((Hakika wale waliokufuru na wakazuilia Njia ya Allaah na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayetaka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi Tutamwonjesha adhabu iumizayo)) [Al-Hajj: 25]


Qataadah amesema kuhusu kauli ya Allaah:

(( فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم))

((Basi msidhulumu nafsi zenu humo))

"Dhulma itakayotendeka katika miezi mitukufu ni mbaya na kubwa (au hatari) kuliko dhulma itakayotendeka katika miezi mingine. Hakika dhulma daima ni makosa, lakini Allaah Hufanya baadhi ya vitu kuwa ni vizito kuliko vingine kama Anavyopenda". Akaendelea kusema: "Allaah Amechagua baadhi ya viumbe Vyake na baadhi ya vitu kuwa bora zaidi kuliko vingine. Amechagua Wajumbe kutoka Malaika na kutoka binaadamu. Vile vile Amechagua baadhi ya kauli Zake kuwa ni bora kuliko nyingine, Misikiti kuwa bora kuliko sehemu nyingine za ardhi, Ramadhaan na miezi mitukufu kuwa bora kuliko miezi mingine, siku ya Ijumaa kuwa ni bora kuliko siku nyingine, na usiku wa Laylatul-Qadr kuwa ni bora kuliko masiku mengine. Kwa hiyo takasa vile Alivyovitakasa Allaah, kwani kufanya hivyo ni vitendo vya watu wenye akili na wenye kufahamu" [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr]   

Miongoni mwa yaliyokatazwa katika miezi hii mitukufu ni kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): 


   
(( يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللّهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللّهِ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ ))

((Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa Lakini kuzuilia watu wasiende katika Njia ya Allaah na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasiende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Allaah. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua..))[Al-Baqarah:  217]




Hivyo basi kwa vile tumeingia katika mwezi mtukufu wa Muharram maasi na mema yafuatayo yanatupasa kuzingatia: 




Maasi Mengine Ambayo Tunatakiwa Tujikumbushe Kuyaacha: 


-        Kuiba;

-        Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama kwenda kwa wachawi na waganga na kuwaamini wanayoyatabiri kwa watu;

-        Kuzini;

-        Kulewa;

-        Kumdhulumu mtu haki yake;

-       Kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, kudharauliana n.k.;

-       Kusengenya (Ghiybah);

-                  Kusema uongona kila aina ya uovu mwengine.




Mambo Mema Ya Kukumbushana Kufanya Katika Mwezi Huu Mtukufu




-        Kuongeza Sunnah za Swalah*(tazama maelezo chini)

-       Kufunga Swawm za Sunnah kama Jumatatu na Alkhamiys, Masiku meupe (Ayyaamul-biydhw) (tarehe 13, 14 na 15) na Swawm ya Nabii Daawuud (kufunga kila baada ya siku moja);

-        Kujielimisha mambo ya Dini kwa kusoma vitabu na kusikiliza mawaidha;

-        Kuomba Maghfirah na Tawbah;

-        Kufanya kila aina ya dhikr (kumkumbuka na kumtaja Allaah), kwa kusoma Qur-aan kwa wingi, kumshukuru, kumtukuza, kuomba du'aa n.k.; 

-        Kuwasiliana au kutembeleana na ndugu na jamaa;

-        Kutenda wema kwa jirani, marafiki na watu wote kwa ujumla;

-        Kutoa sadaka;

-        Kulisha masikini;

-        Kupatanisha waliogombana;

-                  Kuamrishana mema na kukatazana maovu, na mengi mengineyo katika vitendo vyema.




* Swalah za Sunnah


Ratiba Ya Swalah Za Sunnah  Zilizosisitizwa Na Zisizosisitizwa




NYAKATI ZA
SWALAH

*MUAKKADAH
(ZILOSISITIZWA)
GHAYR MUAKKADAH (ZISOSISITIZWA)
KABLA
BAADA
KABLA
BAADA
ALFAJIRI
**2
Soma Suratul-Kaafiruun na Ikhlaasw
-
-
-

ADHUHURI

4
2
-
-
ALASIRI

-
-
4
-
MAGHARIBI

-
2
Soma Suratul-Kaafiruun na Al-Ikhlaasw
2
-
'ISHAA

-
2
2
-



Fadhila Zake:


(( مَا مِنْ عبْدٍ مُسْلِم يُصَلِّي للَّهِ تَعَالى كُلَّ يَوْمٍ ثِنْتَيْ عشْرةَ رَكْعَةً تَطوعاً غَيْرَ الفرِيضَةِ ، إِلاَّ بَنَى اللَّه لهُ بَيْتاً في الجَنَّةِ ، أَوْ : إِلاَّ بُنِي لَهُ  بيتٌ في الجنَّةِ  )) رواه مسلم  

((Hatoswali mja Rakaa 12 zisizo za fardhi kwa siku, ila atajengewa [na Allaah] nyumba peponi)) [Muslim]



 Nazo ni hizo Muakkadah (Zilosisitizwa) jumla yake ni 12 


 (( ركْعتا الفجْرِ خيْرٌ مِنَ الدُّنيا ومَا فِيها ))   رواه مسلم

** ((Rakaa mbili (za Sunnah) kabla ya Alfajiri ni kheri kuliko duniya na yaliyomo ndani yake) [Muslim]




 ‏‏((ما من عبد يسجد لله سجدة إلا كتب الله له بها حسنة ومحا عنه بها سيئة ورفع له بها درجة فاستكثروا من السجود))    رواه ابن ماجه

((Mja yeyote atakayesujudu sijda moja ataandikiwa wema mmoja, na atafutiwa baya moja, na atapandishwa daraja yake, kwa hiyo zidisheni kusujudu)) [Ibn Maajah]  




Swalah ya Tahajjud

(( أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))  رواه مسلم

((Swalah iliyo bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku))  [Muslim]




Swalah Ya Dhuhaa na  Swalah Ya Witr



عـَن أبي هـُريْرَة رضيَ الله عنه قال : أوصـَانـِي خـَليلي صـَلـَّى الله عليه وسلم بـِصـِيامِ ثـَلاثـَة ِ أيـَّام ٍ مـِنْ كـُل شـَهر ٍ، وَ ركـْعـَتي الضـُّحى ، وأنْ أوتـِرَ قبلَ أنْ أرقـُـد "  ـ متفق عليه ـ


Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba “Ameniusia rafiki yangu Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam [mambo matatu]; kufunga siku tatu katika kila mwezi, Rakaa mbili Dhuhaa na niswali Witr kabla ya kulala” [Al-Bukhaariy na Muslim]


Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kujitenga na maasi na kuzidisha mema katika mwezi huu mtukufu wa Muharram.
chanzo alhidaaya

Fadhila Za Mwezi Wa Muharram, Siku Ya 'Aashuraa Na Bid'ah Zake

AlhamduliLLaah, Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha tena katika mwaka mwengine mpya wa Kiislamu. Katika mwezi  wa Muharram, kuna fadhila zake maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi Muislamu anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho ili aweze kujichumia thawabu nyingi. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana kama Taasu'aa na 'Aashuraa. Hivyo ndugu Waislamu tusiache kufunga siku hizi mbili kwani thawabu zake ni kama ilivyotajwa katika mapokezi yafuatayo:
 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله))  رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka uliotangulia)) [Muslim]
(soma maelezo chini kujua kwanini tufunge pia na tarehe 9 Muharram)

Jumla ya miezi mitukufu ni minne na mwezi huu wa Muharram ndio mwezi wa kwanza unaoanza kuhesabika kama ni mwaka mpya.

((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَق السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ))

((Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Allaah ni miezi kumi na mbili katika ilimu ya Allaah (Mwenyewe tangu) siku Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajab, Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram) (kufanya) hivi ndiyo dini iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu (kwa kufanya maasi) katika (miezi) hiyo)) [At-Tawbah 9:36]

Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyotoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu):   

 (السنة اثنا عشر شهرا، منها أربعة حرم: ثلاث متواليات، ذو القعدة، وذو الحجة، والمحرم، ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان)) رواه البخاري، ومسلم

((Mwaka una miezi kumi na mbili, minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab ambao uko baina ya (mwezi wa) Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ni neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Kutujuaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au masiku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine.

Kuhesabika Kwa Mwaka Mpya Wa Hijriyah 
 
Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya kuhama (Hijrah) kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba kutoka Makkah kuhamia Madiynah. Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji ambao wataanza kutumia Sharia'h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana kamaMuharram. Na pia inasemekana kuwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipata barua kutoka kwa mabalozi wake wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislam, na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe. Akawashauri Maswahaba wenzake kuwa kuwe na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohamia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah.

Na mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama A.H au H kwa kirefu yenye maana 'After Hijrah' au Hijriyah, tarehe 1 Muharram A.H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622M. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka mwezi wa Dhul-Hijjah unapomalizika na mwezi wa Muharram utakapoingia hivi karibuni

Fadhila Za Mwezi Huu Khaswa

Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika Aayah ya juu ni mitukufu lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine kama ilivyo katika Hadiyth zifuatazo:

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم

Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]

 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان " رواه البخاري

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisubiri kufunga siku yoyote kama siku hii ya siku ya 'Aashuraa na mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhaan" [Al-Bukhaariy]  

Swawm ya 'Ashuraa imependezeshwa hata kwa watoto kuifunga kama walivyokuwa wakifanya Maswahaba katika siku hiyo.

عن الرُّبيّع بنت معوذ رضي الله عنها قالت: "أرسل رسول الله صلى الله عليه وسلم غداة عاشوراء إلى قرى الأنصار  "من أصبح مفطرا فليتم بقية يومه ومن أصبح صائما فليصم" ، قالت : فكنا نصومه بعد ونصوّمه صبياننا ...  رواه البخاري ومسلم  

Kutoka kwa Ar-Rubay'i  bint Mu'awwadh (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituma ujumbe Alfajiri ya siku ya 'Ashuraa katika vijiji vya Answaar "Aliyeamka akiwa amefuturu amalize siku yake (kwa kutokula) na aliyeamka amefunga afunge" Akasema (Ar-Rubay'i: 'Tulikuwa tukifunga baada yake na tukiwafungisha watoto wetu...' [Al-Bukhaariy na Muslim]

Sababu Ya Kufunga Siku Ya 'Aashuraa  
 
 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ"   رواه البخاري

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Aashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa Wana wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy]    

Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa kuongeza siku moja kabla.    

روى عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قال : "حِينَ صَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ يَوْمٌ تُعَظِّمُهُ الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((فَإِذَا كَانَ الْعَامُ الْمُقْبِلُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ صُمْنَا الْيَوْمَ التَّاسِعَ)) قَالَ فَلَمْ يَأْتِ الْعَامُ الْمُقْبِلُ حَتَّى تُوُفِّيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ". رواه مسلم 

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alipofunga Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya 'Aashuraa na akaamrisha ifungwe wakasema: Ewe Mtume wa Allaah, hii ni siku wanayoitukuza Mayahudi na Manaswara.  Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ikifika mwakani In shaa Allaah tutafunga siku ya tisa pia)). Akasema (Ibn 'Abbaas) haukufika mwaka uliofuata ila alifariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Muslim]

Kwa hiyo ni bora kufunga siku ya tisa na kumi Muharram, na kama mtu hakujaaliwa kufunga siku ya tisa na kumi, basi afunge siku ya kumi peke yake ili asikose kupata fadhila ya siku hiyo. 

Kwa vile siku hii ni siku Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyomnusuru Muusa ('Alayhis-Salaam) na Wana wa Israaiyli, na sisi pia tutakaofunga tuwe na tegemeo kuwa nasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatunusuru pia kutokana maadui wetu na mabaya kama Alivyotuahidi In shaa Allaah     

 ((إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ))

((Bila ya shaka Sisi Tunawanasuru Mitume Yetu na wale walioamini katika maisha ya dunia ya siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe)) [Ghaafir 40: 51]

Juu ya kwamba fadhila ya kufunga Swawm ni ibada Aipendayo kabisa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama ilivyo katika Hadiyth mbali mbali, vilevile funga hii itatusafisha na madhambi ya mwaka mzima,       

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم

Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka wa nyuma)) [Muslim]

Ndugu Waislam, hii ni fursa kubwa ya kujisafisha na dhambi na kuzidisha taqwa (ucha Mungu) ili kujibebea zawadi nyingi twende nazo Akhera kwa vile  hatujui  amali njema zipi zitakazokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na hatujijui kama tutakuwa na umri wa  kuchuma zaidi.

Bid'ah Katika Siku Ya 'Aashuraa   
 
Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa, tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu, kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu). Matendo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).   

Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu):
"Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia  wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliharamisha kama ilivyo katika Hadiyth hii  sahihi:

 عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية))  البخاري .

Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy]

Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo."

Ibn Rajab amesema:
"Wanayoyafanya Ma-Rafidhah (Mashia) katika siku hii kuwa ni siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema, wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya huzuni kwa wasio Mitume?"

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema.  Aamiyn.

chanzo www.alhidaaya.com