Kilio
Chetu ni tamthiliya inayojikita kuzungumzia umuhimu wa elimu ya jinsia
na ukimwi kwa vijana, Tamthiliya hii inaonesha namna ukosefu wa elimu ya jinsia
na ukimwi kwa jamii hususani vijana inavyochangia mimba za utotoni au mimba
zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana.
Katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna ambavyo jamii
ikiangaika kujielimisha kuhusu elimu hii ya jinsia na ukimwa na kuwaacha vijana
wakiangamia kwa kukosa elimu hiyo, hali hii inaifanya jamii kugawanyika, wapo
wanaoona kuwa suluhisho la janga hili la Ukimwi, ni jamii nzima wakiwemo na
vijana kupewa elimu hii lakini wapo wazazi wanaopinga wakiamini vijana umri wao
wakupewa elimu hii haujafika bado. Je ni nini hatima ya vijana hawa? Basi
tafuta kitabu hiki cha Kilio chetu kisome utajifunza mambo mengi sana ni kitabu
kinachotakiwa kusomwa na watu wa rika lolote.
WAHUSIKA
Katika kazi ya fasihi
wahusika wanaweza kuwa watu, wanyama au vitu, na wahusika ndiyo wanaobeba
dhamira za msanii, na katika kazi ya fasihi wahusika tunawagawa katika makundi
mawili, wahusika wakuu na wahusika wasaidizi/ wahusika wadogowdogo
(a) Wahusika
Wakuu
Katika tamthiliya hii, ina wahusika
wakuu wawili, ambao ni Suzi na Joti.
1. SUZI
ü Ni
binti anayesoma shule ya msingi
ü Ni
binti asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, Mama yake anashindwa kumpa elimu
hiyo akiamini kuwa umri wa Suzi haujafikia kupewa elimu hiyo.
ü Anajiingiza
katika mapenzi akiwa mdogo.
ü Anakuwa
na mahusiano ya kingono na mwanafunzi mwenzake anayeitwa Joti.
ü Ni
binti wa pekee wa Mama Suzi.
ü Anapata
mimba akiwa mwanafunzi na anafikiria kuiotoa mimba hiyo.
2. JOTI
ü Ni
kijana wa kiume anayesoma shule ya msingi.
ü Ni
kijana asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, baba yake anashindwa kumpa elimu
hiyo akiamini kuwa umri wa joti haujafikia kupewa elimu hiyo.
ü Anajiingiza
katika mahusiano ya kingono akiwa mdogo huku akiwa mwanafunzi.
ü Anajihusisha
na mahusiano ya kingono na wasichana wengi, akiwemo Suzi, Chausiku, Gelda n.k.
ü Ni
mvulana mlaghai, anawalaghai wasichana ili tu kutimiza haja zake za kingono.
ü Anaambukizwa
virusi vya ukimwi
ü Anafariki
kwa ugonjwa wa ukimwi.
(b) Wahusika wadogo wadogo
1. MAMA SUZI
ü Huyu
ni mama yake Suzi
ü Anamlea
Suzi bila baba
ü Anajishughulisha
na biashara ndogondogo kama vile kuuza vitumbua ili kujipatia kipato.
ü Anaamini
kuwa mtoto mdogo hawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi.
ü Anakumbatia
mila na desturi zililozipitwa na wakati zinazokataza watoto/vijana kupewa elimu
ya jinsia na ukimwi.
ü Anakataa
katakata mtoto wake, Suzi kupewa elimu ya jinsia na ukimwi akiamini kuwa umri
wake ni mdogo, na kufanya hivyo ni sawa na kumfundisha umalaya.
ü Anamwadhibu
mtoto wake (Suzi) baada ya kukuta vidonge vya kuzuia mimba katika mfuko wa
sketi yake.
2. BABA JOTI
ü Ni
baba yake na Joti.
ü Anaamini
kuwa ukali wa mzazi na viboko ndiyo suluhisho la kuwazuia watoto kujiingiza
katika mambo mabaya.
ü Anakataa
katakata elimu ya jinsia na ukimwi kutolewa kwa watoto/vijana.
ü Anaangaika
kuokoa uhai wa mtoto wake, Joti, kwa kutafuta tiba yake kila mahali.
ü Anampoteza
mtoto wake(joti) baada ya kufariki kutokana na ukimwi.
3. MAMA JOTI
ü Huyu
ni mama yake Joti.
ü Mke
wa Baba Joti
ü Rafiki
yake Mama Suzi
ü Anahisi
mume wake ana uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine, hali inayomlazimu
kuwanunulia kanga zenye maandishi ya mafumbo ili kuwapasha wezi wake.
ü Yeye
na mumu wake (Baba Joti) wanashindwa kumpa Joti elimu ya jinsia na ukimwi.
4. BABA ANNA
ü Huyu
ni baba yake Anna.
ü Anaamini
kuwa elimu ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru na janga la
ukimwi.
ü Kwa
kushirikiana na mke wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya jinsia na
ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
5. MAMA ANNA
ü Huyu
ni mama yake Anna.
ü Ni
mke wa Baba Anna
ü Kwa
kushirikiana na mume wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya jinsia na
ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
6. ANNA
ü Mtoto
wa kike wa Baba Anna na Mama Anna
ü Ni
mwanafunzi wa Shule ya msingi.
ü Amepewa
elimu ya jinsia na ukimwi, elimu inayomsaidia kupambana na vishawishi vya
kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mdogo
ü Ana
mkatalia Mwarami kuwa naye kimapenzi
7. MJOMBA
ü Huyu
ni kaka yake na Mama Suzi
ü Mjomba
wake na Suzi
ü Anasisitiza
elimu ya jinsia itolewe kwa vijana wote ili kuwanusuru na maambukizi ya virusi
vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa.
ü Anamshauri
Baba Joti kutoangaika kwenda kwa waganga na kumaliza rasilimali zake kwa ajili
ya kutafuta tiba ya UKIMWI kwa mtoto wake Joti kwani ukimwi hauna dawa
8. JIRANI
ü Huyu
ni jirani yake na Baba Joti.
ü Anamshawishi
Baba Joti kwenda kwa mganga wa kienyeji kutibiwa ukimwi.
9. MWARAMI
ü Huyu
ni rafiki yake Joti, Choggo na Jumbe
ü Ni
mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Hana
elimu ya jinsia na Ukimwi anaamini ukimwi unawapata wakubwa tu
ü Wenzake
wanamshawishi kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na hata kumtishia
asipofanya hivyo watamfukuza katika kundi lao la urafiki
ü Anashindwa
kumshawishi Anna
10. CHOGGO
ü Huyu
ni rafiki yake Joti, Mwarami na Choggo
ü Ni
mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Anajiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mtoto mdogo tena mwanafunzi
ü Yeye
na rafiki zake wana tabia ya kwenda katika vibanda vinavyoonesha video za ngono
(sinema za X) kuangalia
11. JUMBE
ü Huyu
ni rafiki yake Joti, Mwarami na Choggo
ü Ni
mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Anajiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mtoto mdogo tena mwanafunzi
ü Yeye
na rafiki zake wana tabia ya kwenda katika vibanda vinavyoonesha video za ngono
(X) kuangalia
12. CHAUSIKU
ü Huyu
ni mwanamke mtu mzima jirani na akina Joti.
ü Anajishughulisha
na biashara ndogondogo hususani biashara ya vitumbua ili kujipatia kipato.
ü Anakuwa
na mahusiano ya kimapenzi na kijana mdogo tena mwanafunzi (Joti)
ü Ana
mahusiano ya kimapenzi na Mpemba muuza duka.
13. FAUSTA
ü Huyu
ni msichana anayesoma darasa la tano
ü Anafariki
kwa ukimwi
14. MPEMBA
ü Huyu
ni mfanyabiashara wa duka
ü Anakuwa
na mahusiano ya kimapenzi na Chausiku
Mfano
wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Wahusika na hasa mhusika mkuu katika tamthiliya ndiye anayeifikishia jamii ujumbe uliokusudiwa. Tumia tamthiliya
mbili kutetea hoja yako.
2. Chagua wahusika watatu wa kike kutoka kila tamthiliya kati ya
tamthiliya mbili ulizosoma, kasha onesha kukubalika kwao kama kielelezo cha
maisha katika jamii.
DHAMIRA
Hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza
katika kazi ya fasihi. Na katika tamthiliya hii kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo ambazo
zimejitokeza, kwa kuanza tunaanza na;
(a) Dhamira
Kuu
Dhamira kuu katika tamthiliya ni
umuhimu wa elimu ya jinsia na ukimwi, mwandishi anaamini kuwa, ili jamii iweze
kunusurika na matatizo yatokanayo na kujamiana kama vile mimba za utotoni
(mimba zisizotarajiwa) magonjwa ya zinaa kama vile kasendwe, kisonono gono na
ukimwi, sharti vijana wapewe elimu ya jinsia na ukimwi, mwandishi anathibitisha
hili akimtumia muhusika Mjomba anaposema, “Upepo umebadilika sasa. Hawa
vijana wetu wapewe elimu ya familia ikiwepo ya jinsia. Watoto waambiwe wazi juu
ya mambo haya ya mapenzi na hatima yake.” Uk. 9
Vilevile, mwandishi anaonesha namna
ambavyo vijana wanapukutika, wanaangamia na ukimwi kwa sababu ya kukosa elimu
hii ya jinsia na ukimwi, hali hii inasababisha vijana kuwa gizani kabisa
wanashindwa namna ya kujikinga na wengine hata kushindwa kutofautisha kati ya
puto na kondomu , rejea ukurasa wa 13, Mwandishi akimtumia muhusika Mtambaji
anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani. Watoto ndio kabisa. Wapo katika giza
nene. Wanashindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu.”
Si hivyo tu, mwandishi anaendelea
kutuonesha kuwa, ukosefu wa elimu hii ya jinsia na ukimwi kwa vijana/watoto
inawafanya watoto/vijana kujitenga na mapambano dhidi ya ukimwi kwakuwa wao
wanaamini kuwa ugonjwa huu wa ukimwi ni wa wakubwa tu kwani watoto hawawezi
kuambukizwa virusi vya UKIMWI kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika
Mwarami anapomwabia Anna, “Ukimwi unawapata wakubwa, Anna.” Uk. 25
Si watoto tu, wapo hata wazazi,
watu wazima ambao nao wanaamini kuwa watoto wadogo hawawezi kuambukizwa virusi
vya ukimwi, kama anavyoamini Mama Suzi, rejea ukurasa wa 4, muhusika Mama Suzi
anaposema, “...Lakini shoga, watu wanatafuta laana ya marehemu. Kitoto kama
kile; kife kwa ukimwi! Ungeingilia kona gani?” {Uk.4}
Mwandishi anaendelea kutuonesha
kuwa, hata mimba za utotoni, mimba zisizotarajiwa kwa vijana husababishwa na
ukosefu wa elimu hii ya jinsia, kwa mfano mwandishi anamtumia muhusika Suzi
ambaye anaamini kuwa, kwa kufanya ngono mara moja hakuwezi kusababisha mtu
akapata mimba, hili tunaliona ukurasa wa 28, Suzi anapomwambia Anna, “Wala sina mimba, kwanza mimi nimefanya mara moja tu na joti.” {Uk.28}
Vilevile, mwandishi anaonesha kuwa,
wapo watoto/vijana ambao kutokana na kukosa elimu hii ya jinsia, wanaamini kuwa
wao kama watoto hawawezi kupata mimba, mwandishi anamtumia muhusika Joti
anapowaambia rafiki zake, “Mara moja tu, hakuna mimba sisi watoto.” {Uk. 16}
Mwandishi hakuishia tu kuonesha
madhara ya kukosa elimu hii ya jinsia, kwa upande mwingine ameonesha faida za
elimu hii ya jinsia na ukimwi kwa vijana, mwandishi anaonesha kuwa, vijana
waliopata elimu hii, huwasaidia sana kupambana na kujizuia na vishawishi vya
kingono kutokana na uelewa waliokuwa nao, kwa mfano mwandishi anamtumia
muhusika Anna, ambaye kutokana na mafunzo aliyopewa na wazazi wake yanamsaidia
sana kupambana na kujizuia na vishawishi hivyo kutokana na kufahamu madhara ya
kushiriki ngono kabla ya wakati, hili mwandishi analithibitisha akimtumia
muhusika Anna anaposema, “...Hujui kama kuna madhara mengine. Hujui magonjwa ya zinaa
wewe: hujui kisonono, kaswende na mengine kedekede. Haya hata UKIMWI hujui?” {Uk. 25}
Hivyo mwandishi anashauri, elimu
hii ya jinsia na UKIMWI, isitolewa kiubaguzi, itolewe kwa watu wote kwani kila
mtu yuko katika hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI, mwandishi anaonesha
namna ambavyo vijana wanateketea kwa kubaguliwa kwao kupewa elimu hii, rejea
ukurasa wa 1-2, Mtambaji anaposimulia, “Wakubwa wakaandika mabuku kupeana
habari. Wakabandika mabango kupeana tahadhari, lakini watoto wakateketea kwa
kukosa habari zozote za kuwaokoa.”
Mwandishi anaonesha kuwa, kama
vijana wangeelimishwa kuhusu madhara ya kufanya mapenzi kabla ya wakati, namna
ya kujilinda, basi wasingetummbukia katika janga hili, mwandishi anathibitisha
kwa kumtumia muhusika Suzi anaposema, “Naapa kwa Mungu wangu, mimi na Joti tungepata bahati ya
kuelimishwa, tusingetumbu...tusi...(Anaanguka chini.)” {Uk. 36}
(b) Dhamira ndogo ndogo
1. Ukosefu wa elimu
Dhamira hii inajitokeza katika
tamthiliya, mwandishi anaonesha kuwa ukosefu wa elimu ya namna ya kupambana na
Ukimwi unaifanya jamii kushindwa kulikabili gonjwa hili, ukosefu wa elimu
unawafanya wengine kuamini ugonjwa huu ni wa kurogwa, wengine wanaamini ni
ugonjwa unaletwa na mizimu na hata wengine kudhani ni majini.
2. Mapenzi na ndoa
Suala la mapenzi na ndoa pia
limepewa nafasi katika tamthiliya hii, tukianza na suala la mapenzi, mwandishi
anajadili mapenzi ya namna mbili, mapenzi ya dhati na mapenzi ya ulaghai.
(a) Mapenzi
ya dhati
ü Baba
Anna kwa familia yake
ü Mjomba
kwa Suzi
ü Anna
kwa wazazi wake
ü Anna
kwa Suzi
ü Suzi
kwa Joti
(b) Mapenzi ya ulaghai
ü Joti
kwa Suzi
ü Joti
kwa Chausiku
ü Chausiku
kwa Joti
3. Malezi kwa vijana
ü Mwandishi
pia amegusia suala la malezi kwa watoto, mwandishi anaonesha kuwa, malezi bora
kwa mtoto ni malezi ya wazazi wote wawili, yaani baba na mama, na anapokosekana
mzazi mmoja huweza kumuathiri mtoto, katika tamthiliya hii tunamuona Suzi
akilelewa na mama peke yake bila baba hali hii inachangia mtoto kuingia katika
matatizo, hili linathibitishwa na mwandishi akimtumia muhusika Mama Suzi
anaposema, “Kila siku ninasema mwanangu mdogo, mwanangu ni mtoto mzuri, leo
Suzi unanifanyia hivi? Hivi baba yako angekuwepo ungefanya hivi? Ah Suzi,
ungefanya?” {Uk.31}
ü Katika
suala hili la malezi, mwandishi anatuambia kuwa kuwa, mzazi ndiyo mwalimu bora
kwa malezi mema ya mtoto,rejea ukurasa wa 11, Mjomba na Baba ANNA wanaposema, “Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza...Na ndiye bora.” {Uk. 11} hivyo wazazi wawafundishe vema watoto wao, lakini
wazazi wasipofanya hivyo, walimwengu watawafundisha na kwa kawaida walimwengu
hufundisha katika upotofu, rejea ukurasa wa 10-11, Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu
watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.” {Uk.10-11}
ü Mwandishi
pia anaonesha kuwa, ili watoto/vijana wawe na maadili mema, wazazi wanatakiwa
kukaa na watoto wao kuwaelimisha mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuwa na
madhara kwao kama alivyofanya Baba Anna na mke wake, rejea ukurasa wa 10 Baba
Anna anapowaambia wenzake, “Hilo ndilo mie nililofanikiwa mwenzenu. Nimemwambia mama Anna
akae na mabinti zake name nikae na vijana wangu wa kiume. Tumefanya kazi hiyo
kwa makini sana. Tumewaelimisha juu ya madhara ya tabia hiyo kwao binafsi na
kwetu sote. Hatukubakiza kitu.” {Uk. 10}
4. Usaliti
Usaliti ni dhamira nyingine
inayojitokeza katika tamthiliya hii, kwa mfano mwandishi anaonesha usaliti
unaofanywa na Baba Joti kwa mke wake, Baba Joti anaisaliti ndoa yake kwa
kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, hili linathibitishwa na
Mama Anna anaposema, “Lakini leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu
nguru anayeichimba ndoa yangu.” {Uk. 7}
Usaliti mwingine, tunaona kwa Joti,
pamoja na kwamba Joti anakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Suzi anaamua
kumsaliti na kuanzisha mahusiano na wanawake wengine, mwandishi analithibitisha
hili akimtumia muhusika Suzi anaposema, “Ndiyo maana mie nilikuwa nakataa
Joti. Nishaambiwa kwamba unawasichana wengi shuleni na mtaani kwetu.” {Uk. 21}
Usaliti mwingine unajitokeza kwa
Joti na Chausiku, mwandishi anaonesha kuwa Joti pamoja na kuwa na mahusiano na
Chausiku anamsaliti Chausiku kwa kuwa na mahusiano na wasichana wengine, Joti
anapewa vitu na Chausiku naye anawapa wanawake wengine, rejea ukurasa wa 22, Chausiku anaposema, “Toka hapa. Nimesikia habari zako.
Kila msichana unamtaka tu. Mie nakununulia fulana ya mazoezi wewe unahonga
kinyago chako kile. Bisha...Nikikupa hela ya kununua peni we unanunulia bazooka
visichana vyako.” {Uk. 22} lakini si Joti tu ndiye anamsaliti mwenzake,
mwanandishi anatuonesha kuwa, hata Chausiku pia, anamsaliti Joti kwa kuwa na
mahusiano na wanaume wengine, rejea ukurasa wa 22-23, Mwarami anapomwambia
Joti, “Sasa ndiyo kuparamia mpaka wasichana wakubwa wa mtaani? Fikiri juu ya
Chausiku, Yule msichana mjuvi wa mji ambaye pia anachukuliwa na Yule mpemba
muuza duka.” {Uk. 22-23}
Tukigeukia katika uhalisia wake,
suala la usaliti katika ndoa au mapenzi bado ni tatizo kubwa sana katika jamii
yetu, wanandoa wanasalitiana, wapenzi wanasalitiana tabia hii ya usaliti huwa
ni kichochea kikubwa sana kwa watu kuambukizana virusi vya ukimwi, kama
tunavyoona kwa Joti. Hivyo jamii iache usaliti.
5. Athari za utandawazi
Mwandishi pia amejadili suala la
utandawazi na athari zake, mwandishi anaonesha namna utandawazi unavyochangia
kwa kiasi kikubwa kuharibu tabia na maadili ya watoto na vijana, kwa mfano
tunawaona akina Joti, Jumbe, Choggo na Mwarami wanajiingiza katika mahusiano ya
kingono wakiwa watoto wadogo kutokana na kuathiriwa na video za ngono (sinema
za X) wanazozitazama mtaani, mikanda hii ya ngono imekuwa rahisi sana
kupatikana kutokana na utandawazi.
6. Athali za ukoloni na ukoloni mambo leo
Suala la ukoloni na ukoloni mambo
leo pia limepewa nafasi katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna wakoloni walivyoharibu utamaduni wetu kwa kuuita ushenzi na hata
tulivyopata uhuru, viongoni wetu wakaendelea kushikilia mawazo hayo potofu ya
kikoloni ambayo kwa kiasi kikubwa tunaangamia wenyewe, hili mwandishi
analithibisha akimtumia Mtambaji anaposema, “Mila zetu hazikukataza kutoa
mafunzo ya elimu ya jinsia...Wakoloni na vibaraka wao ndio wanaostahili
kulaumiwa wakoloni walipiga vita jando na unyago wakidai eti ni ushenzi.” Mtambaji anaendelea kutuambia tena, “Viongozi wetu nao wakaendeleza mawazo hayo hata baada uhuru
bila kutambua kuwa wanajiua wenyewe.” {Uk. 13-14}
7. Nafasi ya mwanamke katika jamii
ü Mwanamke
amechorwa kama mlezi wa familia, mwandishi anatuonesha namna ambavyo mwanamke
anakuwa mlezi mzuri wa familia, anaangaika hapa na pale kuhakikisha mtoto au
watoto wake wanapata mahitaji yote muhimu kama vile chakula, mavazi na hata
elimu, rejea ukurasa 30, Mama Suzi anaposema, “Mimi ninahangaika kukusomesha,
wewe unanifanya hivi...Mama yako nimeungua viganja kwa kupika vitumbu ili
mwanangu usome.” {Uk. 30}
ü Mwanamke
amechorwa kama mtu mwenyemsimamo,
mwandishi anamtumia muhusika Anna kumuonesha mwanamke kama mtu mwenye msimamo
katika maamuzi yake, tunamuona Anna pamoja na kusumbuliwa mara kwa mara na
Mwarami kumtaka kimapenzi bado anashikilia msimamo wake ule ule wa kumkatalia,
hata watu wazima wenye uwezo kipesa wanapomtaka Anna bado Anna anaonesha
kutoyumba kimimamo kwa kuwakatalia. Rejea wimbo anaoimba Anna ukurasa wa 27,
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni x2”
ü Mwanamke
amechorwa kama mtu anayepinga mabadiliko katika jamii, mwandishi anatuonesha kuwa mwanamke ni mtu asiyependa
mabadiliko katika jamii, asiyependa kwenda na wakati, dunia inabadilika jamii
inatakiwa kuwaelimisha vijana wao kuhusu elimu ya jinsia na mahusiano ,Mama
Suzi anapinga, rejea Mama Suzi anaposema, “Tena ishia hapo hapo kaka! Huko si
kunifundishia mwanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono ilitoka wapi
hiyo? {Uk. 9}
ü Mwanamke
amechorwa kama mtu asiye na msimamo, mwandishi anatuonesha kuwa,
mwanamke ni mtu asiye na msimamo katika maamuzi yake, mwandishi anamtumia Suzi,
kuijadili nafasi hii, richa ya Suzi kuamua kuachana na Joti na hata anapogundua
kuwa Joti anamahusiano na wanawake wengine bado anakubali kuendelea naye.
(Rejea uk. 17 na 21)
ü Vile
vile, mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe,anamtumia muhusika Joti ambaye anawatumia wanawake ili
kujistarehesha kingono, lakini pia tunaona namna watu wanavyotumia pesa na vitu
vya thamani ili kuwarubuni wasichana wapate kukidhi mahitaji yao ya kingono.
{rejea ukurasa 27}
ü Mwanamke
amechorwa kama mtu asiye na elimu juu ya mambo ya jinsia na ukimwi, katika kuilezea nafasi hii, mwandishi anamtumia muhusika Mama
Suzi, ambaye anaoneka kutokuwa na ufahamu mzuri juu ya masuala ya UKIMWI, kwa
mawazo yake anaamini kuwa ugonjwa wa UKIMWI ni ugonjwa unaowahusu watu wakubwa
tu, na watoto hawawezi kuambukizwa jambo ambalo si sahihi. Hata katika jamii
yetu, wapo watu wanaoamini kuwa ugonjwa huu wa UKIMWI huwakumba watu wazima
watoto na watu walio katika ndoa hawawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi jambo
ambalo si kweli. Hivyo jamii inatakiwa kuelimishwa sana kuhusu ugonjwa huu.
Mfano
wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Taja maadui sita na fafanua jinsi waandishi wa tamthiliya mbili
kati ya ulizosoma walivyojitokeza kupambana na maadui hao.
2. Waandishi wa tamthiliya wamemchora mwanamke katika sura tofauti.
Thibitisha kauli hii kwa kutumia waandishi wawili (2) wa tamthiliya mbili
(2)ulizosoma.
MIGOGORO
Migogoro ni hali ya kutoelewana
baina ya pande mbili, unaweza kuwa mgogoro kati ya mtu na mtu, mtu na kikundi
cha watu, kikundi kimoja na kikundi kingine cha watu au unaweza kuwa mgogoro wa
mtu na nafsi yake. Katika tamthiliya hii,
mwandishi ameweza kuibua na kuonesha migogoro mbalimbali ambayo kwa kiasi
kikubwa migogoro hiyo imeweza kusaidia katika ujenzi wa dhamira mbalimbali
zilizoweza kujitokeza katika kazi hii, migogoro iliyojitokeza katika tamthiliya
hii ni:
ü Mgogoro
kati ya Mama suzi na mwanaye,(Suzi)
chanzo cha mgogoro ni Mama Suzi kukuta kasha la vidonge vya kuzuia mimba kwenye
mfuko wa sketi ya Suzi, mgogoro unakua zaidi Mama Suzi kuamua kumuadhibu kwa
kumchapa Suzi hadi anapotokea Mjomba na Baba Anna, kuamulia mgogoro huo na
kushauri jambo la msingi ni kumpa elimu ya jinsia na si kutumia ukali na
viboko, kama ambavyo Baba Anna anasema, “Watoto wajazwe elimu, waone uchafu
na hatari ya kufanya haya. Siyo kuwatia hofu tu. Je leo ukifa ama kulazimika
kuwa mbali nawe? Si atafanya tu maana mtia hofu hayupo?” {Uk. 13}
ü Mgogoro
kati ya Mjomba na Mama Suzi, chanzo cha mgogoro ni kitendo cha
Mjomba kumshauri Mama Suzi kuacha kumuadhibu Suzi na badala yake apewe elimu ya
jinsia na mahusiano ya kimapenzi jambo linalopingwa na Mama Suzi na hivyo
kuibua mgogoro. {Rejea ukurasa wa 8-14}
ü Mgogoro
kati ya Suzi na Joti, mgogoro huu unaibuka baada ya Suzi kupigwa na mama yake sababu
ya vidonge vya kuzuia mimba alivyopewa na Joti, mgogoro huu unafikia hatua ya
Suzi kuamua kuachana na Joti, suluhisho la mgogoro huu, wanaamua kurudiana na
kuendelea na uhusiano wao. (Rejea uk. 17 na 21)
ü Mgogoro
kati ya Mwarami na rafiki zake yaani Jumbe, Joti na Choggo. Chanzo cha mgogoro ni kitendo cha Mwarami kutokuwa na uhusiano
wa kimapenzi na wasichana, hatua inayosababisha kumtishia kumfukuza katika
kundi lao, rejea ukurasa wa 24, Jumbe anapomwambia Mwarami, “Sasa bwana hapa
kwenye grupu letu hatutaki tabia hiyo ya ushamba. La sivyotutakutoa umemba.” Suluhisho la mgogoro huu ni Mwarami kuamua kumshawishi Anna
kimapenzi hata hivyo juhudi zake zinagonga mwamba.
ü Mgogoro
kati ya Mama Joti na Mwanamke anayedhani anaingilia ndoa yake,Mama Joti anaona suluhisho la mgogoro huu ni kununua kanga zenye
maneno ya vijembe ili kumpasha na kumuumiza roho, Rejea Mama Joti anaposema, “Lakini leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu
nguru anayeichimba ndoa yangu...Ngoja kwanza nimpashe najua litamuuma tu.” {Uk. 7}
ü Mgogoro
mwingine ni kati ya Chausiku na Joti, chanzo cha mgogoro huu ni baada ya
kugundua kuwa Joti anamahusiano ya kimapenzi na wasichana wengine, mgogoro
unafikia hatua ya Chausiku kumtishia kumdhuru Joti, kama anavyosema,“We
usinifanye mie bwege mwenzio...wewe ndiyo unajigonga gonga. Wewe na visichana
vyako hivyo nitawachoma moto mie! Nyie hamnijui, ohoooo!” {Uk. 22}
ü Mgogoro
kati ya ukale na usasa, huu ni mgogoro mwingine unaojitokeza katika tamthiliya,
mwandishi anaonesha mgogoro kati ya watu wanaokumbatia mambo ya kale, mambo
yaliyopitwa na wakati na wale wanaotaka mabadiliko katika jamii, mwandishi
anawatumia wahusika, Mama Suzi na Baba Joti kama watu wanaokumbatia mambo ya
kale na kwa upande mwingine anawatumia wahusika, Mjomba, Baba Anna na Mama Anna
kama watu wanaotaka mabadiliko katika jamii, wanataka ukuta unaowatenga watoto
na wazazi wao wasipate elimu ya jinsia ubomolewa, mwandishi anaonesha kuwa,
kukumbatia mambo ya kale kunaweza kuleta madhara kwa vijana kama madhara ya
kupata mimba kwa Suzi, rejea Suzi anaposema, “Mama hakuwa radhi kuachana na
utamaduni wa kale wa kuweka ukuta baina ya wazazi na watoto katika kujadili
mambo haya. Haya ndiyo madhara yake.” {Uk. 36}
ü Mgogoro
wa Suzi na nafsi yake, chanzo cha mgogoro huu ni kitendo
cha kuambiwa na mama yake kuwa shangazi yake ataenda kumpima mimba, Suzi anaona
suluhisho la mgogoro huu ni kutokubali kwenda kupimwa mimba na shangazi yake na
badala yake kumtafuta mwanaume anayehusika na mimba hiyo (Joti) kuzungumza naye, rejea Suzi anaposema, “Oh Mungu wangu! Nifanye nini sasa? Siwezi kumruhusu shangazi
akanipime...oh, nifanye nini mie! Nimtafute Joti, lazima niongee naye.”{Uk. 31}
ü Mgogoro
mwingine unaojitokeza ni mgogoro wa Suzi na nafasi yake kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi au la, chanzo cha mgogoro
huu ni baada ya Suzi kugundua kuwa ana mimba na kijana aliyempa hiyo mimba
ameathirika na virusi vya ukimwi, rejea Suzi anaposema, “Na mie Suzi nina mimba, mimba ya Joti. Kasha ina maana na mie
nina ukimwi?” {Uk. 36}
UJUMBE
Ujumbe ni funzo analolipata fanani anaposoma ama
kusikiliza kazi za fasihi, pamoja na ujumbe pia kuna maadili mbalimbali
hupatikana, katika tamthiliya hii kuna mafunzo mbalimbali ambayo msomaji wa
kazi hii anaweza kuyapata, mafunzo hayo ni kama:
ü Elimu
ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru vijana na mimba za
utotoni(mimba zisizotarajiwa) na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
ü Ukimwi
hauchagui rika, mwandishi anatupa ujumbe kuwa gonjwa hili la UKIMWI hauchagui
mtu, kila mtu anaweza kuupata, kama tunavyoona kwa Fausta na Joti, ni
watoto wadogo lakini wanaathirika na virusi vya ukimwi na kusababisha vifo
vyao.
ü Asiyefunzwa
na mama yake, hufunzwa na ulimwengu, hili ni funzo linguine tunalilipata
katika tamthiliya, mwandishi anatufundisha umuhimu wa wazazi kuwafundishi
watoto wao maadili mema na si kuwaacha watoto wakajifunza wenyewe mtaani,
wakiwaacha hivyo, huko hujifunza mambo yasiyofaa, tunaona kwa Suzi, Joti,
Mwarami, Choggo, Jumbe, wazazi wao hawakuwafundisha elimu ya jinsia na
mahusiano watoto wakajifunza wenyewe mambo machafu na hataimaye yakawaletea
madhara.
ü Wazazi
ndiyo walimu bora kwa malezi bora na maadili mema kwa watoto wao. Mwandishi anaendelea kutufundisha kuwa, ili vijana wetu wawe
na tabia njema, mzazi ni mwalimu bora kabisa anayeweza kumfundisha mtoto wake
vema, rejea mwandishi akimtumia muhusika Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu
watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.”
ü Kinga
ni bora kuliko tiba. Ni vizuri jamii ikajikinga na magonjwa mbalimbali, kuliko
kutojikinga na baadaye kuanza kutafuta tiba, tiba huwa gharama sana kuliko
kujikinga, tunamuona Baba Joti akitumia gharama kubwa kutafuta tiba ya mtoto wake, kama ambavyo mwandisha anasema, “Mtani ushauza rasilimali zako kuuguza mtoto. Ushajitia umskini
kwa kuhangaika...” {Uk. 34} Hivyo basi ni vema jamii ikaamua kujikinga dhidi ya
matatizo mbalimbali kwani matatizo hayo pindi yanapokukumba huwa ni gharama
sana kuyatatua na wakati mwingine matatizo mengine huwa hayana tiba kama
tunavyoona katika ugonjwa wa UKIMWI.
ü Ngono
zembe ni chanzo cha maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa, Tunamuona Joti akiambukizwa virusi vya ukimwi kutokana na
kushiriki ngono zemba, vilevile tunamuona Suzi akipata mimba na hata kuwa
katika wasiwasi wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI kutokana na kushiriki ngono
zemba. (Rejea ukurasa wa 4 na 34)
Mafunzo mengine tunayoyapata katika
tamthiliya hii ni pamoja na:
ü Jamii
inatakiwa kubadilika ili kwendana na mabadiliko katika jamii.
ü Mila
na desturi zilizopitwa na wakati hatuna mudi kuachana nazo
ü Huwezi
kumtambua mtu aliyeathirika na virusi vya ukimwi kwa kumtazama kwa macho tu.
Uk. 4-5
ü Vijana
waelimishwe namna ya kukabiliana na changamoto za utandawazi.
ü Utandawazi
ni chanzo cha mmong’onyoko wa maadili ya vijana.
ü Malezi
bora ni muhimu kwa watoto/vijana ili kuwa na maisha bora baadaye.
ü Majuto
ni mjukuu, tunamuona Suzi akijuta kutokana na kutopata elimu ya jinsia na hivyo
kujikuta akitumbukia katika matatizo.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha ya kawaida, sentensi fupifupi
na inayoeleweka kwa urahisi,pamoja na hayo mwandishi pia ametumia lugha ya
kisanaa yenye mbinu mbalimbali za kisanaa kama vile nahau na tamathari za semi.
(a) Matumizi
ya methali
ü “Mzazi
usipomfunza, walimwengu watamfundisha.” Uk.
ü “Shukrani
ya punda mateke.” {Uk. 19}
(b) Matumizi ya misemo na nahau
ü Shoga,
mtakatifu wa kwenye mwanga si lazima awe mtakatifu gizani. {Uk. 4}
ü “Kakanyaga
nyaya.” {Uk. 4}
ü “Potelea
kwao...” uk. 9
ü “Makapera
kibao, mume wangu wa nini. Uk. 7
ü “Wembamba
wa reli treni inapita, uk 6
ü Kifua
simkingii, maana siwi naye. Uk 6
ü “Kwa
mashairi nimekuvulia kofia siku nyingi.” Uk.6
ü “We
pita juu mie nipite chini...”uk 19
ü Mbona
umetuanika juani. Uk 16
ü “Hakikisha
ndege mjanja ananasa katika tundu bovu.” Uk. 24
(c) Matumizi
ya taswira/lugha ya picha
ü Dubwana, Manaa yake ni kitu au mtu mwenye umbo kubwa lisilo la kawaida au
la hovyo hovyo, mwandishi ametumia neno dubwana kitaswira kuufananisha ugonjwa wa Ukimwi sawa na jambo
linalotisha, kuogopesha. (Rejea ukurasa wa 1-2)
ü Gizani, gizani ni mahali pasipokuwa na mwanga, hivyo mwandishi
ametumia neno giza, akimaanisha kukosa maarifa au kutokuwa na ufahamu ya jambo
fulani, kwa kifupi kukosa elimu, Rejea mtambaji anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani...watoto ndio kabisa. Wapo katika
giza nene.” {Uk. 13}
(d) Matumizi ya tamathali za semi.
(i) Tashibiha, hizi ni tamathari ambazo
hulinganisha vitu kwa kutumia viunganishi kama, mfano wa, sawa na, mithili ya,
kama vile. N.k. baadhi ya tashibiha zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
ü “Wewe
nawe unakuwa nyuma nyuma kama koti.” Uk. 4
ü “Shoga
mbona unakuwa mgumu kama mpingo?” uk. 5
ü “Watu
walipukutika, wakapukutika kama majani ya kiangazi.” Uk.1
ü “Lile
Dubwana limetanda kama utando wa buibui.” {Uk.13}
ü “Miti
inayoungua kama mabua.” Uk. 6
(i) Sitiari, hizi ni tamathari za semi ambazo hulinganisha vitu bila kutumia
viunganishi, mfano wa tamathali zilizotumika ni pamoja na:
ü “We
mbwa mweusi.” Uk. 8
ü “Nyoka
wee.” Uk.9
(ii) Mjalizo, hii ni aina ya tamathali za semi ambazo msanii/mwandishi
huitumia kutaja vitu au mambo yaliyo katika orodha bila kutumia viunganishi.
Mfano:
ü “...Lakini
soma maneno yake. Yamejaa kejeli, ushari, uchimvi, kusengenyana na kufumbiana
mafumbo ya kila aina.” Uk. 6
(iii) Nidaa, hizi ni tamathali za semi, zinazoonesha hali ya kushangaa au
kushangazwa na jambo Fulani, mfano wa tamathali hizi ni:
ü “Ai,
ai, lahaula lakwata...weye, hiki kitoto?” {uk. 9}
ü “Oi,
oi, oi, toba! Kile si kitoto kama cha kwangu...” {uk.10}
(iv) Takriri, hii ni hali ya kurudiarudia maneno, neno, silabi au sauti
zinazolingana katika kazi ya fasihi ili kusisitiza au kutia mkazo jambo fulani.
Mfano wa takriri zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
ü “Watu
walipukutika, wakapukutika kama majani ya
kiangazi. Wakapukutika.” Uk. 1
ü “Waongo!
Waongo wakubwa.” Uk. 3
ü “
Vifo vikawazoa, vikawazoa...vikawazoa.” uk. 2
ü “Piga
domo, piga doma, nikashinda.” Uk. 16
(v) Tanakali sauti Hii ni aina ya tamathali ambayo
sauti ya kitu fulani huigwa ili kwa lengo la kuburudisha au kuipa dhamira uzito
falani. Mfano wa tanakali sauti zilizotumika katika tamthiliya hii ni:
ü “Wacha
moyo unipwite pwi,pwi,pwi...” uk.16
(vi) Tashititi Hii ni aina ya tamathari ya semi ambayo mtu huuliza swali huku
jibu lake akilifahamu, mfano wa tashititi zinazojitokea katika tamthiliya hii
ni:
ü “Huyu
ni Suzi kweli au nani?” uk.15
Mfano
wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Lugha ni kipengele muhimu sana kwa mwandishi katika kufikisha
ujumbe wake kwa jamii. Jadili kauli hii kwa mifano toka katika tamthiliya mbili
ulizosoma.
MTINDO NA MUUNDO
(a) Mtindo
Mtindo ni jinsi msanii anavyotumia
ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza jambo fulani katika
kazi ya fasihi, na mtindo ndiyo huweza kumtofautisha msanii/mwandishi mmoja na
mwandishi mwingine. Mtindo hutumika kuipamba kazi ya fasihi, baadhi ya mitindo
nayotumika katika kazi hii ni pamoja na:
ü Matumizi ya hadithi
ndani ya tamthiliya
Mwandishi ametumia mtindo wa hadithi
ambao ni utanzu wa fasihi simulizi ndani ya tamthiliya, mtindo huu
unajidhihirisha ukurasa wa kwanza, Mtambaji anapoanza kusimulia hadithi
anaposema, “Paukwa” na
hadhira inaitikia “Pakawaaaaaaa” na
Mtambaji anaendelea, “Hapo zamani za kale paliondokea kisiwa kimoja...” {Uk.
1} Ni utanzu wa hadithi pekee ndiyo huwa na mwanzo wa namna hiyo.
ü Matumizi ya
wimbo/shairi ndani ya tamthiliya
Mwandishi pia ametumia wimbo kuipamba
kazi yake, wimbo unajitokeza ukurasa wa 27 Anna anaimba wimbo unaowataka
wanaume wanaomtaka kimapenzi kuacha kumfuatafuata, muda wake wa kujihusisha na
mahusiano ya kimapenzi haujafika bado mwanafunzi.
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni
x2”
ü Matumizi ya lugha ya
majibizano/dialojia na masilmulizi
Kama ilivyo ada, mtindo wa lugha
unaotumika katika tamthiliya, kwa asilimia huwa ni mtindo wa majibizano, yaani
dialojia. Hivyo basi hata katika tamthiliya hii, mwandishi kwa kiasi kikubwa
ametumia mtindo wa majibizano na kidogo ametumia masimulizi, (Rejea masimulizi
ya Mtambaji ukurasa wa 1-2, 3-4, na 36)
ü Matumizi ya nafsi zote
tatu
Pia nafsi zote tatu zinajitokeza katika
tamthiliya hii,
ü Nafsi
ya kwanza, mfano,Mimi nawashangaa... {Uk.
6} Najua
litamuuma tu (uk.7), Tumebomoa
ghala imara...” {Uk. 6}
ü Nafsi
ya pili, mfano, “Utamaliza
kanga zilizoandikwa kila aina ya maneno...”
Wewe unamwona
Fausta alikuwa mdogo?
ü Nafsi
ya tatu, mfano,
...alikufa kwa ukimwi” uk. 9, atakutafuta
tu mwenyewe.” (uk 17), “Wanashindwa kutofautisha kati
ya puto na kondomu.” (Uk.
13)
ü Matumizi ya picha,
mwandishi pia ametumia michoro mbalimbali inayoonesha matendo/matukio
mbalimbali ya wahusika, picha hizi zimesaidia sana kuipamba na kuipendezesha
kazi yake, picha hizo zinapatikana ukurasa wa 3,5,8,11,17,20,23,27, 29 na 35.
(a) Muundo
Muundo ni mfuatano wa masimulizi au visa
katika kazi ya sanaa ya fasihi, hivyo basi.muundo wa tamthiliya hii ni wa moja
kwa moja, yaani visa vyake vimepangwa kuanzia kisa cha kwanza , kati hadi
mwisho, katika kuvipanga visa vyake, mwandishi ameigawa kazi yake katika sehemu
sita, ambazo amezipa majina, Sehemu ya kwanza, Sehemu ya Pili, ya Tatu, ya Nne,
Tano na Sehemu ya Sita.
Sehemu ya kwanza.
Mtambaji anasimulia habari za Dubwana(Ukimwi),
anasimulia namna wakubwa wanavyoelimishana namna ya kujilinda na ugonjwa huo,
huku wakiwaacha watoto wakiangamia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi.
Sehemu ya Pili
Hapa mwandishi anatuonesha nyumbani kwa
Mama Suzi, Mama Suzi na Mama Joti wanapeana habari za kifo cha Fausta
kilichosababishwa na ukimwi, Mama Suzi anakuta kasha la vidonge kwenye mfuko wa
sketi ya Suzi wakati akifua jambo linalozua mgogoro kati ya Suzi na mama yake,
Mjomba na Baba Anna wanamshauri Mama Suzi kuacha kutumia ukali na badala yake anatakiwa
kumpa elimu ya jinsia binti yake ili ajitambue jambo linalopingwa vikali na
Mama Suzi.
Sehemu ya Tatu
Hapa mwandishi anatuonesha mtaani, Joti
anakutana na Suzi, Suzi anaamua kuachana na Joti kwa sababu ya vidonge vya
kuzia mimba alivyopewa na Joti kumsababishia kupigwa na mama yake. Joti
anawasimulia wenzake namna alivyofanikiwa kumpata Suzi, Joti, Jumbe, Choggo na
Mwarami wanaenda mtaani kuangalia sinema za X.
Sehemu ya Nne
Tukio linatendeka njiani, Joti na Suzi
wanakutana, Suzi anamlaumu Joti kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wasichana
wengine, wanaamua kurudisha uhusiano wao, Joti anaanza kujisikia vibaya, Jumbe
anaamua kumpeleka nyumbani, Mwarami anaonekana akimshawishi Anna amkubalie ombi
lake la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi, Anna anaonesha msimamo anamkatalia,
mwandishi pia anatuonesha namna Anna anavyoshinda vishawishi vya kingono.
Sehemu ya Tano
Tukio linatendeka chumbani kwa Suzi
akiwa na Anna, Suzi anajisikia vibaya, anahisi huenda ana mimba, anataka
kuitoa, rafiki yake Anna anamshauri kuachana na mpango huo kwani ni hatari,
anaamua kwenda kwa Joti kuzungumza naye suala hilo.
Sehemu ya Sita
Hii ni sehemu ya mwisho, mwandishi
anatuonesha nyumbani kwa Baba Joti, tunaona namna Baba Joti alivyoangaika kwa
waganga mbalimbali kutafuta tiba ya Joti bila mafanikio, mwisho wanaamua
kumpeleka hospitali, huko wanapata wajibu kuwa Joti amethirika na virusi vya
ukimwi, Jirani anamshauri Baba Joti kumpeleka Joti kwa mganga mwingine, Mjomba
anamshauri Baba Joti kuachana na mpango huo kwani ugonjwa alionao Joti hauna
tiba wala dawa. Suzi anawasili kwa akina Joti anagundua Joti ana ukimwi, Joti
anafariki dunia, Suzi anakuwa na wasiwasi kama naye atakuwa ameambukizwa virusi
vya ukimwi, anabaki akijutia kwa kukosa elimu ya jinsia na ukimwi. Na
mchezo unaishia hapo.
MANDHARI
Mandhari ni sehemu au eneo ambalo visa na matukio hutendeka
katika kazi ya fasihi, katika kazi ya fasihi mandhari huweza kuwa mandhari
halisi au ya kubuni, katika tamthiliya mwandishi ametumia mandhari ya kubuni,
hivyo basi, mandhari ya tamthiliya hii yanaweza kuwa sehemu yoyote ile katika
nchi za Kiafrika. Pia mwandishi anatuonesha visa na matukio yakitendeka
mandhari ya nyumbani, mtaani, njiani n.k.
Mandhari ya nyumba
Katika mandhari ya nyumbani, tunaona nyumbani kwa Mama Suzi na
Nyumbani kwa Baba Joti, kwa Mama Suzi tunaona ukuta uliowekwa kati ya mzazi na
mtoto kuhusu elimu ya jinsia kwa mtoto, Mama Suzi anamuadhibu Suzi kwa kukuta
vidonge vya kuzuia mimba kwenye mfuko wa sketi ya Suzi, Suzi anaanza kujisikia
vibaya, anafikiria kuitoa mimba. Nyumbani kwa Baba Joti, tunaona kuumwa kwa
Joti, kugundulika kuwa ana ukimwi na kufariki kwake.
Hivyo mwandishi ametumia mandhari hii, ili kufikisha dhamira ya
umuhimu wa elimu ya jinsia kwa watoto, malezi bora ya mtoto, tatizo la ugonjwa
wa ukimwi na athari zake katika familia, n.k.
Mandhari ya Mtaani
Katika mandhari haya, mwandishi, anatuonesha Joti na Suzi wakiwa
katika mazungumzo ya uhusiano wao wa kimapenzi, pia tunaoneshwa kuwa ni mahali
ambapo Joti na wenzake hukutana na kupanga mambo yao ya mapenzi. Mwandishi
anatumia mandhari haya, kuonesha namna watoto wanavyoharibikiwa kitabia mtaani,
mandhari ya njiani inatuonesha namna watoto wakike wanavyosumbuliwa na wanaume
wasiokuwa waadilifu ambao huwataka kimapenzi.
Mfano
wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Jadili jinsi fani ilivyotumika kukamilisha kazi za
waandishi wawili wa tamthiliya ulizosoma ukizingatia mtindo na mandhari.
FALSAFA, MTAZAMO NA MSIMAMO WA MWANDISHI
(a) Falsafa
ya mwandishi
Falsafa ni mchujo wa mawazo ya mwandishi
kuhusu maisha na jamii yake. Falsafa ya mwandishi wa tamthilia hii anaamini
kuwa, ili jamii yoyote ile iweze kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazoikabili jamii husika, elimu ni nyenzo muhimu sana ya kupambana na
changamoto hizo. Na elimu hiyo isitolewe kimatabaka.
(b) Mtazamo wa mwandishi
Mwandishi ana mtazamo wa
kiyakinifu, ana mtazamo kuwa, matatizo yote yanayotokea katika jamii chanzo ni
jamii yenyewe na jamii yenyewe ndiyo inayotakiwa kukabiliana na matatizo hayo,
na ndiyo maana anaitaka jamii yake ibadilike.
(c) Msimamo
wa mwandishi
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anaitaka jamii yake
ibadilike ili kuendana na wakati, na anaitaka jamii kuachana na mila na desturi
zilizopitwa na wakati ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu au tamthiliya hii ni Kilio Chetu,kilio chetu ina maana ya tatizo,
balaa au janga linapoingia katika jamii ni letu sisi sote. Hivyo basi, jina la
kitabu Kilio Chetu linasadifu sana yaliyomo katika tamthiliya hii. Tukianza na:
Tatizo la ukimwi
Mwandishi anajadili ukimwi kuwa ni ugonjwa hatari sana, ni
ugonjwa usiobagua mkubwa wala mtoto, kama mwandishi anavyosema, “Ukimwi hauchagui mkuwa wala mdogo.” {Uk. 25} hii inathibitisha kuwa tatizo hili la ukimwi ni letu
sote tunatakiwa wote kupambana nalo, na hapa ndipo linapokuja suala la Kilio Chetu.
Elimu ya jinsia
Mwandishi pia anaonesha kuwa suala
la watoto/vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi ni kilio cha jamii, jamii
inasisitiza na kupigia kelele suala la vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi,
kwa mfano, mwandishi anamtumia muhusika Baba Anna anaposema, “Mimi bwana
nitaendelea kusisitiza juu ya elimu hii.” Mwandishi anaendelea kwa kusema
akimtumia muhusika Mjomba, “Tutaendelea kuwaelimisha wazazi umuhimu wa elimu
hii.” {Uk.12} Hivyo tunaona kuwa Baba Anna na Mjomba wanatoa kilio chao cha
kutaka watoto kuelimishwa elimu ya jinsia.
Si vivyo tu, hata vijana wenyewe,
wanapaza sauti, wanatoa kilio chao kutaka kupewa elimu hii ya jinsia na ukimwi,
mwandishi anatuonesha kuwa kama vijana wangepata elimu hii wasingeatwa na
matatizo, kama anavyosema Suzi, ““Naapa kwa Mungu wangu, mimi na
Joti tungepata bahati ya kuelimishwa, tusingetumbu...” {Uk. 36} Pia rejea Mtambaji anaposema, “Watoto hawana uwezo
wa kukabiliana nalo...Sikieni kilio chetu!” {Uk. 15}
Hivyo basi, kwa ushahidi huu ni wazi kuwa, jina la kitabu
linasadifu yale yote yanayozungumzwa katika tamthiliya hii, na kwa hili
mwandishi amefanikiwa sana.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
(a) Kufaulu
kwa mwandishi.
Hapa tunaangalia kufanikiwa kwa
mwandishi katika vipengele vya fani na maudhui, Kifani mwandishi amefanikiwa
sana, tukianza na:
Wahusika
Mwandishi amefanikiwa kuwajenga
wahusika wake vizuri, amewajenga wahusika katika rika tofauti tofauti na kila
rika amefanikiwa kuwavisha uhusika unaendana na rika husika, na amafanikiwa
kuonesha namna kila rika linavyoweza kuathiliwa na UKIMWI na kuitaka jamii
kutoa elimu ya jinsia kwa kila rika.
Lugha
Mwandishi amefanikiwa kuifanyanga lugha yake kiufundi,
amefanikiwa kutumia lugha nyepesi inayoeleweka na kila mtu inayoambatana na
matumizi ya methali, misemo/nahau na tamathali za semi, matumizi yote haya ya
lugha yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha ujumbe uliokusudiwa na kuipamba
kazi husika. (Rejea kipengele cha Matumizi ya lugha)
Mtindo, katika suala la mtindo, mwandishi amefanikiwa kwa kiasi
kikubwa sana, kwani amefanikiwa kutumia utanzu wa hadithi na wimbo kuipamba
kazi yake na ikawa kazi ya kuvutia na inayovuta hisia za msomaji kupenda
kuendelea kukisoma kitabu hiki zaidi na zaidi. (Rejea kipengele cha Mtindo)
Muundo
Mwandishi ametumia muundo rahisi,
muundo unaeleweka kwa urahisi na hivyo kumsaidia mwandishi kufikisha ujumbe
alioukusudia kwa jamii husika, visa vyake amevipangalia vizuri hali inayomfanya
msomaji apende kuendelea kukisoma kitabu hiki ukurasa mmoja hadi mwingine hadi
anakimaliza kitabu hiki.
Kwa upande wa maudhui, mwandishi amefanikiwa kuonesha dhamira mbalimbali ambazo kwa
kiasi kikubwa zina uhalisia katika jamii yetu. (Rejea dhamira)
Vilevile, kwa upande wa ujumbe, mwandishi amefanikiwa kutupa ujumbe au mafunzo muhimu sana ambayo
kama jamii itayazingatia basi mafunzo haya yanaweza kuwasaidia sana. (Rejea
Kipengele cha ujumbe)
Migogoro, mwandishi amefanikiwa kuibua migogoro, kuonesha chanzo, upeo na
hata baadhi ya migogoro amefanikiwa kuitolea suluhisho. (rejea kipengele cha
Migogoro)
(b) Kutofaulu kwa mwandishi
Kutofaulu kwa mwandishi tunaangalia
mapungufu tunayokutana nayo katika kazi ya fasihi, hivyo basi, kama ilivyo
kawaida huwa hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro, hivyo hivyo katika tamthiliya
hii, tunakutana na baadhi ya kasoro ambazo si nyingi, baadhi ya kasoro hizo au
mapungufu ni pamoja na,
ü Mwandishi
ameshindwa kutuonesha mwanamke aliyemuambukiza Joti virusi vya UKIMWI.
ü Mwandishi
pia ameshindwa kutuonesha hatima ya akina Jumbe na Choggo kama nao waliathirika
na UKIMWI au la, maana hawa wote matendo yao alikuwa yanafanana tu na Joti.
ü Mwandishi
ameshindwa kutuambia alipo baba yake, kama amesafiri au amefariki.
ü Mwandishinpia
ameshindwa kuonesha umuhimu wa watu kujitokeza kupima afya zao, kwa mfano Suzi
anaoenesha kuwa na wasiwasi kama naye ameambukizwa au la, mwandishi alitakiwa
aoneshe Suzi anaamua kwenda kupima afya yake.
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa
sehemu hii
1. Ukitumia vitabu viwili vya tamthiliya, jadili jinsi waandishi wa
vitabu hivyo walivyofanikiwa kifani na kimaudhui.
·
No comments:
Post a Comment