Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Katika mada hii utajifunza juu ya mambo ya kuzingatia katika ufahamu wa kusoma na pia vilevile mambo ya kuzingatia katika ufahamu wa kusikiliza.
Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.
Ufahamu wa kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.
Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:
- Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
- Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
- Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.
Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:
- Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
- Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
- Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
- Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.
Ufahamu wa kusoma
Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma makala, kifungu cha habari, kitabu au gazeti.
Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:
- Uelewa wa msamiati na
- Uelewa wa matini
Ili kuilelewa habari/matini ni lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo. Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote hataeleweka.
Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
- Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
- Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
- Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
- Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.
Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma.
Kusoma kwa burudani
Huu ni usomaji ambao lengo lake kuu huwa ni kujiburudisha tu. Katika usomaji wa aina hii, msomaji hujisomea zaidi magazeti, majarida na vitabu tofauti na vile vinavyotumika darasani.
Wakati mwingine sio lazima msomaji awe na vitabu vyote ambavyo anahitaji kuvisoma au magazeti na majarida. Inapotokea hivyo, msomaji anaweza kwenda maktaba kuazima kitabu nachokihitaji.
Ingawa lengo la msomaji huwa ni kujiburudisha tu, lakini pia hujiongezea maarifa. Hii ni kwa sababu, magazeti, majarida na vitabu sambamba na kutuamia lugha sanifu huelezea mambo mabalimbali yanayoihusu jamii.
Hivyo msomaji kutokana na kusoma vitabu na majarida mbalimbali hujiongezea kiwango cha welewa wa lugha na mambo mengine ya kijamaii yanayojadiliwa humo.
ni jambo zuri kwa msomaji kujijengea tabia ya kujipima ili aweze kuelewa kiwango cha maarifa aliyopata katika kujisomea. Kujipima huku kunaweza kufanywa kwa kujiundia utaratibu w kuweka kumbukumbu ya vitu au makala zilizosomwa na kufanya ufupisho wa kila makala.
Utaratibu unaopendekezwa katika kujipima na kujiwekea kumbukumbu ya usomaji wa burudani ni kama ufuatao:
1. Tarehe...
2. Jina la kitabu/makala/gazeti....
3. Mchapishaji......
4. Mwaka/tarehe ya uchapishaji.....
5. Ufupisho wa habari(yasizidi maneno 20)
6. Fundisho/ujumbe mkuu ni.....
7. Jambo lililokuvutia sana......
8. Maoni kwa ujumla kama yapo....
Matumizi ya Kamusi
Maana ya kamusi
Kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa. Au kamusi ni orodha ya maneno yaliyo katika karatasi au nakala tepe yaliyopangwa kialfabeti na kutolewa maana pamoja na maelezo mengine na kuhifadhiwa katika kitabu, santuri, simu, tarakilishi au katika mfumo wowote wa kielekroniki.
Kamusi huweza kuwa ya lugha moja, yaani orodha ya maneno pamoja na maelezo yake yakiwa katika lugha moja.
Mfano: chatu, ni nyoka mkubwa na mnene
Kamusi nyingine huwa za lugha mbili yaani orodha ya maneno ipo katika lugha moja na maelezo ya maana ya maneno hayo yapo katika lugha nyingine.
Mfano: chatu, ni python
Kamusi ni hazina ya lugha inayohusika, kwani tofauti na vitabu vingine vya lugha, huwa na orodha ya maneno mbali mbali yanayotumiwa na wazungumzaji wa lugha ile pamoja na maana zake. Japokuwa wingi wa maneno hutegemea ukubwa wa kamusi, kitabu hiki kina manufaa makubwa kwa mtumiaji wake kwani humpatia msamiati asioufahamu pamoja na maana zake au humpatia maana zaidi ya maneno anayoyafahamu.
Taarifa zinazopatikana katika kamusi
Awali kamusi zilipoanza kutungwa zilikuwa ni orodha ya maneno magumu pamoja na maana zake. Kamusi za siku hizi huwa na taarifa zaidi ya maana. Miongoni mwa taarifa ambazo kamusi huwa nazo ni:
- tahajia za maneno mfano. Tasinifu Vs Tasnifu, Burangeti Vs Blanketi, Kula Vs Kura, -ingine vs -engine
- matamshi
- sarufi ya lugha kama inavyojitokeza katika kila neno kama vile maumbo ya wingi wa nomino, vinyamuo vya neno kama vile chezesha, chezeka, chezea, mchezo, mchezaji n.k ambavyo vinatokana na kitenzi cheza
- maana
- etimolojia ya neno (asili ya neno husika)
- matumizi ya neno
Jinsi ya kutumia kamusi
Maneno yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi a, yote huwekwa chini ya herufi A. Maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano hapa chini unavyoonyesha.
Mfano: ja, jabali, jabiri, jadhibika, jadi.
Maneno yote yanaanza na herufi [j]. herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. herufi ya tatu ni [b] na [d]. Kwa kuwa [b] hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti maneno yenye [b] kabla ya yale yenye [d]. Kwa kuwa maneno yenye herufi [b] ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya hya maneno ili tuchague litakaloorodheshwa mwanzo. Neno ‘jabali’ litaorodhewshwa kabla ya ‘jabiri’ kwa kuwa [a] (herufi ya nne) ya ‘jabali’ hutangulia [i] ya ‘jabiri’ ambayo pia ni herufi ya nne. Kisha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya ‘jadhibika’ na ‘jadi’. Kwa kuwa [h] hutangulia [i] basi ‘jadhibika’ huorodheshwa mwanzo ndipo lifuatiwe na ‘jadi’.
Kwa hiyo hivi ndivyo unavyopaswa kutafuta neno kwenye kamusi. Nenda kwenye herufi ya neno ulalotafuta alafu litafute kwa kufuata mlolongo huo huo wa herufi ya kwanza kuorodheshwa.
Neno linaloorodheshwa kwenye kamusi ili lifafanuliwe linaitwa kidahizo. Kidahizo huandikiwa maelezo ya kukifafanua. Maelezo haya ni matamshi ya kidahizo, maana ya kidahizo, kategoria ya kisarufi, sentensi ya mfano wa matumizi ya kidahizo n.k. Kidahizo pamoja na maelezo yake ndio huitwa kitomeo cha kamusi.
Mfano: Kitomeo cha kamusi
Dhabihu nm mahali pa kuchinjia wanyama
kidahizo kategoria ya neno maana ya neno.
Taarifa ziingizwazo katika kamusi
Maana za maneno
Kwa mfano: Dhabihu nm mahali pa kuchinjia wanyama.
Kategoria za maneno
Kategoria za maneno kama vile kielezi (ele), kitenzi (kt), kivumishi (kv), nomino (nm), kihisishi.
Mifano ya matumizi
Kwa mfano, Waiziraeli huwapeleka koondo wao kwenye dhabihu kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Lengo la kutoa mifano ni kumsaidia msomaji asiye fahamu vyema neno husika aelewe jinsi neno hilo linavyotumika.
Uingizaji wa nomino
Nomino nyingi katika lugha ya kiswaili zina maumbo ya umoja na wingi.
Mfano: dume nm ma-
mkopo nm mi-
Viambishi ambatishi huwekwa kando ya nomino kuashiria umbo la wingi la nomino.
Ngeli za nomino
Mfano: mkopo nm mi- [u-/i-]
Kutafuta maana unayoitaka
Neno linaweza kuwa na maana moja au zaidi ya moja. Maana inapokuwa moja mtumiaji kamusi hana tatizo kwani hiyo ndiyo atakayoipata na kuichukua. Lakini neno linapokuwa na maana zaidi ya moja, mtumiaji kamusi hutatizika asijue ni ipi aichague. Ili kupata maana inayosadifu itafaa mtumiaji kamusi kutafuta maana ambayo inahusiana na muktadha wa neno linalotafutwa.
Mfano: kifungo nm vi-
- kitu cha kufungia
- kitu kinachotumiwa kufungia vazi kama vile shati, gauni, suruali n.k
- adhabu ya mtu kuwekwa jela kwa muda fulani
iwapo mtumiaji aliona neno ‘kifungo’ kwa muktadha wa: “Juma alihukumiwa kifungo cha miaka kumi baada ya kupatikana na hatia ya kubaka….” Maana ya mukatadha huu itakuwa ni ile maana ya 3 kwa sababu ndiyo yenye kuhusiana na muktadha ambapo neno kifungo limetumika na wala sio maana ya 1 wala ya 2.