Mwenyezi Mungu anasema;
“Na kama mkiogopa kutowafanyia uadilifu mayatima (basi ogopeni vile vile kutowafanyia uadilifu wanawake). Basi oeni mnaowapeda katika wanawake (maadamu mtawafanyia insafu). Wawili au watatu au wane (tu). Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi (oeni) mmoja tu.”
Surat an Nisa - 3
Mwenye kuichunguza aya hii vizuri ataona kuwa Mwenyezi Mungu hapa hakutufaridhishia kuoa zaidi ya mke mmoja, isipokuwa ameruhusu (ametowa rukhsa) kufanya hivyo kwa mwenye uwezo wa kutimiza masharti yake, nikimaanisha kuwa katika lugha ya fiq-hi, kufaridhisha na kuruhusu ni mambo mawili tofauti.
Bila shaka anayekijuwa zaidi chombo chochote kile ni yule aliyekitengeneza chombo hicho, na bila shaka mwenye kumiliki kitu chochote kile, ndiye mwenye haki ya kukifanya vile anavyoona sawa.
Kwa vile Mwenyezi Mungu ndiye aliyetutengeneza (aliyetuumba), basi bila shaka Subhanahu wa Taala ndiye Mwenye kutujuwa zaidi kuliko mwengine, na kwa vile Yeye ndiye Mwenye kutumiliki, basi bila shaka Yeye ndiye Mwenye haki ya kutuwekea sheria yoyote ile anayoiona kuwa ndiyo sawa kwa ajili yetu, na bila shaka Mwenyezi Mungu hamdhulumu mja wake isipokuwa waja ndio wenye kudhulumu nafsi zao.
Makala yafuatayo nimeyafasiri kutoka katika kitabu kiitwacho; ‘Nahwa thaqaafa Islamiyah Asiylah’, kilichoandikwa na mwanachuoni maarufu Dr. Omar Suleiman Al Ashqar:
Katika kitabu chake hicho Dr. Al Ashqar anasema;
“Maadui wa Uislamu wanadai kuwa kuoa mke zaidi ya mmoja ni dhulma kwa wanawake na kwamba si jambo la haki na kwamba rukhsa hii ya kuowa zaidi ya mke mmoja ni dharau kwa kinamama na kwamba wanaume wanapewa haki zaidi ambazo kina mama nao hawapewi haki hizo na kwamba rukhsa hii ni sababu kubwa ya kutengana kwa familia nk.
Kwanza - Ningependa kuwajulisha ndugu zangu kuwa jambo hili limewekewa sheria na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala katika kitabu chake na kwamba Mtume (SAW) ametenda hivyo, yeye na Sahaba zake (RA) halikadhalika, na kwamba umma wote umekubaliana juu ya usahihi wake, na Muislamu lazima aitakidi kuwa sheria za Mwenyezi Mungu amezileta kwa maslahi ya viumbe vyake, na kwamba hapana sheria nyingine yoyote ile inayoweza kuwafaa wanadamu kuliko sheria waliyowekewa na Mola wao Subhanahau wa Taala na kwamba sheria yoyote ile inayokwenda kinyume na sheria ya Mwenyezi Mungu ni batil na yenye kupotosha.
Pili - Kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo la dharura katika jamii na hii ni kwa sababu takwimu zote zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake ni kubwa zaidi kuliko idadi ya wanaume, na kwa ajili hiyo kukataza kuoa mke zaidi ya mmoja kutaifanya idadi kubwa ya wanawake kukaa bila kuolewa, jambo litakaloifanya idadi hiyo kubwa ya wanawake hao kusukumwa katika ulimwengu wa zina na kufanya yale yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, na kutokana na hayo mwanamke atageuka kuwa ni chombo cha kuchezewa mikononi mwa wanaume na kugeuka kuwa mwenye kumstarehesha kila mwenye uwezo wa kumlipa, na ataishi bila ya kupata haki anazopata mke.
Kisha itakuwaje hali ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa?
Bila shaka baba zao hawatawatambua wala kuwakubali na watageuka kuwa mizigo kwa mama zao.
Mwanamke ataweza kuepukana na mtoto wa aina hiyo kwa njia ya kutoa mimba, au baada ya kumzaa kwa njia ya kumweka mtoto mahali popote ili aokotwe na mtu yeyote yule, au kwa njia ya kumwacha katika sehemu za kulea mayatima mahali atakapokosa ulezi wa kibinadamu na kukosa mapenzi ya mama na malezi ya baba na kwa ajili hiyo mtoto huyo hatokuwa na raha katika nafsi yake.
Takwimu zinazotolewa na nchi zinazokataza mtu kuowa zaidi ya mke mmoja zinastusha sana. Katika mwaka 1901 ulifanywa mkutano kwa ajili ya kuzungumzia tatizo la watoto wachanga wanaotupwa, na pia juu ya mimba zinazotolewa na juu ya sababu za kuongezeka kwa tatizo hilo, na takwimu iliyotolewa juu ya mji mmoja tu katika miji ya Kifaransa nchi ambayo watoto wanalelewa kwa msaada wa serikali, basi idadi ya watoto hao wanaotupwa ilifikia idadi ya elfu hamsini.
Na katika ripoti ya Umoja wa mataifa iliyotolewa katika mwaka 1959 imeeleza kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa katika ulimwengu imefikia sitini katika mia 60%, na katika dola nyingine mfano nchi ya Panama, idadi hiyo imepindukia sabini na tano katika mia 75%.
Hii ndiyo athari ya kukataza watu kuowa zaidi ya mke mmoja. Si ingekuwa bora kwa mwanamke kuolewa akawa mke wa pili au wa tatu na akawa ana mahali pake katika jamii, na watoto wake wakawa na nasaba yao na wakaweza kujinasibisha na kulelewa na baba yao bila upendeleo baina ya ndugu zao?
Bila shaka katika kuruhusu kuowa zaidi ya mke mmoja mna faida kubwa kwa wanawake, ama katika kuharimisha jambo hili, ndani yake mna hasara kubwa.
Tatu - Ukiuchunguza uwezo wa kupata mtoto, utaona kuwa mwanamke anapofikia umri wa miaka hamsini au hata kabla ya hapo, uwezo wake wa kuzaa unasimama. Amma mwanamume anaendelea kuwa na uwezo wa kuzaa hata kama ataishi miaka mia.
Mwanamke hujiwa na damu ya hedhi kila mwezi kwa muda unaofikia siku saba mara nyingine, na uwezo wake wa kuingiliana na mumewe unapungua sana pale anapopata mimba kwa muda wote wa miezi tisa, kisha huzaa na hatimaye huwa katika nifasi kwa muda unaofikia siku arubaini, na bila shaka ni haramu kwa mwanamume kumsogelea mwenye hedhi au mwenye nifasi.
Ukizihesabu siku ambazo mwanamke hawi na uwezo wa kukutana na mumewe, utaona kuwa ni siku nyingi sana zinazofikia theluthi nzima ya umri wake, wakati mwanamume hafikiwa na yote haya.
Kuwakataza wanaume kuowa zaidi ya mke mmoja ni kuwadhulumu wanaume hao, kwa sababu mwanamume kimaumbile hakumbani na yale anayokumbana nayo mwanamke, na pia kwa sababu yeye anakuwa na uwezo na nguvu za kupata mtoto wakati mwanamke anapokuwa hana uwezo huo, na kwa ajili hiyo unapomkataza kuoa zaidi ya mke mmoja unaunyima umma wa Kiislamu kupata ongezeko la watu.
Nne – Wakati mwengine mwanamke hupata maradhi ya kuondokewa na hamu ya kuingiliana na mwanamume, lakini wakati huo huo mume na mke hupendelea kuendelea na uhusiano wao wa mtu na mkewe na kuendelea kuyahifadhi mapenzi na huruma iliyopo baina yao. Ikiwa itawekwa sheria ya kukataza kuowa mke zaidi ya mmoja, basi mwanamume atajikuta amelazimika kumtaliki mke huyo ili aruhusiwe kuowa mke mwingine.
Tano – Kuowa zaidi ya mke mmoja ni nidhamu iliyokuwepo tokea hapo zamani, kwani katika Taurati imeandikwa kuwa Nabii Ibrahim na Nabii Yaakubu na Nabii Suleiman na Nabii Daud , wote hawa waliowa zaidi ya mke mmoja, na katika Injili hakuna mahali palipokataza ukewenza, bali sheria zilizotangulia juu ya kuowa mke zaidi ya mmoja hazikuwa zimefungwa na masharti yoyote, lakini Qurani ikaja na msimamo wa kati na kati, ikaruhusu kuowa, lakini wakati huo huo ikaweka idadi maalum na masharti maalum.
DHULMA KWA WANAWAKE?
Miongoni mwa wanawake wapo ambao hawakubali waume zao kuwaolea juu yao wake wengine, na jambo hili linasababisha matatizo mengi na hitilafu nyingi.
Sisi hatukatai kuwa jambo hili linaweza kuleta matatizo na hitilafu, lakini maslahi yanayopatikana ndani yake ni makubwa sana kuliko madhara yake, bali madhara hayo hayafikii hata asilimia moja katika elfu (moja juu ya elfu) ya faida inayopatikana ndani yake. Isitoshe Uislamu haukuyapuuza matatizo yanayoweza kupatikana, na kwa ajili hiyo hakubaliwi mtu kuowa mke mwingine ikiwa hana uwezo wa kuwasimamia wake zake hao, kisha mwanamume akaamrishwa kuwa muadilifu baina ya wake zake katika makazi na chakula na mavazi na pia ukamuamrisha mwanamume awe muadilifu baina ya watoto wake, kwani haijuzu kwa mwanamume kuwabaguwa wanawe kwa hali yoyote ile. Yote haya kwa ajili ya kuzuwia mtafaruku wowote ule unaoweza kupatikana katika kuowa mke zaidi ya mmoja.
KWA NINI MWANAMKE NAYE HARUHUSIWI KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA?
Kwa mwanamke kuolewa na mume zaidi ya mmoja ni jambo lililoharimishwa kisheria, ni jambo ovu ki khulqa hata kwa kulifikiria tu, kwani mwanamke ni mahali pa uzazi, na ikiwa atakuwa na waume wengi, basi maji ya uzazi yatachanganyika na nasaba zitapotea.
Mwanamume anaweza kuwa na wake wengi na akawa na uhakika kuwa watoto wote ni wake, lakini kwa upande wa mwanamke jambo hilo haliwezekani.
Kisha mwanamume ndiye mwenye kumsimamia mwanamke, sasa ikiwa mwanamke mmoja atakuwa na waume wengi, atamtii yupi kati ya waume wote hao?
Isitoshe wanawake wengi hawana uwezo wa kutimiza mahitajio ya mwanamume mmoja tu. Vipi basi atakuwa na uwezo wa kutimiza mahitajio ya wanaume wengi?”
Mwisho wa maneno ya Sheikh Al Ashqar
Wallahu taala aalam
Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
No comments:
Post a Comment