Sunday, February 1, 2015

Aqiyqah Afanyiwayo Mtoto Mchanga

1.    ‘Aqiyqah ni jina lililopewa kichinjwa (mnyama) achinjiwacho mtoto mchanga aliyezaliwa ni mamoja awe ni wa kike au wa kiume.
2.    Ni Sunnah si waajibu. Ushahidi wa hili ni uko katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: "Atakayepata mtoto na akapenda amchinjie basi na afanye hivyo; kwa mwanamume mbuzi wawili na kwa mwanamke mbuzi mmoja". Hadiyth hii imepokewa na Maimaam Abuu Daawuud na An-Nasaaiy kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “na akapenda amchinjie” ni dalili kuwa ‘Aqiyqah si lazima bali ni jambo linalopendeza Muislamu kulifanya. Lakini kwa mwenye uwezo wa kufanya hivyo basi iliyo bora zaidi kwake ni kufanya ama yule asiye na uwezo wa kufanya hivyo, basi si lazima kwake  maana Mwenyeezi Mungu Haikalifishi nafsi yoyote ila yale yaliyo sawa na uwezo wake na pia Hakufanya uzito katika dini.
3.    Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yeye kasema: “Kila mtoto azaliwaye anafungamana na ‘Aqiyqah yake, anachinjiwa siku ya saba, ananyolewa kichwa chake na anapewa jina.” Wanachuoni wamelizungumzia neno ‘kufungamana’ hapa kuwa linaweza kuwa linamaanisha mambo mengi, miongoni mwa mambo hayo ni:
  1. Anakuwa kama mwenye kujisikia uzito na unyonge na mwenye kukosa wepesi na furaha maishani hadi achinjiwe
  2. Ni deni lililo mithili ya Rehani ambayo hulazimiana na mtu hadi alilipe.
4.    Iliyo bora zaidi na timilifu ni kuwa wale mbuzi wawili au kondoo wawili ambao anatakiwa mtoto wa kiume achinjiwe wanatakiwa wawe ni wenye kufanana au kukaribiana kufanana kimaumbile na kiumri. Lakini kama itashindikana kuwapata mbuzi wawili wenye sifa kama hizo itafaa hata kama watatofautiana kiumbile na kiumri maadamu tu wana sifa zinazofaa kisheria kwa ajili ya ibada hii. Sifa hizo tutazitaja baadaye.
5.    Iliyo bora zaidi na timilifu ni kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi wawili lakini ikiwa mtu atashindwa kabisa kuchinja mbuzi kama kutokana na yeye kupata mbuzi mmoja tu au kumiliki kiwango cha mbuzi mmoja tu basi huyo huyo mbuzi mmoja atatosha.
6.    Sunnah ni kumchinjia mtoto atakapofikisha siku ya saba kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Samrah, lakini ikiwa mtu hakuweza kuchinja siku ya saba basi na afanye hivyo siku yoyote atakayojaaliwa.
7.    Nywele za mtoto mchanga anazonyolewa siku ya 'Aqiyqah' hupimwa uzito kwa sonara. Uzito huo huchukuliwa ili kulinganisha thamani ya fedha yenye uzito kama huo kwa wakati huo, kisha pesa hizo hutolewa sadaqa.
8.    Ibada hii ya kuchinja hufanyika hata kama mtoto kafariki maadamu tu alizaliwa hai au hata kama mimba ilitoka lakini mtoto tayari alikuwa ameviviwa roho, yaani alikuwa amefikisha miezi minne au siku mia na ishirini na kuendelea lakini kama alikuwa hajafikisha miezi minne au siku mia na ishirini hapo hatofanyiwa ‘Aqiyqah.
9.    Kuna imani imeenea kwa watu wengi kuwa kichinjwa cha ‘Aqiyqah hakivunjwi mifupa hii ikiwa kama ishara ya kumtakia mtoto salama na asivunjike maishani mwake. Hili si sahihi wala halina mashiko katika Qur-aan wala Sunnah. Kwa hiyo ieleweke wazi kuwa mifupa ya ‘Aqiyqah inafaa kuvunjwa wala hii haitokuwa sababu ya kuvunjika kwa mtoto hata kama itatokea kama watu wanavyoamini. Vile vile kuna jambo jingine nalo ni kuwa nyama ya ‘Aqiyqah huchanganywa au hupikwa kwa maji yaliyotiwa vitu vitamu vitamu kama sukari au huchanganywa na asali wakati wa kuliwa, hii ikiwa ni kama ishara ya kumtakia mtoto tabia njema; hili nalo pia halina mashiko. Hivyo iwekwe chumvi na kupikwa kama nyama ya kawaida
10.           Kinachotakiwa kuchinjwa katika ‘Aqiyqah katika wanyama ambao kishari’ah wanaitwa Bahiymatul An’aam ambao ni; mbuzi, kondoo, ng’ombe na ngamia. Kwa mantiki hii haifai kumchinja farasi kwa ajili hii, wala swala hata kama anafugwa na amekuwa kama mbuzi kitabia na pia haifai kuchinja kuku wala bata kwa ajili ya ibada hii
11.           Ama kuhusiana na umri unaofaa wa kichinjwa ni miaka mitano kwa ngamia na miaka miwili kwa ng’ombe, dume la mbuzi na dume la kondoo ni mwaka mmoja na mbuzi jike na kondoo jike ni miezi sita
12.           Ni sharti katika kichinjwa cha ‘Aqiyqah kiwe kimesalimika na aibu mbalimbali kwa kifupi kabisa kichinjwa hichi kinafanana na kichinjwa cha ‘Iydul Adhwhaa au Idi kubwa yaani kisiwe na chongo cha wazi, kiguru cha wazi, kilichokonda sana, wala kisiwe ambacho kimetobolewa masikio yake wala kisiwe kilichokatwa mkia au kukatika pembe.
13.           Ikiwa mtu anamiliki takribani wanyama wote wanaofaa kuchinja kwa ajili ya ‘Aqiyqah kiasi kuwa anaweza akitaka akachinja ng’ombe au ngamia au kondoo au mbuzi, iliyo bora zaidi ni kuchinja mbuzi maana ndiye aliyetajwa katika Hadiyth.
14.            Inafaa mtu kuipika nyama ya ‘Aqiyqah au kuigawa pasina kuipika lakini iliyo bora zaidi ni kuipika nyama ya ‘Aqiyqah kuliko kuigawa kwa kuwa kwa kufanya hivyo utawarahisishia masikini na majirani gharama za kupika.
15.           Hakuna ubaya wowote katika kula nyama ya ‘Aqiyqah kwa aliyechinja, kwani kwa hakika hii ni nyama kwa ajili ya kumshukuru Allaah na kile ambacho ni kwa ajili ya kumshukuru Allaah kinafaa kuliwa kishari’ah wala hapana ubaya bali hii ni kama nyama ya ‘Iydul Adhwhaa.
16.           Pia inafaa kuiweka nyama ya ‘Aqiyqah katika jokofu pasina kuigawa lakini iliyo bora zaidi na timilifu katika ibada hii ni kuigawa kwa mafaqiri na marafiki hata kama ni kidogo.
17.           Haifai kununua mbuzi aliyechinjwa na kumfanya kuwa ni ‘Aqiyqah bali ni lazima kumununua mbuzi mzima na kisha kumchinja kwa nia ya ‘Aqiyqah
18.           Ikiwa baba hayuko, kama kwa mfano kafariki, mama atasimamia jukumu la kufanya ‘Aqiyqah.
19.           ‘Aqiyqah ni Sunnah kwa baba kumfanyia mtoto wake lakini mtoto hakufanyiwa ‘Aqiyqah na akapenda ajifanyie mwenyewe inafaa hata kama ni ni kitambo kirefu kimepita na umri ukawa mkubwa.
20.           Inafaa kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi hao wawili kwa utaratibu wa kugawa kwa maana ya kuwa anamchinja mbuzi mmoja mwezi huu na mwengine akamchinja mwezi mwingine wala haishurutishwi wachinjwe mara moja, bali inafaa kwa mtoto akajichinjia mbuzi mwingine ikiwa baba alimchinjia mbuzi mmoja kwa sababu ya hali yake kifedha. Bali inafaa kumchinjia mbuzi mmoja sehemu moja na mwengine sehemu nyingine wala si sharti wachinjwe wote sehemu moja wala si sharti wachinjwe sehemu alipo mtoto anayefanyiwa.
21.           Haifai kisheria kupigia thamani ya mbuzi wa ‘Aqiyqah na kuwapa kiwango hicho masikini bali ni lazima achinjwe mbuzi
22.           Haifai kushirikiana watoto katika ‘Aqiyqah kwa mantiki ya kuwa wachangie kwa mfano mbuzi wawili watoto wawili wa kiume. Watoto wawili wa kiume wanapaswa wachinjiwe mbuzi wanne hata kama ni mapacha. Kama ni mapacha wawili wa kike watachinjiwa mbuzi wawili, kama mmoja ni wa kike na mwengine ni wa kiume watachinjiwa mbuzi watatu. Bali ngamia na ukubwa wake hafai kuwachinjia watoto wawili na ikifanyika hivyo inazingatiwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja. Bali haitofaa kwa watoto wawili ambao hawakufanyiwa ‘Aqiyqah kwa wao kujiamulia kuchinja ngamia mmoja ili awe ni ‘Aqiyqah kwa wote wawili. Bali ngamia huyo atazingatiwa kuwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja tu.
23.           Si lazima wakati wa kumchinja mnyama wa ‘Aqiyqah kusema kuwa hii ni ‘Aqiyqah bali inatosha mtu kunuia moyoni mwake na kilicho lazima kutamka ni BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym.
24.           Si lazima kuwaambia waliohudhuria kuwa watakula nyama ya ‘Aqiyqah, lakini ni vizuri kuwaambia ili wamuombee mtoto du’aa njema, uongofu, uchaji, kutengenekewa na kheri za dunia na Akhera.
‘Aqiyqah ni mnyama ambaye huchinjwa kwa ajili ya mtoto mdogo kama tulivyotangulia kusema. Jambo hili ni katika mlango wa kumshukuru Allaah. Kuna pia vyakula vingine ambavyo ni katika mlango huu wa kumshukuru Allaah na vinafaa kuliwa kishari’ah navyo ni:
a.     Waliymah: chakula au karamu ya harusi.
b.     Qiraa: chakula cha mgeni, kile cha mgeni njoo wenyeji tupone!
c.      Ma-adabah: ambacho ni chakula cha mwaliko.
d.     Tuhfah: ambacho ni chakula cha mwenye kutembelea pahala.
e.     Khiraasu: ambacho ni chakula cha kujifungua.
f.       Ghadiyrah: ambacho ni chakula cha wakati wa khitaani au kutahiri wanawake au wanaume
g.     Naqiy’ah: ambacho ni chakula cha anayekuja kutoka safari.
h.     Wakiyrah: ambacho ni chakula baada ya kumaliza kujenga.

Isipokuwa chakula cha msibani au cha siku ya tatu au cha Khitmah au arobaini. Vyakula nilivyotaja hapo juu vinafaa kuliwa Kishari’ah. Jariyr bin ‘Abdillaah anasema kuwa kukusanyika kwa wafiwa na kupikiwa chakula ni miongoni mwa mambo aliyokataza Mtume wetu Mtukufu.

No comments:

Post a Comment