Sunday, February 22, 2015

Mapitio na tafsiri ya sera mpya ya elimu na mafunzo Tanzania

FEBRUARI 13, 2015, Rais Jakaya Kikwete alizindua rasmi sera mpya ya elimu na mafunzo nchini. Hii ni baada ya takribani miaka 10 ya vuta nikuvute, kati ya wadau wa elimu na serikali juu ya maudhui ya sera mpya. Katika makala hii ninafanya mapitio ya sera hii mpya na kuainisha maeneo makubwa manne yaliyobadilika na ambayo utekelezaji wake utaathiri na kubadilisha mfumo wetu wa elimu. Aidha, katika hitimisho ninatoa angalizo juu ya tafsiri pana ya sera mpya ya elimu. Wigo wa sera na umuhimu wa wizara Badiliko la kwanza kabisa katika sera mpya ni wigo wa sera yenyewe. Wakati sera ya zamani, ambayo imedumu kwa takribani miaka 20 tangu ilipotungwa mwaka 1995, haikujumuisha elimu ya juu na elimu ya mafunzo ya ufundi, sera mpya ina wigo mpana kwa maana kwamba inajumuisha sekta zote za elimu, ikiwemo elimu ya juu. Hata hivyo, wakati mtunzi wa sera hii mpya ni Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi, utekelezaji wake kwa upande wa elimu ya msingi na sekondari umewekwa mikononi mwa wizara inayohusika na tawala za mikoa na serikali za mitaa. Ndiyo kusema, kiutekelezaji, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi sasa inabaki na jukumu la menejimenti ya elimu ya juu, pamoja na kwamba huko nako wizara hii haina kazi ya maana kwa sababu taasisi za elimu ya juu zina mifumo ya kiutawala inayovifanya vijitegemee. Hii inamaanisha kwamba, kwa sera hii, watunga sera na watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wasipokuwa wabunifu watajikuta hawana kazi za maana za kufanya na wizara hiyo itakosa umuhimu. Mfumo mpya wa elimu Kwa mujibu wa sera mpya ya elimu, mfumo wa elimu na mafunzo utabadilika kutoka 2-7-4-2-3+ kwenda 1(2)-10-2-3+. Hii inamaanisha kuwa watoto watasoma shule ya awali kwa mwaka mmoja au miwili kuanzia wakiwa na umri wa miaka mitatu badala ya kuanza na miaka mitano kama ilivyo sasa. Baada ya kumaliza elimu ya awali, ambayo sasa nayo ni ya lazima, watoto wanatarajiwa kuanza shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka sita na watasoma elimu hiyo kwa miaka sita na kuunganisha na elimu ya sekondari kwa miaka mingine minne. Kwa hiyo, wigo wa elimu ya msingi umepanuka na sasa utajumuisha miaka minne ya elimu ya sekondari. Kwa hiyo elimu ya msingi sasa itakuwa miaka 10 (miaka sita ya elimu ya msingi na miaka minne ya elimu ya sekondari) na kwa pamoja sasa itaitwa Elimu Msingi, ambayo itakuwa hailipiwi ada. Sera mpya italazimisha mabadiliko katika mitaala Sera imetoa maelekezo mengi ambayo utekelezaji wake utalazimisha mitaala ifanyiwe mapitio na mabadiliko makubwa. Kwa mfano, tamko namba 3.2.5 limeweka mkazo katika kumuwezesha mwanafunzi kupata umahiri katika maeneo ya mawasiliano, kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na sayansi na teknolojia katika elimu ya msingi. Ili kutekeleza agizo hili la kisera, italazimika kupitia mitaala upya ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanazingatiwa vya kutosha. Kwa sasa mtaala wa elimu ya awali na msingi umejaa masomo mengi jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau wa elimu kwa muda mrefu. Sera mpya inatoa fursa ya kurekebisha kasoro hii. Badiliko jingine kubwa ambalo ni muhimu kimitaala ni pale ambapo sera mpya imetoa maelekezo ya kuwepo kwa kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo na kwakila mwanafunzi. Sera pia imetoa maelekezo ya kufundishwa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafundishwi kabla. Kwa mfano, sera mpya inaelekeza kufundishwa kwa masomo yanayohusu amani na namna ya kutatua migogoro. Maeneo mengine ni pamoja na mazingira, ujinsia na ukimwi. Eneo lingine muhimu litakalohitaji mapitio ya mitaala ni tamko linaloagiza utambuzi wa matumizi ya lugha ya alama, ambalo ni eneo jipya kabisa katika elimu ya Tanzania. Mkanganyiko wa lugha ya kufundishia, kujifunzia Kwa muda mrefu tangu nchi yetu ipate Uhuru mwaka 1961, pamekuwa na mjadala mpana juu ya lugha inayofaa kufundishia na kujifunzia. Mjadala huu umepamba moto zaidi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na baadhi ya watu wanaounga mkono matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia na kujifunzia kuhusisha kufeli kwa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne na kushindwa kumudu ya Kiingereza, ambayo ndiyo lugha inayotumika kufundishia na kujifunzia kuanzia elimu ya sekondari hadi elimu ya juu. Wadau hawa walitarajia kwamba sera mpya ingetamka waziwazi kwamba lugha ya kufundishia na kujifunzia itakuwa Kiswahili na Kiingereza kingefundishwa kama somo tu. Hata hivyo, sera mpya ya elimu imetambua lugha zote mbili za Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia na kujifunzia. Katika ukurasa wa 38, sera imetamka kwamba “..kuna umuhimu wa kuimarisha matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa kuzifanya kuwa lugha za kufundishia katika ngazi mbalimbali”. Katika Tamko Namba 3.2.19, sera inatamka kuwa “Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo….”. Hapo hapo katika Tamko Namba 3.2.20 sera inatamka kuwa “Serikali itaendelea na utaratibu wa kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kufundishia na kujifunzia, katika ngazi zote za elimu na mafunzo”. Kwa hali ilivyo katika sera hii, ni wazi kwamba mjadala kuhusu lugha inayofaa kufundishia na kujifunzia utaendelea. Kwa vyovyote vile, haitarajiwi kwamba maelekezo ya kisera kuhusu lugha ya kufundishia na kujifunzia yatatekelezwa mapema katika miaka ya hivi karibuni. Katika kipindi hiki cha mpito, pengine itakuwa ni jambo jema kwa serikali na wadau wa elimu kutafakari kwa makini juu ya uamuzi sahihi wa kuchukua katika jambo hili. Muhimu ni kwamba uamuzi ufanyike kwa mujibu wa sababu za kitaaluma na sayansi badala usahihi wa kisiasa na mapenzi ya kitamaduni. Mambo mawili katika hitimisho Katika kuhitimisha ningependa tuzingatie mambo mawili muhimu katika utekelezaji wa sera mpya. Mosi, sera mpya ya elimu ni mpya kwa maana kwamba imekuja na maelekezo ambayo yakitekelezwa yatabadilisha muundo wetu wa elimu. Hata hivyo, utekelezaji wa sera hii utahitaji uwekezaji wa kutosha kirasilimali. Bahati mbaya sera hii imekuja kipindi ambacho Rais Kikwete anamaliza muda wake. Katika mazingira ya siasa zetu, utekelezaji kamili wa sera hii utategemea na utashi na vipaumbele vya Rais ajaye. Pili, sera haijajengwa katika msingi wa kifalsafa. Kwa sababu hii tusitarajie mabadiliko makubwa ya maana katika fikra, mitazamo na uwezo wa watu watakaopita katika mfumo wa elimu utakaotokana na sera hii tofauti na hali ilivyo sasa. Hata hivyo, kukosekana kwa dira ya kifalsafa katika sera ya elimu sio tatizo la sera yenyewe kwa sababu falsafa ya elimu hujengwa katika falsafa pana ya nchi, na kwa kweli falsafa ya elimu ni zana tu ya kutekeleza falsafa ya taifa. Ndiyo maana elimu ya kujitegemea ilikuwa falsafa ya kutekeleza falsafa ya ujamaa na kujitegemea. Katika mazingira ambayo nchi haina falsafa ya kueleweka inayoongoza harakati za maendeleo tusitarajie pawepo na falsafa ya elimu. Ndiyo kusema kama ambavyo tunahesabu maendeleo yetu kwa kuangalia vitu ambavyo tumefanikiwa kujenga kama vile barabara na majengo badala ya aina ya maisha ambayo watu wanaishi, hivyo hivyo, bila falsafa ya elimu, tutaendelea kutoa wahitimu ambao wapo ‘busy’ kujitafutia riziki na ambao hawana habari na mustakabali wa jamii wanamotoka na taifa kwa ujumla. Pamoja na maangalizo haya, bado sera mpya ni bora kuliko ya zamani na utekelezaji wake kamili unaweza kutupeleka hatua moja mbele katika maendeleo ya elimu nchini. 
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/mapitio-na-tafsiri-ya-sera-mpya-ya-elimu-na-mafunzo-tanzania#sthash.XHUxeb82.dpuf

No comments:

Post a Comment