Sala ni ibada iliyo katika daraja ya juu kupita ibada zote katika dini ya Kiislam na ni nguzo muhimu sana kupita nguzo zote za dini, na ni ibada ya pekee ambayo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala amemfaradhishia mja wake Muhammad (SAW) kwa kuzungumza naye moja kwa moja usiku ule wa Miraji alipomnyanyua na kumfikisha juu ya mbingu ya saba, kisha akamsogeza mpaka penye Sidratul Muntaha na huko akamfaridhishia ibada hii ya Sala bila ya kumtumia malaika Wake Jibril (AS) kama alivyofanya katika kuzifaridhisha ibada nyingine.
Sala ni jambo la mwanzo atakaloulizwa mja na Mola wake siku ya kiama, na ikiwa ameitimiza sawa kama alivyoamrishwa basi mambo yote yaliyobaki yatakuwa sawa.
Mtume (SAW) amesema;
“Cha mwanzo atakachoulizwa mja siku ya Kiama ni Sala, ikiwa ameitimiza basi yote yaliyobaki yatatimia, la kama ikiharibika basi yaliyobaki yataharibika”.
Attabarani – Attirmidhiy – Annasai na wengineo.
NGUZO YA DINI
Sala ni nguzo ya mwanzo katika dini baada ya kuzitamka shahada mbili.
Kutoka kwa Abdillahi bin Omar (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Uislam umejengeka juu ya nguzo tano. Shahada ya La ilaaha illa Llah, Muhammadun Rasulu Llah, kusimamisha Sala na Kutoa Zaka na Kufunga mwezi wa Ramadhani na Kuhiji Makka kwa mwenye uwezo wa kufika huko.”
Na akasema (SAW)
“Kichwa cha jambo ni Uislam, na nguzo yake ni Sala na kilele chake ni Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu”.
Kwa vile nyumba haiwezi kusimama bila ya nguzo, basi asiyesali anahesabiwa kuwa ni mbomoaji wa nyumba hiyo na si mwenye kuijenga na makaazi yake ni Motoni.
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala akituelezea juu ya sababu zitakazowaingiza watu Motoni alisema;
“Isipokuwa watu wa kuliani (watu wa kheri).
(Hao watakuwa) katika Mabustani,
Wawe wanaulizana.
Juu ya watu wabaya (wawaambie).
‘Ni kipi kilichokupelekeni Motoni?’
Waseme;
‘Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali…”
Al Mudathir - 39-43
USIA WA MTUME (SAW) KWA UMMA WAKE
Kwa ajili ya umuhimu wake, Mtume (SAW) aliendelea kuwausia umma wake juu ya Sala mpaka pale alipokuwa akipumua pumzi zake za mwisho.
Imepokelewa kuwa Mtume (SAW) alipokuwa akipumua pumzi zake za mwisho kabla ya kufariki dunia alikuwa akiusia kwa kusema;
“Salaa Salaa na mliowamiliki kwa mikono yenu ya kulia”.
Na imepokelewa pia kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Yatakuja kuachwa maamrisho ya kiislamu moja baada ya jingine. Kila ikitoweka amri moja, watu wataing’ang’ania inayofuatia. La mwanzo kuachwa itakuwa hukmu (ya Mwenyezi Mungu) na la mwisho ni Sala”.
Ibni Haban.
Katika hadithi hii Mtume (SAW) anatutabiria juu ya wakati wetu huu ambapo hukumu ya Mwenyezi Mungu ishapigwa vita na kuachwa, na kwamba ibada nyingine nazo pia zitapigwa vita moja baada ya nyingine mpaka mwisho haitobaki isipokuwa ibada ya Sala ambayo nayo pia itapigwa vita na kuachwa.
SALA NDANI YA QURANI
Anasema Sh. Sayed Sabeq katika Fiqhil Sunnah;
“Atakayefuatilia aya za Qurani atagundua kuwa Mwenyezi Mungu mara nyingi anaitaja ibada ya Sala kwa kuipambanisha na ibada mbali mbali. Kwa mfano;
Ameipambanisha Sala na Dhikri (kumbusho) aliposema;
“Bila shaka Sala (ikisaliwa vilivyo) humzuiliya (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na maouvu, na kwa yakini kumbusho la Mwenyezi Mungu (lililomo ndani ya Sala) ni jambo kubwa kabisa (la kumzuwilia mtu na mabaya)”.
Al Ankabuut – 45
Na akasema;
“Hakika amekwishafaulu aliyejitakasa (na mabaya). Akakumbuka jina la Mola wake na akasali”.
Al Alaa –
Na akasema;
“Basi niabudu na usimamishe Sala kwa kunitaja”.
Ta Ha- 14
Ameipambanisha na Zaka;
“Na shikeni Sala na toeni Zaka”
Al Baqarah – 110
Akaitaja pamoja na Subira;
“Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali”.
Al Baqarah-45
Mwenyezi Mungu pia ameitaja pamoja na ibada ya kuchinja;
“Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi”.
Kauthar – 2
Na akasema;
“Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu”.
Al An am – 162-163
Mtu hata atende mema ya namna gani, lakini akiwa hasali, au anaposali hamnyenyekei Mola wake, basi matendo yake yote hayo yanapotea bure na anakuwa miongoni mwa waliokula hasara.
Mwenyezi Mungu anasema;
“HAKIKA wamefanikiwa Waumini, Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
Na ambao wanatoa Zaka,
Na ambao wanazilinda tupu zao,
Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.
Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
Na ambao Sala zao wanazihifadhi.
Hao ndio warithi,
Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo milele.
Al Muuminun – 1-11
Atakayezingatia vizuri mfumo wa aya hizi ataona kuwa Mwenyezi Mungu ameitaja Sala mara mbili. Mara ya mwanzo kwa ajili ya kutufahamisha umuhimu wake na unyenyekevu unaotakiwa ndani yake, na mara ya pili kwa ajili ya kututaka tuihifadhi (tusiiache) pamoja na kutujulisha kuwa ni watu wa aina hiyo tu ndio watakaoirithi Pepo ya Firdausi.
POPOTE ULIPO LAZIMA USALI
Sala ni ibada ya pekee ambayo mja analazimika kuitimiza anapokuwa katika mazingira ya aina yoyote. Anapokuwa safarini, wakati wa hofu, anapokuwa mgonjwa na hata anapokuwa vitani.
Mwenyezi Mungu anasema;
“Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo kuwa hamyajui”.
Al Baqarah – 238-239
Na akasema
“Na unapo kuwa pamoja nao (vitani), ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni SALA kama dasturi. Kwani hakika SALA kwa Waumini ni FARADHI iliyo wekewa nyakati maalumu”.
Annisaa – 102-103
Mwenyezi Mungu amewakemea sana wale wanaojaribu kuipuuza ibada hii tukufu na kufuata matamanio ya nafsi zao.
Mwenyezi Mungu akasema;
“Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha SALA, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kupata malipo ya ubaya”.
Maryam – 59
Na akasema
“Basi, ole wao wanao sali,
Ambao wanapuuza Sala zao”.
Maaun – 4-5
Kutokana na umuhimu wa ibada hii, Nabii Ibrahim (AS) alimuomba Mola wake amjaalie yeye na vizazi vyake wawe wenye kuishika.
Mwenyezi Mungu anasema juu ya Dua ya Nabii Ibrahim;
“Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu”.
Ibrahim – 40
Katika aya nyingine Mwenyezi Mungu amesema;
“Lakini wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoka Zaka basi iacheni njia yao (waacheni huru), hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu”.
Suratut Tawba – 5
Na maana yake ni asiytubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa kutoa Zaka asiachwe huru.
Na katika Sura hiyo hiyo ya Attawba aya ya 11 Mwenyezi Mungu anasema;
“Kama wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini”.
Na kinyume chake ni kuwa; Yule asiyetubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa kutoka Zaka, basi huyo si ndugu yetu katika dini.
HUKMU YA MWENYE KUACHA KUSALI (TAARIKU SALAAT)
Maulamaa wote bila hitilafu yoyote baina yao wamekubaliana kuwa mwenye kuiacha Sala kusudi kwa jeuri na kwa kuikanusha, huyo anakuwa kafiri aliyekwisha toka katika dini ya Kiislam.
Isipokuwa wamehitalifiana juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia lakini haikanushi na anaamini kuwa ni fardhi juu yake.
Wapo wanaosema hata huyu naye pia anakuwa kafiri aliyekwishatoka katika dini ya Kiislam, na dalili walizoziegemea maulamaa hao ni hadithi za Mtume (SAW) zifuatazo;
“Kutoka kwa Jabir (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Baina ya mtu (kuwa Muislam) na baina ya (kuwa) kafiri, ni kuacha Sala”.
Muslim – Ahmed – Atttirmidhiy na wengineo
Na kutoka kwa Buraida (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Ahadi iliyopo baina yetu na baina yao ni Sala, atakayeacha (kusali) kesha kufuru”.
Ahmed na wengineo
Na kutoka kwa Abdillahi bin Amru bin Al Aas (RA) kuwa Mtume (SAW) siku moja alizungumza juu ya Sala kisha akasema;
“Atakayeisimamisha atakuwa na nuru na dalili na ataokoka siku ya Kiama, ama asiyeisimamisha hatokuwa na nuru wala dalili wala hatookoka, na atakuwa siku ya Kiama pamoja na Qaruni na Firauni na Hamana na Ubaya bin Khalaf”.
Imam Ahmed na Attabarani na wengineo
Katika kuifasiri hadithi hii, anasema mwanachuoni maarufu Ibnul Qayim al Jouzi kuwa;
“Mwenye kuacha Sala huwa ameshuhgulika na mojawapo kati ya yafuatayo; ama atakuwa imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaruni, na aliyeshughulika na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Firauni, na aliyeshughulika na cheo chake atakuwa pamoja na Hamana na yule aliyeshughulika na biashara zake (akaacha kusali), huyo atakuwa pamoja na Ubaya bin Khalaf”.
Kutoka kwa Abdillahi bin Shaqiq Al Aqliy anasema;
“Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) hawakuwa wakiona amali yoyote nyingine mtu akiiacha anakuwa kafiri isipokuwa Sala”.
Attirmidhiy na Al Hakim
Anasema Ibni Hazm;
“Imepokelewa kutoka kwa Omar bin Khatab na Abdul Rahman bin Auf na Muadh bin Jabal na Abu Huraira na Masahaba wengi (RA) kuwa;
“Atakayeacha kusali (Sala moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati wake (Sala hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri”.
Hadithi zifuatazo zinaelezea juu ya hukmu ya kuuliwa kwa Taariku ssalaat (Asiyesali);
Kutoka kwa Ibni Abbas (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Heshima ya Uislam na misingi ya dini ni mitatu, juu yake misingi hiyo umejengeka Uislam. Atakayeacha mojawapo anakuwa kafiri na damu yake halali;
Kushuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah,
Na Sala zilizofaradhishwa,
Na Funga ya Ramadhani”.
Abu Yaala
Na kutoka kwa Ibni Omar (Abdillahi bin Omar bin Khattab (Radhiyallahu anhum) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Nimeamrishwa nipigane vita mpaka pashuhudiwe kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na isimamishwe Sala na itolewe Zaka, watakapofanya hivyo, itakingika kwangu damu zao na mali zao ila kwa haki ya Uislam na hesabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka”.
Bukhari na Muslim”
RAI ZA BAADHI YA WANAVYUONI
Anaendela kusema Sayed Sabeq kuwa;
“Kutokana na Aya pamoja na Hadithi zilizotangulia, inatubainikia kuwa Asiyesali ni kafiri na kwamba damu yake ni halali. Hata hivyo baadhi ya maulamaa waliotangulia na wa siku hizi wakiwemo Imam Abu Hanifa na Imam Shafi na Imam Ahmed wanasema kuwa hawi kafiri moja kwa moja, bali anahesabiwa kuwa ni mtu fasiq na anakamatwa na kutubishwa na akikataa kutubu basi maulamaa wote hao wanasema kuwa mtu huyo anahukumiwa kuuliwa.
Anasema Annawawi katika Sharhi Muslim;
“Anakatwa kichwa chake kwa upanga”.
Imam Abu Hanifa anaona kuwa aliyertadi na akastahiki kuhukumiwa kuuliwa ni yule tu anayeikanusha Ibada hiyo ya Sala, lakini yule anayeacha kusali kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia, huyo si kafiri bali ni fasiq na hukmu yake ni kumhamisha mbali na mji wake, wakiegemea dalili zinazobeba maana kwa ujumla kama vile kauli Yake Subhanahu wa Taala aliposema;
“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe(dhambi ya) kushirikishwa na kitu, lakini Yeye husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye”.
Annisaa - 114
Na hadithi iliyosimuliwa na Abu Huraira kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Kila Mtume ana dua yake inayokubaliwa. Kila Mtume akafanya haraka kuiomba dua yake hiyo. Ama mimi nimeiweka dua yangu kwa ajili ya kuwaombea shafaa ummati wangu siku ya Kiama, ataipata Inshaallah kila aliyekufa na asimshirikishe Mwenyezi Mungu na chochote”.
Na hadithi nyingine za mfano huo.
Maulamaa wengine wakasema kuwa hauliwi mtu kwa ajili ya kutosali, na hawa wameegemeza hoja zao kutokana na hadithi iliyomo ndani ya Bukhari na Muslim isemayo;
“Si halali kumwaga damu ya Muislamu ila kwa mojawapo ya matatu; Mzinzi aliyekwishaoa, nafsi kwa nafsi (aliyeuwa auwawe) na aliyertadi (aliyetoka katika dini) na kujitoa katika jamii ya Kiislam”.
Wanasema kuwa hapa Mtume (SAW) hakumtaja asiyesali kuwa ni miongoni wa waliohalalishwa damu yao.
MAJADILIANO BAINA YA IMAM SHAFI NA IMAM AHMED
Imepokelewa kuwa Maimam waiwili wakubwa, Imam Shafi na mwanafunzi wake Imam Ahmed bin Hanbal walijadiliana juu ya maudhui haya ya mtu asiyesali, na majadiliano hayo yalikwenda kama ifuatavyo;
Imam Shafi;
“Ewe Ahmed! Unasema kuwa anayeacha kusali anakuwa kafiri?”
Imam Ahmed;
“Ndiyo nasema hivyo”.
Imam Shafi;
“Ikiwa atakuwa kafiri, vipi atarudi katika Uislam?”
Imam Ahmed;
“Kwa kutamka; ‘Ash-hadu an laa ilaaha illa Llah Muhammadan Rasulu Llah”.
Imam Shafi;
“Lakini mtu huyo hajaikanusha shahada hiyo”.
Imam Ahmed;
“Anarudi katika Uislam kwa kusali”.
Imam Shafi;
“Sala ya kafiri haikubaliwi, na kafiri hahesabiwi kuwa ni Muislamu hata kama atasali”.
Imam Ahmed akanyamaza.
TAHAKIKI YA IMAM ASHAUKANI
Anasema Ashaukani kuwa;
Kwa hakika asiyesali ni Kafiri, kwa sababu hadithi zote zilizopokelewa katika maudhui haya zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni ‘Sala’.
No comments:
Post a Comment