Sunday, February 22, 2015

Sura na mwelekeo mpya wa elimu Tanzania

Lugha ya kufundishia
Hiki ni kilio kikuu cha wadau wengi wa elimu nchini. Kwa muda mrefu suala la lugha ya kufundishia limezua mkanganyiko.
Hoja kuu ikiwa ni kushindwa kwa Serikali kuwa na msimamo thabiti kuhusu lugha hiyo, jambo ambalo wadau wanasema linawachanganya wanafunzi.
Ilivyo ni kuwa, wakati elimu ya msingi ikifundishwa kwa lugha ya Kiswahili, wanapomaliza ngazi hiyo, wanafunzi wanakumbana na lugha ya Kiingereza inayotumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi ya sekondari.
Kuhusu mkanganyiko huu, sera mpya inapendekeza kutumika kwa Kiswahili kama inavyobainisha:
“Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo na Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija kitaifa na kimataifa.”
Hata hivyo, sera hajaiweka kando lugha ya Kiingereza kwani inasema: “Serikali itaendelea na utaratibu wa kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kufundishia na kujifunzia, katika ngazi zote za elimu na mafunzo.’’
Kitabu kimoja
Mgogoro mwingine katika sekta ya elimu kwa miaka mingi ulihusu utaratibu holela ulioruhusu matumizi ya vitabu mbalimbali vya kiada.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwani katika mkoa mmoja, shule zilifikia hatua ya kuwa na vitabu tofauti vya kufundishia.
Athari ya matumizi ya vitabu vingi ambavyo vimekuwa vikichapishwa na kampuni binafsi, ni pamoja na baadhi ya vitabu kubainika kutokuwa na ubora stahiki, huku vikigubikwa na kasoro mbalimbali kama kuwa na makosa ya uchapaji na udhaifu wa maudhui.
Kuepuka kasoro hizi, Serikali inasema itahakikisha upatikanaji wa kitabu bora kimoja cha kiada kwa kila somo kwa kila mwanafunzi katika elimu msingi ambavyo vitaandaliwa kwa utaratibu maalumu.
“Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu msingi ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu,’’ inasema sehemu ya sera.
Elimu msingi kuwa miaka 10
Kumekuwa na kilio kuwa wanafunzi wa Kitanzania wamekuwa wakimaliza masomo yao wakiwa na umri mkubwa.
Kwa kawaida wanafunzi nchini wanaanza elimu ya msingi yaani darasa la kwanza wakiwa na miaka saba. Wanapomaliza elimu ya juu wanakuwa na miaka kuanzia 23 na kuendelea.
Hii ni tofauti na ilivyo katika nchi nyingi ambazo wastani wa wanafunzi kumaliza elimu ya juu ni miaka 20 hadi 22.
Sera mpya inapendekeza muundo mpya utakaojumuisha elimu msingi itakayosomwa kwa miaka 10, ikijumuisha masomo ya msingi na sekondari.
Sera inapendekeza muundo wa 1+6+4+2+3+ (shule ya awali mwaka mmoja, msingi miaka sita, sekondari miaka sita na chuo kikuu miaka mitatu au zaidi)
Wadau nao
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam, Lilian Sawiya anasema Serikali imekuwa na sera na mikakati mizuri zaidi katika kuboresha elimu, lakini changamoto iliyopo ni utekelezaji wake.
Anatoa mfano akisema awali kabla ya kutangaza sera hiyo, wanafunzi wote waliotakiwa kujiunga darasa la kwanza hadi darasa la saba walitakiwa kusoma bure, lakini hadi sasa watoto wengi wanakwama kuanza darasa la kwanza kutokana na mzigo wa michango ya shule.
“Na hatukusikia kiongozi aliyesimama kukemea au kuchukua hatua kali dhidi ya udhaifu huo...sasa kama chombo hicho kitafanya kazi kwa ufasaha bila kuingiliwa na mdudu wa rushwa, matokeo yatakuwa mazuri, kwani ujanja wa utoaji vyeti feki na tuzo imekuwa kawaida sana kwa mazingira ya sasa,” anasema Lilian.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya kitabu kimoja, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventura anasema hatua hiyo ni ya kupongezwa.
Anasema wanafunzi wengi walikuwa wakifeli siyo kwa sababu ya kutoelewa bali ni kwa kufundishwa vitabu tofauti vya kiada.
“Kitabu cha kiada kinasaidia kujenga msingi wa uelewa sawa kwa wanafunzi wote nchini, hivyo hata katika utungaji wa mitihani inarahisisha wanafunzi kuwa na uhakika wa kile walichojifunza kuliko kubahatisha kwa ufundishaji wa vitabu tofauti vya kiada,” anasema.
Kwa upande wake, Katibu mkuu wa umoja wa wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya anasema amekunwa na muundo mpya wa miaka ya ngazi mbalimbali za elimu anaosema utasaidia kupunguza muda wa mwafunzi kukaa shuleni.
Anasema muundo mpya umesaidia kupunguza miaka miwili pamoja na umri wa kuanza shule ya msingi, hatua itakayowawezesha wanafunzi kumaliza elimu ya juu wakiwa na miaka isiyopungua 18.
“Hatua hiyo hufanyika katika mataifa yaliyoendelea, yaani mwanafunzi anakuwa na nafasi ya kutumikia Taifa kwa miaka mingi siyo kama ilivyo sasa.
Kwa mfano, tajiri wa dunia Bill Gate alianza kufanya kazi akiwa na miaka 13 hadi sasa dunia inamtegemea. Hivyo, hata sisi tunatakiwa kumwandaa mtoto kitaaluma na kukuza kipaji chake tangu awali,” anasema Nkonya.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mapambano, iliyopo Sinza, Dar es Salaam, Amina Msangi anasifu uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili akisema utasaidia wanafunzi wengi kuelewa kwa kuwa ni lugha wanayoitumia pia katika mazingira wanayoishi.
Hata hivyo, anapata hofu na lugha hiyo akihoji kama ina nguvu katika soko la ajira lililogubikwa na matumizi ya lugha ya Kiingereza.
“Mwingiliano na uhusiano wa kimataifa kwa sasa vimetekwa na lugha za kigeni, hususani katika soko la ajira, je, itakuwaje na wazazi wanaamini Kiingereza zaidi,” anasema na kuongeza:
“Pia, huo utaratibu wa matumizi ya Kiswahili itakuwa kwa shule za Serikali pekee? Je, shule binafsi zitaendelea kutumia Kiingereza? Kwa hivyo, nadhani sera ingebana shule zote ili kuondoa tofauti iliyopo.”
Nini kimechangia kutungwa kwa sera mpya?
Awali, Tanzania ilikuwa na sera kadhaa kuhusu elimu ambazo bila shaka changamoto zake, ndizo zilizochangia kutungwa kwa sera mpya ya mwaka 2014.
Sera hizo ambazo sasa zimefutwa ni pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996), Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu Msingi (2007). Kwa jumla utekelezaji wa sera za elimu na mafunzo, umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kukosekana kwa mfumo nyumbufu.
Wataalamu wa sera wanasema mfumo huu ni ule unaoruhusu elimu na mafunzo kupatikana na kutambulika kwa njia mbalimbali mbadala; kuwapo kwa elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora visivyotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.
Changamoto nyingine ni kutokuwa na mfumo wa ajira unaowezesha upatikanaji wa wataalamu wa kada mbalimbali wanaohitajika katika sekta ya elimu na mafunzo nchini.
Kukosekana fursa zitolewazo kwa kila Mtanzania kulingana na mahitaji yake na sehemu na mazingira aliyopo.
Nyingine ni kutokuwa na mfumo wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo wenye wigo mpana na endelevu na kutozingatia masuala mtambuka kikamilifu katika elimu na mafunzo.
Changamoto hizi na hata mabadiliko mbalimbali yaliyoikumba nchi na sekta ya elimu kuanzia mwaka 1995, yanatajwa kuwa chachu kwa Serikali kutunga sera mpya kwa minajili ya kukidhi mahitaji ya sasa.
Kwa mfano, sera inasema kuwa kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia ambayo yameleta changamoto na kuzifanya sera hizo zipitwe na wakati.
“Mabadiliko ya kiuchumi duniani yameleta msukumo kwa nchi zinazoendelea na zilizoendelea ama kubadilisha au kuimarisha sera, programu na mikakati yake ili ziweze kuhimili ushindani wa kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii, kisayansi na kiteknolojia,’’ yanasema maelezo ya sera mpya.
Inaongeza kusema: “Kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa, sera hii inajikita katika kuimarisha utangamano katika elimu na mafunzo ili kumjengea Mtanzania ujuzi, umahiri na uwezo wa kukabiliana na mahitaji yanayojitokeza katika ulimwengu wa kazi na maisha kwa jumla.’’

No comments:

Post a Comment