BismiLlaahi waswalaatu wassalaamu ‘alaa
RasuuliLlaah wa ba’ad,
Ndugu Wapenzi Waislam,
Tunaukaribia
mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Mwezi wenye fadhila tele zisizohesabika idadi yake.
Mwezi ambao ndani yake utakapofunga Swawm yake kwa Iymaan ya dhati na kuitakidi
kuwa kuna malipo, basi utasamehewa madhambi yako yaliyotangulia. Mwezi ambao
haufananishwi na miezi mingine kwa mavuno na ujira; du’aa ya mfungaji
haikataliwi, anapofunga Muislam huwa na furaha mbili; furaha wakati anapofungua
na furaha wakati anapokutana na Mola wake. Mwezi ambao Swawm itamuombea
shafa’ah mja siku ya Qiyaamah, itakaposema siku hiyo kumuambia Allaah, “Ee
Mola, nimemzuia chakula chake, na matamanio yake ya kimwili mchana kutwa, basi
niache nimwombee shafa’ah.” *
Mwezi
ambao ni hifadhi na kinga nzito kabisa ya mja kutokana na moto, na harufu ya
mdomo wa aliyefunga (japo atakuwa anapiga mswaki) itakuwa ni bora kuliko harufu
ya misk mbele ya Allaah. Atakayefunga siku moja katika mwezi huo akitaka radhi
za Allaah na ikiwa hiyo itakuwa ndio siku ya mwisho ya maisha yake, basi
ataingia peponi. Kuna mlango maalum peponi kwa wale wafungao uitwao Ar-Rayyaan,
ambao wataingia wao tu, na watakapoingia mlango wake utafungwa na hatoingia
yeyote mwengine. Huo ndio mwezi ambao ni nguzo ya Uislam, ndani yake
kunapatikana usiku mtakatifu ambao ni bora kuliko miezi elfu moja, katika mwezi
huo milango ya pepo huwa wazi, milango ya moto hufungwa na mashetani hufungwa
minyororo. Mwezi utakapoufunga wote, Swawm yake ni sawa na kufunga miezi kumi.
Na katika kila wakati wa kufutari, Allaah Huchagua watu wa kuwaweka huru na moto.*
Ndugu
Muislam, baada ya kujua fadhila zote hizo za mwezi huu Mtukufu, badala ya watu
kujiandaa kwa mambo mema ya kheri kama kuanza kujizoesha na Swawm za Sunnah
kama zile za Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe n.k., au kutoa Swadaqah kwa
maskini ili nao wapate maandalizi mazuri ya mwezi huo wenye baraka, au
kujiandaa kwa kufanya mengi ya kheri ambayo yametanawai, kinyume chake kumekuwa
kuna wengi wenye majina ya Kiislam ambao huukaribisha mwezi huu Mtukufu kwa
kila aina ya maasi kwa jina la ‘Vunja Jungu’ kama ijulikanavyo katika maeneo
mengi Tanzania, au ‘Mfungo’ kama inavyojulikana katika maeneo ya Sawaahil (pwani)
ya Kenya.
Jambo hilo licha ya kuwa halipo katika Dini yetu hii Safi, Tukufu,
bali ni jambo ambalo haliwezi kufanywa na Muislam mwenye Iymaan na khofu ya
Mola wake na ndio maana tukawaita hao wayafanyao hayo kuwa ni Waislam jina.
Katika masiku ya mwisho ya Sha’abaan, na haswa zaidi siku ile ya
mwisho, watu hao hukusanyana na kufanya sherehe (party) kwa kusikiliza
nyimbo na kucheza muziki na kunywa vinywaji vya haramu. Pombe siku hiyo kwa
wale walevi ndio inanywewa kama kisasi, wengine ndio siku ya uzinzi kwa kuwa
Ramadhaan wanaogopa kuyafanya hayo, wale wavuta sigara ambao kidogo wanachelea
kuvuta katika mwezi wa Ramadhaan nao paketi zitavutwa kwa mfululizo, wala unga
na mirungi hali kadhalika na mengi mengineyo machafu huwa ndio siku yake rasmi
hiyo. Bila kuwasahau wenye kwenda mapikniki na kutumbua.
Watu hao kwa kufanya hivyo, wanamkebehi na wamemfanya Allaah kuwa
ni Mungu wa Ramadhaan! Ama miezi kumi na moja iliyobaki, huyo Mungu anakuwa
kama hana thamani, au kuwepo kwake kumekuwa si kiutendaji!
Wengine ndio wanaukaribisha kwa kufanya manunuzi (shopping)
ya mikeka ya kuswalia – maana miezi yote iliyopita, kwao Mungu hakuwepo, kanzu
hununuliwa kwa wingi, misikiti huanza kushehena hadi inakuwa kero badala ya
furaha kwa wale wenye kudumisha Swalah za Jama’ah kwa miezi yote ya mwaka kwani
hata nafasi za mbele walizozoea kuzipata huwa ni adimu au hata kukosa kabisa
kwa hao wavamizi wa Ramadhaan. Vilevile kina dada waliokuwa hawajui hata kuvaa
Hijaab, basi utawaona wanaanza kununua leso za kujitanda, kanga zimeongezeka
biashara, wanaojitahidi zaidi baibui nazo zimekuwa ni pato kwa wauzaji. Nyumba
mbalimbali utaanza kusikia Qur-aan zikisomwa kwenye maredio, kofia na kanzu
zimeanza kushamiri kwenye miili ya wengine. Hayo
yote ni dhana ya wayafanyayo kuwa ni ‘heshima’ na ‘taadhima’ kwa mwezi huu. Ila
walichoghafilika ndugu zetu hao, ni kuwa mafuhumu hiyo, ni mafuhumu
inayoonyesha kuwa katika miezi iliyobaki, hakuna kinachowapasa wao kufanya
hayo, hivyo, kumfanya Allaah Mtukufu, kuwa Kuwepo Kwake na Uwezo Wake, Nguvu
Zake na Amri Zake hazina uzito wowote ila Ramadhaan tu. Nayo ni mafuhumu potofu
na dhana iliyo ovu.
Ni wajibu wa jamii linapoonekana jambo
lolote ovu, kulizuia, kulikemea au kulikasirikia/ kulisusia endapo tutakuwa
tupo katika udhaifu wa kutumia njia mbili za awali. Na hii ni amri ya Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema:
((Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki
walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Swalaah, na hutoa Zakaah,
na humtii Allaah na Mtume Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni
Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hekima)) At-Tawbah: 71
Vile vile Hadiyth kutoka kwa Mtume wetu mpenzi (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abu Sa'iyd
Al-Khudriy (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye
amesema: Nilimsikia Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) akisema: "Yeyote yule atakayeona
kitendo kiovu basi akiondoe (akibadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi
kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake
(achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) Muslim.
Uongofu Ni Ule Wa Mtume, Na Upotofu Na Uzushi Ni Njia Ya Shaytwaan
Muislamu inampasa afuate mafunzo yaliyo sahihi na kujiepusha na
yasiyo sahihi kwani kufuata uzushi ni kumpotosha mtu na hatari yake ni kama
alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kila
khutbah yake:
Akisema katika Khutbah za Ijumaa,
((Amma Ba'ad, hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu
cha Allaah, na uongofu ulio bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi
wake na kila uzushi ni upotofu)) [Muslim] na katika
riwaaya nyingine ((na kila upotofu ni katika moto))
Na pia alieleza katika Hadiyth nyingine:
((Atakayezusha katika jambo lisilokuwa
(katika Dini) yetu basi litarudishwa [haitopokelewa])) Al-Bukhaariy
na Muslim
Uzushi huu wa Vunja Jungu ambao ni mchafu
na muovu, ni jambo linalopaswa kukemewa na Waislam wote wa hali zote; Mashaykh,
Maimaam, Maustaadh, walinganiaji na watu wa kawaida. Katika kila mnasaba na
kila khutbah kukemewe hayo hadi jamii ifahamu ubaya wake na madhara yake na
mwisho mbaya ambao unaoweza kumfika mtendaji wa tendo hilo.
Kila mwenye kuvunja jungu angepaswa
ajiulize wakati anapofikiria kufanya uovu wake, kuwa kufanya hivyo ni kufuata
mafundisho ya nani? Ikiwa hayo hayapo katika Dini, achilia mbali kumuudhi
Muumba. Ajiulize pia, ana uhakika gani wa kuwa ataishi hadi kuikuta hiyo
Ramadhaan? Je, akichukuliwa katikati ya tendo lake
ovu kama hilo anafikiria khatima yake ni nini? Kuna uhakika gani wa kuufika huo
mwezi na kuumaliza na hata kughufuriwa madhambi hayo aliyoyatenda? Nani
anayemiliki uhai mikononi mwake? Wangapi wenye siha wameondoka na siha zao?
Wangapi vijana wameondoka na ubarubaru wao? Je, hawajiulizi yote hayo?
Na hao ndugu zetu wanapofikiwa na mawaidha
haya, au wakapata kujua ubaya wa wayafanyayo, basi wasiwe wenye ukaidi wa
kuyafuata na kuyafanyia kazi. Wasiwe kama watu wa zamani walivyokuwa
wakipelekewa Mitume kuwatoa katika kiza cha kuabudu masanamu na kumshirikisha
Allaah na kuwaingiza katika mwanga ya uongofu ulio na hoja za wazi, ikawa kila
wakipewa mawaidha, wao hutaka kubakia katika ujinga na ukaidi wao,
{{Na haiwafikii hata ishara moja katika
ishara za Mola wao ila wao huwa wenye kuipa nyongo}} Al-An’aam:4
Na
Ndiyo maana pia wameambiwa baada yao na sisi pia kuwa tuende tukaone hizo
athari za kuangamizwa kwao ili iwe funzo kwetu:
{{Sema:
Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanaokanusha}} Al-An’aam:11
Athari
zao hizi nyingi zimejulikana kwetu kutokana na mafunzo haya ya Qur-aan lakini
ni nani mwenye kutaka kutafakari na kujitoa katika upotofu na kupata uongofu?
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa hao wasiotaka kupata uongofu ni
vipofu wa moyo:
{{Je!
Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio
ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo
ziliomo vifuani}} Al-Hajj: 46.
Naam ndugu Waislamu, mwenye kupofoka macho
anaweza kuwa na iymaan ya dini, kwani wangapi waliokuwa vipofu lakini wamepata hidaaya,
wangapi wameweza kuhifadhi Qur-aan na hata kuwa ni Maulamaa wakubwa wa Ummah na
mifano ni mingi. Lakini wangapi waliokuwa na macho kamili lakini wakawa ni vipofu
wa nyoyo; wakiwa wametawaliwa na upotofu na ufisadi?
Kuacha Maovu Ni Kufanya Jihaad Ya Nafsi
Ambayo Ni Jihaad Bora Kabisa
Aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) na Swahaaba, "Je, Hijrah gani iliyo bora?"
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu:
((Ni kuhama yale Anayochukia Mola
wako Mtukufu ((Swahiyh Al-Albaaniy kutoka kwa An-Nasaaiy.
Hivyo mwenye kuacha maovu kama haya ya
uzushi wa Vunja Jungu bila shaka atakuwa amepata daraja ya kufanya Jihaad.
Na thawabu hizo ambazo usawa wake pia ni
wa Hijrah pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
anaweza kuzipata mtu atakapokuwa katika twaa'a wakati wa fitnah, nao ni kama
wakati wetu huu uliojaa fitnah (mitihani, misukusuko, Uislam kukabiliwa na
Uadui ndani na nje n.k.) kila aina, khaswa kwa zama hizi zilizojaa mkorogo ulio
katika Dini wa yale yaliyo sahihi na yaliyo ya uzushi (Bid’ah). Kwa hiyo,
anapojikita mtu katika msimamo thabiti na kujiepusha na fitnah hizo, bila shaka
atakuwa amepata fadhila hizo za Hijrah iliyokusudiwa:
Kutoka kwa Ma'qil bin Yasaar (Radhiya
Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam): ((Kufanya ibada wakati wa fitnah, ni sawa na kufanya Hijrah kwangu))Muslim.
Basi na tujiepushe na yote Aliyokataza
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kuzidisha ibada kwa wingi khaswa katika miezi
mitukufu na mwezi kama huu wa Sha’abaan ambao una fadhila na pia ni ni mwezi
ambao tunategema kughufuriwa madhambi yetu. Kwa nini tujiongezee madhambi baada
ya kughufuriwa? Tumekosa hata chembe cha shukurani kwa Mola Muumba!
Nyakati hizi ndugu Waislamu tuzitumie
katika ibada ili tujichumie mema mengi, kwani ni nyakati ambazo kwa neema ya
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) zinatumiminikia kila kukicha, angalau tuzingatie
na kushukuru kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
{{Naye Ndiye Aliyefanya usiku na mchana
kufuatana kwa nafuu ya anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru}} Al-Furqaan: 62.
Ndugu Waislam, kama wanataka kuvunja jungu
kama waitavyo hao wavunjaji, basi kwanini wasifanye kama Maswahaba (Radhiya
Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa kila ukikaribia kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan
wakizidisha kusoma Qur-aan na wale wenye uwezo kimali wakitoa mali kuwapa
maskini ili kuwapa nguvu (Kujiandaa na mfungo wa Ramadhaan).
Ni muhimu kwa Waislamu kufanya maandalizi
ya Ramadhaan kwa kujielimisha juu ya namna ya kuukabili mwezi mtukufu hasa
kuelewa maana na makusudio ya funga, namna ya kufunga kwa kuzingatia masharti,
mambo yanayobatilisha Swawm, pamoja na Sunnah zilizokokotezwa na Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) ametufundisha namna iliyo bora ya kukaribisha funga ya Ramadhaan, hivyo
tunapaswa kufunga Sunnah za Jumatatu na Alkhamiys pamoja na kuisoma Qur-aan kwa
wingi kama alivyotuagiza.
Vilevile Ramadhaan inapoingia Waislam
wanatakiwa wajiepushe kabisa na mambo yote ya laghwuambayo hupoteza
Swawm kama vile kuangalia mpira, sinema za kipuuzi, misalsalaati, kucheza bao,
karata, usoro, dhumna, drafti, keramu n.k. Laghwu ni
jambo lolote la kipuuzi ambalo hupoteza muda na kumsahaulisha mja kumkumbuka
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Katika zama hizi Sunnah zimetupiliwa mbali
na bid’ah ndizo zenye kufuatwa na kuwa ndio mwendo wa Waislamu wengi, kwa
sababu ya ujinga wa kuigiza tu watu bila ya dalili, na kutopenda kujifunza
mafunzo mema yaliyo sahihi ya Kiislamu. Mafunzo
ambayo yamekamilika na kumfaa kila binaadamu popote na wakati
wowote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema yangu,
na Nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini}} Al-Maaidah: 3.
Tumuombe Allaah Atuthibitishe mioyo yetu katika Iymaan, na
Atuongeze kwenye uongofu, na Atughufurie madhambi yetu makubwa na madogo.
Aamiyn
-----------------------------------------------------------------------
* Maelezo yote hayo yametolewa katika Hadiyth Sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika vitabu vifuatavyo:
* Maelezo yote hayo yametolewa katika Hadiyth Sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika vitabu vifuatavyo:
Swahiyhul-Bukhaariy
Swahiyhu Muslim
Musnad Ahmad
Swahiyhut-Targhiyb
Sunnan An-Nasaaiy
Al-Bayhaqiy
Silsilatus-Swahiyhah
Swahiyhul-Jaami’i
Fat-hul-Baariy
No comments:
Post a Comment