(1) Kumwamini Allaah
Mimi ni Muislamu…
· Ninamwamini
Allaah Pekee Asiye na mshirika na hakuna mola mwingine isipokuwa Yeye,
Hakuzaa wala Hakuzaliwa, na hakuna kamwe kifano chake.
· Ameumba
mbingu na ardhi, Naye Ndiye Anayezimiliki. Anayajua yaliyofichikana na
yenye kuonekana. Yu Hai na Hafi, Anayasimamia mambo yote milele na
Halali.
· Ana
Majina Mazuri Kabisa na Sifa za Juu. Kati yake ni Majina tisini na
tisa, mwenye kuyajua na kuyadhibiti vyema na akamwomba Allaah Kwayo,
ataingia peponi.
· Kati
yake ni Sifa za Upweke, kwani Yeye Subhaanahu wa Ta’alaa ni Mmoja wa
Dhati, Sifa na Vitendo, Aliyepwekeka, Aliye Pekee, Mkusudiwa, Mmiliki wa
ufalme.
· Na
Sifa za Utukufu, kwani Yeye ni Mwenye hekima, Mwenye habari ya kila
jambo, Mwelekezaji wa manufaa, Haki, wa Mwanzo, wa Mwisho, wa Dhahiri,
wa Siri, Mrithi, Mwenye Kubakia, Mkwasi, Mtakasifu, Mwenye Kushuhudia,
Aliye Karibu, Mbora wa Kupangilia, Mwadilifu, Nuru ya mbingu na ardhi,
Mwenye Utukufu na Ukarimu.
· Na
Sifa za Uadhama, kwani Yeye ni Mshindi Asiyeshindika, Mwenye Sifa zote
Tukufu, Mwenye Uadhama, Mwenye Sifa za Utukuzo, Mwenye Kulazimisha,
Mwenye Nguvu, Aliye Imara, Mteza nguvu, Mweza, Mwenye uwezo wa juu,
Mwingi wa Kunusuru, Aliye Juu, Aliye Juu ya vyote.
· Na
Sifa za Uwezo, kwani Yeye ni Mwingi wa Ujuzi, Mwenye Kusikia, Mwenye
kuona, Yu Hai, Mwenye Kukamata, Mwenye Kukunjua, Mwenye Kushusha, Mwenye
Kupandisha, Mwenye Kutukuza, Mwenye Kudhalilisha, Mwenye Kutoa, Mwenye
Kuzuia, Mwenye Kunufaisha, Mwenye Kudhuru, Mwenye Kuhuisha, Mwenye
Kufisha, Mwenye Kutanguliza na Mwenye Kuchelewesha.
· Na
Sifa za Uumbaji, kwani Yeye ni Muumbaji, Msanifu wa Maumbile, Mtiaji
Sura, Hakimpiti au Kumshinda kitu, Mbunifu, Mwenye Kuanzisha, Mwenye
Kurejesha, Mwenye Kufufua, Mwenye Kukusanya, Mpaji Mkuu, Mfunguzi wa
kila jambo, Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Kutajirisha, Mdhibiti wa idadi,
Mwenye Kudhibiti mambo, Mwenye Kuhifadhi, Mlinzi na Muumbaji wa mbingu
na ardhi bila ruwaza.
· Sifa
za Rehma, kwani Yeye ni Mwingi wa Rehma, Mwingi wa Kurehemu, Mwingi wa
Huruma, Mwenye Kuneemesha neema nzuri, Mwingi wa Penzi, Mtenda Wema,
Mwingi wa Kughufiria, Mwenye Kusamehe, Mwingi wa Kukubali toba, Mwenye
Amani, Mtoaji amani na imani, Mpole, Mwenye Kulipa vyema, Mkarimu,
Mwenye Kuneemesha, Mwingi wa Kutoa, Mwenye Kusaidia, Mwenye Kujibu,
Mkunjufu, Mwingi wa subira, Mvumilivu kwa Waja Wake, Latifu, Wakili,
Mwenye Kutoa Misaada, Mwenye Kuombwa msaada na Mwenye Kukubali toba.
· Amemneemesha
mwanadamu neema nyingi zisizo na hesabu. Na hakuna neema yoyote
anayoneemeka nayo mja ila hutoka kwa Allaah Pekee, kwani Yeye Ndiye
Aliyemuumba na Akampa uhai, Akamfanya asikie na aone, Akamkirimu, kisha
Akamruzuku na Akamfanyia wema.
· Kwa
ajili hiyo, ni lazima mja amwabudu Allaah Peke Yake – nako ni kufuata
amri Yake na kuacha makatazo Yake – kwa kuwa hastahiki yeyote kuabudiwa
isipokuwa Allaah Peke Yake.
· Vile vile, bila shaka Allaah Anazijua hali zote za mja kati ya utiifu na uasi. Hivyo basi, ni wajibu moyo wa mja ujae haiba kwa Allaah Mtukufu, utukuzo na mapenzi, na aone haya kumwasi na aachane na maasi, kwani Allaah Humwona wakati akiyafanya.
· Anafurahi
kwa amali zake njema zinazomkurubisha kwenye radhi za Muumbaji wake
Subhaanahuu wa Taala. Hivyo huzidi kufanya amali hizo hadi kufikia ngazi
ya ihsani, kwani imani huzidi kwa matendo mema na hupungua kwa maasi.
· Asivutike
kwenye matamanio, hawaa au bid'a, bali avutike kwa Allaah Pekee huku
akifuata maamrisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam). Asitafute kwa amali yake starehe ndogo ya dunia bali atafute
kwayo malipo toka kwa Allaah tu.
· Aidha,
hakika Allaah Ana huruma mno kwa mwanadamu kuliko huruma ya mama kwa
mwanaye. Na rehma Yake imekienea kila kitu. Hivyo basi, ni wajibu kwa
mja amwombe na anyenyekee Kwake katika haja zake za kidunia na za
kiakhera, na wala asimwombe yeyote mwingine.
· Kwa
vile hakuna faida yoyote ya kumwomba asiye Allaah, kwa kuwa hamiliki
uwezo ulio kamili isipokuwa Allaah, na hakuna asikiaye ya siri na
minong'ono ila Allaah, na hakuna anayemiliki makadirio isipokuwa Allaah,
basi kwa maana hiyo, hakuna wa kujibu dua isipokuwa Allaah.
· Na
kwa ajili hiyo, haijuzu kwa Muislamu kuliomba kaburi, au kumwomba
aliyezikwa humo vyovyote awavyo, kwa kuwa yeye hamsikii. Na kama
hamsikii, basi ni vipi atamjibu au kumnufaisha? Hakika Allaah Pekee
Ndiye Mwenye Kunufaisha na Mwenye Kudhuru. Na kwa ajili hiyo, ni wajibu
kwa Muislamu asijenge Msikiti juu ya makaburi, kwani Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelikataza hilo.
· Kadhalika,
ni wajibu kwa mja alinganishe kati ya udhaifu wake na Nguvu za Allaah
Mtukufu, na kati ya umasikini wake na Utajiri wa Allaah Mtukufu, na kati
ya ujinga wake na Elimu ya Allaah Mtukufu, na kati ya unyonge wake na
Utukufu wa Allaah Mtukufu.
· Na ajue kwamba utukufu ni wa Allaah, Mtume Wake na Waumini.
· Hivyo
yampasa awe ni miongoni mwa Waumini hawa ambao hawatawakali isipokuwa
kwa Allaah Pekee, wala hawaombi msaada isipokuwa kwa Allaah, wala
hawaombi kinga na kujilinda isipokuwa kwa Allaah, wala hawaombi msaada
wa dharura ila kwa Allaah, wala hawamwogopi isipokuwa Allaah, wala
hawataraji isipokuwa kwa Allaah, wala hawamwombi isipokuwa Allaah, wala
hawachinji isipokuwa kwa ajili ya Allaah, wala hawaweki nadhiri
isipokuwa kwa ajili ya Allaah, wala hawaapi isipokuwa kwa Jina la
Allaah, wala hawaweki talasimu na hirizi (amali), wala hawasadiki wasemayo makuhani, watabiri (wanajimu) na wachawi, na wala hawawaendei.
· Na wao hawakosi rajua, na huwa na tahadhari ya mponyoko wa ndimi zao ili wasije kutelezea motoni. Hawasemi: "Amependa Allaah na amependa fulani", "lau si Allaah na wewe", "nimetawakali kwa Allaah na kwako". Bali waseme: "Nimetawakali kwa Allaah Pekee", "Amependa Allaah kisha amependa fulani".
Maneno haya humsawazisha Allaah na waja Wake,
na ni katika shirki ndogo.
- Na kama ilivyo wajibu kwetu kumwamini Allaah, ni wajibu wetu vile vile tuwakatae matwaghuti.
- Na kigogo wa matwaghuti ni Shaytwaan na kila yule aliyeabudiwa badala ya Allaah naye akaridhia hilo.
- Na kati ya matwaghuti hawa ni yule aliyetunga shari’ah zinazoharamisha Aliyoyahalalisha Allaah, au kuhalalisha Aliyoyaharamisha Allaah.
- Aidha, twaghuti ni kila yule aliyelingania hilo, au akawaamuru watu hilo, au akahukumu kwa hilo, kwa vile ametaadi na akavuka mpaka wa kiumbe wa kusikia na kutii.
- Basi Allaah Pekee Ndiye Aliyewaumba wanadamu, na Ndiye Anayejua yanayowafaa, na kwa hivyo, hakuna yeyote awezaye kuwapangia shari’ah isipokuwa Yeye tu.
(2) Kuwaamini Malaika
- Ninaamini kuwepo Malaika ambao Allaah Amewaumba kutokana na nuru, na Akawafanya kuwa na mbawa mbili mbili, tatu tatu, na nne nne. Nao hawali, hawanywi, hawalali wala hawaoi. Amewaamuru kufanya kazi na kusimamia majukumu mbalimbali, nao hutekeleza hayo.
- Malaika siku zote humtii Allaah bila kuchoka. Hawamwasi na humwogopa Mola wao toka juu yao. Kuna kati yao aliyesujudu toka siku Alipoziumba Allaah mbingu na ardhi hadi siku ya Qiyaamah. Na atakaponyanyua kichwa chake atasema: "Subhaanak! Hatujakuabudu ukweli wa kukuabudu".
- Wao ni waja wa Allaah na si wanawake, na wala si wasaidizi Wake, na wao watawaombea shifaa Waumini – kwa idhini ya Allaah – siku ya Qiyaamah.
Kati ya Malaika hawa, wapo:
· Walinzi ambao huwalinda viumbe na madhara.
· Watukufu waandishi ambao huandika matendo ya wanadamu, mema yao na mabaya yao.
· Wenye kumsabihi Allaah. Hawa humsabihi Allaah mchana na usiku na hawachoki mpaka siku ya Qiyaamah.
· Wenye kuvinjari ambao huhudhuria vikao vya dhikri, kisomo cha Qur-aan na vikao vya elimu.
· Wabebaji ‘Arshi ambao idadi yao
ni wanane. Ni viumbe wakubwa mno kati ya viumbe wa Allaah. Ndege huruka
toka ncha ya sikio la mmoja wao hadi shingoni kwa muda wa miaka mia
tano.
· Malaika wa mauti anayezitoa roho za viumbe kwa Amri ya Allaah. Huyu ana wasaidizi wake.
· Israfiyl
atakayelipuliza baragumu, kisha viumbe vyote vitakufa kabla ya kutokea
Qiyaamah. Kisha litapulizwa jingine, na hapo watasimama viumbe
wakiangalia.
· Miykaiyl anayesimamia jukumu la mvua.
· Ridhwaan ambaye ni mlinzi wa Pepo. Yeye ana wasaidizi wake wamechangamka kuwahudumia Waumini Peponi.
· Maalik
ambaye ni mlinzi wa moto. Ana wasaidizi wake ambao viongozi wao ni kumi
na tisa. Wana marungu ya chuma ya kuwaadhibu makafiri motoni - Allaah
Atuepushe na hayo.
· Mkuu wa Malaika ni Jibriyl aliyewakilishwa kupeleka wahyi kwa Manabii na Mitume.
· Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona katika umbile
lake. Kutokana na ukubwa wake, alizifunika peo za mbingu. Ana mbawa mia
sita, naye ndiye aliyekikamata kijiji cha Lut kwa ncha ya ubawa wake,
akakinyanyua hadi juu mbinguni, kisha akakipindua juu chini.
· Kuna Malaika wengineo wengi zaidi ya hawa, na hakuna ajuaye askari wa Mola wako isipokuwa Yeye tu.
· Malaika huwapenda Waumini ambao Allaah Huwapenda na huwaombea maghfira.
· Malaika mbali na nguvu zao hizi hupigana pamoja na Waumini.
(3) Kuviamini Vitabu
- Ninaviamini Vitabu vya Allaah Alivyoviteremsha kwa Mitume Wake, na kwamba katika asili ya kuteremshwa Kwake, ni Maneno ya Allaah Aliyowafunulia ili waifikishe shari’ah na Dini Yake. Vitabu vikubwa zaidi ni:
- Qur-aan Tukufu iliyoteremshwa kwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
- Injili iliyoteremshwa kwa ‘Iysa (‘Alayhis Salaam).
- Taurat iliyoteremshwa kwa Muusa (‘Alayhis Salaam).
- Zaburi iliyoteremshwa kwa Daawuud (‘Alayhis Salaam).
- Sahifa zilizoteremshwa kwa Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).
- Kati ya hivi, kuna vilivyopotolewa na kubadilishwa kabla ya kushuka Qur-aan.
- Na Qur-aan ndiyo iliyo juu ya Vitabu hivi, na ndiyo yenye kuongoza shari’ah zote na hukumu zake, na yenye kuondosha yale yote yenye kwenda kinyume na hukumu zake baada tu ya kuteremka kwake.
- Na kwamba Allaah Hatokubali siku ya Qiyaamah ila amali kupitia uongofu wa Qur-aan. Hatokubali amali kwa kufuata Vitabu vilivyotangulia baada ya kuteremka Qur-aan kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
- Na kwamba Qur-aan ni Maneno ya Allaah ya miujiza. Maneno haya yana utukufu wake, na wala hayaingiliwi na batili kabla yake wala baada yake. Mwenye kuyasema, amesema kweli, na mwenye kuhukumia kwayo, amefanya uadilifu, na mwenye kuyafanyia kazi basi hakika ameongolewa katika njia iliyonyooka, mwenye kushikamana nayo amefuzu na kuokoka, na mwenye kuyakengeuka atakuwa ni katika wenye kuhiliki.
- Ni kwamba watu wa Qur-aan, hao ndio watu wa Allaah waliokurubishwa Kwake, na kwamba mbora zaidi wa watu ni yule aliyejifundisha Qur-aan na akawafundisha watu, kwani Qur-aan hii itakuja siku ya Qiyaamah ikimwombea shifaa kila aliyeisoma, akaihifadhi na akaifanyia kazi, na itawaombea watu wake Pepo.
- Qur-aan huzitwaharisha nyoyo kutokana na shubha na matamanio yanayozichafua, huzikurubisha kwa Muumbaji Wake Subhaanahuu wa Ta'alaa, na huzihimiza kufanya kazi ili kufuzu na kupata neema za kudumu milele.
- Kati ya adabu za kusoma Qur-aan ni:
1. Kuwa twahara na wudhuu.
2. Kuelekea Qiblah.
3. Kukaa kwa adabu na heshima.
4. Kutoisoma kwa haraka.
5. Kuwa na unyenyekevu.
6. Kuonyesha huzuni kwa madhambi na kuvuka mipaka.
7. Kulia kutokana na kumwogopa Allaah na Utukufu wa Maneno Yake.
8. Kusoma kwa sauti nzuri.
9. Kusoma kwa sauti ya chini ili kutowabughudhi wenye kuswali.
10. Kuzingatia maana ya maneno.
11. Kuhudhurisha moyo.
12. Kutaamuli kwa kina Aayah za Allaah.
13. Tuwe
na yakini kuwa kusimamisha hukumu za Kitabu hiki kwa watu ni moja kati
ya sababu za kumakinishwa katika ardhi na kuwashinda maadui.
Basi
harakia ndugu yangu Muislamu kwenda kwa Mola wako, na kikamate Kitabu
hiki kwa hima. Kuwa na shime asikutangulie yeyote kuelekea kwa Allaah,
kwani Allaah Hufurahi zaidi kwa kurejea kwako Kwake kuliko wanavyofurahi
watu kwa kurejea mtu wao aliyekuwa mbali.
(4) Kuwaamini Mitume
· Ninawaamini
Mitume wa Allaah. Hakika Allaah Aliwateua Mitume kati ya wanadamu,
Akawafunulia Shari’ah Yake kwa njia ya wahyi, na Akawaamuru kuifikisha
kwa watu, na kwamba mwenye kuwatii ataingia peponi, na mwenye kuwaasi
ataingia motoni.
· Kisha Akawatilia nguvu kwa miujiza yenye kuonyesha ukweli wao ili iwasaidie mbele ya wakadhibishaji, na ili iwe ni hoja kwao.
· Na kwamba Mtume wa mwanzo ni Nuhu, na wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
· Na
kuwa Mitume hawa ni watu; wanakula, wanakunywa, wanaoa, wanaugua na
wanakufa. Wao ndio viumbe bora kabisa wa Allaah na wamehifadhiwa na
maasi.
· Mitume wa Allaah ni wengi. Allaah Amewataja baadhi yao
katika Qur-aan. Nao ni Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam), Ibrahim Khalili wa Ar-Rahmaan, Muusa aliyesemeshwa na Allaah,
‘Iysa Neno la Allaah na Nuuh. Hawa ndio Mitume wenye azma ya juu Rehma
na Amani ziwe juu yao.
Pia Ismaa’iyl, Is-haaq, Ya’aquub, Haaruun, Ayyuub, Yuunus, Sulaymaan,
Daawuud, Yahya, Zakariya, Huud, Swaalih, Yuusuf, Shu’ayb, Ilyaas, Luut,
Dhul-Kifl, Idriys, na wengi wengineo. Kati yao kuna Aliowahadithia Allaah katika Qur-aan na wengineo Hakuwahadithia.
· Jambo
la kwanza walilolilingania Mitume ni Tawhiyd, na jambo kubwa zaidi
walilolikataza ni shirki, na wote wamekuja na Uislamu na wito wa
Tawhiyd. Lakini shari’ah zao na mifumo ya kumwabudu Allaah Mtukufu
ilitofautiana kutokana na kutofautiana zama zao na nchi zao.
· Na
kwamba Mitume walitoa bishara ya kuja kwa Nabii Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakawaamrisha kaumu zao
kumwamini Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
atakapotumwa kwao.
· Tofauti
kati ya Rasuli (Mtume) na Nabii ni kuwa Rasuli ni yule aliyefunuliwa
shari’ah mpya na akaamrishwa kuifikisha kwa watu. Ama Nabii, ni yule
aliyetumwa ili kuithibitisha na kuipitisha shari’ah ya Rasuli
aliyemtangulia.
· Ninaamini
kuwa mbora wa Mitume mbele ya Allaah ni Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) toka kwa mwana wa Ismaa’iyli bin Ibraahiym
(‘Alayhimas Salaam). Allaah Amemtuma kwa watu wote, Akahitimisha Unabii
kwa Unabii wake, na Utume kwa Utume wake.
· Akamtilia
nguvu kwa miujiza, Akamfanya bora kuliko Mitume wote. Pia Ameufanya
Utume wake kuwa bora kuliko Utume wote uliotangulia, na shari’ah yake
kuwa bora kuliko shari’ah zinginezo zilizopita, na Kitabu chake Qur-aan
kuwa bora kuliko Vitabu vyote, na umati wake – Waislamu – kuwa bora
kuliko uma nyinginezo.
· Na Mola wake Akampa mambo ambayo Hakumpa yeyote katika Manabii waliomtangulia. Kati ya mambo hayo ni:
(1) Al-Wasiylah:
Nayo ndiyo daraja ya juu kabisa Peponi ambayo Allaah Amemwandalia Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
(2) Al-Kawthar: Nao ni mto Peponi wenye kupita chini ya ‘Arshi ya Ar-Rahmaan.
(3) Al-Hawdh: Ni sehemu ambayo Waislamu peke yao
ndio watakayokunywa siku ya Qiyaamah. Siku ambayo watu watapatwa na kiu
kikali, na jasho litawafika hadi magotini, viunoni na mabegani – kila
mmoja kwa mujibu wa amali yake – na Waislamu watakunywa hapo kwa vikombe
atakavyowapa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa
mikono yake mitukufu. Baada ya hapo hawatapatwa na kiu milele.
(4) Shafa’ah:
Ni makamu ya kuhimidiwa siku ya Qiyaamah. Hapo Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) ataomba shifaa kwa Allaah ili Waislamu
waliofanya maasi watolewe motoni, na hatobakia ndani ya moto yeyote
anayeshuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mtume
wa Allaah. Aliyefanya maasi hatosalia milele motoni, bali atatoka baada
ya kutakaswa na maasi yake.
· Aliyewaamini Manabii wote na wala hakumwamini Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi hatatoka motoni.
(5) Na
kwamba Allaah Amemnusuru na Akawanusuru askari wake na wafuasi wake
hadi siku ya Qiyaamah kwa kuzagaza hofu ndani ya nyoyo za maadui umbali
wa mwendo wa mwezi. Na hakuna Nabii yeyote aliyepewa hili kabla yake
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
(6) Na
ardhi imefanywa kwake na Waislamu kuwa Msikiti (sehemu ya kuswalia) na
twahara, na haikufanywa hivyo kwa Manabii waliomtangulia.
(7) Na Allaah Amemtuma kwa watu na majini wote, lakini Mitume wengine wametumwa maalumu kwa watu wao tu.
(8) Na kuwa yeye ndiye wa mwanzo kaburi lake kufunguka,
na ndiye mwombezi wa kwanza, na ndiye wa kwanza kupewa shifaa, na ndiye
wa kwanza kugonga mlango wa Pepo. Atakapougonga, mlinzi wa Pepo
Ridhwaan atamuuliza: "Nani wewe?" Atajibu: "Muhammad". Ridhwaan
atamwambia: "Kwako nimeamrishwa nisimfungulie yeyote kabla yako".
Na kati ya miujiza ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni:
1. Kupasuka mwezi.
2. Alilirejesha jicho la Qataadah lilipopofuliwa siku ya Uhud, macho yake yakarudi yakawa mazima kabisa.
3. Aliurejesha muundi wa Ibn Al-Hakam kama ulivyokuwa ulipovunjwa siku ya Vita vya Badr.
4. Aliutaka mti utamke shahada, nao ukatamka shahada mbili mara tatu mbele ya kafiri, naye akasilimu.
5. Kigogo cha mti alichokuwa akihutubia juu yake kililia wakati alipokiacha na hakikunyamaza mpaka alipoiweka mikono yake juu yake.
6. Alikifanya
chakula kidogo kuwa kingi baina ya mikono yake miwili, na wakaweza kula
na kushiba zaidi ya watu 80 chakula cha kujaa viganja viwili.
7. Aliyafanya
maji kidogo kuwa mengi siku ya Hudaybiyah wakati jeshi lilipobakiwa na
bakuli moja tu ya maji. Hapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) aliingiza mikono yake ndani, maji yakaanza kububujika kati ya
vidole vyake kama chemchemu, wakanywa maji Waislamu wote na wakatawadhia maji hayo. Walikuwa kiasi cha watu 1400.
8. Alipelekwa usiku hadi Msikiti wa Al-Aqswaa, na kisha alipandishwa hadi mbingu za juu na kukomea Sidrat Al-Muntahaa.
9. Alielezea
na kuhadithia habari za umma zilizotangulia na Manabii wao nailhali
yeye hana kisomo; hajui kusoma wala kuandika. Pia alielezea matukio
yatakayotokea siku za usoni kwa kufunguliwa Fursi na Rome,
kusambaratishwa ufalme wa Kisra aliyechanachana barua ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomtumia, pamoja na miujiza
mingineyo mingi.
10. Muujiza
mkubwa zaidi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni
Qur-aan Tukufu. Ni muujiza utakaosalia hadi siku ya Qiyaamah.
11. Kisha
Allaah Ameunyanyua utajo wake, Akaliandamisha jina la Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Jina Lake Subhaanahuu wa
Ta’alaa, na Akaifanya shahada ya kuwa hapana mola isipokuwa Allaah na
kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah kuwa ndio jambo la kwanza analoingia
nalo mja katika Uislamu,na jambo la mwisho analotoka nalo duniani. Basi
yeyote ambaye neno lake la mwisho litakuwa ni "Laa ilaaha illa Allaah",
ataingia peponi.
· Ni
wajibu wetu kwa upande wa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) tusilitangulize neno la kiumbe yeyote juu ya neno lake, au
rai ya yeyote hata kama ana sauti kwa watu. Na ikiwa watu watakutangulia kuhamia kwake, basi hama
wewe kwenda katika Sunnah yake katika kila jambo lako na wala usimfuate
mwingine zaidi yake. Ni wajibu wetu tushikamane sote pembezoni mwa amri
yake na tumtii, kwani mwenye kumtii Mtume, basi huwa amemtii Allaah.
· Na tusimwiite ila kwa kusema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tusiseme (Muhammad) basi.
· Tujipambe
kwa adabu zake, na tumwige katika hali zake zote; kulala kwake, kula
kwake, kutembea kwake, kuswali kwake, kufunga kwake, kutoa kwake sadaka,
na jihadi yake.
· Na tumpende zaidi kuliko nafsi zetu, wana wetu, wazazi wetu na watu wote.
· Na
tumpende kila yule anayempenda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) na kumfanya kiigizo chake, na tumchukie kila yule
anayemchukia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) na wala hawajibiki na shari’ah yake.
· Hivyo basi, ni lazima kwa Muislamu awapende Waumini, awanusuru, ajifananishe nao, ashughulikie mambo yao, asaidiane nao katika mambo ya kheri, na awafanye kuwa marafiki zake wa dhati.
· Ni
wajibu kwake awabughudhi makafiri na ukafiri wao, asiwatii, asiungane
nao dhidi ya Waislamu, wala asisaidiane nao katika ubatilifu wao, na
wala asishiriki katika sikukuu zao. Ni haramu kwake kuwadhulumu, na
linalotakiwa ni kuwatendea haki.
· Ni
wajibu wetu tuwapende Mama wa Waumini; Wakeze Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam), na tuwapende Maswahaba Wake (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani wao ndio bora wa watu baada
ya Manabii.
· Pia
ni wajibu wetu tuihuishe Sunnah yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam), tuidhihirishe shari’ah yake, na tubalighishe
ulinganio wake kwa watu wote. Kisha tusubiri maudhi na kero zinazotupata
katika kuyapigania hayo, kwani hayo hayaepukiki.
· Kwa
vile Mwenendo wa Allaah uliopita kwa viumbe Vyake unahukumia kuwa
hakuna Nabii au walii yeyote aliyelingania haki hii ila alifanyiwa uadui
na kuudhiwa.
· Zindukana
ndugu yangu Muislamu! Maudhi ya makafiri yasikufanye ukaiacha Dini
yako. Kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
aliudhiwa wakati Maswahaba walipokuwa wachache, nao pia waliudhiwa
wakafanya subira.
· Na wala usilegeze azma yako hata kama
watakwambia kuwa unayoyazungumza ni upuuzi, una misimamo migumu, au
umepitwa na wakati. Au wakisema: "ashachezewa akili huyo". Kwani wewe
una kiigizo chema kwa Mtume wa Allaah, yeye ashaambiwa mshairi na hata
mwendawazimu.
· Wala usisononeke ukiambiwa mpotevu mwenye siasa kali. Hii ndio tabia ya makafiri kwa Waumini.
وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ
“Na wanapowaona, husema hakika hawa bila shaka ni wapotevu.” [Al-Mutwafifiyn: 32]
· Ikiwa
watu wako makundi mawili, je haikutoshi wewe kuwepo katika kundi
aliloko Mtume wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam)?!
· Achana nao hao mpaka ifike siku ambayo dhalimu ataviuma vidole vyake aseme: "Laiti mimi ningeliifuata njia pamoja na Mtume".
· Wala usibabaike au kuchanganyikiwa kama
watakwambia kuwa wewe ni gaidi au mwovu, kwani hayo ndio madai ya
madhalimu dhidi ya Waumini duniani na akhera. Ni kuwa pale Malaika
watakapowaongoza kwenda Jahannamu wakisunukia, wataangalia humo kisha
waseme:
وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُم مِّنَ الْأَشْرَارِ
“Na watasema: Mbona hatuwaoni watu tuliokuwa tukiwazingatia kuwa ni katika waovu?” [Swaad: 62]
· Na hapa, Waumini (ambao makafiri wamewaita kuwa ni waovu) watawaita toka kwenye magorofa ya juu kabisa ya Firdaws wakiwaambia:
أَن قَدْ وَجَدْنَا مَا وَعَدَنَا رَبُّنَا حَقًّا
“…Hakika sisi tumeyakuta Aliyotuahidi Mola wetu kuwa ni kweli” [Al-A’araaf: 44]
(5) Kuamini Siku Ya Mwisho
· Ninaiamini
siku ya mwisho, nayo ni siku ambayo dunia (nyumba ya amali)
itamalizika, na akhera (nyumba ya malipo) itasimama, wema wakalipwa
Pepo, na waovu wakalipwa moto.
· Katika
siku ya Qiyaamah, mizani itawekwa, na kila mja atapewa kitabu chake.
Atakayepokea kitabu chake kwa mkono wake wa kuume, basi Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa pamoja naye Peponi. Ama
yule atakayepokea kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, basi atakuwa
pamoja na Fir’awn – laana ziwe juu yake – motoni.
· Swiraat
itawekwa, atakayefanikiwa kuivuka basi atafikia Peponi. Ama ambaye
kulabu zitamnyakua kutokana na amali zake mbovu, basi ataangukia motoni.
· Siku ya Qiyaamah ina dalili, ina alama ndogo na ina alama kubwa.
· Miongoni
mwa alama ndogo ni kupotea uaminifu, kukithiri mauaji, madaraka
kukamatwa kwa mabavu na mafasiki, na wasio na elimu kuzungumzia masuala
muhimu.
· Na
miongoni mwa alama kubwa ni kuibuka Al-Mahdi, kusimama ukhalifa wongofu
utakaokwenda juu ya misingi ya njia ya Utume kabla ya kutokea Qiyaamah,
na kudhihiri masihi muongo.
· Pia
kuteremka Iysa (‘Alayhis Salaam) ili awaongoze Waislamu, apigane na
makafiri, avunje vunje misalaba, aue nguruwe, na azikatae Dini zote
nyingine ila Uislamu tu.
· Basi haitobakia nyumba yoyote ya mjini au ya mashambani ila Allaah Ataiingiza Dini hii, kwa heshima ya mwenye nguvu, au kwa udhalili wa mnyonge.
· Vile
vile kutoka Yaajuuj na Maajuuj. Pia atatoka mnyama anayewasemesha watu,
na jua litachomoza toka Magharibi, Qur-aan itaondoshwa na mambo
mengineyo.
· Basi
yeyote atakayefanya amali ya uzito wa atomu ikiwa ni ya kheri au ni ya
shari, ataiona siku ya Qiyaamah ndani ya kitabu chake.
· Basi
harakieni kwenye mambo ya kheri kabla haujamalizika muda wa kusajiliwa
kwa kufa mja katika muda ambao haujui yeyote ila Allaah Pekee.
· Wakamwosha
jamaa zake, wakamkafini, wakamswalia, wakamzika. Kisha akajiwa na
Malaika wawili; Munkar na Nakiyr, wakamkalisha kitako na kumwuuliza:
"Nani Mola wako? Ni ipi Dini yako? Nani Nabii wako?"
· Ikiwa
atajibu kuwa: "Allaah ni Mola wangu, na Uislamu ndiyo Dini yangu, na
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye Nabii wangu
na Mtume wangu" – na Allaah Akamwezesha hilo – basi itafunguliwa katika kaburi lake harufu
ya rayhaan hadi peponi, akaona mashukio yake huko, na makasri yake na
ufalme wake. Hapo atashangilia kwa furaha kubwa, na kaburi lake litapanuliwa upeo wa macho.
· Na ikiwa ni katika makafiri, basi hatoweza kujibu chochote, kwani majibu wakati huo si kwa akili au werevu wa mtu.
· Bali
Allaah Huwathibitisha na kuwaimarisha watu wa imani wakati huo kwa yale
waliyoyatanguliza kati ya amali njema zilizosimamia juu ya Tawhiyd,
utekelezaji wa faradhi, kushiriki jihadi, kutenda mema, kuamrisha mema,
kukataza mabaya, kutoa sadaka, kusoma Qur-aan, kufunga siku za joto
kali, na kusimama kuswali muda mrefu usiku wa baridi kali.
· Ama akiwa ni katika makafiri, basi kaburi lake humbana hadi mbavu zake zikaingiana katika mwili wake, na kaburi lake huwa ni shimo katika mashimo ya motoni kutokana na amali zake mbaya.
· Basi jitahidi ndugu yangu Muislamu, kwani leo ni amali na hakuna hisabu, lakini kesho ni hisabu na hakuna amali.
· Na siku hiyo, Waislamu watiifu wataingia Peponi peke yao, kwa vile Allaah Hatoikubali Dini yoyote siku ya Qiyaamah isipokuwa Uislamu.
· Ndani
ya Pepo kuna neema ambazo hakuna sikio lililowahi kuzisikia, wala jicho
lililowahi kuziona, wala hata kuwaziwa katika akili ya mwanadamu. Neema
zake zitasalia milele wala hazitomalizika, na waliomo humo hawatakufa
milele. Neema kubwa zaidi ya zote humo, ni kuuangalia Uso wa Allaah Mola
wa walimwengu wote.
· Na
waasi, waovu na makafiri wataingia motoni. Ndani ya moto, kuna adhabu
Alizoziandaa Allaah kwa ajili ya makafiri. Ni adhabu zisizoweza
kuvumilika, kwani hata milima mirefu thabiti haiwezi kuzivumilia adhabu
hizi, na hao wataadhibiwa humo bila kupumzishwa.
· Na
humo, wafuasi wa matwaghuti wataomba adhabu iongezwe maradufu kwa
wakubwa wao waliowapoteza. Na hapo Allaah Ataamuru adhabu iongezwe
maradufu kwa wote.
· Basi
thibiti ndugu yangu Muislamu juu ya haki hii, wala usidanganyike kabisa
kuona kuwa wavunjaji shari’ah ni wengi zaidi, kwani ikiwa wewe utawatii
na ukawafuata wengi waliomo ardhini, basi watakupoteza wakutoe nje ya
njia ya Allaah. Nawe pita pamoja na wenye kupita kuelekea kwa Allaah.
· Kwani
kundi katika umma wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) litaendelea kuwa juu ya haki likiwa na nguvu, hawezi kuwadhuru
yeyote aliyekwenda nao kinyume au aliyewasaliti mpaka siku ya Qiyaamah.
· Basi
ni mbinu zipi za kuzijua ngazi hizo za kupanda juu, na mbinu zipi za
kuokoka na ngazi hizo za kuporomokea chini? Na ni mbinu zipi za
kuwafikia waliotangulia wenye kukurubishwa, na kujiweka mbali na
wapingaji wenye kuangamia? Bila shaka ni toba ya kweli ya kusahihisha na
kurekebisha yaliyopita, na amali njema za kuweka sawa umri uliosalia,
na kuweka nia ya kweli ya kunyooka na kutokengeuka.
· Basi kuwa pamoja na watu kwa kiwiliwili chako, ukiuza, ukinunua, ukioa na ukiiamirisha ardhi kwa yale Aliyokuhalalishia Allaah.
· Wala
moyo wako usifungamane na kitu chochote cha kidunia, bali nenda na moyo
wako pale ambapo unatakikana uwe, huko chini ya ‘Arshi ya Ar-Rahmaan,
na sujudu kwa moyo wako sijdah ambayo utaendelea kuisujudu hadi siku ya
Qiyaamah.
(6) Kuamini Qadhwaa Na Qadar
· Nako
ni kuamini kwamba Allaah Anayajua yote yaliyomo ulimwenguni, yote
yanayofanyika na yatakayotokea hadi siku ya Qiyaamah. Hata chembe ndogo
mno, Yeye Hakosi kuijua. Na kwamba Yeye Anavijua vitendo vya waja,
riziki zao, muda wao wa kuishi, na nani kati yao atakuwa wa peponi, na nani kati yao atakuwa wa motoni kabla Hajawaumba.
· Na
kwamba Allaah Ameyaandika makadirio haya katika Lawh Al-Mahfuudh kabla
hata Hajaziumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu hamsini, na kwamba Lawh
Al-Mahfuudh hii hakuna Malaika wa karibu au hata Nabii aliyetumwa
awezaye kuichungulia.
· Hata kiinitete kinapokuwa ndani ya tumbo la uzazi la mama yake, Allaah Huwaamrisha Malaika waandike kama
ni cha kike au kiume, waandike na riziki yake, amali yake, muda wake wa
kuishi na hatima yake (ima peponi au motoni). Pia waandike mazuri na
mabaya atakayokabiliana nayo.
· Kisha
unapoingia usiku wa cheo (Laylatul Qadr), huteremka makadirio ya mwaka
mzima toka Lawh al Mahfuudh kati ya ajali za watu, riziki zao, nani kati
yao atahiji mwaka huo na mengineyo. Katika usiku huo, hukadiriwa mambo ya mwaka mzima.
· Kisha huteremka makadirio ya kila siku kwa nyakati zake na watu wake, hapo Allaah Huwanyanyua watu na wengine Huwashusha.
· Na
tuamini kuwa Mapendeleo ya Allaah ndiyo yawayo, Alilolitaka huwa na
Asilolitaka haliwi. Allaah Hana wa kumshinda, na Yeye Ndiye Mwenye
kuzipindua nyoyo. Humwongoa Amtakaye kwa fadhila Zake na rehma Zake, na
Humpoteza Amtakaye kwa Uadilifu Wake na Hekima Yake, kwani Yeye Ndiye
Ajuaye zaidi nani anastahiki uongofu na nani anastahiki upotevu.
· Na Allaah Haulizwi yale Ayafanyayo lakini watu huulizwa.
· Na
tuamini kuwa Allaah Amekiumba kila kitu, na hakuna chembe yoyote ndogo
ulimwenguni isipokuwa Allaah Ameiumba na Akaumba kutikisika kwake na
kutulia kwake.
· Na kwamba Yeye Amewaumba waja na vitendo vyao, na kwamba Yeye Amewaumbia waja uwezo na mapendeleo yao ili wajichagulie wenyewe vitendo vyao.
· Na
kwamba Allaah Mtukufu Amewaamuru viumbe Wake wamtii, na Akawaahidi
kuwapa Pepo Yake wakifanya hivyo, na Amewakataza kumwasi Yeye, na
Akawapa onyo la kuwaingiza ndani ya moto Wake wakifanya hivyo, na wala
Hakuwakalifisha kazi isipokuwa ile ambayo wanaweza kuifanya. Na hapo
wakagawanyika makundi mawili: Waumini na makafiri; kwa hiari yao wenyewe, kwa mapendeleo yao wenyewe na kwa uwezo wao wenyewe, na yote hayo Allaah Amewaumbia.
· Na
kwamba thawabu na adhabu hutokana na kuifuata shari’ah, si kwa
kutangulia Elimu ya Allaah kwao. Basi yeyote atakayefanya amali yoyote
ya kheri ya uzito wa atomu, atalipwa kwayo. Na yeyote atakayefanya amali
yoyote ya shari ya uzito wa atomu, basi ataadhibiwa kwayo.
· Na
kwamba kinachozingatiwa ni mwisho wa matendo, na kwamba kila mja ni
mwenye kuendeshwa katika lile aliloumbiwa kati ya kufurahika Peponi au
kupata shakawa motoni.
· Na
kwa ajili hiyo, ni wajibu kwa mja aogope mwisho mbaya, na aendelee
daima kumwomba Allaah na amhitajie, Amhidi katika njia iliyonyooka, na
adumu kumwomba Amsaidie katika kumtii, na ajilinde Kwake na maasia, kwa
vile mja hana hila wala nguvu zozote za kuyafanya hayo ila kwa Uwezo wa
Allaah.
· Na
kwamba Waumini Huridhia Qadhwaa ya Allaah na Qadar Yake; ya kheri yake
na ya shari yake, katika misukosuko na katika furaha, na wana yakini
kuwa hawezi yeyote kuwanufaisha isipokuwa kwa Qadar ya Allaah, na wala
hawadhuru isipokuwa liwe lisha andikwa na Allaah.
· Na
mja hatopata utamu wa imani mpaka pale atakapojua kwamba lililompata
lisingekuwa la kumkosa, na lililomkosa lisingekuwa la kumpata.
· Na
mwisho naomba nikisema: "Ninamhimidi Allaah, na ninamwomba Aniingize
Peponi mimi na Waislamu wengine, na Anilinde na moto mimi na Waislamu
wengine". Aamiyn.
وصلى الله على محمد وعلى آله وصحبه وسلم
وآخر دعوانا أن الحمد لله رب العالمين
No comments:
Post a Comment