Maana Ya Funga
Maana
ya kufunga (Swawm) ni kujizuilia. Neno Swawm kwa maana ya kujizuilia
linaweza kutumika katika kujizuia kufanya jambo lolote la kawaida mtu
alilozoea kulifanya. Katika Qur-aan tunafahamishwa kuwa Bibi Maryam
baada ya kumzaa Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) alijizuia (alifunga) ili
asiseme na mtu neno lolote juu ya mtoto wake.
“...Na kama
ukimwona mtu yoyote (akauliza habari za mtoto huyu) sema: Hakika mimi
nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rehema ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema
na mtu.” (19: 26).
Katika
Uislamu kufunga (Swawm) ni kujizuilia kula, kunywa, kuvuta sigara,
kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na
masikio, kujizuia na kujamii, kujitoa manii kwa makusudi au kwa
matamanio na kujizuia kujitapisha kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala), kwa kipindi cha kati ya Al-fajri ya kweli mpaka kuingia
magharibi. Hii ndio maana ya nje ya Swawm katika Uislamu.
Kufunga katika Uislamu kuna maana ya ndani zaidi, ambayo kama haikufikiwa, kuzuilia kufanya vitendo hivyo vilivyoelezwa hakutakuwa na maana yoyote kwa mfungaji.
Kufunga
kwa maana ya ndani ni pamoja kujizuilia kutenda maovu yote
yaliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ili Swawm ya mfungaji
iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi kukizuilia (kukifungisha)
kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono na miguu-
pamoja na fikra na hisia zake na matendo aliyokataza Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala).
Funga
ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala); Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama vile kusengenya, kusema uwongo,
kugombana na kadhalika, funga ya masikio ni kujizuia kufanya yale yote
aliyoyaharamisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); funga ya miguu ni
kujizuilia na kuendea yale yote aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya
ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala). Ni katika maana hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam)anasema katika Hadithi zifuatazo:
Abu Hurayrah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah amesema:
“Yule
ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allaah
hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yaani
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hana haja na funga yake.” (Al-Bukhaariy).
Abu Hurayrah ameeleza kuwa Mtume wa Allaah amesema:
“Ni
wangapi wanaofunga lakini hawana funga ila kukaa na kiu tu ni wangapi
wanao swali usiku ambao hawana Swalah ila huambulia kupoteza usingizi
tu.” (Ad-Daarimiy).
Hadithi
hizi zinatuthibitishia kuwa ufungaji usioambatana na kujizuia na mambo
maovu na machafu, haumpatii mfungaji faida yoyote.
Umuhimu Wa Funga Katika Uislamu
Funga ya Ramadhaan ni miongoni mwa nguzo za Uislamu na ni faradhi kwa Waislamu kama inavyobainika katika aya ifuatayo:
“Enyi mlioamini! Mmeamrishwa kufunga (Swawm) kama walivyofaradhishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.” (2: 183)
Kama
ilivyo katika nguzo nyingine za Uislamu, mtu atakapoivunja makusudi
nguzo hii hatabakia kuwa Muislamu japo atajiita Muislamu na watu
wakaendelea kumwita hivyo. Katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas,
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Kuna
viungo vitatu vinavyomuunganisha Muislamu na dini ya Uislamu na yeyote
yule atakayevunja kiungo kimoja katika hivi atakuwa amekana Uislamu na
kuuawa kwani ni halali. Viungo hivi ni: Kushuhudia kuwa hapana Mola ila
Allaah, Kusimamisha Swalah tano na kufunga mwezi wa Ramadhaan.”
Katika Hadiyth nyingine Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Yeyote
yule atakaye acha makusudi kufunga siku moja ya mwezi wa Ramadhaan,
hawezi kuifidia siku hiyo hata akifunga kila siku katika umri wake wote
(uliobakia).” (Abu Daawuud)
Funga ni ibada maalum iliyo muhimu sana
katika kumuandaa mja kuwa mcha Mungu kwa kule kukataa kwake matamanio
ya kimwili. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa ukaribu wake
ameahidi malipo makubwa kwa wenye kutekeleza ibada hii ili iwe motisha
kwao ya kuwawezesha kutekeleza ibada hii kwa hima kubwa na kwa ukamilifu
unaotakikana kama tunavyojifunza katika Hadiyth zifuatazo:
Abu Hurayrah ameeleza kuwa Mtume wa Allaah amesema:
“Mwenye
kufunga Ramadhaan akiwa na imani na akawa na matumaini ya kupata malipo
kutoka kwa Allaah dhambi zake zote zilizopita husamehewa, Na mwenye
kusimama kwa Swalah (tarawehe) katika mwezi wa Ramadhaan akiwa na imani
na matumaini ya kupata malipo (kutoka kwa Allaah), dhambi zake zote
zilizopita zitasamehewa. Na yule atakayesimama (kwa Swalah) katika usiku
uliobarikiwa (Lailatul-Qadri) akiwa na imani na matumaini ya kupata
malipo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) dhambi zake zote
zilizotangulia zitasamehewa.” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Pia Abu Hurayrah ameeleza kuwa Mtume wa Allaah amesema:
“Kila
amali njema anayoifanya mwanaadamu italipwa mara kumi (Al-Qur-aan
6:160) mpaka kufikia mara mia saba (Al-Qur-aan 2:261). Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) amesema: Ila kufunga kwa sababu
funga ni kwa ajili Yangu, na ni mimi mwenyewe nitakayeilipa. Mwenye
kufunga anakata matamanio yake ya kimwili na anaacha chakula kwa ajili
yangu. Kwa mwenye kufunga kuna furaha mbili, furaha moja anaipata wakati
wa kufuturu na nyingine wakati atakapokutana na Mola wake. Na hakika
harufu ya mdomo wa mwenye kufunga ni bora mbele ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) kuliko harufu ya miski. Na funga ni ngao. Kwa hiyo atakayefunga
miongoni mwenu hataongea maneno ya upuuzi wala hatagombana. Kama itatokea achokozwe na yeyote, au mtu atakakupigana naye, na aseme: Nimefunga.” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Historia Ya Kufunga
Funga, kama ilivyo katika ibada nyingine kama
tulivyoona katika kusimamisha Swalah na kutoa zakat, imetekelezwa na
Mitume wote pamoja na umma zao. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
ametukumbusha hili wakati alipotupa amri ya kutekeleza ibada hii maalum,
kama tunavyorejea katika Qur-aan:
Enyi mlioamini! Mmeandikiwa (mmefaradhishiwa) kufunga kama walivyofaridhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu. (2:183)
Katika
historia tunajifunza kuwa, kila Mtume alipoondoka, baada ya kipindi
kupita, watu waliacha mafundisho yake na kuingia katika ushirikina.
Lakini bado tunakuta funga, japo si katika madhumuni na asili yake
iliyoachwa na Mitume wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), imebakia katika
jamii za kishirikina kwa kipindi chote cha historia. Hebu tuangalie
mifano michache ya dini za ushirikina ambapo funga, kwa maana ya
kushinda na njaa na kiu, imekuwa miongoni mwa ibada muhimu za dini hizo.
Jamii Ya Nabii Ibraahiym
Nabii
Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) aliinuliwa katika jamii ya washirikina.
Walikuwa wakiabudu jua, mwezi, nyota na masanamu chungu nzima
waliyoyachonga wenyewe. Pamoja na ushirikina wao huo walikuwa wakifunga
siku 30 mfululizo katika kila mwaka kwa heshima ya mwezi.
Wahindu (Hinduism)
Dini ya Kihindu ni miongoni mwa dini za kishirikina katika bara la India. Katika dini hii funga, ni kitendo kilichosisitizwa sana japo si lazima, katika siku maalum kama vile kupatwa kwa jua, kumbumbuku ya kuzaliwa mwanzilishi wa dini yao na kadhalika. Funga kwao ni kujizulia na kula na kunywa kuanzia alfajiri mpaka saa tisa mchana.
Mayahudi (Judaism)
Dini
ya Kiyahudi ni dini waliyoibuni Mayahudi baada ya Nabii Muusa (‘Alayhis
Salaam) ambapo walimfanya Uzairi mwana wa Mungu. Pamoja na hivyo
wachaji wa Kiyahudi walikuwa wakifunga Alhamisi na Jumatatu kama
kumbukumbu ya kwenda na kurudi kwa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) katika
safari yake ya Sinai kwenda kuchukua Taurati. Kutokana na kumbukumbu ya
historia, Nabii Musa alikwenda kwenye mlima Sinai siku ya Alhamisi na
kurejea siku ya Jumatatu baada ya siku arobaini kupita.
Pia
Mayahudi hufunga kwa saa 24 katika kila mwezi 10 Muharamu, kwa
kumbukumbu ya siku Wanaisraili (Mayahudi) walipookolewa na Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na udhalimu wa Fir’awn. Siku hii ambayo
hata Waislamu wamesuniwa kufunga huitwa siku ya ‘Ashuuraa.
Pamoja
na funga hizi, pia Mayahudi wana tabia ya kufunga mara kwa mara
kulingana na haja. Kwa mfano mtu anaweza kuamua kufunga siku kadhaa kama
kumbukumbu ya matukio fulani katika maisha yake, au anaweza kufunga
funga kama kitubio cha madhambi yake, au anaweza kufunga wakati akiwa na matatizo ili kupata huruma ya Mungu.
Ukiacha
siku ya ‘Ashuuraa ambapo funga huchukua saa 24, funga za Mayahudi
huanza alfajiri na huishia pale inapojitokeza nyota ya kwanza usiku.
Wakristo
Dini
ya Ukristo imebuniwa baada ya Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam). Katika
dini hii Nabii ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) amefanywa mwana wa Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) na kwamba yeye ndiye mkombozi wa Wakristo. Pamoja
na hivyo, Wakristo wanakiri kuwa kufunga ni kitendo cha uchaji - katika
dini yao. Wakristo wa mwanzo walikuwa wakifunga siku 40 mfululizo kasoro siku za Jumapili kama kumbukumbu ya siku zile alizofunga Yesu (Nabii ‘Iysaa ‘Alayhis Salaam) kama inavyobainishwa katika Biblia.
Historia inatuonyesha vile vile kuwa funga hizi za Washirikina zimetofautiana sana
katika mfumo na funga ya Kiislamu aliyoiamrisha Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala). Ambapo Waislamu wakifunga hujizuia kula, kunywa na kujamii
mchana kutwa kuanzia alfajiri mpaka kuchwa kwa jua, funga za washirikina
zilichukua mifumo mbalimbali. Wengine walijizuilia kula na kunywa tu
lakini waliendelea kujamii, wengine walijizulia kunywa na kula kuanzia
alfajiri mpaka saa 9 alasiri, wengine walijizulia kula aina fulani tu ya
chakula kama vile nyama, wengine walijizulia kwa kunywa tu maji yaliyochanganywa na chumvi au maji ya ndimu, na kadhalika.
No comments:
Post a Comment