Saturday, July 6, 2013

‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jama’aah Kuhusu Kutokudumu Milele Waislamu Motoni



Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah wanaamini kwamba baadhi ya Waislamu wataingia Peponi bila ya kufanyiwa hesabu au kupewa adhabu. Wengine wataingia Peponi baada ya kufanyiwa hesabu, Wengine wataingia Peponi baada ya kuadhibiwa motoni kama Anavyotaka Allaah kisha Atawatoa humo.

Kutolewa motoni kisha kuingizwa Peponi hakutawasababishia huzuni au dhiki Peponi kwasababu Pepo ni makazi ya raha tupu. Kama ilivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah, watapata kila walichokipata wakaazi wengine wa Peponi.

Hakuna dalili inayoashiria kwamba watu hao watakuwa na hisia za majuto baada ya kuingia kwao Peponi kutokana na adhabu watakazozipata motoni.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutajia hali zao zitakavyokuwa baada ya kutolewa motoni kama ifutavyo:
1.     Watatumbukizwa Kwenye Mto Wa Uhai Wabadilike Kuwa Wapya

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
 ((إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ وَأَهْلُ النَّارِ النَّارَ يَقُولُ اللَّهُ : مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ حَبَّةٍ مِنْ خَرْدَلٍ مِنْ إِيمَانٍ فَأَخْرِجُوهُ، فَيَخْرُجُونَ، قَدْ امْتُحِشُوا، وَعَادُوا حُمَمًا، فَيُلْقَوْنَ فِي نَهَرِ الْحَيَاةِ ، فَيَنْبُتُونَ كَمَا تَنْبُتُ الْحِبَّةُ فِي حَمِيلِ السَّيْلِ)) وَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((أَلَمْ تَرَوْا أَنَّهَا تَنْبُتُ صَفْرَاءَ مُلْتَوِيَةً)) رواه البخاري ومسلم
 
((Watu wa Peponi watakapoingia Peponi watapaoingia Peponi na wa motoni watakapoingia motoni, Allaah Atasema [kuwaambia Malaika]: “Yeyote aliyekuwa na Iymaan moyoni mwake, uzito wa chembe cha atomu, mtoeni!” Watamtoa humo, watatoka kama kwamba ni mifupa iliyounguzwa na watabadilika kuwa makaa. Watatumbukizwa katika mto wa uhai, kisha watakuwa [kimaumbile] humo kama mfano wa mbegu zinapomea katika ufa [mwatuko] wa mafuriko)). Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Je huwaoni wanavyomea [wanavyokuwa kimaumbile] manjano na kupinda?)). [Al-Bukhaariy na Muslim].

2.     Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba watabadilika watakapotolewa motoni.

Imesimuliwa toka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusu Jahannamiyuwn (watu wa motoni):
((يَخْرُجُونَ مِنْ النَّارِ بَعْدَ أَنْ يَكُونُوا فِيهَا، فَيَخْرُجُونَ كَأَنَّهُمْ عِيدَانُ السَّمَاسِمِ، فَيَدْخُلُونَ نَهَرًا مِنْ أَنْهَارِ الْجَنَّةِ فَيَغْتَسِلُونَ فِيهِ فَيَخْرُجُونَ كَأَنَّهُمْ الْقَرَاطِيسُ)) رواه مسلم  
 
((Watatolewa motoni baada ya kuweko humo. Kisha watatoka kama kwamba ni matawi ya chembe za ufuta. Kisha wataingia katika Mto miongoni mwa mito ya Peponi ambako wataoga kisha watatoka [weupe] humo kama karatasi)). [Muslim].

Imaam An-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Ufuta imekusudiwa chembe za ufuta maarufu zinazotoa mafuta ya ufuta”. 
Imaam Abu as-Sa’adaat al-Mubaarak bin Muhammad bin ‘Abdil-Kariym al-Jazariyy anayejulikana kama: Ibn Al-Athiyr (Rahimahu Allaah) amesema: “Inamaanisha - na Allaah Anajua zaidi – kwamba matawi ya ufuta yanapokusanywa na kuachwa juani ili mbegu zake zikusanywe, hubadilika kuwa membamba na meusi kama kwamba zimeunguzwa. Ndio wakafananishwa watu hawa. Kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). ((Kisha watatoka humo kama karatasi)) wamefananishwa kama karatasi kwa sababu watakuwa weupe mno baada ya kuoga mtoni na weusi wote waliokuwa nao utaondoshwa.” [Sharh Muslim].

Kadhaalika, imesimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((يَخْرُجُ مِنْ النَّارِ بِالشَّفَاعَةِ كَأَنَّهُمْ الثَّعَارِيرُ، قُلْتُ: مَا الثَّعَارِيرُ؟ قَالَ: الضَّغَابِيسُ)) البخاري
((Watatoka motoni kwa sababu ya shafa’ah (uombezi) wakiwa kama matango)). [Al-Bukhaariy].
Al-Haafidhw Ibn Hajr al-‘Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: “Kuhusu matango madogo, makusudio ni, kama kitu cheupe na kidogo”

Tanbihi:
Sifa ya weupe huu unakusudiwa vile watakavyokuwa baada ya kukua (kumea) [Fat-h al-Baaariy (11/429)]. Lakini mwanzo watakapotoka motoni watakuwa kama makaa kama inavyoelezea Hadiyth ifuatayo:

3.     Watakua kama Lulu kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atawaruzuku Radhi Zakke na Hatawaghadhibikia tena.

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((فَيَقُولُ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ : شَفَعَتْ الْمَلَائِكَةُ، وَشَفَعَ النَّبِيُّونَ، وَشَفَعَ الْمُؤْمِنُونَ، وَلَمْ يَبْقَ إِلَّا أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ، فَيَقْبِضُ قَبْضَةً مِنْ النَّارِ فَيُخْرِجُ مِنْهَا قَوْمًا لَمْ يَعْمَلُوا خَيْرًا قَطُّ قَدْ عَادُوا حُمَمًا، فَيُلْقِيهِمْ فِي نَهَرٍ فِي أَفْوَاهِ الْجَنَّةِ يُقَالُ لَهُ " نَهَرُ الْحَيَاةِ " فَيَخْرُجُونَ كَمَا تَخْرُجُ الْحِبَّةُ فِي حَمِيلِ السَّيْلِ ... قَالَ : فَيَخْرُجُونَ كَاللُّؤْلُؤِ فِي رِقَابِهِمْ الْخَوَاتِمُ ، يَعْرِفُهُمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ، هَؤُلَاءِ عُتَقَاءُ اللَّهِ الَّذِينَ أَدْخَلَهُمْ اللَّهُ الْجَنَّةَ بِغَيْرِ عَمَلٍ عَمِلُوهُ وَلَا خَيْرٍ قَدَّمُوهُ ، ثُمَّ يَقُولُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ فَمَا رَأَيْتُمُوهُ فَهُوَ لَكُمْ، فَيَقُولُونَ : رَبَّنَا أَعْطَيْتَنَا مَا لَمْ تُعْطِ أَحَدًا مِنْ الْعَالَمِينَ، فَيَقُولُ لَكُمْ عِنْدِي أَفْضَلُ مِنْ هَذَا ، فَيَقُولُونَ: يَا رَبَّنَا أَيُّ شَيْءٍ أَفْضَلُ مِنْ هَذَا، فَيَقُولُ  رِضَايَ فَلَا أَسْخَطُ عَلَيْكُمْ بَعْدَهُ أَبَدًا)) رواه البخاري  ومسلم 

((Allaah Atasema [Peponi]: “Malaika wameshaombea shafa’ah, Mitume wameshaombea shafa’ah, Waumini wameshaombea shafa’ah, hakuna aliyebakia isipokuwa Mwingi wa Rahma, Mwenye Kurehemu kuliko wote wanaorehemu.” Kisha Atateka kutoka motoni na Atatoa watu wasiopata kufanya jema lolote [duniani] na ambao wamebadilika kuwa makaa. Atawatumbukiza katika Mto ulio kingoni kwa Peponi unaoitwa ‘Mto wa Uhai’ watatoka humo kama zinavyotoka mbegu katika ufa wa mafuriko. Kisha watatoka wakiwa kama lulu wakiwa na mapambo shingoni mwao na watu wa Peponi watawatambua. Hawa ni waliofidiwa [waliokombelewa] na Allaah Akawaingiza Peponi bila hata ya kuwa wametenda ‘amali njema au kheri yoyote waliyoitanguliza. Kisha Atasema: “Ingieni Peponi, mtakayoyaona humo ni yenu.” Watasema: “Ee Mola wetu, Umetupa ambayo Hujapatapo kumpa yeyote kati wa walimwengu.” Atasema: “Mtapata kutoka Kwangu yaliyo bora kuliko haya” Watasema: “Ee Mola wetu! Kitu gani tena kitakachokuwa bora kuliko haya?” Atasema: “Radhi Zangu kwani Sitoghadhibika tena nanyi kamwe.”)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

Hii ni Hadiyth muhimu ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametaja daraja ya juu kabisa itakavyokuwa ya watu watakaotolewa motoni ambao Mola wao Atawaruzuku, karama, heshima, na fadhila zikiwemo:
·         Kutumbukizwa katika Mto wa Uhai ili wakuwe (waumbike) kama wapya.

·         Kutoka katika Mto kama kwamba lulu wakiwa wamevaa mapambo shingoni mwao.

·         Kupewa kila watakachokiona Peponi.

·         Kudhania kwao kutokana na kheri na baraka na furaha ya hali ya juu watakayoipa kwamba Allaah Amewakirimu kwa jambo Hajapatapo kumkirimu yeyote mwengine.

·         Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atawaruzuku Radhi Zake na Hatowaghadhibikia tena kamwe.

Daraja ambazo Allaah Atawakirimu watu watakoingia Peponi zimethibitika katika usimulizi ufuatao wa Hadiyth:

Imesimuliwa kutoka kwa ‘Abdulllaah bin Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
  ((إِنِّي لَأَعْلَمُ آخِرَ أَهْلِ النَّارِ خُرُوجًا مِنْهَا وَآخِرَ أَهْلِ الْجَنَّةِ دُخُولًا، رَجُلٌ يَخْرُجُ مِنْ النَّارِ كَبْوًا فَيَقُولُ اللَّهُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَيَأْتِيهَا فَيُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهَا مَلْأَى، فَيَرْجِعُ فَيَقُولُ: يَا رَبِّ وَجَدْتُهَا مَلْأَى، فَيَقُولُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَيَأْتِيهَا فَيُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهَا مَلْأَى، فَيَرْجِعُ فَيَقُولُ: يَا رَبِّ وَجَدْتُهَا مَلْأَى، فَيَقُولُ: اذْهَبْ فَادْخُلْ الْجَنَّةَ، فَإِنَّ لَكَ مِثْلَ الدُّنْيَا وَعَشَرَةَ أَمْثَالِهَا)) - أَوْ: ((إِنَّ لَكَ مِثْلَ عَشَرَةِ أَمْثَالِ الدُّنْيَا - فَيَقُولُ: تَسْخَرُ مِنِّي)) - أَوْ: ((تَضْحَكُ مِنِّي - وَأَنْتَ الْمَلِكُ)) فَلَقَدْ رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ضَحِكَ حَتَّى بَدَتْ نَوَاجِذُهُ، وَكَانَ يَقُولُ: ((ذَاكَ أَدْنَى أَهْلِ الْجَنَّةِ مَنْزِلَةً)) رواه البخاري  ومسلم  

((Nawajua watu wa mwisho kabisa watakaotoka motoni, na watu wa mwisho kabisa watakaoingia Peponi. Atakuwa ni mtu atakayetoka akitambaa kutoka motoni kisha Allaah Atamwambia: “Nenda na ungie Peponi” Ataifikia lakini atadhania kwamba imejaa. Atarudi na kusema: “Mola wangu! Nimeikuta imejaa!” Allaah Atasema: “Nenda ingia Peponi” Atafikia lakini atadhania kwamba imejaa. Atarudi na kusema: “Mola wangu! Nimeikuta imejaa!” Allaah Atasema: “Nenda ingia Peponi, kwani utapata mfano wa dunia na mara kumi yake”)) Au: ((“Utapata mfano wa mara kumi ya dunia” Atasema [mja]: “Je unanifanyia masikhara?)) Au: ((“Je unanidhihaki na hali Wewe ni al-Malik?”)). Nikamuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akicheka mpaka magego yake yakadhihirika na huku akisema: ((Huyo ndiyo mtu wa daraja ya chini kabisa Peponi)). [Al-Bukhaariy na Muslim].

4.     Watajulikana kama ni Al-Jahannamiyuwn (watu wa motoni) au ‘Utaqaa al-Jabbaar’ (waliokombolewa na Mwenye Ujabari) Kisha wataondoshewa jina hilo.
Jina la Al-Jahannamiyuwn ni wingi wa Jahannam yaani moto. Ina maana kwamba Allaah Amewakomboa motoni.

Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((يَخْرُجُ قَوْمٌ مِنْ النَّارِ بَعْدَ مَا مَسَّهُمْ مِنْهَا سَفْعٌ فَيَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ فَيُسَمِّيهِمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَهَنَّمِيِّينَ)) رواه البخاري 

((Miongoni mwa watu watatolewa motoni baada ya miale yake imewagusa [na kuwabadilisha rangi] kisha wataingizwa Peponi. Na watu wa Peponi wataiwa al-Jahannamiyuwn)). [Al-Bukhaariy].

Na pia kauli nyingine kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): kwa Hadiyth iliyokusanywa na Imaam Ahmad:
((... فَيَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ فَيَقُولُ لَهُمْ أَهْلُ الْجَنَّةِ: هَؤُلَاءِ الْجَهَنَّمِيُّونَ! فَيَقُولُ الْجَبَّارُ: بَلْ هَؤُلَاءِ عُتَقَاءُ الْجَبَّارِ عَزَّ وَجَلَّ)) 

((…wataingia Peponi na watu wa Peponi watasema: “Hawa ni Al-Jahannamiyuwn lakini Al-Jabbaar [Mwenye Ujabari] Atasema: “Hapana! Bali wao ni waliokombolewa na Al-Jabbaar ‘Azza wa Jalla)). [Imepewa daraja ya Swahiyh na Ibn Mandah katika ‘al-Iymaan’ (2/847), Ibn Khuzaymah (2/710) na Al-Albaaniy katika ‘Hukm Taarik As-Swalaah’ (uk. 33).

Ibn Hibbaan amesimulia kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu):
((فَيُسَمَّوْنَ فِي الْجَنَّةِ الْجَهَنَّمِيِّينَ مِنْ أَجْلِ سَوَادٍ فِي وُجُوهِهِمْ، فَيَقُولُونَ : بَّنَا أَذْهِبْ عَنَّا هَذَا الاسْمَ ، قَالَ : فَيَأْمُرُهُمْ فَيَغْتَسِلُونَ فِي نَهْرِ الْجَنَّةِ , فَيَذْهَبُ ذَلِكَ مِنْهُمْ)).

((Wataitwa humo Peponi: “al-Jahannamiyyuwn” kutokana na weusi katika nyuso zao. Watasema: “Mola wetu! Tuondoshee jina hili!”)) Akasema: ((Kisha Atawaamrisha waoge katika Mto wa Peponi, wataondoshewa hilo [Jina])). [Imepewa daraja ya Swahiyh na Ibn Hibbaan (16/457) na pia Ash-Shu’ayb al-‘Arnauwtw].

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kwamba mchovyo mmoja tu wa Peponi utamfanya Muislamu asahau tabu zote alizozokabiliana nazo duniani, itakuwaje basi ikiwa Pepo ndio makazi yake ya milele?

Imesimuliwa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((يُؤْتَى بِأَنْعَمِ أَهْلِ الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَيُصْبَغُ فِي النَّارِ صَبْغَةً ثُمَّ يُقَالُ : يَا ابْنَ آدَمَ هَلْ رَأَيْتَ خَيْرًا قَطُّ ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ نَعِيمٌ قَطُّ ؟ فَيَقُولُ : لَا وَاللَّهِ يَا رَبِّ ، وَيُؤْتَى بِأَشَدِّ النَّاسِ بُؤْسًا فِي الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيُصْبَغُ صَبْغَةً فِي الْجَنَّةِ فَيُقَالُ لَهُ : يَا ابْنَ آدَمَ هَلْ رَأَيْتَ بُؤْسًا قَطُّ ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ شِدَّةٌ قَطُّ ؟ فَيَقُولُ : لَا وَاللَّهِ يَا رَبِّ مَا مَرَّ بِي بُؤْسٌ قَطُّ، وَلَا رَأَيْتُ شِدَّةً قَطُّ)) رواه مسلم

((Mtu aliyeneemeka kabisa duniani ambaye ni miongoni mwa watu wa motoni ataletwa Siku ya Qiyaamah na atachovywa mara moja motoni kisha ataulizwa: “ee mwanadamu! Umepatapo kuona zuri lolote?  Umewahi kupata raha yoyote?” Atasema: “Hapana Mola wangu!” Kisha ataletwa mtu aliyepata shida kabisa duniani akiwa miongoni mwa wa watu wa Peponi atachovywa Peponi ataambiwa: “Ee mwanadamu! Je umepatapo kuona ubaya wowote? Je imekupitia shida yoyote?” Atasema: “Hapana Mola wangu! Sijapatapo kuona ubaya wowote wala haijanipitia shida yoyote.”)) [Muslim].

Dalili nyingine kwamba mchovyo mmoja wa neema za Pepo utamuondoshea tabu zote za awali, mpaka tabu za kuadhibiwa motoni. Hivi ni kuhusiana na yaliyotajwa kuhusu kubadilishwa kwake mtu baada ya kutumbukizwa katika ‘Mto wa Uhai’ ni katika mapokezi yaliyosimuliwa na Imaam Muslim (2836) kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaah ‘anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:

((مَنْ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ يَنْعَمُ لَا يَبْأَسُ لَا تَبْلَى ثِيَابُهُ وَلَا يَفْنَى شَبَابُهُ))

((Atakayeingia Peponi atastarehe na hatokuwa na kuhuzunika, nguzo zake hazitochakaa wala ujana wake hautatoweka [hatozeeka])).

Neema hiyo inathibitisha kwamba atakayeingizwa Peponi ataondoshewa tabu zote na inamaanisha kwa ujumla kila atakayeingia Peponi, ikiwa ni mwenye kuingizwa motoni kwanza au hakuingizwa.

Al-Qaadhwiy amesema: “Kinachomaanishwa hapa ni kwamba Pepo ni makazi ya kuthibiti na neema ambazo hazitobadilika au kuathirika kwa tabu zozote au ufisadi.”  [Tuhfat al-Ahwadhi (7/194)]. 

Kwa sababu hizo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuambia hali za watu wa Peponi watakapoingia:  
((وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ* الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِنْ فَضْلِهِ لا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ))

((Na watasema: “AlhamduliLLah – Himdi Zote ni za Allaah [Pekee] Ambaye Ametuondoshea huzuni [zote]. Hakika Mola wetu bila shaka ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kupokea Shukurani. Ambaye Ametuweka nyumba za makazi kwa Fadhila Zake, haitugusi humo tabu wala haitugusi humo machovu)). [Faatwir: 34-35].

‘Allaamah As-Sa’diy (Rahimahu Allaah) amesema: “Inamaanisha maskani ya makazi ya milele, maskani ambayo mtu atataka kuishi milele kwa sababu ya mazuri mengi yaliyomo humo na kwa sababu ya starehe zinazodumu na kwa sababu ya kutokuweko cha kuondosha starehe hizo.

Na hayo ni kutokana ((kwa Fadhila Zake)) kwetu na Neema Zake, si kwa sababu ya ‘amali zetu, kwani ingelikuwa si Fadhila Zake, tusingelifikia tulivyofikia.
((haitugusi humo tabu wala haitugusi humo machovu)) yaani, hakutakuweko na machofu katika miili yetu, nyoyo au nguvu, wala katika raha nyingi.  Hii inaonyesha kwamba Allaah Atafanya miili yao iumbike vizuri upya na Atawafanyia kila sababu za kuwafanyia makazi yao yawe ni yenye raha za kudumu, ili wasiguswe na tabu au wahka wala huzuni.” [Tafsiyr As-’Sa’dy 689].


Na Allaah Anajua zaidi

MOTO AN NAAR


Baada ya kusoma kuhusu Pepo, leo tutazama upande wa pili ambao ni moto. Tutazame habari zake na balaa zake.

Katika Qur-aan na Hadiyth kumetajwa moto kuonesha mazingira mabaya watakayoshukiwa watu waovu, Waliompinga Allaah na kuendesha maisha yao ya hapa duniani kinyume na kanuni na taratibu alizoziweka Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

Maisha ya motoni ni kinyume na maisha ya Peponi ambayo picha yake tumeshaiona. Tunafahamishwa katika Qur-aan kuwa motoni kuna Daraja au Milango saba, na kila mlango iko sehemu iliyogawanywa.

“Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipoahidiwa wote. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. [Suratu-Al-Hijr:43-44].

Daraja hizi za moto zimepewa majina kama tusomavyo katika Qur-aan:


Jahannam:

Katika Aayah nyingi jina hili limetumiwa, Kama jina la ujumla la maisha ya Motoni. Kama katika baadhi ya Aayah hizi Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu” [Al-Anbiyaa: 98].
“…kisha Tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam, wapige magoti (hapo)” [Maryam: 68].


Lahab: Moto wenye muwako mkubwa kabisa.

“Atauingia Moto wenye mwako”. [Suratul-Masad: 3].


Hutwamah: Moto wa kuvunja vunja-Moto uliowashwa kwa ukali.

“Hasha! Atavurumishwa katika Hutwamah”. [Suratul-Humazah: 4].


Sa’iyra: Moto mkali wa kuunguza.

“Basi wapo miongoni mwao waliyoyaamini, na wapo walioyakataa. Na Jahannam yatosha kuwa ni (Sa’iyra) moto wa kuwateketeza”.  [Suratun-Nisaa: 55].


Saqara: Moto unaobabua.

“Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar”. [Suratul-Mudaththir: 26].


Jahiym: Moto mkali.

”Na Jahiym itadhihirishwa kwa wapotovu”. [Suratush-Shu’araa: 91].

Basi bila ya shaka mtaiona Jahiym”. [Suratut-Takaathur: 6].


Haawiyah: Moto uokwao kwa ukali.

“Huyo maskani yake yatakuwa Moto wa Haawiyah”. [Suratul-Qaari’ah: 9].


Wakosaji wataingia katika aina hizi za Moto kulingana na makosa yao. Kwa ujumla aina yoyote ya moto ulioandaliwa kwa ajili ya makafiri hata ukiwa na daraja ya chini namna gani, Utakuwa ni mkali usio na mfano na usiovumilika hata kwa  muda mfupi sana kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anavyotufahamisha:

“Hakika hiyo (Jahannaam) ni kituo kibayana mahali (pabaya kabisa) pa kukaa (hata kwa muda mfupi.” [Suratul-Furqaan: 66]

Pia tuone anavyotufahamisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kiwango wa adhabu ya motoni.

Nuuman bin Bashiyr amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema; “Hakika atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa katika wakazi wa motoni ni yule atakayekuwa na viatu vya moto, Kwa moto huu, (wa miguu utachemsha ubongo wake kama maji yachemkavyo kwenye birika). Haitaonekana kuna kiwango cha chini kabisa cha adhabu.” (Al-Bukhaariy na Muslim).


Kwa ujumla moto wa adhabu alioandaa Allaah (Subhaananu Wa Ta’ala) kwa watu waovu ni mkali sana.

Ndani ya mazingira ya motoni patakuwa na miti michungu, Na mti maarufu kwa uchungu ni “Zaqquum”. Tunapata maaelezo kamili ya mti wa “Zaqquum” ambao umeenea katikati ya Jahannam na watakaostahiki kuula ni katika Aayah zifuatazo:

“Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqquum?

Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa waliodhulumu.

Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Jahannam.

Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashetani.

Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.

Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.” [Asw-Swaffaat: 62-67].


Pia katika mazingira ya motoni patakuwa na nyoka na n’ge wakubwa wenye sumu kali watakaowauma wakazi wa humo kama sehemu ya adhabu yao kama tunavyo fahamishwa katika Hadiyth ifuatayo:

‘Abdullaah bin Haarith bin Jaazin amesimulia kuwa  Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa: “kuna nyoka huko motoni wakubwa kama ngamia, Mmoja wao akikuuma mara moja uchungu wake hubakia kwa miaka arubaini. Kuna nnge huko motoni wakubwa kama nyumba, Mmoja wao akimuuma mtu uchungu wake utabakia kwa muda wa miaka arubaini.” [Ahmad].

Kwa vyovyote itakavyokuwa maisha ya motoni yatakuwa magumu sana kwa wakazi wake. Chakula chao kitakuwa cha moto wa kuunguza kila kitu tumboni, Mavazi yao yatakuwa ya moto, Kinywaji chao cha moto kitakachochemsha matumbo yao kama maji yachemkavyo kwenye sufuria ya shaba. Picha halisi ya mazingira ya motoni, Maisha ya wakazi wake na sifa zinazowafanya wastahiki kuingia humo. Tutazame baadhi tu ya Aayah hapa:

“Nao husema (kwa maskhara): Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi.

Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi.

Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.

Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu.

Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.” [As-Sajdah: 12-14].


Na katika Suratun-Nabaa tunaona:

“Hakika Jahannamu inangojea!

Kwa walio asi ndio makaazi yao,

Wakae humo karne baada ya karne,

Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji,

Ila maji yamoto sana na usaha,

Ndio jaza muwafaka.

Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu.

Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu.

Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika.

Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu!” [An-Nabaa: 21-30].


Na katika Suratul-Fajr:

“Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!

Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.” [Suratul-Al-Fajr: 23-26].

Kama tunavyoona Aayah hizi kwa ujumla zinatilia mkazo wale watakaostahiki adhabu ya motoni ambao ni wanaadam na majini waovu walioendesha maisha yao hapa duniani kwa kibri kinyume na utaratibu uliowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Ndugu katika Iymaan, tujilinde na adhabu hiyo kali kabisa ya moto, adhabu isiyo na mfano na moto usioweza kulinganishwa na moto wa aina yoyote uliopo hapa duniani. Tujikinge sisi na familia zetu kwa kufanya ‘amali njema zitakazomridhisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’ala) na tuzitekeleze kwa njia safi na sahihi kama tulivyoelekezwa kwazo na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Tunamuomba Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Atukinge na adhabu ya moto, sisi na vizazi vyetu na Waislam wote kwa ujumla, Aamiyn.