Wednesday, February 4, 2015

SAJDA YA KUSAHAU


Imethibiti kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amewahi kusahau ndani ya Sala, na imethibiti pia kuwa aliwahi kusema:
"Hakika mimi ni mwanadamu, ninasahau kama mnavyosahau, kwa hivyo ninaposahau nikumbusheni."

Hukmu
Sajda ya kusahau (Sujuud al Sahau) inasujudiwa mara mbili kabla ya kutoa salamu au baada yake, na imesihi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alifanya namna zote mbili.
Katika hadithi sahihi, amesema Abu Said al Khudary  (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
"Mmoja wetu akitia shaka ndani ya sala yake akawa hana uhakika amesali rakaa tatu au nne, basi aache kutia shaka na ahesabu zile alizo na uhakika nazo, kisha asujudu sajda mbili kabla ya kutoa salamu."
Sharhi:
Maana ya kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema: "Aache kutia shaka na ahesabu zile alizo na uhakika nazo" ni kuwa; Mtu anapokuwa ndani ya sala akatia shaka iwapo yupo katika rakaa ya tatu au ya nne, huwa na hakika kuwa wakati ule kesha Sali rakaa tatu, isipokuwa ile ya nne ndiyo anayoitilia shaka. Kwa ajili hiyo anatakiwa ahesabu zile tatu tu alizo na uhakika nazo – na asali rakaa moja tu kwa ajili ya kukamilisha rakaa nne, kisha asujudu sajda ya kusahau.

Sababu za kusujudu
Mtu anaposahau akatoa salamu kabla ya kukamilisha sala;
Na hii inatokana na hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibni Siriyn kutoka kwa Abu Hurairah  (Radhiya Llahu anhu) kuwa amesema:
"Alitusalisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) sala mojawapo za mchana, (adhuhuri au alasiri) akasali rakaa mbili kisha akatoa salamu kisha akainuka na kukaa akiwa ameegemea nguzo akionesha dalili ya kughadhibika, na Abubakar na Omar  (Radhiya Llahu anhu) walikuwepo, na alikuwepo pia mtu mmoja anayejulikana kwa jina la 'Dhul Yadayni' aliyeuliza:
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, umesahau au umefupisha?"
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
"Sijasahau wala sijafupisha.", kisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akauliza:
"Ni kweli maneno anayosema Dhul Yadayni?"
Wakamwambia:
"Ndiyo."
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akainuka, akatangulia mbele (mahali aliposimama alipokuwa akisalisha), kisha akakamilisha rakaa mbili alizozisahau, kisha akatoa salamu, kisha akasema: "Allahu akbar", kisha akasujudu sajda kama ya kawaida au ndefu zaidi kidogo, kisha akakaa, kisha akasema tena: "Allahu akbar,kisha akasujudu tena kama alivyosujudu mwanzo kisha akakaa.
Bukhari na Muslim

Hadithi nyingine
Kutoka kwa Ataa amesema: "Mwana wa Al Zubair  (Radhiya Llahu anhu) alisalisha sala ya magharibi kisha akatoa salamu baada ya kusali rakaa mbili, na aliponyanyuka kutaka kulibusu jiwe (la Al Kaaba) watu wakasema: "Subhana Llah!", akarudi na kuwauliza: "Mna nini?" Anasema Ataa: "Akakamilsha rakaa aliyoiacha kisha akasujudu sajda mbili ."
Al Tabarani

Anapoongeza
Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwahi kusahau akaongeza rakaa moja na watu wakasema: "Subhana Llah", kisha wakamwambia: "Umezidisha rakaa moja, umesalisha tano." Akasujudu sajda mbili baada ya kutoa salamu.

Anaposahau Kusoma Tahiyatu
Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwahi kusahau kusoma tahiyatu ya mwanzo na baada ya kumaliza sala akasujudu sajda mbili kisha akatoa salam.

Maamuma anasujudu anaposujudu imamu sajda ya kusahau, lakini anaposahau yeye maamuma hatakiwi kusujudu sajda ya kusahau.

Ndani ya Sajda ya kusahau unasoma dua zile zile unazosoma katika sajda ya kawaida.
Unaweza kusujudu Sajda ya kusahau wakati wowote utakapokumbuka hata kama usharudi nyumbani kutoka msikitini.

Sunday, February 1, 2015

Historia Ya Luqmaan Mwenye Hikma

Luqmaan alizaliwa katika Bara la Afrika. Jina lake ni Luqmaan bin 'Anqa' bin Saadun. Ama Ibn Jariyr at-Twabariy, yeye anasema jina lake lilikuwa Luqmaan bin Tharan kutoka watu wa Aylah (Quds).
Alikuwa ni mtu mwema aliyefanya juhudi katika Ibaadah na kutunukiwa busara. 
Alikulia katika msitu na kutembea bila viatu. Kule kukutana kwake na wanyama kulifanya awe mwenye nguvu, ujasiri, madhubuti na kutoogopa chochote. Alikuwa na ada ya kutafakari sana kuhusu maumbile yaliyomzunguka. Huko kulimfanya awe ni mwenye kujifunza vitu vizuri vizuri kila uchao.
Luqmaan alishikwa na wafanyabiashara wa utumwa waliovamia Afrika na kuuzwa kama mtumwa. Alijikuta amevuliwa uhuru wake, hivyo kumfanya asiweze kutembea wala kuzungumza anavyotaka. Huu ulikuwa ni mtihani wa kwanza aliolazimika kuuvumilia. Aliumia katika utumwa lakini alivumilia kwa kusubiri huku akiwa na matumaini kuwa Allaah Aliyetukuka Atamtoa katika janga hilo.
Aliyemnunua alikuwa ni mtu mzuri, mwema na mwenye busara. Hivyo, alimtendea wema Luqmaan. Aliweza kutambua kuwa Luqmaan alikuwa si mtu wa kawaida kwa werevu aliokuwa nao.
Mtu huyu mwenye huruma aliacha wasiya kuwa anapoaga dunia tu Luqmaan aachwe huru. Na alipokufa, ombi hilo lilitekelezwa na hivyo kumfanya Luqmaan kwa mara nyingine tena kuwa huru. Luqmaan alisafiri kwa muda na kuweka makazi yake pamoja na wana wa Israili. Alichaguliwa kwa hakimu katika utawala wa Nabii Daawuud ('Alayhis Salaam), naye aliheshimiwa na watu wote kwa busara yake na hukumu zake za uadilifu. Alioa na kulea familia.
Amesema Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma): Luqmaan alikuwa mtumwa wa kutoka Ethiopia akifanya kazi ya useremala.
'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema, nilimuuliza Jaabir bin 'Abdillaah kuhusu Luqmaan. Akasema: 'Alikuwa mfupi na pua mseto na alikuwa Mnubi'.
Imesimuliwa na Yahya bin Sa'iyd al-Answaariy kutoka kwa Sa'iyd bin al-Musayyib akisema: 'Luqmaan ni mtu mweusi kutoka Misri'.
Al-Awza'iy amesema: Niliambiwa na 'Abdur-Rahman bin Harmalah kuwa mtu mmoja mweusi alikuja kwa Sa'iyd bin AI-­Musayyib akimuomba sadaka. Sa'iyd alimwambia: Usihuzunike kwa sababu ya rangi yako nyeusi kwani kulikuwa miongoni mwa walio bora kati ya watu ni watu weusi watatu: Bilaal bin Rabaah, Mahja' (mwachwa huru 'Umar bin Al-Khatwtwaab) na Luqmaan, mtu mweusi mwenye busara, kutoka Nubia, ambaye midomo yake ilikuwa mipana.
Imepokewa kwa Ibn Wahb: 'Mtu mmoja alikuja kwa Luqmaan, mwenye hekima na kumuuliza: Je, wewe ni Luqmaan? Je, wewe ni mtumwa wa fulani? Akajibu: Ndio. Yule mtu akasema: Wewe ndiye yule mchungaji mweusi. Luqmaan akasema: Ama kuhusu rangi yangu nyeusi, inaonekana dhahiri, kwani ni lipi linalokustaajabisha? Akasema yule mtu: Umekuwa ukizuriwa na watu kila mara ambao wanakubali hukumu yako. Luqmaan akasema:  Ewe ndugu yangu! Ukifanya ninayokuambia utakuwa kama hivi. Yule mtu akasema: Ni nini hayo? Luqmaan akasema: Inamisha macho yako, chunga ulimi wako, kula kilicho halali, kuwa mtwaharifu, timiza ahadi, kuwa mkarimu kwa wageni, waheshimu majirani, acha lisilokuhusu. Zote hizi zilinifanya mimi nikawa hivi.
Hata hivyo, wanazuoni wengi wana rai na muono kuwa Luqmaan alikuwa si Nabii bali mtu mwenye busara. Zaidi ya hayo, ametajwa katika Qur-aan na amesifiwa na Allaah Aliyetukuka, Ambaye Ametusimulia wasiya wake kwa mwanawe pale aliposema:
'Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah kwani kufanya hivyo ni dhuluma kubwa' (31: 13).
Kwa hiyo, alimuonya mwanawe na kumkataza kuingia katika shirki.
Imaam Al-Bukhaariy amesema: Niliambiwa na Qutaybah kutoka kwa Jariyr kutoka kwa Al-A'mash kutoka kwa Ibraahiym kutoka kwa 'Alqamah kutoka kwa 'Abdullah kwamba alisema:
'Aayah ifuatayo ilipoteremka: 'Ni wale wenye kuamini na hawachanganyi Imani na dhuluma' (6: 82) tulisema: 'Ewe Mtume wa Allaah! Ni nani katika sisi asiyefanya dhuluma kwake yeye mwenyewe'. Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) akawajibu: 'Si kama msemavyo, kwani dhuluma katika Aayah na kutochanganya imani na dhuluma inamaanisha SHIRKI. Je hamjasikia kauli ya Luqmaan kwa mwanawe: 'Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah kwani kufanya hivyo ni dhuluma kubwa' (31: 13).
Katika nasaha alizompatia mwanawe ni kuwatendea wema wazazi, kutokua na kibri, kusimamisha Swalah, kuamrisha mema na kukataza maovu, kusubiri, kutonyanyua sauti na kadhalika kama Alivyotupa maelezo hayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
'Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Allaah Atakileta. Hakika Allaah ni Mjuzi wa yaliyofichika, Mwenye khabari za yote'.  
'Ewe mwanangu! Shika Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa'
'Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Allaah Hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha' [Luqmaan:16-18].
Ibn Abi Haatim amesema: Niliambiwa na babangu kutoka kwa Qatadah aliyesema: Allaah Aliyetukuka Alimpatia fursa Luqmaan kuchagua baina ya utume na kuwa na hekima, naye akachagua hekima. baadaye, Jibriyl alikuja kwake akiwa amelala na kummiminia hekima. Luqmaan alianza kuitamka siku ya pili yake. Inasemekana kuwa Luqmaan aliulizwa kwa nini alichagua hekima juu ya utume. Alisema: Lau kama Allaah Alinipatia utume ningeukubali na ningejaribu sana kupata radhi Yake, lakini Alinichaguza. Niliogopa kuwa dhaifu sana kwa utume, hivyo nikachagua busara. 
Masimulizi haya si sahihi kwani mpokeaji mmoja Sa'iyd bin Bashiyr, si mwaminifu. Hata hivyo, watangu wema wengi wa mwanzo na wanazuoni, kamaMujaahid, Sa'iyd bin Al-Musayyib and Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhum) walikuwa na muono kuwa ile kauli ya Allaah inayosema:
'Na hakika Tulimpatia Luqmaan Hikmah' (31: 12).
Hii ina maana uchambuzi na ufahamu wa kidini. Kwa hiyo, hakuwa Mtume na hakuna chochote kilichoteremshwa kuonyesha kuwa aliteremshiwa wahyi.
Hikma zake nyingine kama zilivyosimuliwa ni hizi:
Kutoka kwa Damurah As-Sariy Ibn Yahia: Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa  'Abdah Ibn Sulaymaan kutoka  kwa Ibn Mubaraak kutoka kwa 'Abdur-Rahmaan al Mas'uud  kutoka kwa 'Awn Ibn 'Abdillaah akisema:' ' Luqmaan alimwambia mwanawe: Ewe mwanangu ukikutana na watu anza kwa salaam [Assalaamu 'alaykum]. Kisha kaa upande na usiseme kitu hadi waseme wao. Ukiwaona wanamdhukuru Allaah, waunge, lakini wakishughulika na mengine, geuka uondoke mbali nao na tafuta wengineo [wanaomdhukuru Allaah].
Nimeambiwa na baba yangu kutoka kwa 'Amr Ibn 'Uthmaan kutoka kwa Damura Ibn Hafsw Ibn 'Umar akisema: 'Luqmaan aliweka gunia la chembe za haradali karibu yake na akaanza kumpa nasaha mwanae, kwa kumpa kila nasaha moja chembe moja ya hardali hadi zikaisha zote. Akasema: 'Ewe mwanangu nimekupa nasaha ambazo zingepewa mlima ungelipasuka'
'Abdur-Razaaq amesema: Niliambiwa na Hasan kutoka kwa Al-Junayd  kutoka kwa Sufyaan akisema: Luqmaan alimwambia mwanae: 'Ewe mwanangu! Sijapata kujuta kwa sababu ya kukaa kimya. Ikiwa maneno ni fedha basi kukaa kimya ni dhahabu'.  
Ibn Jariyr amenuku kwamba Khaalid ar-Rabaai alisema: 'Luqmaan alikuwa mtumwa wa ki-Ethiopia aliyekuwa na ujuzi wa useremala. Bwana (Tajiri) wake alimwambia: 'Tuchinjie kondoo huyu' Akamchinja, kisha akamwambia: 'Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni bora kabisa'. Akampelekea ulimi na moyo. Baada ya siku kupita, alimtaka tena amchinjie kondoo, akachinja kisha Bwana wake akamwambia tena: 'Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni viovu kabisa'. Akamletea vile vile ulimi na moyo. Bwana wake akamuuliza: 'Nilipokutaka uniletee viungo bora kabisa umeniletea ulimi na moyo; na nilipokutaka uniletee viungo viovu kabisa umeniletea hivyo hivyo' Luqmaan akamwambia: 'Hakuna vilivyo bora kuliko hivi vinapokuwa vizuri, na hakuna vilivyo viovu kabisa kuliko hivi vinapokuwa vibaya' [At-Twabariy: 20:135] 
Tusome mafunzo tunayopata kwenye kisa hiki cha mja mwema huyu aliyejaaliwa hikma, kisa chenye mafundisho mengi ndani yake, tujitahidi kuyafanyia kazi hayo tuliyosoma inshaAllaah.

Aqiyqah Afanyiwayo Mtoto Mchanga

1.    ‘Aqiyqah ni jina lililopewa kichinjwa (mnyama) achinjiwacho mtoto mchanga aliyezaliwa ni mamoja awe ni wa kike au wa kiume.
2.    Ni Sunnah si waajibu. Ushahidi wa hili ni uko katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: "Atakayepata mtoto na akapenda amchinjie basi na afanye hivyo; kwa mwanamume mbuzi wawili na kwa mwanamke mbuzi mmoja". Hadiyth hii imepokewa na Maimaam Abuu Daawuud na An-Nasaaiy kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “na akapenda amchinjie” ni dalili kuwa ‘Aqiyqah si lazima bali ni jambo linalopendeza Muislamu kulifanya. Lakini kwa mwenye uwezo wa kufanya hivyo basi iliyo bora zaidi kwake ni kufanya ama yule asiye na uwezo wa kufanya hivyo, basi si lazima kwake  maana Mwenyeezi Mungu Haikalifishi nafsi yoyote ila yale yaliyo sawa na uwezo wake na pia Hakufanya uzito katika dini.
3.    Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yeye kasema: “Kila mtoto azaliwaye anafungamana na ‘Aqiyqah yake, anachinjiwa siku ya saba, ananyolewa kichwa chake na anapewa jina.” Wanachuoni wamelizungumzia neno ‘kufungamana’ hapa kuwa linaweza kuwa linamaanisha mambo mengi, miongoni mwa mambo hayo ni:
  1. Anakuwa kama mwenye kujisikia uzito na unyonge na mwenye kukosa wepesi na furaha maishani hadi achinjiwe
  2. Ni deni lililo mithili ya Rehani ambayo hulazimiana na mtu hadi alilipe.
4.    Iliyo bora zaidi na timilifu ni kuwa wale mbuzi wawili au kondoo wawili ambao anatakiwa mtoto wa kiume achinjiwe wanatakiwa wawe ni wenye kufanana au kukaribiana kufanana kimaumbile na kiumri. Lakini kama itashindikana kuwapata mbuzi wawili wenye sifa kama hizo itafaa hata kama watatofautiana kiumbile na kiumri maadamu tu wana sifa zinazofaa kisheria kwa ajili ya ibada hii. Sifa hizo tutazitaja baadaye.
5.    Iliyo bora zaidi na timilifu ni kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi wawili lakini ikiwa mtu atashindwa kabisa kuchinja mbuzi kama kutokana na yeye kupata mbuzi mmoja tu au kumiliki kiwango cha mbuzi mmoja tu basi huyo huyo mbuzi mmoja atatosha.
6.    Sunnah ni kumchinjia mtoto atakapofikisha siku ya saba kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Samrah, lakini ikiwa mtu hakuweza kuchinja siku ya saba basi na afanye hivyo siku yoyote atakayojaaliwa.
7.    Nywele za mtoto mchanga anazonyolewa siku ya 'Aqiyqah' hupimwa uzito kwa sonara. Uzito huo huchukuliwa ili kulinganisha thamani ya fedha yenye uzito kama huo kwa wakati huo, kisha pesa hizo hutolewa sadaqa.
8.    Ibada hii ya kuchinja hufanyika hata kama mtoto kafariki maadamu tu alizaliwa hai au hata kama mimba ilitoka lakini mtoto tayari alikuwa ameviviwa roho, yaani alikuwa amefikisha miezi minne au siku mia na ishirini na kuendelea lakini kama alikuwa hajafikisha miezi minne au siku mia na ishirini hapo hatofanyiwa ‘Aqiyqah.
9.    Kuna imani imeenea kwa watu wengi kuwa kichinjwa cha ‘Aqiyqah hakivunjwi mifupa hii ikiwa kama ishara ya kumtakia mtoto salama na asivunjike maishani mwake. Hili si sahihi wala halina mashiko katika Qur-aan wala Sunnah. Kwa hiyo ieleweke wazi kuwa mifupa ya ‘Aqiyqah inafaa kuvunjwa wala hii haitokuwa sababu ya kuvunjika kwa mtoto hata kama itatokea kama watu wanavyoamini. Vile vile kuna jambo jingine nalo ni kuwa nyama ya ‘Aqiyqah huchanganywa au hupikwa kwa maji yaliyotiwa vitu vitamu vitamu kama sukari au huchanganywa na asali wakati wa kuliwa, hii ikiwa ni kama ishara ya kumtakia mtoto tabia njema; hili nalo pia halina mashiko. Hivyo iwekwe chumvi na kupikwa kama nyama ya kawaida
10.           Kinachotakiwa kuchinjwa katika ‘Aqiyqah katika wanyama ambao kishari’ah wanaitwa Bahiymatul An’aam ambao ni; mbuzi, kondoo, ng’ombe na ngamia. Kwa mantiki hii haifai kumchinja farasi kwa ajili hii, wala swala hata kama anafugwa na amekuwa kama mbuzi kitabia na pia haifai kuchinja kuku wala bata kwa ajili ya ibada hii
11.           Ama kuhusiana na umri unaofaa wa kichinjwa ni miaka mitano kwa ngamia na miaka miwili kwa ng’ombe, dume la mbuzi na dume la kondoo ni mwaka mmoja na mbuzi jike na kondoo jike ni miezi sita
12.           Ni sharti katika kichinjwa cha ‘Aqiyqah kiwe kimesalimika na aibu mbalimbali kwa kifupi kabisa kichinjwa hichi kinafanana na kichinjwa cha ‘Iydul Adhwhaa au Idi kubwa yaani kisiwe na chongo cha wazi, kiguru cha wazi, kilichokonda sana, wala kisiwe ambacho kimetobolewa masikio yake wala kisiwe kilichokatwa mkia au kukatika pembe.
13.           Ikiwa mtu anamiliki takribani wanyama wote wanaofaa kuchinja kwa ajili ya ‘Aqiyqah kiasi kuwa anaweza akitaka akachinja ng’ombe au ngamia au kondoo au mbuzi, iliyo bora zaidi ni kuchinja mbuzi maana ndiye aliyetajwa katika Hadiyth.
14.            Inafaa mtu kuipika nyama ya ‘Aqiyqah au kuigawa pasina kuipika lakini iliyo bora zaidi ni kuipika nyama ya ‘Aqiyqah kuliko kuigawa kwa kuwa kwa kufanya hivyo utawarahisishia masikini na majirani gharama za kupika.
15.           Hakuna ubaya wowote katika kula nyama ya ‘Aqiyqah kwa aliyechinja, kwani kwa hakika hii ni nyama kwa ajili ya kumshukuru Allaah na kile ambacho ni kwa ajili ya kumshukuru Allaah kinafaa kuliwa kishari’ah wala hapana ubaya bali hii ni kama nyama ya ‘Iydul Adhwhaa.
16.           Pia inafaa kuiweka nyama ya ‘Aqiyqah katika jokofu pasina kuigawa lakini iliyo bora zaidi na timilifu katika ibada hii ni kuigawa kwa mafaqiri na marafiki hata kama ni kidogo.
17.           Haifai kununua mbuzi aliyechinjwa na kumfanya kuwa ni ‘Aqiyqah bali ni lazima kumununua mbuzi mzima na kisha kumchinja kwa nia ya ‘Aqiyqah
18.           Ikiwa baba hayuko, kama kwa mfano kafariki, mama atasimamia jukumu la kufanya ‘Aqiyqah.
19.           ‘Aqiyqah ni Sunnah kwa baba kumfanyia mtoto wake lakini mtoto hakufanyiwa ‘Aqiyqah na akapenda ajifanyie mwenyewe inafaa hata kama ni ni kitambo kirefu kimepita na umri ukawa mkubwa.
20.           Inafaa kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi hao wawili kwa utaratibu wa kugawa kwa maana ya kuwa anamchinja mbuzi mmoja mwezi huu na mwengine akamchinja mwezi mwingine wala haishurutishwi wachinjwe mara moja, bali inafaa kwa mtoto akajichinjia mbuzi mwingine ikiwa baba alimchinjia mbuzi mmoja kwa sababu ya hali yake kifedha. Bali inafaa kumchinjia mbuzi mmoja sehemu moja na mwengine sehemu nyingine wala si sharti wachinjwe wote sehemu moja wala si sharti wachinjwe sehemu alipo mtoto anayefanyiwa.
21.           Haifai kisheria kupigia thamani ya mbuzi wa ‘Aqiyqah na kuwapa kiwango hicho masikini bali ni lazima achinjwe mbuzi
22.           Haifai kushirikiana watoto katika ‘Aqiyqah kwa mantiki ya kuwa wachangie kwa mfano mbuzi wawili watoto wawili wa kiume. Watoto wawili wa kiume wanapaswa wachinjiwe mbuzi wanne hata kama ni mapacha. Kama ni mapacha wawili wa kike watachinjiwa mbuzi wawili, kama mmoja ni wa kike na mwengine ni wa kiume watachinjiwa mbuzi watatu. Bali ngamia na ukubwa wake hafai kuwachinjia watoto wawili na ikifanyika hivyo inazingatiwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja. Bali haitofaa kwa watoto wawili ambao hawakufanyiwa ‘Aqiyqah kwa wao kujiamulia kuchinja ngamia mmoja ili awe ni ‘Aqiyqah kwa wote wawili. Bali ngamia huyo atazingatiwa kuwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja tu.
23.           Si lazima wakati wa kumchinja mnyama wa ‘Aqiyqah kusema kuwa hii ni ‘Aqiyqah bali inatosha mtu kunuia moyoni mwake na kilicho lazima kutamka ni BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym.
24.           Si lazima kuwaambia waliohudhuria kuwa watakula nyama ya ‘Aqiyqah, lakini ni vizuri kuwaambia ili wamuombee mtoto du’aa njema, uongofu, uchaji, kutengenekewa na kheri za dunia na Akhera.
‘Aqiyqah ni mnyama ambaye huchinjwa kwa ajili ya mtoto mdogo kama tulivyotangulia kusema. Jambo hili ni katika mlango wa kumshukuru Allaah. Kuna pia vyakula vingine ambavyo ni katika mlango huu wa kumshukuru Allaah na vinafaa kuliwa kishari’ah navyo ni:
a.     Waliymah: chakula au karamu ya harusi.
b.     Qiraa: chakula cha mgeni, kile cha mgeni njoo wenyeji tupone!
c.      Ma-adabah: ambacho ni chakula cha mwaliko.
d.     Tuhfah: ambacho ni chakula cha mwenye kutembelea pahala.
e.     Khiraasu: ambacho ni chakula cha kujifungua.
f.       Ghadiyrah: ambacho ni chakula cha wakati wa khitaani au kutahiri wanawake au wanaume
g.     Naqiy’ah: ambacho ni chakula cha anayekuja kutoka safari.
h.     Wakiyrah: ambacho ni chakula baada ya kumaliza kujenga.

Isipokuwa chakula cha msibani au cha siku ya tatu au cha Khitmah au arobaini. Vyakula nilivyotaja hapo juu vinafaa kuliwa Kishari’ah. Jariyr bin ‘Abdillaah anasema kuwa kukusanyika kwa wafiwa na kupikiwa chakula ni miongoni mwa mambo aliyokataza Mtume wetu Mtukufu.

Vidokezo Muhimu Kwa Wazazi Wenye Wasichana Na Wavulana

1.     Yatilie Bidii Malezi Kuliko Hata Kazi Yako Ya Kutwa Nzima
Hii ina maana kwamba wazazi wote wawili ni lazima waelewe kuwa watoto wao ni wa kweli kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), na baba atakuja kuulizwa vipi kawalea watoto wake.  Ikiwa watoto wao hawatokulia katika kuutekeleza Uislamu kwa sababu ya mapuuza ya wazazi wao, halitokuwa ni jambo la kukubalika kwa maisha ya hapa duniani na hata ya baadae.
2.     Punguza Au Badilisha Masaa Ya Kazi Kwa Ajili Ya Kupata Muda Wa Kuwa  Pamoja Na Familia Yako
Ni bora kuwa na kazi moja yenye muda wa kudumu, anasa chache katika nyumba (yaani sio magari mengi, nguo za gharama nyingi, nyumba kubwa ya fakhari, televisheni kila pahali), na muda zaidi wa kuwa pamoja na familia, kuliko kuwa na mambo mengi ya anasa na kukakosekana malezi. Haya yote yanawahusu mababa na mamama. Wazazi hawawezi kuwafunza watoto wao bila ya wao kuwepo nao kikawaida.  Acha kazi za ziada kwenye siku za mwisho wa wiki au kazi za jioni na badala yake nenda na watoto Msikitini kwa ajili ya Halaqah (darsa za dini) na shughuli nyenginezo. Au tilia maanani kugeuza nyakati za kazi ili uwe nyumbani wakati ambao watoto wapo.
3.     Soma Qur-aan, Ifahamu Maana Yake, Angalau Kwa Dakika Tano Kila Siku
Angalau dakika tano. Inawezekana ikawa kwenye gari wakati (umesimama kwa ajili) ya msongamano wa magari, mapema baada ya Swalah ya alfajiri, au mara tu kabla ya kulala, soma Qur-aan pamoja na maana au tafsiri.  Baadae angalia umuhimu wa taathira yake.  In shaa Allaah utajikurubisha kwa Allaah, na baada ya muda mrefu, utakuwa mfano bora wa kuigwa na kuisaidia familia nzima kujikurubisha kwa Allaah vile vile.
4.     Hudhuria Halaqah Kila Wiki
Fanya biashara ya kubadishana mchezo wa karata, au kuangalia televisheni siku za jumapili kwa kuhudhuria Halaqah (darsa duara za dini; ima misikitini au majumbani au kwenye kumbi za kukodishwa). Ikiwa (katika Msikiti) hakuna utaratibu uliowekwa tayari kwa wakati huo, basi msaidie Imamu ili auweke. Hudhuria kwa uangalifu Natija ya kufanya haya ni kule watoto kuwaona wazazi wao wanafanya bidii ya kuusoma Uislamu, na wao kwa namna yoyote ile watapata hamu ya kufanya vile vile (wafanyavyo wazazi wao).
5.     Waheshimu Watoto Wako
Kuwaheshimu watoto wako ina maana usiwafanye kama wapumbavu, bali ni kuwachukulia kama wao ni watu wazima, usiseme nao kitoto au kuwafedhehesha na kuwatukana.  Wajumuishe kwenye shughuli za nyumbani zenye manufaa na waombe ushauri kwenye maamuzi ya mambo muhimu. 
6.     Kuwa Na Hamu Ya Kushiriki Katika Mambo Wanayoyafanya
Hudhuria michezo yake kikawaida pindi ikiwezekana na harakaat mbalimbali wazifanyazo.
7.    Yatambue Matatizo Yaliyopo Na Wajulishe Wazi Wazi
Kwa kadiri unavyotumia wakati wako kuwa pamoja na vijana wako, utakuwa na uwezo zaidi wa hisia ya kugundua kitu gani kinawakera Usifagilie hisia hii chini ya zulia (usiufiche ukweli). Ujulishe kwa uwazi. Lakini usifanya kwenye mkutano wa familia au mbele ya wengine. Fanya hivyo wakati wa fikra inayofuata.
8.     Weka Miadi Ya Kuonana Na Kijana Wako
Kwa vile mara nyingi uwekaji wa miadi ya kuonana inahusishwa na kukutana kwa msichana na mvulana, wazo hili linaweza kutumiwa kwa aina yoyote ya mkutano baina ya watu wawili wanaotaka kutambuana vyema.
Ni muhimu sana kuweka miadi ya kuonana na vijana wako katika kiwango tofauti mara wanapoingia kwenye umri wa usichana/uvulana kwa sababu wao si watoto wadogo tena. Unaweza kuweka miadi na Sumayyah wakati anapomaliza masomo yake ya sekondari (badala ya kwenda kwenye sherehe za ngoma), Yaasir naye wakati anapopata leseni yake ya kuendesha gari au ikiwa unahisi kuna kitu kinawakera na unataka kuwajulisha peke yao ili kuwasaidia kutatua mashaakil yao
9.     Usiwe Tu Ni Mzazi Kwa Mtoto Bali Uwe Pia Ni Rafiki Kwake
Kujenga urafiki nae ina maana ya kuwapa majukumu katika familia. Mpe mvulana wako wa miaka 16, 'Uthmaan, ambaye ana leseni ya gari, majukumu ya kumsaidia mama yake siku za jumamosi anapokwenda madukani kununua vyakula.  Mpe msichana wako wa miaka 15, Khadiyjah, ambaye anapenda maua, kuwa ni mwangalizi wa bustani pamoja na kukatakata majani. Kwa njia hii vijana watajihisi kuwa na wao ni sehemu ya familia, wanajumuishwa na wanahitajiwa.
10.             Jenga Msikiti Katika Nyumba Yako (Tenga Sehemu  Maalum Ya  Kuswalia Ikiwezekana)
Chagua sehemu ya chini ya nyumba yako au katika ukumbi wako uwe ni Msikiti wa nyumbani. Itayarishe hiyo sehemu kwa kuweka miswala, misahafu na iwe sehemu khaswa ya kuswaliwa.
Fanya Msikiti huu kuwa waangalizi wake ni watoto tu peke yao. Muweke mkubwa wao kuwa ni msimamizi na mpangaji wa majukumu kwa wadogo zake. Majukumu hayo yawe ni pamoja na kuuweka Msikiti uwe safi, kuwaamsha watu Alfajiri, kuadhini, na kadhalika.
11.             Usijenge (Fikra Kuwa) “Uislamu Ni Kwa Wanaume Tu”
Hii ina maana usibague wake zako na wasichana kwenye Swalah. Wakati wanaume wanaposwali Swalah ya jama'ah, hakikisha wanawake wapo nyuma yaoau wanaswali Swalah ya Jama'aah (sehemu nyengine) na wao.  Vile vile hakikisha Imaam anasoma kwa sauti kiasi ya kusikika na wanawake ikiwa wapo sehemu nyengine ya nyumba.  Vile vile wahimize wanawake waswali Swalah ya Jama'Aah pindi ikiwa wanaume hawapo nyumbani.
12.             Anzisha Maktaba Ya Kiislamu Na Chagua Muangalizi Wake
Iandae nyumba yako yenye maktaba ya Kiislamu kwa vitabu, kanda za kusikiliza zenye maadili ya Kiislamu, mpatie kila mmoja kwa mujibu wa umri na hamu yake. Ikiwa 'Abdullaah mwenye umri wa miaka 13 anapenda vitabu vya hadithi za hatari, kwa mfano, hakikisha unavyo vitabu vya Kiislamu vya kila aina vyenye hadithi za aina hiyo.
Mfanye mmoja katika vijana wako kuwa ni mwangalizi wa maktaba. Aipangilie na kuiweka katika hali nzuri. Kitu chochote kinachotakiwa kuingizwa kwenye maktaba ni lazima kipitishwe kwake. Mpe msimamizi wa maktaba bajeti ya kila mwezi ya kununulia vitabu, kanda za kusikiliza na kadhalika.
13.             Wachukue kwenye shughuli za Kiislamu
Badala ya kwenda kwenye Mgahawa (Restaurant) kwa ajili ya vyakula vya kila aina, hifadhi pesa zako kwa ajili ya kumchukua kila mmoja katika chakula au shughuli za jamii ya Kiislamu. Fanya bidii kwenda kwenye matukio ambayo vijana wengine wa Kiislamu watahudhuria na kutakuwa na msemaji atakayetoa ujumbe kwenye mkusanyiko (huo).
Ni muhimu vile vile  kufanya mazoea ya kumchukua 'Abdur-Rahmaan na 'Aaishah kwenye kambi za  Kiislamu na mikutano ambayo watakutana na watoto wenzao wa Kiislamu kwa wingi na wenye umri unaolingana na wao.
14.             Hamia Kwenye Maeneo Yenye Waislamu Wengi
Wazo hili limekusudiwa haswa kwenye eneo lilo karibu na Msikiti. Hatua hii ni muhimu kwa kuwa watoto wako ili wawe wanaambatana na watoto wengine wa Kiislamu wenye umri ulio chini, sawa au zaidi na wao, katika mambo yao ya kimsingi ya kila siku.
15.             Wasaidie Vijana Wako Ili Waanzishe Wao Wenyewe Kikundi Cha Vijana
Baada ya kuwa unaishi kwenye eneo la Waislamu na unahudhuria shughuli za Kiislamu kikawaida, vijana wako katika mambo mengi wataukuza urafiki na  Waislamu wengine wenye umri unaolingana na wao.  Usiyaachie haya yakaishia hapo.
Wasaidie kuanzisha kikundi cha vijana, sio tu kwa ajili ya kusoma Uislamu bali pia kutembea pamoja kwenye viwanja vya kupendeza, kuogelea, na kadhalika.  Kihusishe kikundi hichi kwenye kazi muhimu kama za kusafisha takataka Msikitini au kuhudhuria nyumba zinazolelewa wazee.  Kikundi hiki  ni lazima kiwe na uangalizi wa wazazi, ijapokuwa maamuzi ya vijana yasiingiliwe mpaka ionekane kikweli kweli upo umuhimu/haja ya kufanya hivyo.
16.             Kuwepo Mikutano Ya Familia Kwa Kila Wiki
Madhumuni  ni kutafuta kinachoendelea katika maisha ya kila mmoja wao na kutoa ushauri wa mambo muhimu katika familia. Hafswah ameanza kuhudhuria Halaqah, Hasan naye amerejea kutoka kwenye kambi ya Kiislamu, na Husayn amekaribia jaribio lake la mwisho katika hesabu za algebra.  Sio tu kutoa taarifa kwa mfumo wa muhtasar, bali ni kujadiliana na kuwasiliana baina ya kila mmoja, na kuweka taarifa mpya kabisa kwa kila kinachoendelea katika maisha ya kila mmoja wao, ambapo inakuwa ni vigumu (kuyafanya haya) pale watoto wanapokuwa wanakaribia kuingia kwenye umri wa ujana.
Huu vile vile ni wakati wa kuishauri familia na kuamua juu ya mambo makubwa  yanayomuathiri  kila mmoja kati yao kama kuhamia mji mwengine, harusi ya mmoja kati yao, iwapo yupo mwenye wakati mgumu skuli kwa sababu ya wanao mbughudhi, na kadhalika.
Tafadhali kumbuka: Mashauriano katika familia haimaanishi kwamba maamuzi ya walio wengi ndio yafuatwe kuhusu hali inayojadiliwa.  Bali wazazi watabaki kuwa ndio wenye dhamana, fikra na rai za vijana na watoto wadogo, wazazi watayazingatia kwenye kufanya maamuzi yao ya mwisho.
17.             Weka Kigezo Cha Majukumu - Nini Abu Bakr Kafanya?
Mbali ya kuwa wewe mwenyewe ni kigezo juu ya kuutekeleza Uislamu kwa vitendo, hakikisha unawawekea vijana wako vifaa vya kusoma kuhusu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), wote wanawake na wanaume, la sivyo, huenda watoto wako wakaiga wahusika wa vipindi vya televisheni ambavyo watoto wako wanaangalia na wakawa ndio Maswahaba wao. 
Jadiliana nao nini Maswahaba walikuwa wakifanya katika kukabiliana na maisha ya vijana. Swahaba Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) angelifanya nini pindi angelimuona mtu anauza majawabu ya mtihani wa mwisho ya hesabu za darasa la saba au darasa la kumi na mbili (form IV)? Na 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) angelifanya nini pindi angelikabiliana na mtu mwenye kudanganya wazazi wake?
18.             Soma Vitabu Kwa Ajili Ya Malezi Ya Uhakika
Hivi vinaweza kuwa ni vitabu vilivyoandikwa na Waislamu, lakini vitabu vilivyoandikwa na wasiokuwa Waislamu pia vinaweza kusaidia.  Hata hivyo, jitayarishe na pia hakikisha kuwa unao uwezo wa kugundua ni vitabu vipi vinakubalika Kiislamu dhidi ya visivyokubalika.
19.             Waache Waoe/Waolewe Mapema
Fitna kutoka nchi za Magharibi zimeeneza picha za ngono kwenye televisheni, mabango ya matangazo, mitaani, kwenye mabasi, katika filamu za maigizo, na kadhalika, nazo zinapatikana wazi katika baadhi ya nchi zetu.  Inakuwa ni ngumu kwa kijana wa Kiislamu kuyakabili haya bila ya kuwa na matamanio na kushindwa kujizuia na maovu hayo. Ni jambo la maana kuwaacha waoe/waolewe mapema (Soma baadhi ya vidokezo vinavyowahusu wazazi juu). Hii itarahisisha shinikizo, na hapana haja ya kukatisha masomo yao kwenye suala hili.
Kumbuka, kama ni mzazi utabeba jukumu ikiwa mvulana au msichana wako atataka kuoa au kuolewa na wewe ukamkataza na akaishia kwenye kufanya uzinifu. Vile vile ni lazima ukumbuke kuwa unapotekeleza hatua hii usimlazimishe mvulana au msichana wako kuoa au kuolewa na mtu asiyempenda.
20.             Mwisho Lakini Pia Muhimu - Omba Du'aa
Omba Dua. Ni Yeye Allaah Pekee Anayeongoa au Kutoongoa, lakini ikiwa umetekeleza wajibu wako kama ni mzazi kuwafanya watoto kuwa ni wenye kuutekeleza Uislamu kwa vitendo, In shaa Allaah, ni rahisi kuwalea kuliko kulipuuza jukumu hili. Pia waombee Du'aa vijana wako mbele yao. Kufanya hivyo kutawakumbusha wao jinsi gani unavyowapenda na kujihusisha nao.
Du'aa Mojawapo Katika Qur-aan
رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا
Rabbanaa Hab-Lanaa Min Azwaajinaa Wa-Dhurriyaatinaa Qurrata A'yuniw-Waj'alnaa Lil-Muttaqiyna Imaama.
((Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na Utujaalie tuwe waongozi kwa wacha Mungu)) [Al-Furqaan: 74]