Monday, January 26, 2015

Wanawake Waliobashiriwa Pepo

1. Mama Wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'Anha)

Nasaba yake

Jina lake ni Khadija binti Khuwaylid bin Asad bin Abdul Uzza Qusay bin Kilab anayetokana na kabila la Kikureshi aliyezaliwa katika mwaka wa 68 kabla ya Hijra yaani mwaka 556 baada ya Nabii Issa (Alayhis Salaam).
Wazee wake walimlea kwa heshima na adabu ya hali ya juu na alikuwa akijulikana kwa jina la ‘Aliyetakasika’ hata kabla ya kuja kwa Uislamu.

Anaolewa na Atiyq bin Aidh

Imepokelewa kuwa siku moja vijana wa kabila la Kikureshi walipokuwa wamekaa karibu na Al Kaaba wakizungumza, aliinuka mmoja wao anayeitwa Al Harith akasema:
“Enyi ndugu zangu nimetia nia ya kuowa”.
Mmojawao akamwambia:
“Uamuzi mzuri huo, kwani tokea alipofariki mama yako na baada ya baba yako kuowa mke mwingine umekuwa unaishi peke yako”.
Mwengine akasema:
“Umefanya vizuri kuamua kuoa, kwani kila mwanamke anatamani kuolewa na mtu kama wewe, maana baba yako ni katika watu wanaoheshimika katika kabila la Kikureshi, na wewe unamiliki mali nyingi sana, sidhani kama yupo mwanamke atakayekukataa”.
Al Harith Akawatizama wenzake kwa muda, kisha akasema:
“Nyinyi mnadhania hivyo kwa sababu ni rafiki zangu, lakini mnakosea”.
“Tunakosea vipi?  Hebu tufahamishe”.
Akawaambia:
“Nilitaka kumuowa Khadija, lakini baba yake alinikatalia kwa sababu eti anasema kuwa kabila langu ni duni kuliko kabila lake”.
Wenzake wakasema:
“Bila shaka hiyo, kwani Khadija ni binti wa Khuwaylid bin Asad naye ni mtu mtukufu miongoni mwa mabwana wa kabila la Kikureshi mwenye kumiliki mali nyingi sana na nyumba kubwa ambayo daima inapokea wageni mbali mbali wanaokuja Makka”.
Mwengine akasema:
“Na Khadija binti yake ni uwa katika mauwa ya Makka, kwani yeye ni mzuri wa umbo na mbora wa mwenendo na tabia, na sifa zake njema pamoja na hekima na uhodari wa kuyapima mambo katika akili yake, vyote hivyo vinajulikana na kila mtu”.
Walipokuwa katika hali ile alipita mbele yao mtu mrefu, mwingi wa haiba aliyevaa nguo zilizoshonwa vizuri na kupambwa, pamoja na kilemba, na nyuma yake kundi la watu lilikuwa likimfuata.
Watu wote walinyamaza kimya huku wakimtazama mtu huyo alipokuwa akipita, kisha mmoja wao akasema kwa sauti ndogo hafifu:
“Huyu ndiye Khuwaylid baba yake Khadija, na walio nyuma yake ni watu wa kabila lake”.
Mwengine akasema:
“Amekuja kutufu Al Kaaba kama kawaida yake ya kila siku”.
Baada ya kutufu Al Kaaba, Khuwaylid akatafuta mahala karibu na Al Kaaba ili aweze kukaa na kujipumzisha, na alipokuwa katika hali ile, kijana mmoja aliiunuka na kwenda kumkabili.
Kijana huyo alikuwa mwenye sura na umbile la kupendeza ambaye kutokana na vazi lake alionyesha kuwa ni mtu tajiri sana, na nyuma yake pia kundi la watu lilikuwa  likimfuata kwa heshima na adabu.
Mtu huyo alikuwa ni Atiq bin Aidh, mmoja katika watu wanaoheshimika miongoni mwa matajiri wakubwa wa kabila la Kikureshi.anayetokana na kabila la Bani Makhzum.
Mmoja katika wale vijana akasema:
“Mtizameni vizuri! Mtu huyu anapigiwa mifano katika ushujaa na ukarimu”.
Baada ya kumkabili Khuwaylid bin Asad, Atiq akamwambia:
“Asubuhi njema ewe Khuwaylid”.
Khuwaylid akamjibu:
“Njema kwako pia ewe Atiq”.
Atiq:
“Nimekuja kwa ajili ya mazungumzo na wewe ewe mwana wa ami yangu, lakini mazungumzo yenyewe hayafai kuzungumzwa hapa penye Al Kaaba mbele ya watu”.
Khuwaylid akamwambia:
“Karibu nyumbani kwangu”.
Siku ya pili yake Atiq akamwendea nyumbani kwake na kumwambia:
“Nimekuja kumposa binti yako ewe bin ami yangu”.
Khuwaylid akamuuliza:
“Umekuja kumposa Khadija au Hala?”
“Bali nimekuja kumposa Khadija ewe bin ami yangu”.
“Vyema, lakini itabidi kwanza nimuulize Khadija mwenyewe ili nijuwe rai yake."
Atiq akasema kwa mshangao:
“Lakini wewe ni baba yake na unanijuwa mimi vizuri na unaijuwa daraja yangu katika kabila la Kikureshi pamoja na mwenendo na tabia zangu”.
Khuwaylid akamjibu:
“Bila shaka ewe bin ami yangu natambuwa yote hayo, natambua vizuri pia kuwa anakustahikia mwanamke yeyote wa Kikureshi, isipokuwa mimi siwezi kuamua lolote juu ya Khadija mpaka kwanza nimuulize mwenyewe na aridhike.”
Atiq akaondoka huku akisema kumwambia Khuwaylid:
“Vyema, fanya hivyo na mimi nitasubiri”.
Baada ya Atiq kuondoka, Khuwaylid akaingia kwa binti yake Khadija na kumjulisha juu ya Atiq, akamwambia:
“Ewe Khadija, kwa hakika Atiq amekuja kukuposa, nini rai yako?”
Khadija akasema kumwambia babake:
“Nini rai yako wewe kwanza ewe baba yangu?”
Baba yake akamwambia:
“Yeye ni bwana katika mabwana wa Kabila la Bani Makhzum na ana mali nyingi sana”.
Bibi Khadija akasema:
“Baba yangu, mimi sikuulizi juu ya sifa hizo, bali nataka kujuwa juu ya sifa zake nyingine kama vile ushujaa na ukarimu na kwamba hawafanyii ubakhili wenye kuhitaji wanapomwendea.”
Baba yake akamwambia:
“Atiq bin Aaidh yuko kama ulivyosema ewe Khadija. Yeye ni shujaa, mkarimu anayependa wageni. Hakika sifa zote unazozitafuta anazo mwanamume huyu”.
Bibi Khadija akasema:
“Basi, ikiwa ni hivyo fanya vile unavyoona wewe kuwa ni sawa ewe baba yangu”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akaolewa na Atiq wakapata mtoto waliyempa jina la Hind, na wakaishi kwa wema mpaka alipofariki mumewe jambo lililomfanya Bi Khadija awe na huzuni kubwa.

Anaolewa na Abu Halah

Haukupita muda mrefu bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaolewa na Nibash bin Zirarah Al Tamimi aliyekuja kujulikana kwa jina la ‘Abu Halah”,  na wakapata watoto wawili waliowapa majina ya Hind na Halah. Waliishi kwa wema mpaka mumewe wa pili naye pia alipofariki dunia, na haukupita muda mrefu baba yake Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) naye pia akafariki dunia, jambo lililozidisha huzuni moyoni mwake. (zipo riwaya zinazosema kuwa baba yake bi Khadija alifariki dunia baada ya binti yake kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba yeye ndiye aliyeifunga ndoa yao. Hata hivyo riwaya zenye nguvu zaidi zinasema kuwa alifariki kabla ya bibi Khadija kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba aliyefunga ndoa ya bibi Khadija na Mtume (Swalla Laahu alayhi wa sallam)alikuwa kaka yake anayeitwa Amru bin Khuwaylid.

Baada ya misiba hiyo iliyofuatiliana, Bibi Khadija aliyerithi mali nyingi sana kutoka kwa baba yake na kutoka kwa waume zake waliofariki, aliamua kujitenga na watu akawa anajishughulisha na ulezi wa wanawe.
Watu wengi walipeleka posa kutaka kumuoa, lakini Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliwakataa kwa sababu alihisi kuwa wote hao walikuwa wakimtaka kwa ajili ya tamaa ya mali yake na uzuri wake.

Hakupata kulisujudia sanamu

Baada ya kupatwa na misiba miwili hiyo, (kufiwa na mumewe wa pili na kufiwa na baba yake) Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliishi akiwa mwingi wa huzuni na mwingi wa kutafakari. alijitenga mbali na watu na aliacha hata kwenda kutufu Al Kaaba kama alivyokuwa akifanya hapo mwanzo.
Inajulikana kuwa Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu yaliyokuwepo hapo, na hii ni siri aliyomjulisha bin ami yake maarufu Waraqah bin Noufel aliyekuwa akifuata dini ya Manasara.
Waraqah bin Noufel huyu alikuwa mcha Mungu sana na alikuwa akisoma sana vitabu vilivyotangulia na kwa ajili hiyo alikuwa akijulikana sana miongoni mwa waarabu wa Makka kwa ucha Mungu wake na wema wake.

Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na uso uliojaa huzuni alikwenda kumtembelea bin ami yake huyo aliyemuuliza:
“Kuna nini binti ami yangu, mbona nakuona una huzuni nyingi?”
Bibi Khadija akamwambia:
“Sijaiona tena furaha tokea alipofariki baba yangu, na mali nyingi niliyoirithi haikuweza kuziba pengo lake”.
Waraqah akamwambia:
“Usihuzunike ewe binti ami yangu, utakuja kuonana naye Akhera”.
Bibi Khadija akashangaa:
“Akhera? Ni kitu gani hicho kinachoitwa akhera ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Hayo ni maisha baada ya kifo, na katika maisha hayo kila nafsi itapata jaza yake kutokana na yale yaliyotanguliza mikono yake”.
Bibi Khadija akauliza huku akitetemeka:
“Ina maana kuwa baba yangu hivi sasa yuhai?”
Waraqah akamwambia:
“Ndiyo, roho yake iko hai, isipokuwa mwili wake ushachanganyika na udongo wa ardhi”.
Bibi Khadija akaanza kusema huku mwili wake ukiwa unamtetemeka:
“Bin ami yangu, nataka kukupa siri niliyoizuwia moyoni mwangu tokea nilipokuwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita”.
Waraqah akasema:
“Sema ewe binti ami yangu wala usiwe na khofu”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akasema:
“Nilipokuwa na umri wa miaka sita hivi, nilikwenda siku moja pamoja na baba yangu penye Al Kaaba nikamuona akisimama mbele ya masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe kisha anayakabili na kukiinamisha kichwa chake kwa kuyaheshimu. Nikamuuliza:
“Nini haya masanamu ewe baba yangu?”
Akaniambia:
“Hii ni miungu tunayoiabudu”.
Nikashangazwa nikiwa bado mdogo, vipi watu wanayaabudu mawe yasiyoweza kudhuru wala kunufaisha?”
Waraqah akamtizama Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) huku akitabasamu, kisha akamwambia:
“Uliwahi kumhadithia mtu yeyote katika watu wa nyumbani?”
Bibi Khadija akasema:
“Abadan, abadan. Sijapata kumhadithia mtu yeyote, kwani nilikuwa nikiogopa sana, nikaificha siri hii mpaka nilipokuja kukuhadithia wewe sasa hivi. Nini rai yako ewe bin ami yangu?”
Waraqah akamwambia:
“Huo ndio ukweli wenyewe. Yale ni mawe tu yasiyodhuru wala kunufaisha. Na atatokea katika zama zetu hizi Mtume anayesubiriwa atakayeyavunja masanamu haya na kuondoa ushirikina na uonevu katika ardhi”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akauliza:
“Na lini atakuja Mtume huyo?”
Waraqah akasema:
“Mwenyezi Mungu ndiye Anayejuwa zaidi, isipokuwa vitabu vinasema kuwa; atatokea Mtume katika wakati huu wetu na yeye ndiye atakayekuwa mwisho wa mitume”.
Bibi Khadija akauliza:
“Na katika kundi lipi atatokea mtume huyo?”
Waraqah akasema:
“Allahu aalam, lakini Mayahudi wanasema kuwa atakuwa katika wao, na vitabu vinasema kuwa atakuwa miongoni mwa Waarabu”.
Bibi Khadija:
“Na uliyajuaje yote haya ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Haya yameandikwa katika Tuarati kitabu cha Mayahudi na katika Injili kitabu cha Manasara”.
Bibi Khadija akaondoka hapo huku mawazo yake yote yakiwa juu ya huyo Mtume mpya aliyebashiriwa na bin ami yake atakayeuondoa ushirikina na dhulma na jeuri iliyopindukia mipaka, lakini wakati huo huo mazungumzo hayo yalimsaidia sana katika kupunguza uzito uliokuwepo kifuani pake na huzuni aliyokuwa nayo, na kwa ajili hiyo akaanza tena kufanya shughuli zake za kawaida pamoja na za kibiashara.

Anamuajiri Muhammad

Katika shughuli zake za kibiashara bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alikuwa akiwaajiri wanaume wawili kila mwaka. Mmoja kwa ajili ya kwenda Sham wakati wa Kusi na mwengine kwa ajili ya kwenda Yemen wakati wa Kaskazi. Na hivi ndivyo yalivyokuwa maisha ya kibiashara Bara ya Arabu yote.
Wakati huo huo Muhammad bin Abdillah (Swalla Laahu alayhi wa sallam) (kabla ya kupewa utume) alikuwa akiishi pamoja na ami yake Abu Talib baada ya kufariki kwa babu yake Abdul Muttalib, na alikuwa akimsaidia ami yake katika shughuli za kibiashara na katika kuchunga kondoo na mbuzi mpaka alipofikia umri wa miaka ishirini na mitano, na kutokana na  uaminifu wake na ukweli wake, watu wa Makka walikuwa wakimuheshimu sana.
Hii ukijumuisha pia kuwa Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu waliyokuwa wakiyaabudu na kuyaogopa wala hakupata kunywa pombe, na hakuwa akijishughulisha na anasa wala starehe ya aina yoyote ile katika starehe walizokuwa wakijishughulisha nazo vijana wa wakati ule.
Alikuwa mwema, msema kweli, muaminifu, mwenye tabia na mwenendo mwema uliompendeza kila mtu, na alikuwa na haiba kubwa sana pale Makka hata akawa maarufu miongoni mwao kwa jina la ‘Al Swaadiqul Amin’, bimaana Mkweli Mwaminifu.au ‘Muhammad Al Amin’, na maana yake ni Muhammad muaminifu.

Sifa zote hizo zilikuwa zikimfikia bibi Khadija aliyekuwa mfanya biashara maarufu pale Makka pamoja na sifa nyingine mbali mbali, na pia zilikuwa zikimfikia habari za kusafiri kwake pamoja na ami yake Abu Talib katika shughuli za kibiashara kwenda nchi ya Sham, na kwamba ami yake alikuwa akipata faida kubwa sana tokea alipoanza kushirikiana naye katika shughuli hizo.
Habari hizo zikawa zinamshughulisha sana bibi Khadija na usiku mmoja katika siku za joto alipokuwa amekaa juu ya dari la nyumba yake pamoja na mwanamke mmoja aitwae Nafisa binti Munabih, bibi Khadija alikuwa akitazama chini sana huku akitafakari, jambo lililomfanya Nafisa amuulize:
“Unatafakari juu ya nini ewe Khadija?”
Bi Khadija:
“Natafakari juu ya jambo la ajabu sana”.
Bi Nafisa:
“Unanificha mimi?”
Bi Khadija:
“Mimi siwezi kukuficha kitu ewe Nafisa, jambo lenyewe linahusiana na Muhammad bin Abdillah!”.
Bi Nafisa:
“Ah! Muhammad Muaminifu. Unataka nini kwake?”
Bi Khadija:
“Muhammad Muaminifu husafiri baadhi ya wakati kwa ajili ya shughuli za kibiashara pamoja na ami yake Abu Talib, ningefurahi kama angekubali pia kushughulikia biashara zangu maana yeye ni mtu wa pekee ninayeweza kumuaminisha katika mali yangu. Lakini sijuwi vipi nitaweza kumjulisha?”
Nafisa:
“Mimi, mimi ndiye nitakayemjulisha ewe Khadija, lakini nitazungumza na ami yake Abu Talib maana naona haya kumkabili Muhammad juu ya jambo hili.”
Abu Talib akalikubali ombi hilo na akamnasihi Muhammad akubali pia, na Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akamwambia ami yake:
“Ikiwa wewe unaona sawa, basi na mimi nimekubali”.
Bibi Khadija alifurahi sana alipojulishwa kuwa Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amelikubali ombi lake, akatayarisha msafara wa biashara na kumtaka mtumishi wake Maysara afuatane na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kwa ajili ya kumhudumia na kumshughulikia katika safari ndefu hiyo.
Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akafanikiwa kuuza bidhaa zote za bibi Khadija katika masoko ya Sham na akarudi akiwa amempatia faida kubwa sana kuliko alivyowahi kupata miaka yote iliyopita.

Rudi naye Makka haraka sana

Tokea waliporudi kutoka safari ya Sham yule kijana Maisara aliyevutiwa sana na tabia na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alouona walipokuwa safarini, akawa anamuhadithia bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) juu ya yale aliyokuwa akiyaona safarini walipokuwa wakienda na walipokuwa wakirudi na baadhi ya miujiza iliyokuwa ikitokea.
Bibi Khadija naye aliyekuwa wakati wake wote anawaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kila mara kuhadithiwa juu ya sifa zake hizo, na siku moja alipokuwa amekaa pamoja na mtumishi wake huyo, akamwambia:
“Enhe! Hebu nihadithie vizuri juu ya safari yako na Muhammad”.
Maisarah akasema:
“Sikupata kuona mtu bora wa kusafiri naye kuliko yeye. Alikuwa mtulivu, hana kiburi, mkarimu na mpole sana. Nilikuwa ninapoumwa ananishughulikia na ninapochoka ananisaidia, na alikuwa akigawana na mimi sawa sawa chakula chake na maji yake. Kwa hakika alikuwa akinitendea kama kwamba ni ndugu yake.
Lakini jambo lililonistaajabisha zaidi ewe bi Khadija,” akaendelea kusema: “kulikuwa na kiwingu kilichokuwa kikimfuata wakati wote tokea tulipoondoka mpaka tuliporudi. Kilikuwa kikimfuata na kumkinga na juwa kali wala hakuwa akihisi joto hata kidogo wakati wote wa safari.
Isitoshe, Muhammad hapendi kusema sana, na kila tunaposimama kwa ajili ya kupumzika alikuwa akijitenga peke yake na alikuwa akipenda kutizama mbinguni kwa khushuu na mdomo wake ulikuwa daima ukitikisika huku akisema maneno yasiyosikika”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa na shauku ya kutaka kujuwa zaidi habari za Muhammad akasema:
“Enhe! Kisha? Endelea, nini kilichotokea baadaye?”
Maisarah akasema:
“Tulipokuwa tukirudi Makka, tulisimama mahali muda mdogo kwa ajili ya kujipumzisha, na mimi nikaondoka kwenda kutafuta chakula cha ngamia, na mahali hapo palikuwa na mti mkubwa sana na Muhammad alikaa chini ya mti huo huku akitizama mbinguni kama kawaida yake kama kwamba anatafuta kitu, na karibu na mahali hapo palikuwa na hekalu la mcha Mungu mmoja aitwae Nastwur aliyenijia mimi na kuniuliza:
“Nani huyu kijana aliyekaa chini ya mti ule?”
Nikamwambia;
“Huyu ni kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi”.
Akaniambia:
“Umeona lolote lisilo la kawaida kutoka kwake?”
Nikamwambia:
“Nimeona kiwingu kikimfuata kikimkinga kutokana na jua kali tokea tulipoondoka na wala hakikumuacha abadan”.
Akauliza tena:
“Macho yake yakoje?”
Nikamjibu:
“Meusi na makubwa na katika weupe wake umo wekundu khafifu ndani yake”.
Akasema:
“Kijana huyu atakuwa na shani kubwa, rudi naye Makka haraka sana, kwani hakupata kukaa chini ya mti huu isipokuwa Nabii”.
Maneno haya yalimtia kizunguzungu bibi Khadija na tokea alipoondoka hapo akawa usiku na mchana hana analowaza isipokuwa juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

Sifa za aliyetakaswa

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akaanza kufikiri huku akikumbuka na kuunganisha maneno ya Maisarah na maneno aliyoambiwa na bin ami yake Waraqah bin Noufel, akawa anajisemesha:
“Kwa nini isinipitikie wakati wote huu? Huyu ndiye kijana anayetokana na mabwana wa kabila la Kikureshi anayejulikana kwa ukweli na uaminifu na upole na ukarimu, na Makureshi wote wanamuheshimu na kumtukuza kutokana na kujitenga kwake mbali na tabia zote mbaya walizokuwa nazo vijana wa kabila la Kikureshi na wengineo.
Na huyu ndiye kijana aliyesafiri na mali yangu na kunipatia faida kubwa sana, na huyu ndiye kijana ambaye kiwingu kilikuwa kikimkinga kutokana na juwa kali tokea alipoianza safari yake mpaka aliporudi. Na huyu ndiye kijana ambaye mcha Mungu Nastwur amesema juu yake kuwa atakuwa na shani kubwa akamtaka Maisarah arudi naye Makka haraka sana”.
Bibi Khadija akawa anawaza na kukumbuka yote hayo mpaka akawa na uhakika ndani ya moyo wake kuwa sifa kama hizi haziwezi kumuandama mtu wa kawaida.
Sifa njema kama hizi ambazo si kila mtu anaweza kuwa nazo hazipatikani isipokuwa kwa watu waliochaguliwa na kutakaswa.
Kutokana na yote haya, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akazidi kujishughulisha na kuwaza juu ya Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

Lakini umri wangu mkubwa

Baada ya kuwaza na kufikiri muda mrefu, bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akafikia uamuzi wa kutaka kuolewa na Muhammad (Swalla Laahu alayhi wa sallam).
“Kwa nini nisimtake Muhammad aniowe? Inagawaje fikra hii ni mfano wa ndoto, lakini ni jambo linalowezekana. Lakini vipi? Nani atakayekubali kunifikishia ombi langu?”
Alipokuwa katika hali ile, mlango ukagongwa.
“Nani anayegonga mlango?”
“Mimi dada yako Halah.”
Bibi Khadija akamkaribisha dada yake.
“Ahlan wa sahlan, karibu ewe Halah”
Halah:
“Ahsante Khadija vipi hali zenu?”
Khadija:
“Hatujambo, ziara hii ya ghafla naona.”
Khadija:
“Bila shaka ewe dada yangu, kwani nimekuja kukujulia hali yako tu”.
Khadija:
“Kuijua hali yangu tu! Mbona unasema maneno ya kiajabu, au kuna jambo unataka kunificha?”
Halah akamtizama dada yake mtizamo wa kuchunguza, kisha akamwambia:
“Abadan, hakuna la kukuficha isipokuwa mchana wa leo ulinichukuwa usingizi nikakuota unatembea mfano wa mtu aliyepotea katika njia ya kiza na nyuma yako sauti inakwambia: “Nenda mbele, nenda mbele”. Nikaona bora nije kukujulia hali yako, ingawaje sijuwi ndoto hiyo tafsiri yake nini”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) akatabasamu kidogo kisha akasema:
“Kusema kweli mimi siku hizi ninaishi ndani ya mawazo mengi sana.”
Halah:
“Unawaza juu ya nini na wewe upo katika neema kubwa kama hii?”
Khadija:
“Muhammad, ewe dada yangu. Nafikiri juu ya sifa zake na utukufu wake ambao hajapata kuufikia hata mmoja katika watu wa kabila la Kikureshi.”
Halah:
“Na nini mwisho wa fikra hizo?”
Khadija:
“Nataka aniowe”.
Halah:
“Basi muombe akuowe”.
Bibi Khadija akamjibu kwa uoga:
“Naogopa asije akanikataa, kwani yeye ni kijana anayeheshimika kupita vijana wote”
Halah:
“Na wewe pia dada yangu ni mtu mtukufu unayeheshimika na watu wote”.
Khadija:
“Lakini umri wangu mkubwa unaokaribia miaka arubaini, na nishaolewa mara mbili, wakati yeye bado ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitano na bado hajapata kuowa. Vipi Muhammad atakubali kumuowa mwanamke aliye na umri sawa na mama yake aliyekwisha olewa mara mbili na ana watoto?”
Halah akasema:
“Nani aliyekujulisha na Muhammad mara ya mwanzo hata ukaweza kumpa mali yako aifanyie biashara?”
Khadija:
“Rafiki yangu mmoja anayeitwa Nafisa”.
Halah:
“Basi Nafisa huyo huyo ndiye atakayeweza kukufikishia ombi lako hilo”.
Kisha Halah akamuaga dada yake na kuondoka

Anaolewa na Muhammad

Ziara ya Hala ilikuwa mfano wa ufunguo wa kheri katika nafsi ya bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), kwani siku ya pili yake Nafisa alipokuja kumtembelea bibi Khadija, akamhadithia juu ya mazungumzo yaliyopita baina yake na baina ya dada yake Halah, na Nafisa akakubali kuchukuwa jukumu la kulifikisha ombi hilo kwa Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Alipoondoka, Nafisa alielekea moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Talib alipokuwa akiishi Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na alipomuona akamwambia:
“Ewe Muhammad, wewe una umri wa miaka ishirini na tano na mpaka sasa bado hujaowa.”
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akashangazwa sana na maneno hayo, akamuuliza:
“Kipi kilichokufanya ujishughulishe na jambo hili ewe Nafisa?”
Nafisa:
“Bibi anayeheshimika anataka umuowe, nini rai yako?”
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam):
“Bibi gani huyo?”
Nafisa:
“Bibi huyo ni Khadija binti Khuwaylid, na wewe unamuelewa vizuri juu ya heshima yake na utukufu wake na sifa zake zote njema”.
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
“Naam, hakika yeye ni mtu anayeheshimika, lakini mimi sina mali hata niweze kumuowa.”
Nafisa;
“Yeye hana haja ya mahari, kwani unajuwa vizuri kuwa yeye hana shida ya mali na anao utajiri mkubwa”.
Muhammad:
“Mimi utajiri haunishughulishi, kwani mali inakuja na kuondoka, na Khadija pia ni mwanamke mzuri wa umbo na tabia na mwenendo, lakini niache nimshauri ami yangu kwanza juu ya jambo hili”.
Ami yake akamwambia:
“Ewe Muhammad, hii ni bahati iliyokujia kutoka mbinguni. Naapa kuwa Khadija ni mwanamke aliyetakasika kupita wote katika Makka na mwenye akili na uwezo wa kupima mambo kupita wote, na mwenye hekima kupita wote na anayetokana na ukoo bora kupita wote. Wangapi wenye mali na jaha walitaka kumuoa akawakataa, na leo anakutaka wewe wakati huna mali yoyote, hii ni bahati kubwa.
Kubali ewe mwana wa ndugu yangu, kwani asingekutaka isipokuwa amekuwekea heshima kubwa sana”.
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akakubali, na bibi Khadija akafanya arusi kubwa sana iliyohudhuriwa na watu wengi, na wanyama wengi sana wakachinjwa siku hiyo na kila muhitaji alifaidika.

Kuzaliwa kwa Qassim

Bibi Khadija (Radhiya Llahuu anha) alizaa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) watoto sita. Wanaume wawili na wanawake wanne. Watoto wa kiume aliwapa majina ya Qassim na Abdullah, aliyekuwa akijulikana pia kwa jina la Al Taher. Na watoto wa kike ni Ruqayyah na Zeinab na Ummu Kulthum na Fatima (Radhiya Llahuu anhunna).

Katika mwaka wao wa mwanzo tokea kuoana walijaaliwa kupata mtoto wa kiume waliyempa jina la Qassim, wakafurahi sana, na kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawa anajulikana kwa jina la ‘Abal Qassim’, na maana yake ni 'baba yake Qassim'.
Lakini Qassim hakuishi muda mrefu, kwani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka miwili, na wazee wake walihuzunika sana, lakini walisubiri na kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Kisha akazaliwa Abdullah aliyefariki pia akiwa mtoto mchanga, kisha Zeinab, kisha Ruqayah aliyefanana na mama yake, kisha akazaliwa Ummu Kulthum, kisha akazaliwa Fatima aliyefanana sana na baba yake hasa katika mwendo na sauti.

Sikubali kuachana naye

Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) aliingia nyumbani akiwa amemshika mkono mtoto mdogo, akamkabili Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Mtoto huyu nakupa zawadi, mchukuwe, atakusaidia na kukuhudumia”.
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtizama mtoto yule machoni akaona dalili ya hekima ndani yake, akamuuliza:
“Jina lako nani na ilikuwaje ukatekwa?”
Mtoto akajibu:
“Jina langu ni Zeid bin Harithah, natokana na kabila la Kalbin na nilikamatwa na kundi la mabedui walionileta katika soko la Akadha na kuniuza huko”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akafurahishwa naye, akawa anampenda na kumkirimu sana, na Zeid naye alikuwa akimpenda sana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na katika nyakati za usiku pale Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anapojishughulisha na kutafakari na kuomba, mtoto huyo alikuwa karibu yake kwa ajili ya kumtumikia.
Baba yake Zeid alipopata habari za kutekwa kwa mwanawe na baada ya kuulizia ulizia na kujulishwa kuwa mwanawe alikuwa amemilikiwa na Muhammad bin Abdillah, akaifunga safari ya kuelekea Makka na alipowasili alisimama mbele ya Al Kaaba akasema kwa sauti kubwa:
“Enyi watu wa Makka! Nyinyi ni watu wakarimu mnaohudumia mahujaji na mnaowasaidia mateka. Nimekujieni kwa ajili ya mwanangu aliye mikononi mwenu nataka munirudishie mwenyewe”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposikia maneno hayo akatangulia mbele na kumkabili Harithah huku akiwa amemshika mkono Zeid, akainama na kumuuliza:
“Unawajua ni nani hawa?”
Zeid akasema:
“Ndiyo. Huyu ni baba yangu na yule ni ami yangu”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)akamwambia:
“Basi wazee wako hawa wamekuja kukuchukua ili urudi nao”.
Kisha akamuacha mkono na kumtanguliza mbele yao.
Zeid (Radhiya Llah anhu) akamkabili baba yake na kumwambia:
“Baba yangu, mimi sikubali kuachana na mtu huyu abadan, huyu ni mtu adhimu mwenye moyo mkubwa uliobarikiwa, na kama mmoja wenu ataishi naye siku moja tu, basi hatokubali kuachana naye maisha yake yote.”
Kisha akamkabili Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Sitomchaguwa mwengine isipokuwa wewe tu. Wewe ndiye baba yangu na wewe ndiye ami yangu”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alitokwa machozi ya furaha, akamshika mkono Zeid huku akiyafuta machozi yake, kisha akasogea naye mpaka penye uwanja wa Al Kaaba na kusema kwa sauti kubwa:
“Shuhudieni kuwa Zeid ni mwanangu, ananirithi na mimi namrithi”.
Maneno haya yalimfurahisha sana hata Harithah baba yake Zeid kwa kujuwa kuwa mwanawe si kama ameachwa huru tu, bali amekuwa mwana wa Muhammad Mkweli Mwaminifu. Na hii ilikuwa ndiyo kawaida iliyokuwa ikitumika wakati ule.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana Zeid (Radhiya Llah anhu) hata akawa anajulikana kwa jina la Zeid bin Muhammad mpaka pale ilipoteremshwa aya ya nne ya Suratul Ahzab iliyoharamisha mtu kuitwa kwa ubini usiokuwa wa baba yake.
Mwenyezi Mungu anasema:
“Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na kama hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika dini na rafiki zenu”.
Kisha Mwenyezi Mungu akaharamisha pia mtu kurithiwa na mwanawe wa kupanga (adopted child) katika aya ya 75 ya Suratul Anfal aliposema:
“Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (katika kurithiana). (Ndivyo ilivyo) Katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.”

Aly (Radhiya Llah anhu)

Katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwepo mtoto mwingine wa kiume naye ni Hindu mtoto wa bibi Khadija kwa mume wake wa  pili ’Abu Halah’, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda sana na akamlea malezi bora, akamuonyesha mapenzi na huruma na alikuwa akimtendea kama anavyowatendea wanawe.
Alipotimia miaka minane, Aly (Radhiya Llah anhu) naye akachukuliwa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kulelewa katika nyumba ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kwa ajili ya kumpunguzia ami yake Abu Talib mzigo wa ulezi baada ya ami yake kupata shida mbali mbali.
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) alimpokea Aly (Radhiya Llah anhu) kwa furaha na akamlea na kumuenzi kama anavyowalea na kuwaenzi wanawe.

Anakwenda Ghaari Hiraa

Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimwambia bi Khadija (Radhiya Llah anha) kuwa anahisi moyoni mwake kama kwamba anatakiwa ende penye pango linaloitwa Ghaari Hiraa nje kidogo ya mji wa Makka.
Bi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia:
“Haya nenda, lakini pango hilo liko nje ya mji na mimi nakuogopea wewe kubaki huko peke yako”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Usiogope Khadija, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja nami”.
Baada ya bibi Khadija (Radhiya Llah anha) kumtayarishia chakula pamoja na baadhi ya mahitajio yake, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaondoka na kuelekea Ghaari Hiraa kwa ajili ya kukaa huko na kutafakari juu ya Mwenyezi Mungu.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kwenda pangoni hapo na kukaa kimya huku akitazama juu mbinguni. Alikuwa akiziangalia nyota na sayari, juwa na mawingu, mvua na upepo huku akitafakari na kujiuliza:
“Nani aliyevitengeneza vyote hivi? Bila shaka ipo nguvu kubwa yenye uwezo wa kuumba uhai pamoja na kuvitengeneza vyote hivi”.
Akawa anaendelea katika hali hii ya kutafakari wakati mkewe bi Khadija (Radhiya Llah anha) akibaki nyumbani na kuendesha shughuli zake. Lakini bibi Khadija alikuwa kila anapomfikiria mumewe akiwa peke yake pangoni tena nje ya mji alikuwa wakati wa mchana hana raha na wakati wa usiku hapati usingizi.
Alikuwa kila siku akimtuma mtu kwenda pangoni huko ili amletee habari za Muhammad na pia kwa ajili ya kumpelekea maji na chakula na baadhi ya mahitajio yake, na mara nyingine alikuwa akienda yeye mwenyewe.
Siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alirudi nyumbani kutoka pangoni akiwa na hofu kubwa sana, na bibi Khadija alipomuona katika hali ile akamuuliza:
“Kuna nini Muhammad?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Ewe Khadija! Nilipokuwa nikitembea huku na kule juu ya jabali, ghafla nikaona nuru iking’ara juu yangu kisha nikasikia sauti ikiniita:
“Ewe Muhammad, ewe Muhammad”.
Bibi Khadija akamuuliza:
“Na umeweza kujuwa sauti hiyo inatokea wapi ewe Abal Qassim?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Sikuweza kujuwa ewe Khadija, na nilikuwa kila ninapoisikia sauti ninageuka huku na kule kumtafuta mwenye sauti hiyo na wala simuoni mtu, nikaingiwa na hofu na kuamua kurudi nyumbani”.
Bibi Khadija akafanya haraka kumwendea bin ami yake Waraqa bin Noufel na kumhadithia yote aliyohadithiwa na Muhammad, na Waraqah akamwambia:
“Ewe binti wa ami yangu, hizi ni bishara njema kutoka mbinguni, mpe hongera zangu Muhammad na mwambie awe mvumilivu”.

Zammiluni zammiluni

Muhammd (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda Ghaari Hiraa, na bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akawa anaendelea kumshughulikia kwa kuwatuma watumishi wampelekee vyakula na mahitajio yake ya kila siku na wakati mwingine yeye mwenyewe alikuwa akienda kumtembelea mumewe pangoni mpaka ilipofika siku ile aliporudi nyumbani Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akiwa anatetemeka huku meno yake yakigongana na kumwambia mkewe:
Zammiluni zammiluni’ – na maana yake (nifunikeni, nifunikeni). Bibi Khadija akamlaza mumewe kitandani kisha akamfunika huku akimpangusa  jasho lililokuwa likimtoka kwa wingi kichwani na huku akimwambia maneno ya kumtuliza mpaka usingizi ulipomchukuwa.
Aliamka akiwa bado uoga unaonekana usoni pake na bibi Khadija akamuuliza:
“Una nini ewe Abal Qassim?”
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Nilikuwa nimekaa pangoni, ghafla nikaona nuru juu yangu iliyonipitia kama umeme, kisha nikamuona mtu anateremka kutoka mbinguni huku akinikaribia. Nikaingiwa na khofu, lakini mtu huyo akaninyanyua na kunibana kwa nguvu kifuani pake kisha akaniacha, kisha akaniambia:
Iqra-a” – (‘soma’)
Nikamjibu kuwa mimi sijuwi kusoma. Akaninyanyua tena na kunibana kwa nguvu zaidi kifuani pake kisha akaniacha na kuniambia tena:
“Iqra-a”
Nikamwambia:
Maa – ana biqaarii – (Mimi sijuwi kusoma).”
Kisha akaninyanyua tena mara ya tatu na kunibana tena kifuani pake kisha akaniacha akaniambia tena:
اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1} خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2} اقْرَأْ وَرَبُّكَ
الْأَكْرَمُ {3} الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4} عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}
(Soma kwa jina la Mola wako Aliyekuumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye amefundisha kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui).
Al Alaq – 1-7
Maneno hayo yalimshituwa sana bibi Khadija, akamtaka Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) avae nguo haraka na afuatane naye mpaka kwa Waraqah bin Noufel ili amhadithie mwenyewe yale aliyoyaona, na Waraqah akamwambia:
“Huyu ndiye Malaika mkubwa ‘Jibril’ ambaye Mwenyezi Mungu aliwateremshia Musa na Issa, yareti kama ningeliishi mpaka pale watu wako watakapokutoa nchini kwako”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuuliza:
“Hivyo watakuja kunitoa?”
Waraqah akasema:
“Ndiyo, hapana aliyekuja na haya uliyokuja nayo wewe isipokuwa lazima atafanyiwa uadui, na nikijaaliwa kuishi mpaka siku hiyo, basi nitakusaidia mpaka utakapopata ushindi”.

Bibi Khadija akarudi nyumbani haraka akiwa amefuatana na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) huku moyoni mwake akiona fahari kubwa kuwa baraka za utume zimeangukia nyumbani kwake.
Siku moja bibi Khadija aliingia nyumbani kwake na kumuona Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akitetemeka mwili mzima juu ya tandiko lake huku akisema:
“Khadija. Jibril amenijia tena, akaniambia:
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1} قُمْ فَأَنذِرْ {2} وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ {3} وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ {4}
وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ {5} وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ {6} وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ {7}
“Ewe uliyejifunika maguo. Simama uonye (viumbe). Na Mola wako umtukuze. Na nguo zako uzisafishe. Na mabaya yapuuze. Wala usiwafanyie ihsani(viumbe) ili upate kujikithirishia (wewe hapa duniani). Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira (kwa kila yatakayokufika).”
(Suratul Mudathir aya ya 1 mpaka 7)
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akainua uso wake kutizama juu mbinguni huku akimshukuru Mola wake, kisha akamtizama Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyekuwa akionyesha kuwa amechoka sana na kumwambia:
“Tulia upumzike ewe Muhammad”.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Zimekwisha zama za kupumzika ewe Khadija. Na umewadia wakati wa jihadi. Jibril keshanijia na ananitaka niianze kazi ya kuufikisha kwa watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu utakaouondoa ushirikina pamoja na uchupaji wa mipaka.”
Bibi Khadija (Radhiya Llah anha) akamwambia mumewe:
Labbayka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mimi ni wa mwanzo kukuamini”.
Akasilimu bibi Khadija pamoja na wanawe wote wakiwemo Aly na Zeyd (Radhiya Llah anhum), lakini haukupita muda mrefu Waraqa bin Noufel alifariki dunia kabla ya kupewa utume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) jambo lililomhuzunisha sana bibi Khadija, kwani Waraqah alikuwa akiwasaidia sana katika kumliwaza Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wakati wa hofu, na kwa ajili hiyo bibi Khadija akahisi kuwa mzigo huo sasa umemuangukia yeye.
Hata hivyo bibi Khadija alikuwa akimsaidia sana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale anapoona dhiki, hasa katika zile siku ambazo wahyi unakatika na Jibril anachelewa kumshukia, hapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) humwendea bibi Khadija na kumsikitikia na bibi Khadija kwa upande wake humpoza na kumwambia:
“Hapana ewe Muhammad. Wallahi Mwenyezi Mungu hawezi kukuhizi abadan, kwani wewe ni mkweli muaminifu, uliyetakasika mwenye kuwaendea watu wako na mwenye kuwasaidia wenye kuhitaji na kumuokoa mwenye dhiki”.

Mpe Khadija salamu

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akawa anaendelea kwenda pangoni kwa kufanya ibada zake, na mara nyingi Jibril (Alayhis Salaam)  alikuwa akimjia.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa asubuhi moja bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alipokuwa njiani kuelekea pangoni alikutana na mwanamume mmoja aliyemsalimia na kumuuliza juu ya Muhammad. Bibi Khadija hakumjibu mtu huyo akihofia asije kuwa adui anayeweza kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam). Ikajulikana baadaye kuwa huyo alikuwa Jibril katika sura ya kibinadamu. Kwani Jibril alitangulia kufika pangoni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Khadija sasa hivi atawasili akiwa amebeba chakula na maji kwa ajili yako. Atakapowasili mpe salamu zitokazo kwa Mola wake na mpe bishara njema juu ya nyumba aliyokwishajengewa Peponi”.
Baada ya kutaabika njiani, bibi Khadija aliwasili pangoni na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alimpokea kwa furaha huku akimwambia:
“Bishara njema kwako ewe Khadija. Amenijia Jibril hivi punde na amenipa salamu zitokazo kwa Mola wako Anayekupa bishara njema juu ya nyumba uliyokwishajengewa huko Peponi”.

Kufariki kwa Bibi Khadija

Watu wakaanza kuingia katika dini ya Kiislamu kwa wingi, na Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alikuwa wa mwanzo katika wanaume akifuatiliwa na Uthman bin Affan, Al Zubeir bin Awaam, Abdul Rahman bin Auf, Saad bin Abi Waqaas na Talha bin Ubaidullah (Radhiya Llahu anhum). Wote hawa walisilimishwa na Abubakar siku ya mwanzo baada ya kusilimu yeye mwenyewe, akaenda nao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliobashiriwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) kuwa wataingia Peponi.
Siku iliyofuata Abubakar (Radhiya Llahu anhu) aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), nao ni Uthman bin Madha-un, Abu Ubaidah Aamir bin Al Jarraah, Abu Salama na Al Arqam bin Abi l Arqam.

Bibi Khadija naye aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam, na kwa ajili hiyo nguvu ikaanza kuongezeka kidogo kidogo jambo lililowaghadhibisha sana Makureshi, wakaamua kuwazunguka na kuwapiga pande Waislamu muda wa miaka mitatu na kuwazuwia wasiweze kununua chochote, hata chakula. Ukawapitikia Waislamu wakati mgumu sana mpaka wakawa wanakula majani ya miti.
Waislamu wakahamia katika nyumba za Abu Talib, na bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wakati mwingine akihatarisha maisha yake kwa kununua chakula na kuwapelekea kwa siri.
Haukupita muda mrefu tokea kumalizika kupigwa pande huko alifariki dunia Abu Talib ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na miezi miwili baadaye akafariki mama wa Waislamu Bibi Khadija binti Khuwaylid (Radhiya Llahu anha) katika mwaka uliokuja kujulikana kama ‘mwaka wa huzuni’ kwa sababu katika mwaka huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alifiwa na wapenzi wake wawili hao waliokuwa wakimsaidia sana na kumkinga.

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akiwa na umri wa miaka sitini na mitano alifariki katika mwezi wa Ramadhani mwaka wa kumi tokea Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kupewa utume. Zipo riwaya zinazosema kuwa alifariki miaka mitatu kabla ya Hijra na riwaya nyingine zinasema miaka minne na nyingine zinasema mitano, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) mwenyewe ndiye aliyeteremka kaburini na kumzika na wakati huo hakukuwa na Swala ya maiti.

Baadhi ya sifa zake

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) hakupata kumpenda yeyote kati ya wake zake kama alivyompenda bibi Khadija (Radhiya Llahu anha), na hakuoa mke mwingine mpaka alipofariki bibi Khadija.
Ingawaje baadaye alioa wake wengi akiwemo bibi Aisha binti Abubakar (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa akipendwa sana kupita wake wenzake wote, lakini hakupata bahati aliyoipata bibi Khadija.
Hebu tumsikilize bibi Aisha mwenyewe (Radhiya Llahu anha) akituhadithia.
Anasema Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa daima akimtaja Khadija, na siku moja alikuja kututembelea Halah dada yake Khadija nyumbani kwetu Madina, na sauti yake ilikuwa imefanana sana na sauti ya Khadija, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alipoisikia tu sauti yake akasema:
“Allahumma huyu ni Halah dada yake Khadija mfungulie mlango upesi”.
Anasema bibi Aisha:
“Nilimuonea wivu Khadija nikasema kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu:
“Nakuona unampenda sana Khadija, huachi kumtaja kila siku kama kwamba hapana mwanamke mwengine duniani isipokuwa yeye. Khadija hakuwa na chochote cha zaidi isipokuwa alikuwa mwanamke mzee, na Mwenyezi Mungu amekwishakupa aliye bora kuliko yeye”.
Anaendela kusema bibi Aisha;
“Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alinikiasirikia sana siku hiyo kwa kauli yangu ile akaniambia:
“Hapana wallahi! Hakunipa aliye bora kuliko yeye, kwani yeye aliniamini wakati watu waliponikadhibisha na akanisaidia kwa mali yake wakati watu waliponinyima, na kupitia kwake akaniruzuku watoto”.
Anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Nikajisemea moyoni mwangu; 'sitomsema tena vibaya Khadija.”

Na katika hadithi nyingine anasema bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) alikuwa anapochinja mbuzi daima akipeleka nyama kwa marafiki wa Khadija, na siku moja nilimuuliza kwa nini anafanya hivyo, akanijibu:
“Mimi nawapenda wote alokuwa akiwapenda”.

Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) alikuwa wa mwanzo kupita wote kumuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), na wa mwanzo kusilimu miongoni mwa wanawake na wanaume, na wa mwanzo kuswali nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) wakiwa peke yao nyumbani.
Alikuwa mara nyingi akimliwaza na kumtuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) anapodhikika au anapoadhibishwa au kukadhibishwa au kutukanwa au anapopata mateso ya aina yoyote kutoka kwa makafiri wa Makka.

Mafunzo

1- Mtu asivunjike moyo hata kama ana tumaini dogo namna gani, kwani bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliliona tumaini ndani ya Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) pale alipokuwa akizihesabu sifa zake tukufu moja baada ya nyingine, akiwa na tumaini kuwa mtu huyu ndiye atakayekuwa Mtume anayesubiriwa, juu ya kuwa hizo zilikuwa ni fikra njema tu, lakini hatimaye zikageuka kuwa ukweli halisi.
    Alipotamani kuolewa naye, aliliona tumaini lake kuwa mfano wa ndoto, lakini hakuiacha iwe ndoto, bali alizindukana na kuifuatilia ndoto hiyo mpaka ikageuka kuwa kweli.

2- Mwenendo wa makafiri wa kuwazunguka Waislam na kuwapiga pande na kuwafanyia vikwazo vya kiuchumi na vya kibiashara na kuwaacha wakiwa na njaa wakidhani kuwa mwisho wake watakuja kuwapigia magoti. Darsi hii inatufundisha kuwa mila za kikafiri ni namna moja tokea wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) mpaka wakati wetu huu.

3- Mstahamilivu hula mbivu. Waislamu walistahamili kila aina ya tabu na adhabu, mateso na uadui uliokuja kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu tokea siku ya mwanzo, lakini ustahamilivu wao huo haukupotea bure, kwani hatimaye waliweza kupata dola yao na kupambana na adui zao waliokuja kuwapiga vita kutoka kila pembe ya dunia na kupata ushindi wa nyumba mbili. Nyumba ya dunia na nyumba ya Akhera.

2. Historia Ya Bibi 'Aaishah Bint Abiy Bakr As-Swiddiyq (رضي الله عنها)

Kwa hakika Uislamu umemkirimu mwanamke takrima kubwa kabisa, awe Mtoto wa Kike, awe Mke, awe Mama, au awe Dada.

Na Qur-aan imetaja baadhi ya wanawake,
mfano Mama yake Muusa (‘Alayhis Salaam), mke wa Fir’aun na Maryam bint ‘Imraan.

Na vile vile kuna miongoni mwa surah katika Qur-aan Kama vile Suratun Nisaa na At-Twalaaq zimezungumzia wanawake, vile vile kuna baadhi yawanawake kama vile Bibi ‘Aaishah ( رضي الله عنها), Bibi Khawlah,  ziliteremshwa Aayah za Qur-aan kwa ajili yao.

Kadhaalika imehadithia Qur-aan kuwa walimjia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلمWanawake Waumini ambao walimpa bai’ah walohama toka Makkah kwenda Madiynah, kama ilivyobainishwa katika  Surat Al-Mumtahinah.

Kwa hakika hizi ni miongoni mwa fadhila kubwa kabisa Alizowafadhilisha nazo Allaah wanawake na kuna nyingi nyenginezo.


'AAISHAH BINT ABIY BAKR ASW-SWIDDIYQ (رضي الله عنها) ALIE TAKASWA KUTOKA JUU YA MBINGU YA SABA

Hakika yeye ni mwalimu wa wanaume ni mkweli na mtoto wa mkweli Al-Qurayshiyah At-Taymiyah Al-Makkiyah.

Mama wa Waumini na ni Mke wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na  katika mke aliyekuwa akipendwa sana na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) vile vile ni mtoto wa Swahaba mtukufu aliyependwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

Bibi ‘Aaishahرضي الله عنها) ) aliyewekwa mbali na kutakaswa na machafu kutoka mbingu ya saba.

ثبت في الصحيحين أن عمرو بن العاص رضي الله عنه - سأل النبي صلى الله عليه وسلم - أي الناس أحب إليك يارسول الله؟ قال: "عائشة"  قال: فمن الرجال؟ قال: "أبوها" (أخرجه البخاري)

Imethibiti kutoka kwa ‘Amru bin Al-‘Aasw alimuuliza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ni watu gani unaowapenda ee Mjumbe wa Allaah? Akasema, “'Aaishah” akasema na katika wanaume? akasema “Baba yake” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].

'Aaishah bint Khalifatu RasuliLlaahi Baba yake ni Abu Bakr 'Abdullaahi bin Abi Quhaafah, na Mama yake ni Mama Rummaan bint ‘Aamar Al-Kinaaniyah ni katika Swahabiyah mtukufu amehama kwenda Madiynah na amekufa baada ya Hadiythul Ifki katika uhai wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na akateremka Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kaburi lake na akamtakia maghfirah.


KUOLEWA KWAKE ‘AAISHAH رضي الله عنها))

‘Aaishah (رضي الله عنها) aliolewa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kabla ya kuhama Makkah kwenda Madiynah katika mwezi wa Shawwaal baada ya kufa Bibi Khadiyjah ((رضي الله عنها nae alikua na umri wa miaka (6) sita, na akaingia dukhuli katika mji wa Madiynah akiwa na umri wa miaka (9) tisa akiwa bikra, na wala Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuoa mke bikra isipokua yeye.

'Aaishah ((رضي الله عنها amesimulia kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuoa nae akiwa na umri wa miaka sita (6) na kuitimiza ndoa yake kwa kitendo cha ndoa (dukhuli) akiwa na umri wa miaka tisa, (9) na baadae alibaki nae kwa miaka tisa. [Swahiyh al-Bukhaariy].


ELIMU YAKE

Hakika yeye ni Swahabiyah mtukufu ambae amejifunza katika Madrassah tukufu ambayo alilelewa kutoka utoto wake nae ni Baba yake m’bora na alie mkweli Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه).
Na akakulia katika nyumba tukufa kabisa katika ujana wake nyumba ambayo ni madrasa ya Iymaani, mwalimu wake mtukufu na m’bora wa viumbe Mume wake kipenzi chake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

Hakika yeye ni muelewa sana mwenye akili mpaka ikasemwa ana robo ya hukmu tukufu alizobeba. Amepokea Ahaadiyth kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) elfu mbili mia mbili na kumi (2210).

Alikuwa mwalimu wa wanaume na ni marejeo kwao kutoka katika Hadiyth, Sunnah na Fiqh.

عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه قال:ما أشكل علينا أصحاب رسول الله صلى الله عليه وسلم قط فسألنا عائشة رضي الله عنها إلا وجد نا عنها منه علما.
.
Kutoka kwa Abiy Muusa Al-Ash’ariy amesema: “Hakukuwa na jambo lolote lililotutatiza sisi Maswahaba wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katu isipokuwa tulimuuliza ‘Aaishah (رضي الله عنها) na kupata jawabu la kielimu kutoka kwake.”

وقال الإمام الزهري رحمه الله:لو جمع علم عائشة إلى علم جميع علم النساء لكان علم عائشة أفضل.

Amesema Imaam Az-Zuhriy: “Lau ingekusanywa elimu ya ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa elimu ya wanawake wote basi elimu ya ‘Aaishah ni bora”

:عن مسروق قال
فحلف بالله لقد رأينا الأكابر من أصحاب رسول الله صلى الله عليه وسلم يسألون عائشة عن الفرائض

Kutoka kwa Masruuq amesema: “Naapa kwa Allaah nimewaona Maswahaba wakubwa wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wakimuuliza ‘Aaishah kuhusu masuala ya Mirathi.”

يقول ابن عبدالبر:إن عائشة كانت وحيدة وعصرها في ثلاثة علوم:علم الفقه،علم الطب،علم الشعر.

Amesema Ibn ‘Abdil-Barr: “Hakika ‘Aaishah ni mwanamke pekee katika zama hizo ambae amekusanya elimu tatu;
(1) Elimu ya Shari’ah
(2) Elimu ya Matibabu
(3) Elimu ya Mashairi


SUBIRA YAKE
         
Kwa hakika ni mwanamke aliyebeba elimu nyingi na zenye manufaa na tunafaidika nazo hadi leo, na mwenye subira ni mfano wa kuigwa kwa Wanawake hakika ni Mwalimu kwa kila Mwanamke katika ulimwengu wa zama zetu hizi na ni mwalimu wa wanaume.

Kwa hakika alikuwa ni Mke bora na mkarimu wa nafsi na ni mwenye kutoa kwa ajili ya Mola wake amesubiri katika maisha yake pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya ufaqiri na njaa mpaka zimepita baadhi ya masiku hakuwashwi moto katika nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم); walikuwa wakiishi kwa maji na tende.

Huu ni mfano mzuri sana wa kuigwa kwetu sisi wanawake twatakiwa tuwe na Subira ingawa ni jambo gumu lakini subira ndio itatuwezesha kufaulu katika maisha yetu ya Dunia ili tuweze kufikia ufaulu wa njia ya Akhera.


UKARIMU WAKE NA UZURI WA TABIA YAKE

يروى عن أم ذرة قالت: بعث ابن الزبير إلى عائشة رضي الله عنها بمال وهي يومئذ صائمة، فجلست تقسمه إلى بين الناس، وليس في بيتها شيء، فلما أمست قالت: ياجارية هاتي فطوري فجائتها بخبز وزيت وقالت لها أم ذرة أما استطعت مما قسمت اليوم أن تشتري لنا لحما بدرهم تفطر عليه؟ فقالت عائشة رضي الله عنها: لا تلومني لو كنت ذكرتني لفعلت.

Imepokewa kutoka kwa Ummu Dharrah amesema: “Alituma pesa Ibn Az-Zubayr kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) nae siku hiyo alikuwa amefunga Swawm, basi akakaa kuzigawa kwa watu pesa zote, Na ndani ya nyumba yake hamna kitu ilipofika jioni akasema ee Kijakazi lete futari, akaja na mkate na mafuta, Akasema Ummu Dharrah kumwambia hukuweza katika ulichogawa ukabakisha japo dirham tukanunua nyama ukafutaria na mkate? Akasema ‘Aaishah usinilaumu lau ungenikumbusha basi ningefanya hivyo”.

Huyu ndie Mama wa Waumini, ‘Aaishah bint Abiy Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنها)
         
Je, mimi na wewe tumefikia wapi katika kutoa fiy sabiyliLlaahi?
Basi huu ni mfano mzuri wa kuiga wa kutoa, kuwapendelea wenzetu kheri kabla ya nafsi zetu. Inahitaji Iymaan na Ikhlaasw ya hali ya juu, kwani unapotoa kwa ajili ya Mola wako ni akiba unajiwekea kesho Aakhera utaikuta in shaa Allaah.


MAMBO 9 ALIYOPEWA ‘AAISHAH (رضي الله عنها)

Anaeleza mwenyewe:

Kwa hakika nimepewa mambo (9) tisa hajapewa Mwanamke yeyote baada yangu:

1)      Ameteremka Jibriyl (عليه السلام) na sura (picha) yangu mpaka akaamrishwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) anioe.
2)      Amenioa nikiwa bikra wala hakuoa mke bikra isipokua mimi.
3)      Na mimi ni mtoto wa Khalifa na Mkweli.
4)      Na nimeteremshiwa utakaso kutoka mbinguni.
5)      Na amefariki Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na kichwa chake kiko juu ya mapaja yangu.
6)      Na kaburi lake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) liko nyumbani kwangu.
7)      Na nimeahidiwa na Mola msamaha na rizki bora.
8)      Na nimeumbwa katika wema kutoka kwa mwema.
9)      Na ilikua wahyi ukishuka niko ndani ya shuka moja pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).


TUKIO LA UZUSHI

Katika maisha yake Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) Mama wa Waumini lilimtokea tukio kubwa ambalo ni la kuzushwa (حادثة الإفك) ambalo wanafiki walilipokea kwa furaha na kuendeleza uzushi huu siku hadi siku wakawa wanalizungumzia na kulieneza kwa Waislamu na kuleta mpasuko baina yao.

Kwa hakika alikuwa huyu ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluul ndie aliyezalisha unafiki na hasadi katika moyo wake tokea mwanzo alipousikia Uislamu, na akawa anatamani limfike jambo baya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Uislamu kwa jumla, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) kwa hikma kubwa na namna ya kuwadhihirisha wanafiki waliumbuka.

Kwa hakika uzushi huu ulimuuma sana Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ndani ya moyo wake na maumivu haya yakapita ndani ya nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na nyumba ya Abu Bakr As-Swiddiyq ((رضي الله عنه.

Ulikuwa wakati mgumu sana, ulichukua takriban mwezi mzima mpaka zikashuka aya za Qur-aan kumtakasa na uchafu huo Mwanamke mtukufu ‘Aaishah (رضي الله عنها) na pia kumtakasa Swahaba mtukufu Swafwaan bin Mu’utal (رضي الله عنه) ambae ndie aliesingiziwa kuwa pamoja na Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) katika dhambi hiyo. Mola Aliwatakasa.
Basi wanafiki wakafedheheka na ikawa ndio mwisho wa mazungumzo hayo.


TUKIO LENYEWE

Lilikua tukio hili ni katika vita vya Bani Al-Mustwaliq mwaka wa (5) tano wa Hijiriyah, na umri wa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) ulikuwa miaka (12) kumi na mbili.
Na hii ni Hadiyth anazungumzia mwenyewe Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) tukio lililomuumiza moyo wake anaelezea:

Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akitaka kusafiri anapiga kura baina ya wake zake, ikatokea mimi kusafiri nae pamoja katika msafara huo baada ya kuteremka Aayah ya Hijaab.
Na nilibebwa katika haudaj (haudaj ni kibanda chenye sitara ambacho anasitiriwa mwanamke na kinawekwa juu ya ngamia) tukaondoka na jeshi na ilikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wanaposafiri huwa wanapumzika njiani. Wakati tunarudi tukapumzika nami nikashikwa na haja nikatoka kwenye haudaj kwenda kukidhi haja nilipomaliza wakati narudi nikagundua kidani changu kimenipotea baada ya kukatika mkufu nikawa nimerudi kukitafuta, huku nyuma jeshi likaondoka wakabeba haudaj na kuweka juu ya ngamia wakidhani mimi nimo ndani na hawakuhisi kama mimi sipo kwani tulikuwa wanawake zamani ni wepesi sana nami nilikuwa mwembamba na tena nilikuwa mdogo, na tulikua tukila chakula ambacho si cha kunenepesha. Jeshi likaendelea na msafara huku wakidhania mimi nimo ndani ya haudaj.

Baada ya kukitafuta kidani nikakiona, ndio niliporudi sikulikuta jeshi limeshaondoka, nikenda ile sehemu ambayo nimeteremka nikaanza kulia na kukaa hapo kwa kudhani huwenda wakajua kama mimi sipo wakarudi kunifuata, nikawa nalia hadi usingizi ukanichukua.
Na alikua Swafwaan bin Mu’utal As-Saalimiy (رضي الله عنه) alibaki nyuma ya jeshi ili kuangalia kama kuna kilichosahauliwa au kudondoka katika jeshi.

Mara akaona kitu cheusi kwa mbali aliposogea akaona mtu amelala, kumuangalia akanijua baada ya kuniona, na alikua akinijua sura yangu kabla ya kushuka aya ya Hijaab, akasema:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Sisi sote ni wa Allaah na Kwake tutarejea”

Basi nikaamka baada ya kusikia hivyo kauli ikanishtua nikachukua Khimaar na kujifunika uso kwa Jilbaab, WaLlaahi hakuzungumza nami neno lolote wala sikumsikia kusema ispokuwa kauli ya istirja'a, akaniashiria kwa mnyama nami nikapanda nae akatembea mpaka tukalifikia jeshi katika mwendo wa mchana dhahir kabisa.
Hakika wakaangamia katika waloangamia baadhi ya Maswahaba katika jambo hili, na mkubwa kabisa wa wanafiki aloanza kueneza uzushi huu ni huyu ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluul.

Tukaingia Madiynah, ukapita takriban mwezi na watu wanaambizana jambo hili kutoka kwa wazushi wala mimi sina khabari kama kumezuka jambo.
Nami nilikuwa naumwa, Khabari hizi zinamfikia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) nami sijui kitu, lakini namuona Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akiingia ndani anatoa salaam na kusema vipi hali yako na kutoka hana uchangamfu kabisa, kwa jambo hilo akawa ana mashaka baina ya kuamini na kutokuamini.

Siku akaja mama yake Mistah tukatoka pamoja kwani nilikua na haja nikahitaji kutoka na tulikua hatutoki ila usiku usiku kabla hatujajenga choo karibu na nyumba, tulipokuwa njiani tunarudi mara Ummu Mistah akajikwaa na akasema aangamie Mistah, nae ni mtoto wake na pia huyu Ummu Mistah bint Ruhm bin ‘Abdu Manaaf, Mama yake ni Mtoto wa Sakhri bin ‘Aamir ni Khali yake Abu Bakr (رضي الله عنه).
Mistah ni mtoto wa Uthaathah bin Muttwalib.

Basi baada ya kusema neno hilo; Mama kusema juu ya Mtoto wake, nikasema kumwambia Ummu Mistah ni jambo baya umesema unamtukana mtu ambae ameshuhudia vita vya Badr? Akasema hivi hujui anayoyasema? nikasema Ni kitu gani? Nipe khabari, akanambia aliyonambia yakanizidi maradhi juu ya maradhi.

Niliporudi nyumbani akaingia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akanisalimia nikamuomba ruhusa ya kwenda nyumbani kwa wazazi, akanipa ruhusa, nami nilikuwa nataka yakini ya hizi khabari kutoka nyumbani ni kweli haya maneno yasemwayo?

Nikawauliza wazazi wangu kuhusu hii khabari, wakanambia ewe mtoto wetu tuliza nafsi yako, WaLlaahi ni mara chache kwa Mwanamke anayependeza zaidi kwa Mumewe naye anampenda illa watamzidishia.

Nikasema SubhaanaAllaah! kwa hakika hivi ndivyo wazungumzavyo watu? Nikaanza kulia usiku na mchana hayakuacha machozi kunitoka wala sijitii wanja wakati wa kulala hasha kwa kulia, nikaendelea na kilio changu.

Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa yuko baina wabaina kati ya kuamini na kutokuamini, akamuiita ‘Aliy bin Abiy Twaalib na Usaamah bin Zayd kutaka ushauri imma amuache au vipi, ama Usaamah akamshauri kua anajua kuwa familia yake imewekwa mbali na mabaya na anajua zaidi juu ya nafsi yake.
Akamwambia ee Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wa Allaah, mke wako yaani ‘Aaishah, sina ninachokijua kwake ila kheri.
Na ama ‘Aliy akasema kumwambia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) usijidhikishe na Allaah (سبحانه وتعالى) hajakudhikisha, wanawake wako wengi, na pia muulize mjakazi wake atakupa ukweli, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwita na kumwambia Barirah je, umeona kitu chochote ambacho kinakutia mashaka juu ya jambo hili?
Akasema hapana naapa kwa yule aliekupa Utume kwa haki, mimi sina nijualo ila nafanya shughuli zangu na sijaona chochote wala sina mashaka juu ya hilo nadhania kheri.

Basi akasimama Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na akataka alipiziwe kisasi juu ya ‘Abdullaah bin Saluul, akasema hali ya kuwa yuko juu ya Mimbari.

"يا معشر المسلمين: من يعذ رني من رجل, قد بلغني أذاه في أهل بيتي, فوالله ما علمت على أهلي إلا خيرا, ولقد ذكروا رجلا ما علمت عليه إلا خيرا, وما كان يدخل على أهلي إلا معي"                     
Enyi kundi la Waislamu nani atanilipizia kisasi kwa mtu aliyeiudhi nyumba yangu na kuichafua? Naapa kwa Mola sina ninalojua juu ya nyumba yangu ispokuwa kheri, na ametajwa mtu sina ninalojua kwake isipokua kheri, na wala haingii kwa watu wangu ispokuwa pamoja nami.”
Hapa anamkusudia Swafwaan bin Mu’utal (رضي الله عنه).

Akasimama Sa’ad bin Mu’aadh (رضي الله عنه) akasema ee Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wa Mola, mimi nitalipiza ikiwa ni katika kabila la Awsi nitamkata kichwa na ikiwa ni katika ndugu zetu wa Khazraj niamrishe nitafanya utakaloniamrisha.
Akasimama Sa’ad bin ‘Ubaadah nae ni bwana wa Khazraj nae alikuwa kabla ya hapo ni mtu mwema lakini uzalendo ukamshika kwa watu wake.
Akasema, muongo! Hutaua wala huwezi kuua, akasimama Asyad bin Hudhiyr nae ni mtoto wa ‘Ammi yake Sa’ad bin Mu’aadh.
Akasema, muongo! Tutamuua, hakika wewe ni mnafiki, basi wakazozana mpaka wakanyamazishwa wakanyamaza.

Nikaendelea na kilio changu! Anasema Bibi Aa’ishah (رضي الله عنها) mpaka nikadhani ini langu litaharibika kwa kulia, akaja mwanamke mmoja akataka idhini nikampa akakaa kulia na mimi.
Mara akaingia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akatusalimia kisha akakaa na hakukaa karibu yangu tangu yaliposemwa maneno haya, ilichukua mwezi mzima wala hakuna wahyi.

Akamhimidi Mola Alietukuka kisha akasema Amma ba’ad,

“Ee ‘Aaishah! kwa hakika limenifikia kutoka kwako jambo kadha wa kadha basi ikiwa uko mbali na haya yasemwayo basi Mola Atakutakasa, Na ikiwa umefanya jambo hilo mtake msamaha Mola wako na utubie kwake. Kwa hakika mja anapojua dhambi yake na akatubia basi Mola humsamehe”.

Basi alipomaliza kusema nikanyamaza kulia nikamwambia Baba yangu mjibu Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa aliyoyasema, akasema WaLlaahi sijui nimwambie nini Mjembe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)! Akamwambia Mama yake mjibu Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa aliyoyasema, akasema sijui nimjibu nini Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

Basi nikasema mimi ni mdogo na sijui  vizuri Qur-aan mpaka iwatulize katika nyoyo zenu na mkaniamini, ama nikisema mimi niko mbali na hayo hamtaniamini, na Allaah Anajua kuwa mimi niko mbali na hayo, naapa kwa Allaah sina ninachowaambia isipokua kauli ya baba yake Yuusuf:

فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ

“Basi (langu mimi) ni subira njema; na Allaah ndie aombwae msaada kwa haya mnayoyasema.” [Yuusuf: 18]


Tanbihi:
“Ama kwa hakika mpaka hapa tumepata mafunzo mengi sana moja kubwa tumeona madhara makubwa ya uzushi mtu huna uhakika wa jambo basi wasikia tu na waanza kueneza, hiyo ni dhambi kubwa na pia kunasababisha mfarakano baina ya watu, ndugu zangu katika Iymaan tujitahidi kujiepusha na tabia hizi mbaya za kusikia majambo bila ya ushahidi na kuyaeneza.
Ni chukizo kubwa mbele ya Allaah (سبحا نه وتعالى).
Na Mola Anajua zaidi.

Anasema 'Aaishah (رضي الله عنها):
Basi baada ya kusema maneno hayo nikageuka na kulala kwenye tandiko langu. Na hali najua mimi niko mbali na hayo yasemwayo, Na hakika Mola wangu Ataniweka mbali na hayo In shaa Allaah .

Lakini WaLlaahi sikudhania kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Atateremsha Aayah za Qur-aan iwe ni shani kwangu na ziwe zinasomwa, bali nilitaraji kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Atamuotesha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Wake katika usingizi iwe utakaso kwa njia ya ndoto.

WaLlaahi hakusimama Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wala hakutoka na yeyote katika watu wa nyumbani mpaka ulipoteremka wahyi. Kwa maana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa na raha.

Basi kwa furaha kubwa kabisa akaja Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na huku anacheka, akasema:

“Ee ‘Aaishah kwa hakika Mola wako Amekutakasa.”

Mama yangu akanambia inuka umuelekee Mume wako, nikasema WaLlaahi simuelekei wala simshukuru ispokuwa Mola wangu Aliyetukuka.

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah hizi:

إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ

 “Hakika wale walioleta uongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu, kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi, na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa.

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ

“Kwa nini mliposikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema; Huu ni uzushi dhaahiri?

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ

Mbona hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyokuwa hawakuleta mashahidi wanne basi hao mbele ya Allaah ni waongo.

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Na lau kuwa si fadhila ya Allaah juu yenu na rehema Yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyoyashughulikia.

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ

“Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Allaah ni kubwa.

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ

“Na mbona mlipoyasikia hamkuseme: Haitufalii kuzungumza haya.  Umetakasika (Mola wetu!) Huu ni uzushi mkubwa’’

يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Allaah Anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!

وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Na Allaah Anakubainishieni Aayah. Na Allaah ni Mjuzi Mwenye hikima.

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Kwa hakika wale wanaopenda uenee uovu kwa walioamini, watapata adhabu iumizayo katika dunia na Akhera. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui.”


وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na (yangetokea machafuko makubwa) lau isingelikua fadhila ya Allaah juu yenu na rehma Yake na kuwa Allaah ni Mpole, na Mwenye huruma.” [Suratun-Nuur: 11-20].


Aayah hizi zimemtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutokana na yaliyozushwa na ndio maana yakaja makemeo na adhabu kali, kwa wenye kuzusha.

Na hili la kudhania ni baya pia kwani dhana mbaya nayo huzaa fitna kubwa, haiwi kumuona mtu amekaa na mwanamume au hata umewaona wanatoka chumbani pamoja ukajenga dhana kuwa wamezini ingawa ni kosa kwa mtu ambae si Mahrimu yake kukaa chumbani na kujifungia, lakini basi isiwe sababu ya kuwatuhumu kuwa wamezini hali huna ushahidi je, kama walikuwa wanaongea tu hawajafanya kitendo chochote utakuwa umebeba dhambi kubwa ya uzushi na ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Akataka mwenye kusema fulani amezini alete mashahidi (4) wa nne kama hana apigwe bakora (80) themanini.

Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema ushahidi wa zinaa ni wa watu wa nne (4) washuhudie kama vile kamba inavyoingia kisimani.


Na ndio Allaah (سبحانه وتعالى) Akasema:

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ

“Mbona mliposikia (habari) hii, Wanaume Waislamu na Wanawake Waislamu hawakuwadhania wenzao kheri, na kusema “huu ni uzushi wa wazi kabisa’’.[Suratun-Nuur: 12].

Amesema tena Allaah (سبحانه وتعالي):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ

“Enyi mlioamini! Jiepusheni sana (kuwadhania watu) dhana (mbaya) kwani (kuwadhania watu) dhana (mbaya) ni dhambi.” [Al-Hujuraat: 12]


Tanbihi:
Kwa utakaso huu alotakaswa na Mola Mtukufu bado kuna makundi yanayojinasibisha na Uislamu wanamtukana mama wa Waumini tena hadharani pamoja na Maswahaba watukufu wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na tujihadhari na makundi hayo tusije tukaangamia kama waloangamia.

Basi pindi ilipoteremka Qur-aan kumtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها), Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه) nae alikuwa akimpa chakula na mahitaji mengine akimsaidia huyu Mistah, akasema WAllaahi simpi tena chochote huyu Mistah baada ya haya aliyoyasema kwa ‘Aaishah, ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah isemayo:

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Na wasiape wale wenye mwendo mzuri (wa Dini) na wenye wasaa (katika maisha yao) miongoni mwenu (wasiape kujizuia) kuwapa walio jamaa na masikini na waliohama kwa njia ya Allaah;  na wasamehe na waachilie mbali, Je, nyinyi hampendi Allaah Akusameheni? Na Allaah ni mwingi wa kusamehe (na) mwingi wa rehema.” [Suratun-Nuur: 22].

Basi baada ya Aayah hii akasema Abu Bakr (رضي الله عنه) hapana Mola wangu napenda nami kusamehewe akarejesha yale yote aliyokua akimfanyia Mistah kama mwanzo na akasema sitamsumbua tena abadan.

Na hili ni fundisho kwetu sote la kusameheana usiweke kitu moyoni na vifundo na kuweka ahadi kama mtu kakukosea ukasema simfanyii kadha wala simsamahe mpaka Qiyaamah. Uislamu umetufunza kusameheyana kwani ukimsamehe ndugu yako Muislamu, Mola nawe Atakusamehe. Hakuna binadamu aliyekamilika. Alkamaaulu LilLlaahi.

Lau Allaah hakutuwekea msamaha na Rahma Zake kwa waja Wake basi hakuna mtu hata mmoja angenusurika na adhabu Zake.
Tunamuomba Mola Atumiminie Rahma Zake na Msamaha Wake Hakika Yeye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu.


Amesema ‘Aaishah (رضي الله عنها), Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuuliza Zaynab bint Jahsh kuhusu jambo hilo. Akasema Zaynab (رضي الله عنها), najikinga na macho yangu na masikio yangu sina ninachokijua kwa ‘Aaishah Isipokuwa kheri.
Hapa ni kuonyesha hakuna haki katika haki isipokua kusema ukweli. Japo Zaynab ni mke mwenza lakini kasema ukweli wa jambo, na haya ni mafunzo tunayojifunza kwa watu wema ya kusema ukweli.

Ikarudi furaha katika nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Fadhila za Mola ('Azza wa Jalla).


KUFA KWAKE

Amekufa ‘Aaishah (رضي الله عنها) usiku wa Jumanne, tarehe kumi na saba (17) Ramadhaan mwaka wa khamsini na nane (58) wa Hijrah nae akiwa na umri wa mika sitini na sita (66), akazikwa katika makaburi ya Baqii usiku baada Swalah ya witri.

Mola Amuwie Radhi mkweli mtoto wa mkweli na Mola Mtukufu Amteremshe katika pepo tukufu milele. Aamiyn

Nasi Twamuomba Mola wetu mtukufu kwa kisa hiki cha Mama yetu ‘Aaishah (رضي الله عنها) tupate mazingatio na tuige mafundisho kwani ni mengi sana tumeyapata kutoka kwake Mama wa Waumini, tujitahidi kusoma na kutafuta yalo na faida na sisi katika maisha yetu


FAIDA TULIZOPATA KATIKA HISTORIA YA BIBI ‘AAISHAH (رضي الله عنها)

·         Ubora wa Bibi ‘Aaishah kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya wanawake wengine. Alikuwa akipendwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko mwanamke mwengine yeyote. Kama alivyokuwa baba yake akipendwa zaidi na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko wanaume wengine.

·         Kumuozesha mtu bint yake kwa rafiki yake maadam ni mtu mwema, Kama alivyomuozesha Abu Bakr bint yake ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

·         Hakuna ubaya mtu kumpenda mke mmoja zaidi ya wengine maadam atawafanyia wote uadilifu. Kama ambavyo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimpenda zaidi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kuliko wake zake wengine lakini hakuacha kuwafanyia wote uadilifu bila kumpendelea fulani au kumbagua fulani.

·         Subira juu ya mitihani. Tumeona namna Bibi ‘Aaishah alivyokuwa na subira kubwa baada ya tukio la kuzuliwa uchafu. Na subira pia kwa kuchelewa sana kushuka kwa Wahyi kwa mwezi mzima.

·         Kutoharakisha kutoa hukumu ya jambo. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakufanya pupa au haraka ya kutoa hukumu.

·         Kujichunga na kumzulia Muislamu mwenzako. Na kujizuia na kutuhumu watu.

·         Hukumu kwa wanaotukana wake za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba kwa ujumla. Wamekubaliana Ma’ulamaa kuwa anayemsingizia Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) uzinifu, basi atakuwa amekufuru kwani Allaah Mwenyewe kamtakasa kwenye Qur-aan na hukumu imetoka mbinguni kuthibitisha usafi na utwahara wake. Hivyo anayemtuhumu anakuwa ameikadhibisha Qur-aan na vilevile kamtukana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) pia.

·         Kuwepo wanawake wenye elimu zaidi ya wanaume katika masaail ya Dini. Kama alivyokuwa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) na elimu kubwa ya Fiqh, Miyraath, Tafsiyr, Hadiyth n.k hata kuwafanya Maswahaba wengi kumwendea na kuchukua elimu na hukumu ya masaail ya kishari’ah.

·         Allaah kumtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutoka juu ya mbingu ya saba.

·         Mtu kutaka ushauri kwa rafiki zake wema kuhusiana na suala la kutengena na mke wake.

·         Kuwapendea wengine kheri kuliko nafsi yako. Tunaona katika upande wa kutoa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) alikua akiwafikiria wenzie kabla ya nafsi yake.

·         Na katika upande wa elimu amebeba elimu kubwa kutoka kwa bwana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) nasi hatuna budi kufanya juhudi katika kuitafuta elimu yenye manufaa na kuifanyia kazi.

·         Kadhalika Suala la Niqaab (kufunika uso) tumepata dalili kutoka kwake pale aliposema Swafwaan alimjua kabla ya Hijaab.

Mola Atuwafiqishe Mema Tuyafate na Mabaya Tuyaepuke. Atusamehe pale tulipokosea na Asitunyime ujira pale tulipopatia.


3. Swafiyyah Bint Abdil-Muttwalib (Radhiya Allahu 'Anha)

Mwanamke Wa Mwanzo katika Uislam Kumuua Mshirikina
Bibi Safiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Llahu 'anha) shangazi lake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa mwingi wa hekima, hodari wa kuyapima mambo, shujaa na mkali. Hata wanaume walikuwa wakipanga na kupanguwa huku wakiwaza na kufikiri kabla ya kuamua kujadiliana au kupambana naye.
Anajulikana kuwa ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya kuwahami wanawake wenzake wa Kiislamu.
Nasaba Yake
Baba yake ni Abdul Muttalib bn Hashim babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) aliyekuwa kiongozi wa Makureshi mwenye kutiiwa. Mama yake Bi Safiyyah ni Halah binti Wahab dada yake Aminah binti Wahab mama yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam).
Mumewe wa mwanzo aliyefariki dunia akiwa naye alikuwa Al Haarith bin Harb ndugu yake Abu Sufyaan bin Harb mkuu wa kabila la Bani Umayyah.
Mume wake wa pili alikuwa Al ‘Awwaam bin Khuwaylid ndugu yake Bi Khadijah binti Khuwaylid (Radhiya Llahu 'anha) mke wa mwanzo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) na mama wa mwanzo wa Waislamu.
Mume wake wa pili Al ‘Awwaam bin Khuwaylid alipofariki dunia alimuacha akiwa na mtoto mdogo wa kiume Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) aliyesilimu pamoja na mama yake akiwa na umri wa miaka minane.
Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) alikuwa sahibu mpenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) aliyesema juu yake:
"Kila Mtume anaye sahibu, na sahibu yangu ni Az Zubayr."
Na akasema:
"Talha na Az Zubayr sahibu zangu Peponi." 
Ulezi Wake
Bi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) alimlea mwanawe Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) malezi magumu na ya shida. Mchezo wake ulikuwa ni kutupa mikuki, kuchonga mishale na kutengeneza pinde.
Alikuwa akimtia vishindo na kumpeleka sehemu zinazotisha na za hatari. Na anapoingiwa na hofu au uoga alikuwa akimpiga kipigo chenye kuumiza. Na kwa ajli hiyo watu wake walikuwa wakimlaumu.
Mmoja katika shangazi zake aliwahi kumuambia:
"Si hivyo anavyopigwa mtoto. Unampiga mfano wa mama anayemchukia mwanawe. Hicho si kipigo cha kumlea mtoto."
Bi Safiyyah akamjibu kishairi akimuambia: "Anayesema namchukia hajasema kweli. Nampiga apate akili, ayashinde majeshi makali na afuzu kikweli."
Kusilimu Kwake
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) alipopewa utume, alitakiwa aanze kwa kuwaonya watu wake na kuwapa bishara njema, na kuwalingania. Aliwakusanya jamaa zake wanaotokana na tumbo Abdul Muttalib wanawake kwa wanaume, wadogo kwa wakubwa na kuwahutubia ifuatavyo:
"Ewe Fatima binti Muhammad. Ewe Safiyyah binti Abdul Muttalib. Enyi wana wa Abdul Muttalib. Hakika mimi similiki chochote kwa ajli yenu mbele ya Mwenyezi Mungu."
Kisha akawataka wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja na kuamini ujumbe aliokuja nao.
Wakakubali miongoni mwao waliokubali na wakakanusha waliokanusha kwa upotofu wao. Na Bi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alikuwa miongoni mwa kundi la mwanzo kumuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) na kumsadiki.
Hijra Yake 
Kwa hivyo Bi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) pamoja na mwanawe Al Zubair bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) wakawa miongoni mwa kundi la mwanzo kujiunga na msafara huu ulioieneza nuru kila pembe ya dunia, na wakapata tabu nyingi kama walivyopata tabu wenzao wote waliotangulia kuingia katika dini hii tukufu tokea siku za mwanzo.
Makureshi waliwaonjesha Waislamu kila aina ya mateso na adhabu, mpaka pale Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Taala) alipomtaka Mtume wake (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) aondoke Makkah yeye pamoja na wafuasi wake na kuhamia Madinah. Na hapo ndipo Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alipoitikia mwito huo kuuhama na kuuacha nyuma mji anaoupenda, Makkah, na kuacha nyuma kila anachokipenda katika mji ule mtukufu na kila kinachomkubusha utoto wake na ujana wake.
Jihadi Yake
Juu ya kuwa umri wake ulikaribia miaka sitini, lakini Bibi huyu mtukufu (Radhiya Llahu 'anha) alikuwa na misimamo madhubuti isiyosahaulika mbele ya adui wa Mwenyezi Mungu katika kupigana jihadi.
Alikuwa akitoka pamoja na wanawake wenzake kuwasaidia Waislamu wanaopigana jihadi kwa kuwapelekea maji na kuwachongea mikuki na mishale pamoja na kutengeneza pinde zinapokatika. Wakati huo huo akiwa karibu na vita aliweza kupata habari za mtoto wa ndugu yake Muhammad (Swalla llahu alayhi wa Ssallam) anapokuwa vitani pamoja na habari za ndugu yake Hamzah bin Abdul Muttalib (Radhiya Llahu anhu) na pia habari za mwanawe Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) na juu ya yote hayo aliweza kujuwa juu ya maendeleo ya vita vinavyopiganwa kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.
Na siku ile alipowaona Waislamu wakikimbia vitani huku majeshi ya makafiri yakikaribia kumfikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) na kumuua, Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) aliruka kama simba jike anavyoruka anapowaona wanawe wakishambuliwa. Akamnyang'anya mkuki mmoja wa waliokuwa wakikimbia uwanja wa vita, akaanza kuelekea mbele kuwakabili maadui huku akiwatolea ukali Waislamu akiwaambia:
"Ole wenu! Mnashindwa kusimama na Mtume wa Mwenyezi Mungu?
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) alipomuona akielekea katika uwanja wa vita aliogopa asije akamuona ndugu yake Hamzah (Radhiya Llahu 'anhu) aliyeuliwa na mwili wake kukatwa katwa vibaya. Akamuambia mwanawe Az Zubayr:
"Mzuwie mama yako ewe Zubayr, mzuie mwanamke ewe Zubayr."
Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) akamuendea na kumuambia:
"Rudi ewe mama yangu, rudi."
Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) akasema:
"Nipishe huko."
Akasema:
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) anakuamrisha urudi."
Akauliza:
"Kwa nini? Nimekwishapata habari kuwa ndugu yangu ameuliwa na kukatwa katwa vibaya. Yote hayo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Muache apite ewe Zubayr."
Akamruhusu.
Baada ya vita kumalizika Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alisimama mbele ya maiti ya ndugu yake Hamzah (Radhiya Llahu 'anhu) huku akiuangalia mwili wake uliokatwakatwa vibaya huku akimuombea maghfira na kusema:
"Yote haya kwa ajli ya Mwenyezi Mungu. Nimeridhika na kile alichokitaka Mwenyezi Mungu kiwe, na ninategemea malipo mema kutoka Kwake Inshaallah."
Huu ulikuwa msimamo wa Bibi Safiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Llahu 'anha) siku ya vita vya Uhud.
Vita Vya Khandaq
Ama msimamo wake siku ya vita vya Khandaq ndani yake mna kisa chenye kusisimua sana.
Kawaida ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) ilikuwa kila anapokwenda vitani akiwaweka wanawake na watoto na wazee na vilema ndani ya ngome akihofia mtu asiwaendee kinyume akawazungukia na kuwateka.
Siku ya vita vya Khandaq aliwaweka wake zake na shangazi zake pamoja na wanawake wengine wa Kiislamu ndani ya ngome ya Hassan bin Thaabit (Radhiya Llahu 'anhu) aliyeirithi kutoka kwa baba yake. Na ngome hii ilikuwa madhubuti zaidi. Haivunjiki kwa urahisi wala haiingiliki kwa wepesi. Na Waislamu walipokuwa wameshughulika na vita wakipambana na Makureshi na wanaowaunga mkono, waliwasahau wake na watoto wao kwa kujishughulisha na maadui  hao.
Alfajiri ilipoanza kuingia, na waliomo ndani ya ngome walikuwa bado wamelala, Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) aliyekuwa yu macho wakati huo aliona mfano wa mwili ukitaharuki huku na kule ndani ya ngome yao. Akausogelea mwili ule kimya na pole pole mpaka alipoukaribia akaona kuwa ni Myahudi aliyefanikiwa kuingia ndani ya ngome. Alimfuata huku na kule bila Myahudi kuhisi, na hatimaye Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) alitambua kuwa huyo ni mpelelezi aliyetumwa na Mayahudi kuja kupeleleza iwapo ndani ya ngome mna wanaume wenye kuilinda au ni ngome iliyojaa wanawake iliyoachwa bila ya ulinzi.
Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) akawa anajiuliza:
"Hawa Mayahudi wa Bani Quraydhah ndio walioivunja ahadi iliyokuwepo baina yao na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) kisha wakajiunga na Makureshi dhidi ya Waislamu. Na hivi sasa hapana mwanamume hata mmoja wa kutuhami, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wote wapo vitani. Akiweza adui wa Mwenyezi Mungu huyu kuwafikia watu wake na kuwajulisha kuwa humu ndani tumo wanawake watupu, watatuteka. Na hilo litakuwa ni balaa kubwa kwa Waislamu."
Hapo hapo akaamua kujifunga uzuri kitambaa usoni na kuzibana vizuri nguo mwilini mwake, kisha akaokota gongo na kuanza kumnyemelea adui yule wa Mwenyezi Mungu kwa tahadhari mpaka alipomkaribia sana. Alipokuwa na uhakika kuwa keshamkaribia vya kutosha na kumkalia vizuri, akanyanyua gongolake juu na kuliangusha kwa nguvu zake zote, akampiga nalo kichwani na kumuangusha chini. Akaendelea kumpiga mpaka alipomuona hawezi tena kuvuta pumzi, kisha akatoa kisu chake na kumkata kichwa kisha akakichukua kichwa na kukitupa juu ya paa, kikabiringitia na kuangukia mbele ya Mayahudi waliokuwa nje wakimsubiri mwenzao.
Walipokiona kichwa cha mwenzao kimekatwa wakasema:
"Tulijuwa sisi kuwa Muhammad hawezi kuwaacha wanawake na watoto peke yao bila ya ulinzi madhubuti wa wanaume."
Kufariki Kwake
Mwenyezi Mungu awe radhi naye Bibi Safiyyah. Alikuwa shujaa na jasiri kikweli, na historia imekwishaandika kuwa yeye ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya dini ya Islamu.
Alifariki dunia wakati wa ukhalifa wa ‘Umar bin Khattaab (Radhiya Llahu ‘anhu) akiwa na umri wa miaka sabini na tatu, Na ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) ndiye aliyeongoza Swalah ya jeneza, na akazikwa bibi huyo katika makaburi ya Al Baqi'y.
 Mwanamke Wa Mwanzo katika Uislam Kumuua Mshirikina
Bibi Safiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Llahu 'anha) shangazi lake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa mwingi wa hekima, hodari wa kuyapima mambo, shujaa na mkali. Hata wanaume walikuwa wakipanga na kupanguwa huku wakiwaza na kufikiri kabla ya kuamua kujadiliana au kupambana naye.
Anajulikana kuwa ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya kuwahami wanawake wenzake wa Kiislamu.
Nasaba Yake
Baba yake ni Abdul Muttalib bn Hashim babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) aliyekuwa kiongozi wa Makureshi mwenye kutiiwa. Mama yake Bi Safiyyah ni Halah binti Wahab dada yake Aminah binti Wahab mama yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam).
Mumewe wa mwanzo aliyefariki dunia akiwa naye alikuwa Al Haarith bin Harb ndugu yake Abu Sufyaan bin Harb mkuu wa kabila la Bani Umayyah.
Mume wake wa pili alikuwa Al ‘Awwaam bin Khuwaylid ndugu yake Bi Khadijah binti Khuwaylid (Radhiya Llahu 'anha) mke wa mwanzo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) na mama wa mwanzo wa Waislamu.
Mume wake wa pili Al ‘Awwaam bin Khuwaylid alipofariki dunia alimuacha akiwa na mtoto mdogo wa kiume Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) aliyesilimu pamoja na mama yake akiwa na umri wa miaka minane.
Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) alikuwa sahibu mpenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) aliyesema juu yake:
"Kila Mtume anaye sahibu, na sahibu yangu ni Az Zubayr."
Na akasema:
"Talha na Az Zubayr sahibu zangu Peponi."
Ulezi Wake
Bi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) alimlea mwanawe Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) malezi magumu na ya shida. Mchezo wake ulikuwa ni kutupa mikuki, kuchonga mishale na kutengeneza pinde.
Alikuwa akimtia vishindo na kumpeleka sehemu zinazotisha na za hatari. Na anapoingiwa na hofu au uoga alikuwa akimpiga kipigo chenye kuumiza. Na kwa ajli hiyo watu wake walikuwa wakimlaumu.
Mmoja katika shangazi zake aliwahi kumuambia:
"Si hivyo anavyopigwa mtoto. Unampiga mfano wa mama anayemchukia mwanawe. Hicho si kipigo cha kumlea mtoto."
Bi Safiyyah akamjibu kishairi akimuambia: "Anayesema namchukia hajasema kweli. Nampiga apate akili, ayashinde majeshi makali na afuzu kikweli."
Kusilimu Kwake
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) alipopewa utume, alitakiwa aanze kwa kuwaonya watu wake na kuwapa bishara njema, na kuwalingania. Aliwakusanya jamaa zake wanaotokana na tumbo Abdul Muttalib wanawake kwa wanaume, wadogo kwa wakubwa na kuwahutubia ifuatavyo:
"Ewe Fatima binti Muhammad. Ewe Safiyyah binti Abdul Muttalib. Enyi wana wa Abdul Muttalib. Hakika mimi similiki chochote kwa ajli yenu mbele ya Mwenyezi Mungu."
Kisha akawataka wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja na kuamini ujumbe aliokuja nao.
Wakakubali miongoni mwao waliokubali na wakakanusha waliokanusha kwa upotofu wao. Na Bi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alikuwa miongoni mwa kundi la mwanzo kumuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) na kumsadiki.
Hijra Yake
Kwa hivyo Bi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) pamoja na mwanawe Al Zubair bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) wakawa miongoni mwa kundi la mwanzo kujiunga na msafara huu ulioieneza nuru kila pembe ya dunia, na wakapata tabu nyingi kama walivyopata tabu wenzao wote waliotangulia kuingia katika dini hii tukufu tokea siku za mwanzo.
Makureshi waliwaonjesha Waislamu kila aina ya mateso na adhabu, mpaka pale Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Taala) alipomtaka Mtume wake (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) aondoke Makkah yeye pamoja na wafuasi wake na kuhamia Madinah. Na hapo ndipo Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alipoitikia mwito huo kuuhama na kuuacha nyuma mji anaoupenda, Makkah, na kuacha nyuma kila anachokipenda katika mji ule mtukufu na kila kinachomkubusha utoto wake na ujana wake.
Jihadi Yake
Juu ya kuwa umri wake ulikaribia miaka sitini, lakini Bibi huyu mtukufu (Radhiya Llahu 'anha) alikuwa na misimamo madhubuti isiyosahaulika mbele ya adui wa Mwenyezi Mungu katika kupigana jihadi.
Alikuwa akitoka pamoja na wanawake wenzake kuwasaidia Waislamu wanaopigana jihadi kwa kuwapelekea maji na kuwachongea mikuki na mishale pamoja na kutengeneza pinde zinapokatika. Wakati huo huo akiwa karibu na vita aliweza kupata habari za mtoto wa ndugu yake Muhammad (Swalla llahu alayhi wa Ssallam) anapokuwa vitani pamoja na habari za ndugu yake Hamzah bin Abdul Muttalib (Radhiya Llahu anhu) na pia habari za mwanawe Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Llahu 'anhu) na juu ya yote hayo aliweza kujuwa juu ya maendeleo ya vita vinavyopiganwa kwa ajili ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.
Na siku ile alipowaona Waislamu wakikimbia vitani huku majeshi ya makafiri yakikaribia kumfikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) na kumuua, Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) aliruka kama simba jike anavyoruka anapowaona wanawe wakishambuliwa. Akamnyang'anya mkuki mmoja wa waliokuwa wakikimbia uwanja wa vita, akaanza kuelekea mbele kuwakabili maadui huku akiwatolea ukali Waislamu akiwaambia:
"Ole wenu! Mnashindwa kusimama na Mtume wa Mwenyezi Mungu?
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) alipomuona akielekea katika uwanja wa vita aliogopa asije akamuona ndugu yake Hamzah (Radhiya Llahu 'anhu) aliyeuliwa na mwili wake kukatwa katwa vibaya. Akamuambia mwanawe Az Zubayr:
"Mzuwie mama yako ewe Zubayr, mzuie mwanamke ewe Zubayr."
Az Zubayr (Radhiya Llahu 'anhu) akamuendea na kumuambia:
"Rudi ewe mama yangu, rudi."
Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu anha) akasema:
"Nipishe huko."
Akasema:
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) anakuamrisha urudi."
Akauliza:
"Kwa nini? Nimekwishapata habari kuwa ndugu yangu ameuliwa na kukatwa katwa vibaya. Yote hayo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Muache apite ewe Zubayr."
Akamruhusu.
Baada ya vita kumalizika Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu 'anha) alisimama mbele ya maiti ya ndugu yake Hamzah (Radhiya Llahu 'anhu) huku akiuangalia mwili wake uliokatwakatwa vibaya huku akimuombea maghfira na kusema:
"Yote haya kwa ajli ya Mwenyezi Mungu. Nimeridhika na kile alichokitaka Mwenyezi Mungu kiwe, na ninategemea malipo mema kutoka Kwake Inshaallah."
Huu ulikuwa msimamo wa Bibi Safiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Llahu 'anha) siku ya vita vya Uhud.
Vita Vya Khandaq
Ama msimamo wake siku ya vita vya Khandaq ndani yake mna kisa chenye kusisimua sana.
Kawaida ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) ilikuwa kila anapokwenda vitani akiwaweka wanawake na watoto na wazee na vilema ndani ya ngome akihofia mtu asiwaendee kinyume akawazungukia na kuwateka.
Siku ya vita vya Khandaq aliwaweka wake zake na shangazi zake pamoja na wanawake wengine wa Kiislamu ndani ya ngome ya Hassan bin Thaabit (Radhiya Llahu 'anhu) aliyeirithi kutoka kwa baba yake. Na ngome hii ilikuwa madhubuti zaidi. Haivunjiki kwa urahisi wala haiingiliki kwa wepesi. Na Waislamu walipokuwa wameshughulika na vita wakipambana na Makureshi na wanaowaunga mkono, waliwasahau wake na watoto wao kwa kujishughulisha na maadui  hao.
Alfajiri ilipoanza kuingia, na waliomo ndani ya ngome walikuwa bado wamelala, Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) aliyekuwa yu macho wakati huo aliona mfano wa mwili ukitaharuki huku na kule ndani ya ngome yao. Akausogelea mwili ule kimya na pole pole mpaka alipoukaribia akaona kuwa ni Myahudi aliyefanikiwa kuingia ndani ya ngome. Alimfuata huku na kule bila Myahudi kuhisi, na hatimaye Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) alitambua kuwa huyo ni mpelelezi aliyetumwa na Mayahudi kuja kupeleleza iwapo ndani ya ngome mna wanaume wenye kuilinda au ni ngome iliyojaa wanawake iliyoachwa bila ya ulinzi.
Bibi Safiyyah (Radhiya Llahu ‘anha) akawa anajiuliza:
"Hawa Mayahudi wa Bani Quraydhah ndio walioivunja ahadi iliyokuwepo baina yao na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) kisha wakajiunga na Makureshi dhidi ya Waislamu. Na hivi sasa hapana mwanamume hata mmoja wa kutuhami, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wote wapo vitani. Akiweza adui wa Mwenyezi Mungu huyu kuwafikia watu wake na kuwajulisha kuwa humu ndani tumo wanawake watupu, watatuteka. Na hilo litakuwa ni balaa kubwa kwa Waislamu."
Hapo hapo akaamua kujifunga uzuri kitambaa usoni na kuzibana vizuri nguo mwilini mwake, kisha akaokota gongo na kuanza kumnyemelea adui yule wa Mwenyezi Mungu kwa tahadhari mpaka alipomkaribia sana. Alipokuwa na uhakika kuwa keshamkaribia vya kutosha na kumkalia vizuri, akanyanyua gongolake juu na kuliangusha kwa nguvu zake zote, akampiga nalo kichwani na kumuangusha chini. Akaendelea kumpiga mpaka alipomuona hawezi tena kuvuta pumzi, kisha akatoa kisu chake na kumkata kichwa kisha akakichukua kichwa na kukitupa juu ya paa, kikabiringitia na kuangukia mbele ya Mayahudi waliokuwa nje wakimsubiri mwenzao.
Walipokiona kichwa cha mwenzao kimekatwa wakasema:
"Tulijuwa sisi kuwa Muhammad hawezi kuwaacha wanawake na watoto peke yao bila ya ulinzi madhubuti wa wanaume."
Kufariki Kwake
Mwenyezi Mungu awe radhi naye Bibi Safiyyah. Alikuwa shujaa na jasiri kikweli, na historia imekwishaandika kuwa yeye ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya dini ya Islamu.
Alifariki dunia wakati wa ukhalifa wa ‘Umar bin Khattaab (Radhiya Llahu ‘anhu) akiwa na umri wa miaka sabini na tatu, Na ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) ndiye aliyeongoza Swalah ya jeneza, na akazikwa bibi huyo katika makaburi ya Al Baqi'y.

4. Ummu Ayman - Mama Muangalizi Wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)


 MIMI NAULIZA, NA NINATARAJI KUWEPO JAWABU KUTOKA KWAKO KWA SUALA NINALOULIZA: JE WAKO WANAWAKE AMBAO WAMEBASHIRIWA PEPO? NA IKIWA LIPO JAMBO HILO, NATARAJI VILE VILE UNISIMULIE HABARI ZAO.
Nikasema: Ndio ewe mwanangu, wapo idadi ya Maswahaba wa kike. Wanawake ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwabashiria pepo. Na nimeazimia kukuarifu kila mmoja miongoni mwao. Kwa kila usiku insha Allaah nitakuhadithia kutokana na umuhimu wa sifa zao ambao waliishi wanawake hao.

Kwa hakika nimekusanya miongoni mwao Ummu Ayman, kwa sababu aliishi na kipenzi chetu, bwana wetu na kipozo cha uoni wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa utoto wake. Aliishi baada ya masiku ya uyatima wake uliokuwa mchungu.

Hii ni baada ya kupitisha Mwenyezi Mungu kadhiya Yake kwa kufa baba yake bwana 'AbduLlaah bin 'Abdil-Mutwalib kabla ya kuingia kwake duniani.

Kisha akaondoka bibi Aamiynah bint Wahab kwa kuelekea kwenye uso wa Mola wake. Alimuacha mdogo aliyetimia miaka sita (6) katika umri wake akilia mbele ya kaburi la mama yake. Kikiumiza moyo kilio hicho na kuporomoka kwa shida za maisha.

Akamkimbilia Ummu Ayman kwa kumuhifadhi kwa utukufu wa Muumbaji, akamuweka bwana wa viumbe (Mtume) juu ya kifua chake na akimshika mikono yake na kumfuta. Na akimfanyia tahafifu kwa machungu yake ya msiba ambao ulifarikisha (kutenganisha) baina yake na mama yake katika wakati ambao alimuhitaji mno.


AKASEMA: LAKINI NINI KITAKUWA MBELE YAKE KWA UMMU AYMAN EWE BABA?

Nikasema: Hakika huyo jina lake ni Barakah bint Tha'alabah. Alikuwa akimsaidia bibi Aamiynah mama yake Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mambo ya nyumbani kwake. Na baada ya kumaliza kipindi cha kumlea (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika ukoo wa banii Sa'ad, alimrejesha bibi Haliymah ambae alikuwa akimlea kwa ridhaa ya mama yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bibi Aamiynah. Na alikuwa Ummu Ayman akimuhifadhi na kumlea na kumuangalia kutokana na shughuli zote zilizokuwepo pembezoni mwa mama yake.

Na mara moja alitaka bibi Aamiynah kuzuru watu wake katika mji wa Yathrib (Madiynah). Akachukua katika ziara yake hiyo mwanawe pekee Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Ummu Ayman. Na baina yao katika njia wakiwa wanarejea, yakamjia maradhi bibi Aamiynah mbele ya kiunga karibu na Makkah. Na wala hakuweza kendelea katika safari yake yakamjia mauti na akafa na kuzikwa katika sehemu hiyo.

Wala hakuwa mbele yake Ummu Ayman ila ni kukibeba kitoto kilichofadhaika na kumpeleka mtoto huyo mpaka babu yake bwana 'Abdul-Mutwalib. Akaanza kumsimulia kwa yale yaliyomtokezea bibi Aamiynah. 'Abdul-Mutwalib Akamtaka Ummu Ayman amlee pamoja nae katika nyumba yake kama alivyokuwa akifanya katika uhai wa mama yake.

Alikuwa Ummu Ayman akimtumikia kwa ubora wa utumishi tofauti kabisa baina ya alivyokuwepo mama yake na baada ya kuondoka kwake. Alizidisha zaidi juhudi yake na alimfunika juu yake kwa upole na huruma, alifanya hivi kutokana na hofu juu yake na machungu kwa kutengana na mama yake. Alimpa hisia ya kwamba yeye hakuondokewa wala hatokutana na misukosuko kwa kufariki mama yake.

Aliishi yatima kitoto hichi kidogo katika nyumba ya babu yake bwana 'Abdul-Mutwalib kwa uangalizi wa Ummu Ayman na kutukuzwa na kukirimiwa kwa kuangaliwa kwa uzuri wa kumlea na ukarimu wa ulezi. Na kinyume chake yalimfika mauti pia babu yake bwana 'Abdul-Mutwalib. Kabla ya kukata roho, bwana 'Abdul-Mutwalib akausia kwa mwanawe Abu Twaalib kumlea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Akafa 'Abdul-Mutwalib, akahama kipenzi kitukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na mlezi wake Ummu Ayman kuelekea katika nyumba ya Abu Twaalib. Na wala hakukuta katika maskani hiyo mpya isipokuwa ukaribishaji mzuri.

Alikuwa mke wa ami yake Abu Twaalib bibi Faatwimah bint Asad mwanamke mwenye upole wa kumkirimu Mtume. Mpaka akasema: Hakunipatia Abu Twaalib lililo bora kwangu mimi (kuliko malezi haya).

Ummu Ayman akamshuhudia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikuwa hatua baada ya hatua hadi kuingia utu uzima. Na kwa hakika hisia za Ummu Ayman zilifanana na hisia za mtoto kwa mwanawe. Na alikuwa akihudumia katika nyumba ya Abu Twaalib kwa nafsi yake yote. Katika siku za Utume, alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema kumwambia yeye: ((Hawa ndio watu waliobakia wa nyumbani kwetu.))


ALISEMA: NA NI KITU GANI KILITOKEZEA KWA KITOTO KILICHOKUWA YATIMA BAADA YA HAYO EWE BABA?

Nikasema: Baada ya kukua (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kulelewa, akaanza ami yake Abu Twaalib kufuatana naye katika baadhi ya safari zake za biashara.

Akasikia bibi Khadiyjah bint Khuwaylid juu ya uaminifu na ukweli wake Sayyidina Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Basi alisimama nae bibi huyo katika haki, na kukubali ujumbe wake wa kwenda Shaam kwa ajili ya biashara zake. Akimfuatisha pamoja na mfanyakazi wake Maysarah ili waweze kurafikiana.

Wakati aliporudi kwenye msafara, Maysarah alimsimulia bibi Khadiyjah aliyoyakuta kutokana na wema aliofungana nao bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na uaminifu wake. Na vipi walikuwa Malaika wakimfunika na kumlinda yeye na joto la jua. Akakubali bibi Khadiyjah kumwita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka aje kumposa.

Baada ya kutimia ndoa hiyo ya vipenzi viwili hivyo, yaani bibi Khadiyjah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alipata utulivu Ummu Ayman ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amepambazukiwa katika uchungaji wa bibi mtukufu. Hajaufikia ubora wake cheo chake mwanamke yeyote miongoni mwa wanawake wa Ki-Quraysh, kutokana na kukubali kuolewa vile vile na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ummu Ayman akachukua hadhi yake (ya kike) katika uhai wa kidunia. Akatanguliza mtumishi Ghabiyd bin Zayd mmoja miongoni mwa wanaotoka katika ukoo wa banii Haarith bin Khazraj kumposa Ummu Ayman. Akawafikiana Ummu Ayman juu ya ndoa hiyo, baada ya kutaka ruhusa kwa kipenzi kitukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambae alitia baraka kutokana na hatua hiyo na furaha kubwa.

Ilikuwa hamu ya Ummu Ayman juu ya kusarifu kwa uchungaji wa mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kushughulikia mambo yake, wakati alipopata utulivu juu yake na kuhakikisha anapata utulivu wa pahala kwa ndoa yake (bwana Mtume) kwa bibi wa Ki-Quraysh wa mwanzo. Akakuta juu ya kitu cha mwanzo katika uhai wake ameweza kukihakikisha. Na kutokana na hayo hatua yake ya pili juu ya kupata utulivu na kuanzisha ukoo wake.

Aliolewa Ummu Ayman na Ghabiyd na ikatowa matunda ndoa hiyo kwa kupata mtoto aliyeitwa Ayman. Na ilikuwa furaha kwa wazee wake wakubwa.

Akashusha wahyi Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliyetukuka kwa mjumbe Wake bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ujumbe wa Uislamu. Baada ya kulingania kwa siri, wakati Alipotuamrisha Mwenyezi Mungu juu ya kuitangaza na kuita watu katika diyn mpya ya Kiislamu alipata uadui mkubwa na upinzani mkubwa hasa hasa kwa jamaa zake wa karibu. Akafa ‘ami yake na mkewe bibi Khadiyjah waliokuwa pembezoni mwake kwa kumsaidia na ilikuwa ni khayr kwa kumnusuru yeye. Na alikuwa bibi Khadiyjah wa mwanzo kuitikia wito wa Uislamu. Na alitilia nguvu Abu Twaalib juu ya kufungamana nae na kumlinda yeye kwa kila kitakachotokea kutokana na utukufu wake na cheo chake. Kwa sababu Ma-Quraysh walikuwa wakihifadhi kwa kutomuudhi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Abu Twaalib sehemu yake ya juu na uongozi wake na wakimkirimu kwa ukarimu wa juu.

Ummu Ayman na mumewe Ghabiyd bin Zayd walisilimu kwa pamoja. Wakachukua nafasi Ma-Quraysh kumfanyia maudhi kama ilivyo ada ya kumuudhi kila aliyemfuata bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kila aliyeacha diyn za baba zao na mababu zao.

Hapo nyuma, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizuiliwa kuteswa kutokana na kinga aliyoipata kutoka kwa ami yake bwana Abu Twaalib. Baada ya kufariki ami yake, yalitokea yale ambayo asiyoyatarajia. Wakati huo huo alikosa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kipenzi cha kumnusuru au pakukimbilia kwake kutokana na kifo cha mkewe bibi Khadiyjah mama wa waumini. Abu Twaalib alianza kutangulia kwa kufariki kabla ya bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘Anha). Hapo Ma-Quraysh walianza kuteremsha maudhi kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakapata wanayoyataka kutokana na fujo na kumzidishia mabalaa ya kila aina.

Wakati yalipozidi maudhi ya Ma-Quraysh juu ya Waislamu, aliwaruhusu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kuhama kuelekea Yathrib (Madiynah) kila walipopata fursa ya kupenya usiku mara moja kutokana na shingo za Ma-Quraysh na wapumbavu wake. Na hayo ni kwa sababu Ma-Quraysh walikuwa wakiwazuia vijana kufuata diyn ya Uislamu. Wakiwaadhibu mpaka warudi nyuma katika diyn yao na kufuata miungu yao.

Na katika siku za ukame lilizidi joto, ikamuwia vigumu Ummu Ayman kuelekea Madiynah mji wenye nuru kwa ajili ya kuhama kwani alikuwa amefunga. Juu ya hivyo, alitoka Ummu Ayman bila ya chakula wala maji. Likaanza joto kumzidi, na kiu ikimzidi juu yake mpaka akafikia sehemu iliyoitwa Rauha – baina ya Makkah na Madiynah – zilipungua nguvu zake na ukaanguka ushupavu wake.

Akaanza kusinzia katika uwanja wa tabu. Akaanza kuona ndoo inaning’inia kwake yeye kutoka mbinguni iliyobeba kitu cheupe, mpaka ikafikia juu ya kifua chake. Akakimbilia kwa kuyapata maji yaliyokuwemo humo. Kisha akanywa na akanywa mpaka akamaliza kiu. Akahadithia Ummu Ayman kwa watu na akasema kwamba hakupata kiu tena baada ya kunywa maji hayo.


AKASEMA: ILIMFIKA KIU WAKATI WA FUNGA LAKINI NI VIPI ILIKUWA KIU YAKE?

Ndio ewe mwanangu, kwa hakika Alitambua Mwenyezi Mungu fadhila zake kwake. Akahifadhi kwake yeye kudra yake, akasogezea maji kwa Ummu Ayman na Akaondosha kwake yeye kiu. Wala hayakuwa hayo isipokuwa ni takirima kutoka kwake Mwenyezi Mungu kwa Ummu Ayman. Kwa kule kumfanyia ukarimu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa kumlea alipokuwa mdogo na kufuata ujumbe mkubwa aliokuja nao.

Wakati alipopata ruhusa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhama kuelekea Madiynah, alikuwa ni mwenye kuwakabili watu wake pamoja na waliohama ambao waliuacha mji wao wa Makkah kuelekea Madiynah. Mtume alisaidiana na wale waliohama pamoja na ndugu zao wa Ki-Answari kwa kujenga Msikiti ulio Mtukufu ambao aliuamrisha kuswaliwa baina yao. Mpaka pale lilipotimia jengo lake wakaanza Waislamu kuongoza kwa ajili ya kuwapita katika Swalah. Aliondosha tofauti zao Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Akanadi mwenye kunadi kwa ajili ya kutoka kwenda kupigana vita. Hakuna aliyekwenda kinyume na wito wake. Wakapata katika unyenyekevu- ama nusra ama shahada.

Wakati wa katika vita vya Khaybar, alitoka Ghabiyd bin Zayd pamoja na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na maswahaba Waislamu kwa ajili ya kupigana na Mayahudi na kuwang’oa katika Khaybar kutokana na kuvunja kwao ahadi. Ama mkewe Ummu Ayman kwa hakika alitoka pamoja na idadi miongoni mwa Maswahaba wakiwa wasafi sio kwa kupigana, lakini kwa ajili ya kuwatibu majeruhi au kuwapa maji wapiganaji na kuwatayarishia chakula. Na ilikuwa furaha ya Ummu Ayman kwa kutelekeza wajibu huo, kwa hakika imefikia upeo. Na imekuwa ni wema wake usiokuwa na mpaka.

Akaingia ndani ya vita kwa ajili ya kuwanusuru Waislamu, na akandoka Ummu Ayman kwa ajili ya kumtafuta mumewe Ghabiyd kwa ajili ya kushirikiana katika furaha ya kuwashinda Mayahudi. Lakini wapi yalikuwa malengo yake?! Kwa hakika alikuwa Ghabiyd mmoja katika waliofuzu kwa shahada, na akapambazukiwa Ummu Ayman katika ujane.

Alipotambua hilo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yale yaliyomsibu yule aliyebeba ulezi wake yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alihuzunika kwa ajili yake na akamtembelea ili kumpa pole. Na alikuwa akirudia rudia ziara yake kwake Ummu Ayman. Hakuweza Ummu Ayman kuificha huzuni yake kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mawazo ambayo yalimjaa katika nafsi yake.

Katika vikao vya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba zake watukufu, ilipita katika moyo wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kumfariji Ummu Ayman, akasema kuwaambia Maswahaba:

((Nani atamfurahishia kumuoa mwanamke anayetokana na watu wa peponi, basi amuoe Ummu Ayman)).

Bwana Zayd bin Haarith alikuwa ametengana na mkewe Zaynab bint Jahsh mtoto wa ‘ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya kupambazukiwa katika maisha yao wawili hao kwamba hawawezi kuishi pamoja.

Ama aliposikia Zayd maneno yale ya Mtume kuhusu Ummu Ayman. Hakuacha kukata tamaa hadi alipotia nia ya kupata utukufu wa ndoa kwa Ummu Ayman, na wala hakukubali kumfikia asiyekuwa yeye bwana Zayd.

Wala haikuwa kwa Ummu Ayman kwamba ni mzuri wa sura, bali ni kinyume chake. Alikuwa mweusi wa ngozi, na pua ya kulala. Lakini alikuwa na vitu viwili vya kuonewa wivu kwa kumlinganisha yeye: akiitwa Barakatan na pia akiitwa Ummu Ayman. Hakuna kitu chenye uzito na baraka kama binaadamu kuwemo katika ndoa.

Akaibariki Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndoa hiyo ambayo imekusanya baina ya watu wawili ambao anawapenda na wa karibu nae. Akaishi Zayd pamoja na Ummu Ayman kwa uzuri katika masiku ya uhai wao. Na ikatoa matunda ndoa hiyo yenye baraka kwa matunda yenye khayr. Waliruzukiwa kwa du’aa ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mtoto aliyeitwa kwa jina lake ni Usaamah. Akapambazukiwa Usaamah ni mwenye mapenzi juu ya mapenzi. Akaishi Usaamah pamoja na ndugu yake Ayman katika malezi ya wazazi wawili. Akalelewa na kushughulikiwa na mapenzi ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ukabaki wema ukiendelea katika ukoo huo katika sura ya ukarimu. Mpaka ikafikia vita vya Mutta. Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaliandaa jeshi lenye wasimamizi alfu thalathini (30,000) kwa ajili ya kupigana. Jeshi lililosheheni wapiganaji na viongozi madhubuti kabisa. Yamekuwa hayo kwa ajii ya kuwapiga Warumi - maadui wa Mwenyezi Mungu.

Ilikuwa ni kawaida ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuweka juu ya kila kundi la majeshi kiongozi mmoja. Isipokuwa siku ya vita vya Mutta, kwa hakika alijaalia kwao wao viongozi watatu katika kila kundi la jeshi. Na akawapa habari ya kwamba kingozi mmoja wa mwanzo ni Zayd bin Haarith, ikiwa atapigwa basi kiongozi wa pili ni Ja'afar bin Abi Twaalib na akipigwa basi kiongozi wa tatu ni 'AbduLlaah bin Rawaah.

Wakakutana wapiganaji wote kwenye mkutano ambao zana hazikutosha za kupiganania. Wakakubaliana viongozi hao watatu juu ya kutegemeana katika mpangilio ambao aliupanga kwao wao Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kutoka kwao kwa ajili ya vita. Na katika mji wa Madiynah uliteremka wahyi kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika yaliyopita. Akasimama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutangaza kwa Waislam kwa mapenzi ya Zayd, bin Ja'afar na mtoto wa Rawaah. Bila ya kusahau kwamba Ummu Ayman amepambazukiwa na ujane kwa mara ya pili, hali ya kuwa waume zake wote wamefariki wakiwa ni mashaahid! Wala hakuwa Ummu Ayman mwenye kuomboleza isipokuwa ni mwenye matarajio na subra na kustaghafiru. Wala hakikuwa kifo cha mumewe wa pili ndio chanzo cha kukatisha uhai wake.

Alipotoka Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupigana na washirikina katika vita vya Hunayn, alitoka pamoja nae Ayman, mwanae Ummu Ayman katika ndoa yake ya mwanzo pamoja na bwana Ghabiyd baada ya kukua kwake na kutimia ujana wake.

Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Aliye juu, Ayman naye akashuhudia kwa kufa shahidi katika vita na kufuata njia ya baba yake na mume wa mama yake. Akasubiri bibi Barakah juu ya uamuzi wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika kulimsaidia yeye juu ya kuwa na iymaan kubwa na nguvu ambayo haikuteteruka juu ya jabali. Akasubiri hali ya kuwa amekwisha tanguliza vijana watatu aliowapandikiza mwenyewe ndani kutokana na kifua chake kwa ajili ya kupata radhi za Mola wake.

Lakini subra ya Ummu Ayman iliweza kuporomoka na azima yake na nguvu zote zilibomoka. Huo ni wakati ambao Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitangaza kuwaaga wafuasi wake. Kwa hakika alihuzunika kwa huzuni isiyosemeka hadi kumkosesha fahamu za akili.

Kwa hakika amepokea Imaam Muslim katika Swahiyh yake Hadiyth iliyosimuliwa na Anas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu), baada ya kufa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha: ((Ni wajibu kwetu sisi kwa Ummu Ayman kumtembelea kama ilivyokuwa (kwangu).)) Alianza kulia na akasema kutwambia sisi: ((Nini kilichobakia? (Hakikubaki kitu) isipokuwa yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu (kifo) ni khayr kwa Mjumbe wake.))

Akasema Ummu Ayman: Kilichoniliza sio kwamba nilikuwa sijui juu ya kile Alichokikadiria Mwenyezi Mungu ni khayr kwa Mjumbe wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini ninalia kwa sababu wahyi umekwisha katika mbinguni. Isipokuwa ni kujishajiisha juu ya kile kilichobakia. Tukawa tunalia pamoja nae. [Swahiyh Muslim, 103/2454]

Kwa hakika Ummu Ayman alishuhudia uongozi wa Sayyidna 'Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na Khaliyfah huyo alimpa heshima yake namna alivyostahiki.

Na katika ukhalifa wa Sayyidna 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Ummu Ayman alikwishaingia katika hali ya uzee na amepata utu uzima. Na imekwishamjia hali ya kuvunja ladha ya uhai pamoja na kutengana na jamaa zake.

Ikarejea nafsi yake kwa Mola wake iliyo radhi na yenye kuridhiwa. Kwa hakika ilikuwa kwake yeye ni mapumziko kutokana na safari ya umri uliokuwa mrefu pamoja na tabu na huzuni.

Amrehemu Mwenyezi Mungu kwa barka Ummu Ayman na Ummu Usaamah kwa mapenzi na mapenzi ya hali ya juu. Akakutane nao mashahidi wake akiwa ni mwenye kung’ara na furaha. Amkutanishe Mwenyezi Mungu pamoja na wacha Mungu wema miongoni mwa Maswahaba wa kike waliochaguliwa. AAMIYN!

5. Al-Khansaa/ Tamaadhwir Radhiya Allaahu 'anhaa (Ummu Ash-Shuhadaa)


Jina  lake hasa ni Tamaadhwur Bint 'Amru bin Ash-Shariyd bin Rabaah As-Sulaymiyyah. Alijulikana kwa jina la Al-Khansaa  na vile vile  Umm Ash-Shuhadaa (mama wa mashahidi) kutokana na watoto wake waliofariki katika jihaad. Pia alijulikana kuwa ni mwanamke mwenye haiba nzuri iliyojaa fadhila, tabia njema njema, ushujaa na subira kubwa.
Alipokuwa kabla ya kuingia katika Uislam, alikuwa akitunga mashairi ya beti mbili tatu hadi walipofariki kaka zake Mu'aawiyah na Swakhar bin 'Amru, alifikwa na huzuni kubwa sana hata akawatungia mashairi. Yakawa maarufu, naye akawa mshairi maarufu kabisa. Inavyosemekana hakuweko mwanamke aliyekuwa hodari wa mashairi kama yeye.
Baada ya vifo vya kaka zake, alikuja kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na watu wake wa Bani Sulaym akasilimu.
Ilipofika wakati wa vita vya Qaadisiyyah alidhihirisha subira yake kubwa alipokwenda vitani pamoja na watoto wake wanne wa kiume na akawausia kwa kuwaambia maneno haya mazito:
"Enyi watoto wangu, naapa kwa Yule Ambaye hakuna Apasaye kuabudiwa ila Yeye, nyinyi ni watoto wa baba mmoja, sikumkhini baba yenu, mmesilimu kwa kutii, mmehama kwa khiari yenu, …" hadi akasema "Mtakapoamka kesho Insha-Allah kwa salama, nendeni vitani kupigana na adui zenu, kwani mnajua Aliyowaandalia Allaah (Subhaana wa Ta'aala) ya thawabu nyingi kwa kupigana na makafiri. Tambueni kuwa nyumba ya milele (Pepo) ni bora kuliko nyumba ya kutoweka (Dunia), Anasema Allaah (Subhaana wa Ta'aala
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اصْبِرُواْ وَصَابِرُواْ وَرَابِطُواْ وَاتَّقُواْ اللّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ))

 ((Enyi mlioamini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Allah, ili mpate kufanikiwa)) [Al-'Imraan: 200].
Wakaenda vitani na alipopata habari ya vifo vyao wote alisema: "Alhamdulillah kwa Yule Aliyenipa heshima ya kuuliwa kwao na namuomba Allaah (Subhaana wa Ta'aala) Aniunganishe nao kwa Rahma Zake".
Al-Khansaa (Radhiya Allahu 'anhaa) alifariki katika Ukhalifa wa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allahu 'anhu).

6.  Rumayswaa Ummu Sulaym Al-Answaariyah (Mama Wa Anas Bin Maalik)


ALISEMA MTOTO WANGU: NA NANI YULE AMBAE ALIYEBASHIRIWA PEPO VILEVILE EWE BABA?
Nikasema: Hakika huyo ni Ummu Sulaym al-Answaariyah ewe mwanangu. Baba yake ni Malhani mtoto wa Khaalid mmoja kati ya Answaari katika kabila la Khazraji. Na mama yake anaitwa Malika mtoto wa Maalik.
 Ama mumewe anaitwa Maalik mtoto wa Nadhar, na walikuwa na watoto wao kwa majina ya Anas na Baraa waliokuwa Swahaba zake Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam
AKASEMA: EWE BABA NIHADITHIE KUHUSIANA NA UISLAMU WA UMMU SULAYM NA LIPI LILIKUWA JINA LAKE?
Nikasema: Alikuwa jina lake ni Rumaysaa au Ghumayswaa. Alisilimu baada ya ubalozi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uliposafiri kwenda Madiynah, ili kuwafundisha watu wake Uislamu, kuwapa utambuzi kuhusiana na Diyn na kuwasomesha juu yao Qur-aan. Kisha wakafungamana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na wanawake wa ki-Answaar. Kuingia kwake katika Uislamu kulitimia pale mumewe (Maalik) aliposafiri katika biashara zake. Wakati aliporejea katika safari yake, alijua kuhusiana na Uislamu wa Ummu Sulaym akamshambulia.
Akasema mumewe: Umefanya ujinga (gani)?
Akarejesha juu yake kwa maneno yake: Hapana, lakini nimeamini.
Alikuwa akimchezesha kitoto Anas, akimtamkisha shahada mbili huku akimwambia aseme: Ewe Anas sema: Ash-had ann laa ilaaha Illa Allaah.
Anas akawa anarejesha juu yake: Ash-hadu ann laa ilaaha Illa Allaah.
Naye mama mtu akasema kumwambia Anas, sema: Ash-hadu anna Muhammadan rasuulu Llaah.
Anas naye akaiga kwa kusema: Ash-hadu anna Muhammadan rasuuluLlaah. Mpaka ikamkaa vizuri.
Wakati wote huo mumewe alikuwa akimsikia Ummu Sulaym akimsemeza mwanawe maneno hayo
Mumewe akasema kumwambia Ummu Sulaym huku akimkodolea macho ya hasira: Usinifisidie mwanangu juu yangu.
Ummu Sulaym akarejesha kauli kwa maneno haya: Mimi simfisidii.
Uislamu ulikuwa ni sababu ya ugomvi ambao ulisimama baina yao. Hadi siku moja akaondoka Maalik katika safari zake huku akiwa mwenye kuuweka ugomvi ndani ya moyo. Yakamfikia mauti kwa kuuliwa.
Akapambazukiwa Ummu Sulaym akiwa kizuka, akaendelea kumlea Anas huku akiwa anasema: Sitomuachisha mpaka atakapoliwacha chuchu kwa nafsi yake, na wala sitoolewa mpaka atakaponiamrisha Anas.
Akaanza Anas kukua mkubwa na akaenda Ummu Sulaym kumpeleka Anas kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akamuomba amuombee du'aa Anas. Wakati huo huo akimuomba Mtume amfanye mwanawe kama ni mfanyakazi wake.
Akamkabili Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuombea du'aa Anas kwa Allaah Amzidishie mali na watoto. Na akapambazukiwa ni mmoja kati ya matajiri wa Madiynah wenye kuhisabiwa. Akapata Anas watoto na kumpatia mama yake wajukuu wengi. Hii ilikuwa baraka ya du'aa ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
AKASEMA: KULIKUWA NA NINI BAADAYE KWA UMMU SULAYM EWE BABA?
Nikasema: Alikuwa Ummu Sulaym ni mwanamke mwenye fadhila, na kwake yeye pia alikuwa na utimamu wa akili na sifa za fadhila kwa yale aliyojaaliwa. Alikuwa ni tegemeo la watu wengi, wanawake watukufu wa ki-Answaar na wanaume baada ya kufa mumewe.
Bwana Zayyid bin Sahli alitokea katika kabila la mafundi wa mbao (seremala), akipewa jina la kupanga la Abu Twalha. Alipotambua ya kwamba Ummu Sulaym amepambazukiwa na ujane (hana mume), alifanya haraka asitanguliwe na mmoja kati ya waposaji.
Kwa hakika Abu Twalha aliona hatokataliwa kwani alishtadi kwa mali nyingi anayeweza kutanguliza kutokana na manjano au nyeupe – dhahabu na fedha. Anachohitaji mtu kupitia kwa AbuTwalha huweza kukipata kama vile anavyoomba. Akaja kwa Ummu Sulaym bila ya kufikiri katika akili yake na kumrejesha kutokana na udhaifu wake. Kwani Abu Twalha alikuwa ni mpambaji na mrembeaji mzuri mwenye kujua usanifu wa vitu.
Akakazania Abu Twalha jambo lake la kumposa Ummu Sulaym. Akatoka tena kuelekea kwenye nyumba ya Ummu Sulaym, akapiga hodi na kukaribishwa kupitia kwa mwanawe Ummu Sulaym (Anas). Akamruhusu kuingia wakati alipoweka wazi Abu Twalha nia ya ndoa yake.
Alisema Ummu Sulaym: Je unadhani mfano wa mtu kama wako anarejeshwa ewe Abu Twalha? Lakini kwako kuna kitu kimoja kinanizuia nisiolewe na wewe. Na unadhani Abu Twalha ya kwamba amebakia juu yako mposaji wa mwisho na ameweka juu yako mahari makubwa ambayo hayatoweza kwa yeye kuyatoa au kuzidisha juu yako?
Akasema Abu Twalha: Ewe Ummu Sulaym, hakika mimi ni mtu niliyemiliki mali nyingi, na nitajaalia kuwa sadaka yako (yaani mahari yako) kutokana na dhahabu na fedha, na watashindwa wengine kutanguliza mfano wa mali hiyo.
Akatabasamu Ummu Sulaym, ya kwamba huwenda fikra za Abu Twalha zilimpeleka katika biashara, lakini ni kinyume na alivyofikiria Abu Twalha. Isipokuwa kilichokuwa kinamzuilia yeye kukubali jambo hili ni kinyume na mali ya Abu Twalha.
Alisema Abu Twalha: Una nini? Nitakupa lolote lililokuwa muhimu bila ya kujikalifisha kwa hayo kutokana na thamani yoyote.
Alisema Ummu Sulaym: Ewe Abu Twalha, hakika wewe ni mtu mshirikina, na mimi ni mwanamke Muislamu, haisihi kuwa pamoja kwa mfano huo.
Kisha akaendelea kwa maneno yake: Je hutambui ewe Abu Twalha unaye kwako unayemuabudia juu yake, na unafanya ibada kinyume na Mwenyezi Mungu ambaye amekuumba?
Akasema Abu Twalha: Hapana.
Akasema Ummu Sulaym: Huoni vibaya ewe Abu Twalha ya kwamba kigogo cha mti kimekuwa mungu wako. Na kinyume chake wanatengeneza juu yake unga au kufanyia kuni kwa kupikia chakula au kuwashia moto siku za baridi kali.
Hatimaye Abu Twalha yalimuingia kwenye moyo wake maneno ya Ummu Sulaym pamoja na ugumu wake na yanaelekea kwenye ukweli. Wala hayarejei kwenye njia ya haki.
Kisha akasema Abu Twalha: Na yepi mahari ambayo unayaridhia ewe Ummu Sulaym?
Akasema: Ikiwa utasilimu nitakubali kuolewa na wewe kinyume na dhahabu wala fedha.
Akaelekea Abu Twalha kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujitambulisha Uislamu baina ya mikono yake.
Ikatimia ndoa nzuri kabisa na wakasema wanawake wa ki-Answaar: Hatukutambua mahari makubwa kuliko mahari ya Abu Twalha kwa Ummu Sulaym. Kwa hakika mahari yake yalikuwa ni Uislamu.
Haki! Hakika ilikuwa neema katika ndoa hiyo. Maadamu imejengwa na msingi madhubuti. Na je lipo jambo lenye maslahi kuliko Uislamu kuwa msingi wa ndoa madhubuti na mtukufu?
Hakika Uislamu ni kisaidizi na ni fadhila za chemchem za mambo yote. Wala usidhani hakika Diyn hii ni ya haki kwa watoto wako tu, bali ni tukufu kwa wote kama ilivyochaguliwa. Na ipi ajabu kwa hayo? Kwa hakika Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{{Leo nimekukakamilishieni Diyn yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Diyn yenu.}} [Suratul - Maidah: 3]
AKASEMA: JE HUNIPI HABARI YA KITU KILICHO KUWA BORA KWA UMMU SULAYM EWE BABA?
Nikasema: Hapana ewe mwanangu. Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haingii katika nyumba ya mmoja kati ya waliooana ila kwa Ummu Sulaym. Mtume akaulizwa kuhusu jambo hilo. Akajibu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika mimi namrehemu, ameuliwa ndugu yake pamoja nami.)) [Imepokewa na Muslim: 04, 2455]
Pia kutokana na masimulizi ya Anas kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliingia Peponi akazisikia sauti – Ni sauti ipi – akasema – Nani huyu? Pakasemwa kuambiwa yeye (Mtume): Huyu ni Ghumayswaa binti Malhan mama wa Anas bin Maalik.)) [Imepokewa na Muslim: 105, 2456]
Na Ummu Sulaym ameudiriki ubora, na baraka hizi zimemsibu pia Abu Twalha kupitia ndoa hii yenye baraka ya Bibi Ghumayswaa mama yake Anas (Radhiya Allaahu ‘Anhum).
AKASEMA: JE HUNIPI HABARI EWE BABA YA KWAMBA UMMU SULAYM ALIKUWA NI MWENYE AKILI MADHUBUTI AMBAZO ZIMEMUANDALIA YEYE WEMA NA MAHANGAIKO NA MIPANGILIO YAKE YA USANIFU, NA IPI DALILI AMBAYO IMEKUPELEKEA KUMSIFU KWA HAYO EWE BABA?
Nikasema: Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika vile vile ilipambika akili yake Ummu Sulaym kwa hikmah katika kujaalia (khayr) mahangaiko yake na kuweka mbali aibu zake na upungufu wa kitu. Na hii mifano inatosheleza kwako kwa hikmah zake kwa yale yaliyomtokezea juu yake.
AKASEMA: NA ALITUMIA VIPI HIKMAH NA UONGOZI WAKE KUTENGENEZA MAMBO?
 Nikasema: Abu Twalha alikuwa ana mtoto mdogo aliyempenda katika nafsi yake kuliko kitu chochote. Na alikuwa Ummu Sulaym akimlea na akimchunga. Siku moja alitoka Abu Twalha katika kutafuta rizki. Muda si mrefu mwanawe huyu alifariki bila ya Abu Twalha kuelewa hilo. Akausia Ummu Sulaym kwa watu wa nyumba yake kwamba asipewe habari Abu Twalha kuhusiana na kifo cha mtoto wake.
Wakati alipomaliza Abu Twalha kazi yake, akaswali Swalah ya 'Ishaa Msikitini, akaelekea nyumbani na kumkuta Ummu Sulaym hakika amemuandalia yeye chakula na amezidisha mapambo juu yake kuliko anavyojipamba.
Wakati alipomuuliza hali ya mtoto, akampa habari ya kwamba ni nzuri kuliko ilivyokuwa. Kisha Ummu Sulaym akatanguliza Swala ya 'Ishaa. Abu Twalha akala mpaka akashiba, ukasimama usingizi juu yao.
Wakati walipoamka alisema Ummu Sulaym kumwambia Abu Twalha kuhusiana na kitendo cha jirani yake juu yao: Ewe Abu Twalha, jirani ameazima cha kuazima, wakati alipotakiwa yeye akirejeshe, alichukizwa na alijizuilia juu ya kurejesha. Je amefanya kosa kwa jambo hilo na anaweza kujitetea kwa kujizuilia
Akastaajabu Abu Twalha: Hana udhuru kwa jambo hilo na ubaya ulioje kwa kujizuilia!
Akasema Ummu Sulaym: Kwa hakika ilikuwa kwa mtoto wako ni kiazimo cha kitu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kukirejesha (ni haki), ikiwa utafanya (subra) basi kitarejea
Akaendelea Ummu Sulaym kwa kusema: Hakika sisi sote tunamtegemea Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea
Abu Twalha akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsimulia kutokana na aliyoyafanya Ummu Sulaym.
Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Abu Twalha: ((Akubarikieni Mwenyezi Mungu usiku wenu))
Ikajibiwa du'aa hiyo na akabeba mimba Ummu Sulaym kisha akazaa kitoto cha kiume. Akamuamrisha mwanawe Anas kumbeba ndugu yake mdogo ili kwenda nae kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili amfungue koo na ampatie jina.
 Akaelekea Anas na ndugu yake huku akiwa na tende. Alipowaona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanakuja alisema kumwambia Anas: ((Je unayo pamoja nawe tende?)) Alisema Anas kumwambia Mtume "ndio". Akaichukua tende huku akisoma du'aa na kuilainisha kwa kuitafuna tafuna. Kisha akakifungua kinywa cha mtoto na kumlisha baadhi ya tende hiyo. Akaanza kitoto kuramba ramba utamu tamu katika midomo yake miwili. Akasema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu: ((Wamekanusha Answaar juu ya mapenzi ya tende)) Kisha akamwita jina la 'AbduLlaah. Anas akamrejesha kwa mama yake.
ALISEMA MTOTO: NIAMBIE UKWELI KUHUSIANA NA JIHAAD YA KILA MMOJA BAINA YA WATU WAWILI HAWA, WANA NDOA NA MASWAHABA WAZURI ZAIDI. NA NI VIPI ULIKUWA UKARIMU WAO?
Nikasema: Kwa kila furaha ewe mwanangu, walikuwa na mwenendo wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukoo wa Abu Twalha uliokuwa na nguvu sana. Kwa hakika aliutumia vizuri Abu Twalha upanga katika kumlinda Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoweka mali yake kwa ajili ya maandalizi ya vita na kutilia mkazo haja za Waislamu. Na alikuwa Abu Twalha ni mwenye kutaraji juu hayo kwa radhi za Mola wake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa hakika alikuwa nayo bustani kubwa iliyojaa miti mizito mizito na aina tofauti za matunda. Siku moja alikuwa anaswali ndani ya bustani hiyo na alimuona ndege akiimba juu ya mti, alikuwa ana rangi tofauti. Akavutiwa juu ya kumuangalia kwa ukali wa uzuri wake, ikashughulika akili yake Abu Twalha mpaka hakuweza kukumbuka rakaa ngapi ameweza kuswali.
Wakati alipomaliza Swalah yake alikimbilia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamsimulia kwa kile kilichomtokea juu yake, na vipi aliweza kumshughulisha ndege mzuri ndani ya Swalah yake.
Kisha akasema: Nishuhudie ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimeijaalia bustani yangu hii ni sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na ifanye unavyotaka.
Hakika mfano wa kitu hichi kilichotolewa ni kizuri, hakipatikani kitendo hichi ila kwa yule mwenye mapenzi ya kweli kwa Mola wake na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuyakinisha kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu kuna khayr na ni yenye kubakia.
Ama kwa upande wa Jihaad, Abu Twalha hakika alifikia nafasi ya mbele katika vita vya Uhud. Hivi ni vita ambavyo walikwenda kinyume (kukhalifu) warembeaji wa mishale wa Kiislamu amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakaacha sehemu zao na kutaka kuokota na kunyang'anyiana ngawira ambazo zilienea kwenye uwanja wa mapambano. Kwa hakika ilikuwa hapana budi kubadilika muelekeo wa ushindi kwa maslahi ya washirikina badala ya kuwa ni kwa maslahi ya Waislamu. Wakakimbia Waislamu pale alipoeneza mmoja wa washirikina ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha uawa.
Na kilikuwa kichwa cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kimepasuka, zimevunjwa taya zake na amejeruhiwa midomo yake. Ikaanza damu kumtiririka mtukufu, na alikuwa amezungukwa mbele yake na kikundi cha Maswahaba watukufu (Radhiya Allaahu ‘Anhum) kama vile bangili zinavyozunguka mkono. Sio hivyo tu, bali wamezitoa panga zao, wakamzunguka na kuvitoa vifua vyao bila ya kupita mmoja kati ya washirikina baina yao.
Naye hakuwa nyuma, kwani Abu Twalha alikuwa ni mmoja kati ya wale walioweka ngome kwa Mtume siku hiyo. Akaanza Abu Twalha kuwarushia washirikina mishale isiyo na idadi.
Abu Twalha alimwambia maneno yafuatayo pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kujinyanyua kutoka sehemu aliyokaa, kwa ajili ya kuona wapi imeangukia mishale: Kwa baba yangu na mama yangu, ewe Mtume, usiwachungulie yakaja kukupata maudhi yao, nijaalie mimi kwa Mwenyezi Mungu ni fidia yako.
Mara aliiingia kwao wao mmoja wa Waislamu akisema kwamba washirikina wanakimbia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kumwambia: ((Rembea mshale wako baina ya mikono ya Abu Twalha na wala usipite (mshale) kutokana na wao ukakimbia))
Aliendelea Abu Twalha kurembea na kumlinda kutokana na hayo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mpaka akavunja mipinde mitatu. Na akauwa idadi kubwa ya maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui dhidi ya Diyn moja, ikafikia idadi yake watu ishirini (20).
Ikaja siku ya vita vya Hunayn, wakatoka wanandoa hao watukufu pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Jihaad dhidi ya washirikina. Na alikuwa Ummu Sulaym juu ya ngamia wa Abu Twalha, wakati alipomuona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Sulaym alinadi: Kwa baba yangu na mama yangu ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nitawauwa hawa wote waliokimbia mlimani (Uhud), kwa ajili yako wewe kama walivyouawa wale ambao walitaka kukuuwa wewe. Mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema: ((Akutosheleze Mwenyezi Mungu ewe Ummu Sulaym))
Hakika Ummu Sulaym alikuwa ni jemedari aliye tayari kwa mapambano. Kwani katika vita hivyo vya Hunayn, Abu Twalha alimuona na kitu mikononi mwake, akamuuliza: Nini hichi ulicho nacho ewe Ummu Sulaym.
Akasema Ummu Sulaym: Panga nimeichukua pamoja nami, atakaponikurubia mmoja kati ya washirikina nitalichoma tumbo lake.
Akasema Abu Twalha: Hivyo hukusikia yale aliyoyasema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?!
Alisema Jubayr bin Mutwghama: Kwa hakika niliona kabla ya kushindwa kwa watu (yaani washirikina) huku watu wanapambana mfano wa mkusanyiko wa guo kubwa jeusi, limetanda kutoka mbinguni mpaka likaanguka baina yetu na baina ya watu. Nikaliangalia nikaona kana kwamba (hao wapiganaji) ni wadudu chungu weusi wametawanywa na wameenea katika jangwa. Basi nikawa nina shaka kwamba hao ni Malaika, na wala hawakuwa Malaika isipokuwa ni kushindwa kwa watu.
Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
{{Bila shaka Mwenyezi Mungu Amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayn (pia); ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu; ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma (mnakimbia).}}
{{Kisha Mwenyezi Mungu Akateremsha utulivu Wake juu ya Mtume Wake na juu ya walioamini. Na Akataremsha majeshi (ya Malaika) ambayo hamkuyaona, na Akawaadhibu wale waliokufuru; na hayo ndiyo malipo ya makafiri.}}
{{Kisha baada ya haya Mwenyezi Mungu Atawasamehe Awatakao (katika wale makafiri maadamu watasilimu watubie). Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}}
[Suratu-Tawbah: 25-27]
Vile vile alimkunjulia Mwenyezi Mungu Mjumbe Wake kwa (kumteremshia majeshi ya) Malaika na ushindi ukawa kwa Waislamu. Wakawashinda makafiri, shukurani zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote.
ALISEMA MTOTO: EWE BABA NIZIDISHIE MIMI MASIMULIZI JUU YA FADHILA ZA UMMU SULAYM
Nikasema: Ummu Sulaym alihifadhi Hadiyth ambazo alizisikia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha akisimulia, na akawa amechukua juu yake idadi ya Hadiyth na baadhi ya Maswahaba wamesimulia kutoka kwake.
Jumla ya wapokezi waliosimulia kupitia kwake ni: mwanawe – Anas bin Maalik, 'AbduLlaah bin Abbaas, Ghamra bin Ghaaswim Answaari, Zubayr bin Thaabit, 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf. Hizi ni fadhila za Mwenyezi Mungu, Humpa Amtaka
Amepokea Ghatwaa kutoka kwa Ummu Sulaym Al-Answaariy: Alisema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza Ummu Sulaym: ((Kwa nini Ummu Sulaym hujaja kuhiji pamoja nasi mwaka huu?)) Akasema Ummu Sulaym: Ewe Mtume kulikuwa kwa mume wangu kuna watu wawili, ama mmoja amehiji juu yake, ama mwengine amemuacha akimwangalia juu yake mitende. Akasema: ((Pindi itakapokuwa Ramadhaan au mwezi wa kufunga, fanya 'Umrah ndani yake, kwani hakika ya 'Umrah ni mfano wa Hijja, au huchukua nafasi ya Hijja))
Akabaki Ummu Sulaym akikata masiku ya uhai wake baina ya funga na kisimamo na kupigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mpaka ikamfikia kikata ladha na kufarikiana na jamaa zake. Akalala katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu, ambao hakuna hata mmoja anaeweza kuwarehemu waja wake sawa sawa.
Akaishi Abu Twalha hadi kukutana na kipindi cha ukhalifa wa mwenye nuru mbili - 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Alimtaka Abu Twalha kutoka pamoja na jeshi la vita vya baharini aliloliandaa Sayyidna 'Uthmaan. Abu Twalha aliweza kutanguliza kwa hilo upanga wake.
Wanawe wakamwambia: Tuache sisi tuende badala yako wewe, unahitaji kwa sasa mapumziko.
Walipokuwa katikati ya bahari yakamsibu maradhi Abu Twalha akafariki. Akawa miongoni mwa Maswahaba waliofariki ambao walitafutiwa sehemu ya kuzikwa miili yao kwa muda wa siku saba. Hatimaye wakakipata kisiwa. Na alikuwa amefunikwa kama vile amelala, na wala hakubadilika kitu chochote.
Amrehemu Mwenyezi Mungu Abu Twalha na Ummu Sulaym na Awakutanishe wawili hao mbele Yake wakiwa ni wenye kung'ara na kufurahi.

No comments:

Post a Comment