`ATHARI YA MALEZI KWA MTOTO
Malezi huanza mbali sana na ni amali inayoendelea (continuous
process). Pia ni amana ambayo Allah (Subhaanahu Wata’ala) atakuja kutuuliza
siku ya siku. Ni kazi inayoanza tokea mtoto anazaliwa na yuko
katika hali ya uchanga mpaka mwisho wa maisha yake. Sehemu kubwa ya tabia
anazokuwa nazo mtu basi alizipata alipokuwa utotoni na hivyo kuendelea mpaka
mwisho wa uhai wake.
Mtoto (kwenye umri mdogo kabisa) ana uwezo mkubwa wa kuiga,
kuweka kumbukumbu (kwenye subconscious mind), na kisha kujaribu kufanya kama
anavyoona wazazi au walezi wake. Hapa tunataka kufuta ile dhana kwamba mtoto
mdogo hana uwezo wa kutambua yanayojiri maishani mwake. Uwezo anao ila
asichoweza kukifanya ni kuuonesha uwezo huo kutokana na umri wake. Wataalamu
wa malezi katika uislamu wameliona hili na kusisitiza wazazi kuitumia nafasi
hii muhimu na adimu na kuhakikisha mtoto anapata muongozo uliokuwa sahihi
tokea mapema.
Mtoto amepewa uwezo na Allah Allah (Subhaanahu Wata’ala) wa
kuwa tayari kupokea chochote atakachopewa kutoka kwa wazazi /walezi wake
ikiwa na tabia nzuri/mbaya mazoea mazuri/mabaya, muongozo mzuri/mbaya. Na
anachokipata kitakuwa na athari katika maisha yake ya baadae.
Ndiyo maana malezi sahihi ya kiislamu yanatakiwa yaanze mapema
kwani matunda yake yanakuwa na mafanikio atapokuwa mkubwa. Kwa hivyo Uislamu
umeweka kiwango cha kuhakikisha mtoto anaanza malezi sahihi ni pale
atakapotimia umri wa mwaka mmoja.
|
Kumfundisha
Mtoto Malezi Ya Kiroho
Wazazi/walezi watakapoanza mapema kuwalea watoto malezi ya kiroho na ya kiimani watamsaidia mtoto kukua katika hali ya kuwa na imani inayojengeka na kuwa madhubuti siku hadi siku na miongoni mwao ni:
1 Kuwapa nafasi watoto kufikiri na kuzingatia yaliyowazunguka
Mtoto, kimaumbile, ana tabia ya kupenda kuuliza na kutafuta majibu kwa yale yanayowazunguka. Ni muhimu kwa mlezi kutumia wakati huu kumfundisha mtoto utukufu wa Allah (Subhaanahu Wata’ala) katika maumbile yake, katika vitu vilivyomzunguka kama ardhi, mbingu, nyota, jua mwezi, bahari n.k
2 Imani ya mtoto huongezeka kwa kuiga waliomzunguka
Mtoto akiona mlezi wake na wanaomzunguka wanatekeleza ibada kikamilifu au kuwasikia wanamtaja Allah (Subhaanahu Wata’ala) au kusikiliza na kutazama mambo ya kidini, basi na yeye hupendelea kuwaiga hasa katika wale anaowapenda miongoni mwao.
3 Kumzoeza mtoto kurudi kwa mola wake kila wakati na hasa kwenye misukosuko.
Mtoto akipatwa na shida yoyote hata kama ni ndogo basi afundishwe na kuzoeshwa kurudi kwa mola wake kumuomba na kuomba msaada( angalia Wosia wa Mtume Muhammad(Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam) .
4 Kumzoesha watoto kuhisi kuwa Allah (Subhaanahu Wata’ala) yupo pamoja nao daima
Allah (Subhaanahu Wata’ala) yupo pamoja nasi daima. Na yeye ndie anaejua yanaoonekana na yaliyofichikana. Ni wajibu wa mlezi kumuandaa mtoto ajihisi kuwa ana Allah (Subhaanahu Wata’ala) karibu yake bila ya kutumia njia za kumtisha au kumkaripia bali kutumia busara kumfanya ahisi Allah (Subhaanahu Wata’ala) anamuona na yupo pamoja nae.(angalia nguzo za ihsani)
5 Kumzoesha mtoto kupenda kumtaja na kumkumbuka Allah (Subhaanahu Wata’ala)
Ni wajibu wa mlezi kumfundisha mtoto du’aa tofauti pamoja na kumfahamisha athari za du’aa hizo. Pia kuhakikisha anaendelea kuzitumia dua kila zinapohitajika kama anapoanza/kumaliza kula, kwenda/kutoka chooni,kulala n.k
Umemuandaa
Mtoto Mwema wa Kukuombea Du’aa?
Wengi wetu tunaifahamu vizuri Hadithi ya Mtume Swalla Allahu
‘Alayhi Wasallam ambayo inaelezea mambo yakatayomfaa mtu baada ya kuondoka
duniani.
Katika mambo matatu yaliyotajwa ambayo ni Sadaka yenye
kuendelea, elimu itakayonufaisha watu na mtoto mwema atakayemuombea mzazi wake,
kwa makala hii tutajaribu kuuliza suala hili la kimsingi kama ni wazazi je
tayari tuna mipango au mikakati ya kumuandaa mtoto wa aina hii ambaye atakuja
kutujaza thawabu na ujira hata kama hatupo duniani.
Maulamaa walivyoifahamu Hadithi hii ya Mtume Swalla Allahu
‘Alayhi Wasallam wanasema kwamba Hadithi hii inatupa changamoto ya kujiandaa na
akhera kama vile tupo duniani kwani hututoweza kufanya amali (tumeshafariki)
lakini tulivyoviacha vimetosheleza kuwa ni amali.
Mtoto aliyetajwa katika hadithi amenasibishwa na sifa ya wema.
Sifa hii si ya kurithi kama mtoto atamrithi baba au mama yake. Ni sifa ya
kuifanyia kazi ili kuipata. Ni sifa ambayo itabidi ijengewe mikakati madhubuti
ya kuweza kumjenga mtoto na kutokana na wema huu ndipo atakapoweza kuomba du’aa
na kuwakumbuka wazazi wake wakiwa tayari wameshaondoka duniani.
Kumzungumzia mtoto mwema kunatugusa katika hali mbili ambazo ni
muhimu kutanabahi nazo. Ya kwanza sisi wenyewe tu watoto na tuna wazazi. Na
hali ya pili sisi ni wazazi na tuna watoto. Katika hali mbili hizi ni
kujiangalia sisi wenyewe kwanza ambao tuna wazazi Je huwa tunawaombea du’aa?.
Je imewahi kutupitia katika nafsi zetu kwamba Wazazi wetu wanahitajia du’aa
zetu kuwasaidia huko walipo?. Na kama hatuna majibu ya masuala haya basi tayari
kuna tatizo katika nafsi zetu kwani sisi wenyewe bado hatujawa na sifa ya wema.
Ndio maana hatuwezi kukumbuka kuwaombea du’aa wazazi wetu.
Mtoto mwenye sifa ya wema hatoweza kupatikana kama katika nyumba
ambayo hakuna msingi madhubuti katika masuala ya kidini. Msingi wa dini ndio
pahala pa kuanzia na kama haupo katika nyumba basi tusitarajie kupata mtoto
mwema ataekuja kutuombea du’aa. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ni msemo wa
Kiswahili na hivyo ikiwa kama upo katika mazingira ambayo dini si moja katika
mambo muhimu katika maisha basi ondokana fikra hii katika maisha ya
baadae ya kupata mtoto atakaeweza kukuombea kama ambavyo umewezwa kukuzwa
katika mazingira hayo hayo ambayo kwayo unayaendelea na kutoijali dini kama ni
mhimili muhimu wa maisha.
Tunakubali kwamba Allah Subhaanahu Wata’ala humuongoa amtakae na
kumpoteza amtakaye na hivyo kudai kwamba ikiwa hakuna msingi katika nyumba si
rahisi kupata mtoto wa aina hii si kigezo cha sifa ya Muumini ambaye kila siku
hutaraji kufanya amali njema za kumridhisha Allah Subhaanahu Wata’ala ikiwemo
kuomba uongofu kutoka kwake. Allah Subhaanahu Wata’ala atatuuliza siku ya siku
masuala nasi tutakuja kosa majibu.
Katika hadithi nyengine ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam
anasema na ujumbe huu umefafanua zaidi hadithi tuliyoitaja kabla na
umemlenga Muumin.
إن مما يلحق المؤمن من عمله وحسناته بعد موته
علما علمه ونشره أو ولدا صالحا تركه أو مصحفا ورثه أو مسجدا بناه أو بيتا لابن
السبيل بناه أو نهرا أجراه أو صدقة أخرجها من ماله في صحته وحياته
تلحقه من بعد موته
رواه ابن ماجه
Katika mambo ambayo Muumin yatamfuatia miongoni mwa amali zake
na mema yake baada ya mauti yake ni elimu aliyojifundisha na kisha akaieneza(kwa
kuifundisha) au mtoto mwema aliyemuacha , au msahafu aliyourithi kisha
akauacha, au Msikiti aliyoujenga, au nyumba, kwa ajili ya waliokatikiwa na
njia, aliyoijenga, au mto alioutengeneza au sadaka aliyoitoa katika maisha yake
wakati wa uzima wake na uhai wake basi vitamfuatia baada ya mauti yake.
Ibnu Maajah
Katika mambo yaliyotajwa katika hadithi, jepesi lao ambalo
halina gharama kubwa kulifanyia kazi ni hili la mtoto mwema ambalo katika mada
hii tunalizungumzia. Kwani asili ya Sadaka yenye kuendelea hutakiwa ifanywe na
mzazi mwenyewe wakati akiwa hai na si kufanyiwa wakati ameshafariki kama
Hadithi nyengine ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam illivyofafanua, ingawa
Maulamaa wamejuzisha kwamba thawabu zitamfikia mhusika kama sadaka itatolewa
kwa niaba yake. Elimu itayowanufaisha watu ni amali ambayo pia ilifanywa na
alieshafariki enzi za uhai wake na hivyo kuchuma thawabu kwa amali yake hii ya
kheri. Ama du’aa ni kitu ambacho gharama yake kubwa ni kuweza kuitamka katika
midomo ikifungamanishwa na Ikhlaas wakati wa kuomba, jambo ambalo kila mtoto
analiweza kulifanya. Hata hivyo bado hili nalo ambalo ni jepesi lao nalo
limekuwa zito.
Mojawapo katika njia nzuri ya kumjenga mtoto ni wakati wake wa
malezi aone kwa mifano jambo hili likitendeka kutoka kwa wazazi wake.
Ninachokusudia wazazi wenyewe, hata kabla ya mtoto, waoneshe kwa vitendo na
kuelezea umuhimu wa kuwaombea du’aa wazee. Wawe ni wazazi wa kupigiwa mfano
ambao ni walezi na waongozi katika kumuonesha dira mtoto kwamba jambo hili ni
muhimu. Hapo mtoto naye ataweza kidogo kidogo huku akiendelea kukua
kulichukulia jambo hili kwamba pia litakuwa muhimu katika maisha yake.
Vipi Tumuandae?
1 Kumchagua mke/mume mwema
Ni wajibu kwa mzazi kumchagua mwenza na mshirika wa maisha yake
atakayejua haki za Mola wake, haki za mume/mke wake, haki za mtoto wake. Kwa
ufupi ni mzazi atakaefahamu majukumu yake na haki zake katika dini na hili
ndilo jambo la msingi kuliangalia wakati wa kuchagua mwenzi na mshirika katika
maisha ya ndoa.
2 Kuomba kupata mtoto mwema
Maandalizi huanzia hata kabla ya mtoto kuzaliwa kwa kuomba du’aa
kwa Allah Subhaanahu Wata’ala kwa tutakachoruzukiwa kiwe ni chema. Amesema
Allah Subhaanahu Wata’ala katika kutupa wasifu wa waja wa Arrahmaan katika
Suuratul Furqaan/74
{وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا
وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَاماً}
[الفرقان: 74].
Na wale wanaosema:Mola wetu! Tupe katika wake zetu na watoto wetu
yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wacha Mungu
3 Kuifungua ndoa kwa du’aa
Du’aa hii ambayo imesuniwa kuombwa na Mume wakati anapokutana na
Mke kwa mara ya kwanza na kumshika kichwa ina ujumbe muhimu wa kuiombea kheri
ndoa na kitakachoruzukiwa katika ndoa kama Anavyosimulia ‘Abdullah Ibn ‘Amr ibn
Al ‘Aasw, Allah Amuwie radhi: Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema:
إذا تزوج أحدكم امرأة، أو اشترى خادما، فليقل:
اللهم إني أسألك خيرها، وخير ما جبلتها عليه، وأعوذ بك من شرها وشر ما جبلتها عليه
Atakapooa mmoja wenu mwanamke au akaajiri mtumishi na aseme:
Allahumma ninakuomba kheri zake na kheri ulizomuumbiya na nnajikinga na shari
zake na shari
ulizomuumbiya Bukhari
4 Jitahidi kumuombea du’aa mtoto
Kila tunapumuomba Allah Subhaanahu Wata’ala, tuombe hidaaya na
uongofu kwa watoto wetu. Tuwaombee yatakayokuwa na kheri kwao na si kuwalaani
na kuwaombea yatakayokuwa na shari nao. Amesema Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi
Wasallam
( ثَلاثُ دَعَوَاتٍ يُسْتَجَابُ لَهُنَّ لا
شَكَّ فِيهِنَّ : دَعْوَةُ الْمَظْلُومِ ، وَدَعْوَةُ الْمُسَافِرِ ، وَدَعْوَةُ
الْوَالِدِ لِوَلَدِهِ ) رواه ابن ماجه وحسنه الألباني في "سلسلة الأحاديث
الصحيحة".
Du’aa (za aina) tatu hutakabaliwa na wala hazina shaka ndani
yake. Du’aa ya aliyedhulumiwa, Du’aa ya Msafiri na Du’aa ya mzazi kwa mwanawe.
Ibnu Maajah Na Sh. Albaaniy anasema ni Hasan (katika
Silsilal Ahaadiyth Asswahiyhah)
5 Jitahidi kuwapenda wazazi
Mapenzi utakayoonesha kwa wazazi yawe ni hayo hayo utakayoonesha
watoto. Kumbuka kwamba vitendo tayari ni fundisho amalia kwa mtoto.Tukiwapenda
Wazee tutapendwa na watoto.
6 Waombee du’aa
wazazi
Tunapojenga mazoea ya kuwaomba du’aa wazazi wetu ndipo
tunayajenga mazoea haya kwa mtoto aombee wazazi wake pia. Ni vyema utakapoomba
umfahamaishe kwanini unaomba ili ajue msingi wa du’aa hii nae
atakapofika wakati wake aweze kukumbuka kwamba jambo hili ni muhimu katika
maisha yake.
Hitimisho
Kwa kila mzazi ana wajibu kufahamu kwamba kumuandaa mtoto mwema
si kazi rahisi kwani inahusisha malezi na makuzi kwa ujumla. Watoto wapate
malezi ya kiImani na kuundeleza msingi huu kwa kumjenga kumfahamu Mola wake na
dini yake kidogo kidogo. Wapate malezi ya kitabia hasa kutoka kwa wazazi wenyewe
wawe mfano bora wa kuigwa na watoto katika tabia zao na hasa katika kujenga
mazoea ya kuwaombea Wazazi.
Ni mtoto wa aina ahii ndiye tunayepaswa tumuandae ili awe amali
zetu njema hapa duniani. Ili awe mwenye kutuenzi wazazi wakati tupo katika
kusubiri siku ya siku. Na kama hatutoweza kuwa na mipangilio madhubuti ya
kumuandaa basi tusijemlaumu yeyote ila tuzirudi nafsi zetu kwa kuitupa fursa
hii adhimu ya kupata thawabu wakati tumeshaondoka duniani kupitia
kwa watoto wetu wenyewe
tuliowazaa.
Tumuombe Mola wetu atupe hima na hamu ya kuwalea watoto wetu ili
wawe pumbazo la macho yetu. Atujaalie tuwe na watoto wema walioleleka katika
misingi ya dini yetu na atupe moyo wa subira na uvumilivu katika kuwaongoa
watoto wetu kufuata misingi na maadili ya dini yetu ili waweze kuja kutukumbuka
kwa kukuomba. Aamiyn.
Wosia wa
Mtume Salla Allahu 'Alayhi Wasalla
Ni wajibu kwa kila mlezi ikiwa ni baba, mama, mwalimu au mwengine yeyote mwenye jukumu la kulea kuwafundisha watoto wosia huu muhimu kutoka kwa Mtume Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kama ulivyokuja katika hadithi iliyomo katika hadithi arubaini za Nnawawiy
عن عَبْدِ اللهِ بنِ عَبْاسٍ رَضي اللهُ عنهما قال: كُنْتُ خَلْفَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم يًوْماً، فقال: " يا غُلامُ، إنِّي أُعَلِّمُكَ كلِماتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَك، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجاهَك، إذا سأَلْتَ فاسْأَلِ اللهَ، وإذا اسْتَعنْتَ فاسْتَعِنْ باللهِ، واعْلَمْ أنَّ الأُمَّة لَو اجْتَمَعَتْ على أَنْ يَنْفَعُـوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيْءٍ قدْ كَتَبَهُ اللهُ لَكَ، وإن اجْتَمَعُوا على أن يَضُرَّوكَ بِشيءٍ لَمْ يَضُروكَ إلا بِشَيء قد كَتَبهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأقْلامُ وَجَفَّتِ الصُّحُفُ
رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ.
Kutoka kwa Abdullah Ibn ‘Abbass Allah amuwie radhi amesema:
Siku moja nilikuwa nyuma ya Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akaniambia: Kijana nitakufundisha maneno (ya kufaa); Mhifadhi Allah (fuata maamrisho Yake na chunga Mipaka Yake) Atakuhifadhi. Muhifadhi Allah na utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah ukitafuta msaada tafuta kwa Allaah (lazima) ujue kuwa ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika ila tu kwa kile alichokwishakuandikia Allaah na wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, hotodhurika ila tu kwa kile Allah alichokwishakuandikia (kuwa kitakudhuru) . Kwani Kalamu zimeshanyanyuliwa (kila kitu kishaandikwa) na sahifa zimeshakauka (Hakuna kupangwa tena wala kupanguliwa).
Imesimuliwa na At-Tirmidhi akasema kuwa ni hadithi Hasan Sahihi.
UFAFANUZI
1 Mhifadhi Allah(Subhaanahu Wata’ala) , atakuhifadhi
Fuata maamrisho yake na chunga mipaka yake ,Allah atakuhifadhi katika dini ,dunia na akhera yako
2 Muhifadhi Allah(Subhaanahu Wata’ala) na utamkuta mbele yako
Chunga tena mipaka pamoja na kuchunga haki zake Allah (Subhaanahu Wata’ala) nae atakuwafikisha na kukulinda.
3 Unapotaka kuomba, muombe Allah(Subhaanahu Wata’ala)
Ukiwa na shida yoyote katika jambo la kidini, kidunia au akhera basi wa kumuomba ni Allah(Subhaanahu Wata’ala) pekee.
4 Unapotaka msaada basi utafute kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala)
Tunaongozwa kumtegemea Allah(Subhaanahu Wata’ala) katika mambo yetu yote madogo na makubwa na hasa katika yale ambayo ni Allah(Subhaanahu Wata’ala) pekee huyawafikisha kama kuponya maradhi, kugawa rizki n.k
5 Ujue kuwa ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika ila tu kwa kile alichokwishakuandikia Allaah na wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, hotodhurika ila tu kwa kile Allah alichokwishakuandikia (kuwa kitakudhuru)
Na hii ndio nguzo ya sita imani kuamini kudra yake ikiwa ya kheri au ya shari . Na endapo muumini akipata yakini(uhakika) wa haya yote anayo haja tena kumuomba asiekuwa Allah(Subhaanahu Wata’ala)?
TUNAYOJIFUNZA
1 Jinsi Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alivyokuwa akiwapenda watoto, kwa kumpakia Abdullah Ibn Abbaas kwenye ngamia wake na kumwita kwa heshima kabisa “Ewe kijana”
2 Kuamrishwa watoto kumtii Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kujiepusha na kumuasi ili waweze kupata mafanikio duniani na huko akhera
3 Allah(Subhaanahu Wata’ala) humuokoa muumini wa kweli wakati atakapopatwa na majanga ikiwa tu atakuwa amezitekeleza haki zake Allah(Subhaanahu Wata’ala) na haki za watu katika hali zote katika uzima, ugonjwa, umaskini na utajiri.
4 Kujenga malezi ya kiroho na kiitikadi(Aqidah) kwenye nafsi za watoto kwa kuwaandaa kuwa tayari kumuomba Allah(Subhaanahu Wata’ala) na kumtaka msaada.
5 Kujenga itikadi thabiti ya kuamini kudra yake Allah(Subhaanahu Wata’ala) katika nyoyo za watoto ili kuwaandaa na kukabili hali zote zitakazowakuta maishani mwao ikiwa kheri au shari. Na kuwa katika hali ya kuikubali mitihani na majaribu yake Allah(Subhaanahu Wata’ala) hasa kwa waja wake walio wema.
6 Kutilia mkazo malezi ya kiroho na kiitikadi tokea utotoni. Malezi haya ya kiimani ndiyo yanayomjenga mtoto katika kujenga imani thabiti na itikadi madhubuti kwa mola wake(Subhaanahu Wata’ala).
Haki
za Mtoto Katika Malezi Sahihi ya Kiislamu
|
Tunapozungumzia haki za mtoto katika malezi tunakusudia wajibu
wa mzazi/mlezi kwa mtoto kama hadithi itakavyobainisha . Na kama kutakuwa na
upungufu katika kutekeleza majukumu hapo ndipo tutakwenda kuulizwa na
Allah(SW) siku ya kiama .Katika kutekeleza wajibu wetu huu; matunda yake ni
kupata watoto watiifu, walioleleka na kuwa na manufaa kwa wazazi/walezi wao
hapa duniani na hata pale ambapo wazazi wameshaondoka katika dunia hii(kwani
watoto hawa watawaombea dua wazazi, watawatolea sadaka ,
watawalipia madeni yao nk.).
Katika mada hii tutaangalia zaidi haki za malezi
tu japo kwa ufupi na hatutaingia katika haki nyengine za mtoto kwa
ujumla kutoka kwa wazazi wake kama haki zake kabla ya kuzaliwa na baada ya
kuzaliwa n.k. Kuelewa malezi haya ni muhimu kwa sababu malezi katika
ulimwengu wa kileo yamekuwa elimu kamili iliyo na mfumo na malengo na
si ada na mazoea tena. Elimu hii inayofundisha mfumo wa malezi,
haki na wajibu za wazazi/watoto, sifa za wazazi n.k. Kwa kawaida hulea watoto
wetu jinsi tulivyolelewa bila ya kujali kama mazoea haya ni miongoni mwa
malezi yanayotakiwa na dini yetu ya kiislamu au laa.
Kama ungelikuwa msingi wa malezi katika kila nyumba
umesimama katika mfumo sahihi wa kiislamu basi tungelikuwa na jamii ya
kiislamu kama ile iliyokuwepo enzi za Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam)
pamoja na masahaba na na waliofuatia miongoni mwa taabiina. Jamii iliyokuwa
imeshikamana na dini yao ,inayofahamu haki na wajibu wa kila mmoja,
iliyoienzi na kuiimarisha familia ya kiislamu. Na haya moja kwa moja
yangelikuwa ni mazoea mazuri ambayo yangerithiwa kutoka kwa mzazi kwenda kwa
mtoto kizazi baada ya kizazi.
.
عبد الله بن عمر قال أن رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم قال
: "
….. وإن لولدك عليك حقاً "
مسلم (1159
Kutoka kwa Abdullah Ibn Umar Allah amuwie radhi amesema :
Mtume Muhammad(SAlla Allahu 'Alayhi Wasallam) amesema:
“…… Bila shaka mtoto wako ana haki juu
yako”
Imesimuliwa
na Muslim
عن عبد الله رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : " كلكم راع فمسؤول عن رعيته فالأمير الذي على الناس راع وهو مسؤول عنهم والرجل راع على أهل بيته وهو مسؤول عنهم والمرأة راعية على بيت بعلها وولده وهي مسؤولة عنهم والعبد راع على مال سيده وهو مسؤول عنه ألا فكلكم راع وكلكم مسؤول عن رعيته " رواه البخاري ( 2416
) ومسلم ( 1829 )
Kutoka kwa Abdullah Allah amuwie radhi kwamba Mtume Muhammad
(SALLA Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema :
“Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya mlivyovichunga.
Kiongozi anaewaongoza watu ni mchunga na ataulizwa juu wachungwa wake.
Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa
wake. Na mwanamke ni mchunga kwa nyumba ya mumewe na watoto wake nae
ataulizwa juu ya wachungwa wake .Mtumwa ni mchunga katika mali ya bwana wake
na anawajibika juu ya mali hiyo. Hakika nyote ni wachunga na na kila mmoja
wenu anawajibika juu ya wachungwa
wake”
Imesimuliwa na Bukhari na Muslim
Katika jumla ya haki za watoto katika malezi ni.
1 KUPATIWA MALEZI YA KIMWILI
2 KUPATIWA MALEZI YA KIIMANI
3 KUPATIWA MALEZI YA KIIBADA
4 KUPATIWA MALEZI YA KITAQWA
5 KUPATIWA MALEZI YA KITABIA
1 MALEZI YA KIMWILI
Ni wajibu wa mlezi kumpatia mtoto malezi ya kimwili
kwa kuhakikisha anapata chakula bora cha halali cha kujenga, kutia nguvu
na kuulinda mwili dhidi ya maradhi na kushughuliwa ipasavyo endapo
atapatwa na maradhi .Kuhakikisha kuwepo usafi
wa mwili,nguo na mazingira na kumtia moyo katika kushiriki michezo
inayokubalika kisheria
عن عبد الله بن عمرو رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : " كفى بالمرء إثما أن يضيع من يقوت "
رواه أبو داود ( 1692 ) ، وحسَّنه الشيخ الألباني في " صحيح الجامع " ( 4481 )
Kutoka kwa Abdullah ibn Amru Allah(SW) amuwie radhi amesema:
Mtume Muhammad(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema :
“Ni tosha kuwa dhambi kwa mtu ikiwa atawapoteza wale anaopaswa
kuwalisha.”
Imepokewa na Abu Daud Na Sh . Albani anasema ni hadith hasan
katika kitabu chake Sahihul Jaami’i
2 MALEZI YA KIIMANI
Ni wajibu wa mlezi kumpatia mtoto malezi ya kiimani. Hapa
mtoto itapaswa afundishwe itikadi sahihi na Tauhid - elimu ya kumfahamu
Allah(Subhaanahu Wata'ala), wajue nini shirki na wafundishwe jinsi ya
kujiepusha nayo. Wazoeshwe na neno la shahada. Waeleweshwe umuhimu wa shahada
tokea kuzaliwa, kuishi nalo na kabla ya kufa kulitamka na ni jambo la kwanza
atakapofika kaburini kuulizwa na kwa hilo ndilo ameumbwa. Malezi
ya kiimani ni muhimu kwa kila Muislamu.
Na kwa tunaoishi nchi hizi zisizokuwa za kiislamu
umuhimu huu unazidi maradufu kwani tunaishi na watu ambao hawamjui Allah.
Hivyo tuna wajibu kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi kamili ya kiimani
kuwawezesha kukabiliana na ukafiri uliowazunguka kwa muda mwingi wanapokuwa
hawapo nyumbani.Na hata wanapokuwepo nyumbani kwa kutazama na
kuathirika na TV, internet na games ambavyo vimekuwa vipenzi vikubwa vya
watoto.
Mtoto huzaliwa katika hali ya kuwa Muislamu (Fitrah)
kimaumbile kama hadithi ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam):
كل مولود يولد على الفطرة ، فأبواه يهودانه أو ينصرانه أو يمجسانه .
" رواه البخاري ومسلم
“Kila mtoto anaezaliwa huzaliwa katika fitrah ( hali ya
uislamu). Na wazazi wake wawili ndio watakaomfanya awe Yahudi au
Nasara(mkristo) au Majusi(mwenye kuabudu moto)”.
Imesimuliwa
na Bukhari na Muslim
3 MALEZI
YA KIIBADA
Ni wajibu wa mlezi kuwafundisha watoto ibada
na kuzoezwa ili wazizoee na ziwazoee. Ni lazima
kuwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha ibada za kimsingi zinatekelezwa.
kama sala, funga, ad’iya na duaa, kumpenda Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam) n.k. Mlezi atapaswa ahakikishe kuna muendelezo wa ibada hizi kwa
utaratibu mzuri utakaomfanya mtoto apendelee na kuona raha kuzifanya na
si kuanza kuzichukia na kuzikimbia.
عن أبي
هريرة رضي الله عنه قال : قال الرسول صلى الله عليه وسلم : " مروا أولادكم
الصلاة وهم أبناء سبع سنين واضربوهم عليها وهم أبناء عشر ، وفرقوا بينهم في
المضاجع ".
رواه أبو
داود
Kutoka
kwa Abu Hurayrah Allah amuwie radhi amesema: Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam) amesema : “ Waamrisheni watoto wenu kusali wanapotimia umri wa
miaka saba na watieni adabu(wakikataa) wanapofikia umri wa miaka kumi na
watenganisheni kwenye malazi( wanaume na wanawake)
Imesimuliwa
na Abu Daud
4 MALEZI
YA KITAQWA
Wafundishwe kumuogopa na kumtii
Allah(Subhaanahu Wata'ala) Hii ndiyo maana ya
Taqwa. Kumnyenyekea na kurudi kwake kwa kila jambo. Jambo hilo
hata likiwa dogo kama chembe ya mtama au kubwa kama bahari kuu. Kidogo hapa
pana mtihani wa mfumo wa malezi kati yetu na hawa wasiokuwa waislamu ambao
tunaishi nao. Sisi tumetakiwa tumlee mtoto wetu kitaqwa
yaani wawe wenye kumuogopa Allah(ubhaanahu Wata'ala) .Asiyekuwa
muislam yeye anamlea wake kwa kueleweshwa “reason” yaani kila
jambo lazima mtoto aeleweshwe .Hivyo panahitaji msingi imara katika malezi ya
kitaqwa kinadharia na kivitendo ili yamsaidie mtoto asije kuyumbayumba na
kuchanganyikiwa(confused). Katika mada ya wosia wa Mtume Muhammad(Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam) tunapata mafundisho muhimu jinsi ya kumfundisha
mtoto malezi ya kitaqwa
5 MALEZI
YA KITABIA
Ni wajibu wa kila mzazi kuwaandalia watoto msingi
wa tabia nzuri na njema kwa hasa kuhusiana
na mola wao na Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na pia kuwafundisha
adabu wakiwa na jamaa na ndugu zao na kwa kila mtu. Pia
kuwaelimisha adabu za kula, kunywa, kulala kuamka kwenda chooni
nk. Kuwatahadharisha na tabia mbaya na kuwafahamisha athari zake.
Wazazi wawe mfano kwa watoto wao, wachunge sana
wanayoyazungumza, wanayoyatazama, wanayoyasikia na wanayoyafanya kwani yote
haya watoto huyachukua kutoka kwa wazazi na walezi wao. Pia
kuhakikisha watoto wanakuwa na marafiki na masahiba wema ambao wataweza
kuchukua tabia njema na nzuri kutoka kwao.Na kuchunga na kuwaepusha watoto na
marafiki wabaya ambao pia wataweza kuwaathiri na kurithi mambo mabaya kutoka
kwao.
Kama hadithi iliyopokelewa na AbuHurayrah kutoka kwa
Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam):
"المرء على دين خليله فلينظر أحدكم من
يخالل"
الترمذي رواه
“Mtu hufuata dini ya rafiki yake, basi awe na tahadhari
mmoja wenu na anaetaka kumfanya rafiki”
Attirmidhiy
Ikiwa mzazi/mlezi atakuwa na programu madhubuti ya malezi kwa
mtoto na kuzingatia vipengele tulivyovitaja katika haki za mtoto asaa kwa
uwezo wake Allah(Subhaanahu Wata'ala) na huku tukirudi kwake kuwaombea watoto
wetu hidaaya(uongofu) ; tunaweza kujaaliwa kupata watoto wenye tabia na sifa
za kupigiwa mfano na kuja kuendeleza maadili mema na kuwa na msingi
imara kwa dini yao na katika tabia zao.Licha ya kuwa tuko katika
mazingira magumu katika kulea watoto wetu. Na kama wazazi/walezi tutakuwa
tumeshatekeleza jukumu letu la kuwaepusha watoto wetu na moto ambao kuni zake
ni mawe na watu kama anavyosema Allah (Subhanahu Wata'ala) katika suuratu
Tahreem /6
يأَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ قُواْ أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَاراً وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَـئِكَةٌ غِلاَظٌ شِدَادٌ لاَّ يَعْصُونَ اللَّهَ مَآ أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ
Enyi mlio amini! Jilindeni (jiokoeni) nafsi zenu na
ahli(familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia
Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na
wanatenda wanayo amrishwa.
Wabillahi
Tawfiq
|
|||||
Kumjenga Mtoto Kiadabu na Kiheshima
|
|||||
Friday, 03 August 2007 18:26
|
Wakati wa utotoni ni
muhimu sana kwa mtoto kwani katika kipindi hiki ndipo mtoto anapoanza kupokea
na kujifunza tabia ambazo zitakuja kuwa sehemu ya maisha yake ukubwani.
Tunaona katika nchi
hizi za kimagharibi kivitendo vipi serikali zinavyowajali watoto katika umri
huu. Baada ya kufanya tafiti nyingi za kisayansi juu ya watoto wameona
umuhimu wa kuwaangalia sana watoto na kuwachunga mpaka serikali kutoa fedha
kuwahudumia na kuwa tayari kuwatia adabu wazazi endapo hawatofuata maagizo ya
serikali . Adabu hizi inawezekana ikawa kupewa mafunzo ya
kulea, kuonywa, kunya’nganywa au hata kufungwa
jela mzazi kwa watoto wake mwenyewe aliowazaa. Hii tu inaonesha
jinsi mikakati ya serikali ilivyokuwa na malengo ya mbali ambayo labda sisi
hatujayafahamu haya na huangalia ya karibu zaidi kama baadhi ya msemo maarufu
kutoka baadhi yetu “ kila ajae ana pesae”. Huwa tunaliangalia
zaidi .
Watoto katika umri
huu mdogo wanakuwa na tayari kuipokea dini yao kutokana na fitrah
ya Allah(Subhaanahu Wata’aala) ambavyo ndivyo walivyoumbwa. Hivyo wanatakiwa
waelimishwe kidogo kidogo na wajielewe kwamba wao ni zawadi kutoka kwa
Allah(Subhaanahu Wata’aala) zawadi hii watatakiwa waifanyie kazi kwa ajili
yake. Watoto watataka waanze kujengewa mazingira ya kujijua wao ni
nani na wana wajibu na majukumu gani toke utotoni mwao na hapa tutaangalia
zaidi kumjenga mtoto kuwa na adabu na heshima.
Pia imethibitika
kitaalamu kwamba miaka kumi ya mwanzo ya mtoto ndiyo dira ya mwelekeo wa
maisha yake atakapokuwa mkubwa. Hivyo mtoto akijengwa katika mazingira
mazuri ya kiadabu na kiheshima ndivyo hivyo atakavyokuwa mkubwa na ikiwa
atalelewa vyenginevyo basi navyo pia atakavyokuwa.
Walezi katika nchi hizi
tuna mitihani hii mzito .
Tukiwa katika nchi hizi
zisizokuwa za kiislamu kadri tutakavyojitahidi kuwalea watoto na
kuwafundisha maadili mema ya kiislamu nyumbani, wakitoka nje (ambapo huwepo
kwa muda mwingi) tu hukutana na tabia ,maadili kinyume kabisa na yale wanayofundishwa
ndani ya nyumba. Hivyo kujikuta katika hali ya mtafaruku washindwe kupambanua
lipi ndilo sahihi la kufuata na lipi silo la kuliacha.
Mtihani mwengine ni
pale ambapo nyumba ni ya kiislamu lakini yanayofanywa ndani ya nyumba hayana
tofauti na yanayofanyika nje ya nyumba ambapo maadili na mazingira si ya
kiislamu na hapa mtoto kuona kwamba haya ndiyo sahihi na akifundishwa maadili
na malezi ya kiislamu huona kinyume nyume.
Hivyo maelekezo haya
labda yataweza kusaidia mzazi jinsi ya kurudisha heshima kwa watoto na adabu.
1 Ni
wajibu wa mzazi kuwafunza watoto wake jinsi ya kuwa na mawasiliano kwa uwazi
na bayana na jinsi ya kuwa wakweli.Watoto hujifunza haraka kivitendo kuliko
kinadharia hivyo ndani ya nyumba lazima kuwe na mawasiliano mazuri kati ya
wazazi. Hata kama mzazi mmoja amekasirika au kufurahi basi ni vyema mtoto
aone na afahamu hasira na furaha hizo.Mzazi anatakiwa asifiche
hasira wala furaha ili mtoto aweze kuiga
2 Katika
kujifunza tabia mtoto atatakiwa askilizwe na athaminiwe anapozungumza na
asidharauliwe. Kwani hujifunza kuweza kuwa na moyo na kujiamini kuzungumza
akijua kwamba anasikilizwa.
3 Kumfunza
mtoto kuweza kuishi na watoto wenzake vizuri na kutojenga tabia ya kujiona
kila akifanacho yeye ni sawa na wengine si sawa. Ni muhimu kwa mzazi
kumuelewesha mtoto kuwasikiliza wenzake pia.
4 Kuwapa
watoto fursa ya maamuzi mara moja moja katika nyumba ni muhimu pia hata ikiwa
maamuzi yao si sahihi kwani ndipio watakaposoma jinsi ya kufikia maamuzi
sahihi.
5 Kuwaonesha
mapenzi, kuwaheshimu na kuwathamini huwajengea watoto mazingira mazuri ya
kujiona na wao wana umuhimu wa aina yake katika familia. Na pia kurudisha
heshima kwa wazazi na watu wengine.
|
No comments:
Post a Comment