Tunapozungumzia haki za mtoto katika malezi tunakusudia wajibu
wa mzazi/mlezi kwa mtoto kama hadithi itakavyobainisha . Na kama kutakuwa na
upungufu katika kutekeleza majukumu hapo ndipo tutakwenda kuulizwa na
Allah(SW) siku ya kiama .Katika kutekeleza wajibu wetu huu; matunda yake ni
kupata watoto watiifu, walioleleka na kuwa na manufaa kwa wazazi/walezi wao
hapa duniani na hata pale ambapo wazazi wameshaondoka katika dunia hii(kwani
watoto hawa watawaombea dua wazazi, watawatolea sadaka ,
watawalipia madeni yao nk.).
Katika mada hii tutaangalia zaidi haki za malezi
tu japo kwa ufupi na hatutaingia katika haki nyengine za mtoto kwa
ujumla kutoka kwa wazazi wake kama haki zake kabla ya kuzaliwa na baada ya
kuzaliwa n.k. Kuelewa malezi haya ni muhimu kwa sababu malezi katika
ulimwengu wa kileo yamekuwa elimu kamili iliyo na mfumo na malengo na
si ada na mazoea tena. Elimu hii inayofundisha mfumo wa malezi,
haki na wajibu za wazazi/watoto, sifa za wazazi n.k. Kwa kawaida hulea watoto
wetu jinsi tulivyolelewa bila ya kujali kama mazoea haya ni miongoni mwa
malezi yanayotakiwa na dini yetu ya kiislamu au laa.
Kama ungelikuwa msingi wa malezi katika kila nyumba
umesimama katika mfumo sahihi wa kiislamu basi tungelikuwa na jamii ya
kiislamu kama ile iliyokuwepo enzi za Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam)
pamoja na masahaba na na waliofuatia miongoni mwa taabiina. Jamii iliyokuwa
imeshikamana na dini yao ,inayofahamu haki na wajibu wa kila mmoja,
iliyoienzi na kuiimarisha familia ya kiislamu. Na haya moja kwa moja
yangelikuwa ni mazoea mazuri ambayo yangerithiwa kutoka kwa mzazi kwenda kwa
mtoto kizazi baada ya kizazi.
.
عبد الله بن عمر قال أن رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم قال
: "
….. وإن لولدك عليك حقاً "
مسلم (1159
Kutoka kwa Abdullah Ibn Umar Allah amuwie radhi amesema :
Mtume Muhammad(SAlla Allahu 'Alayhi Wasallam) amesema:
“…… Bila shaka mtoto wako ana haki juu
yako”
Imesimuliwa
na Muslim
عن عبد الله رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : " كلكم راع فمسؤول عن رعيته فالأمير الذي على الناس راع وهو مسؤول عنهم والرجل راع على أهل بيته وهو مسؤول عنهم والمرأة راعية على بيت بعلها وولده وهي مسؤولة عنهم والعبد راع على مال سيده وهو مسؤول عنه ألا فكلكم راع وكلكم مسؤول عن رعيته " رواه البخاري ( 2416
) ومسلم ( 1829 )
Kutoka kwa Abdullah Allah amuwie radhi kwamba Mtume Muhammad
(SALLA Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema :
“Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya mlivyovichunga.
Kiongozi anaewaongoza watu ni mchunga na ataulizwa juu wachungwa wake.
Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa
wake. Na mwanamke ni mchunga kwa nyumba ya mumewe na watoto wake nae
ataulizwa juu ya wachungwa wake .Mtumwa ni mchunga katika mali ya bwana wake
na anawajibika juu ya mali hiyo. Hakika nyote ni wachunga na na kila mmoja
wenu anawajibika juu ya wachungwa
wake”
Imesimuliwa na Bukhari na Muslim
Katika jumla ya haki za watoto katika malezi ni.
1 KUPATIWA MALEZI YA KIMWILI
2 KUPATIWA MALEZI YA KIIMANI
3 KUPATIWA MALEZI YA KIIBADA
4 KUPATIWA MALEZI YA KITAQWA
5 KUPATIWA MALEZI YA KITABIA
1 MALEZI YA KIMWILI
Ni wajibu wa mlezi kumpatia mtoto malezi ya kimwili
kwa kuhakikisha anapata chakula bora cha halali cha kujenga, kutia nguvu
na kuulinda mwili dhidi ya maradhi na kushughuliwa ipasavyo endapo
atapatwa na maradhi .Kuhakikisha kuwepo usafi
wa mwili,nguo na mazingira na kumtia moyo katika kushiriki michezo
inayokubalika kisheria
عن عبد الله بن عمرو رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : " كفى بالمرء إثما أن يضيع من يقوت "
رواه أبو داود ( 1692 ) ، وحسَّنه الشيخ الألباني في " صحيح الجامع " ( 4481 )
Kutoka kwa Abdullah ibn Amru Allah(SW) amuwie radhi amesema:
Mtume Muhammad(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema :
“Ni tosha kuwa dhambi kwa mtu ikiwa atawapoteza wale anaopaswa
kuwalisha.”
Imepokewa na Abu Daud Na Sh . Albani anasema ni hadith hasan
katika kitabu chake Sahihul Jaami’i
2 MALEZI YA KIIMANI
Ni wajibu wa mlezi kumpatia mtoto malezi ya kiimani. Hapa
mtoto itapaswa afundishwe itikadi sahihi na Tauhid - elimu ya kumfahamu
Allah(Subhaanahu Wata'ala), wajue nini shirki na wafundishwe jinsi ya
kujiepusha nayo. Wazoeshwe na neno la shahada. Waeleweshwe umuhimu wa shahada
tokea kuzaliwa, kuishi nalo na kabla ya kufa kulitamka na ni jambo la kwanza
atakapofika kaburini kuulizwa na kwa hilo ndilo ameumbwa. Malezi
ya kiimani ni muhimu kwa kila Muislamu.
Na kwa tunaoishi nchi hizi zisizokuwa za kiislamu
umuhimu huu unazidi maradufu kwani tunaishi na watu ambao hawamjui Allah.
Hivyo tuna wajibu kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi kamili ya kiimani
kuwawezesha kukabiliana na ukafiri uliowazunguka kwa muda mwingi wanapokuwa
hawapo nyumbani.Na hata wanapokuwepo nyumbani kwa kutazama na
kuathirika na TV, internet na games ambavyo vimekuwa vipenzi vikubwa vya
watoto.
Mtoto huzaliwa katika hali ya kuwa Muislamu (Fitrah)
kimaumbile kama hadithi ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam):
كل مولود يولد على الفطرة ، فأبواه يهودانه أو ينصرانه أو يمجسانه .
" رواه البخاري ومسلم
“Kila mtoto anaezaliwa huzaliwa katika fitrah ( hali ya
uislamu). Na wazazi wake wawili ndio watakaomfanya awe Yahudi au
Nasara(mkristo) au Majusi(mwenye kuabudu moto)”.
Imesimuliwa
na Bukhari na Muslim
3 MALEZI
YA KIIBADA
Ni wajibu wa mlezi kuwafundisha watoto ibada
na kuzoezwa ili wazizoee na ziwazoee. Ni lazima
kuwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha ibada za kimsingi zinatekelezwa.
kama sala, funga, ad’iya na duaa, kumpenda Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam) n.k. Mlezi atapaswa ahakikishe kuna muendelezo wa ibada hizi kwa
utaratibu mzuri utakaomfanya mtoto apendelee na kuona raha kuzifanya na
si kuanza kuzichukia na kuzikimbia.
عن أبي
هريرة رضي الله عنه قال : قال الرسول صلى الله عليه وسلم : " مروا أولادكم
الصلاة وهم أبناء سبع سنين واضربوهم عليها وهم أبناء عشر ، وفرقوا بينهم في
المضاجع ".
رواه أبو
داود
Kutoka
kwa Abu Hurayrah Allah amuwie radhi amesema: Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam) amesema : “ Waamrisheni watoto wenu kusali wanapotimia umri wa
miaka saba na watieni adabu(wakikataa) wanapofikia umri wa miaka kumi na
watenganisheni kwenye malazi( wanaume na wanawake)
Imesimuliwa
na Abu Daud
4 MALEZI
YA KITAQWA
Wafundishwe kumuogopa na kumtii
Allah(Subhaanahu Wata'ala) Hii ndiyo maana ya
Taqwa. Kumnyenyekea na kurudi kwake kwa kila jambo. Jambo hilo
hata likiwa dogo kama chembe ya mtama au kubwa kama bahari kuu. Kidogo hapa
pana mtihani wa mfumo wa malezi kati yetu na hawa wasiokuwa waislamu ambao
tunaishi nao. Sisi tumetakiwa tumlee mtoto wetu kitaqwa
yaani wawe wenye kumuogopa Allah(ubhaanahu Wata'ala) .Asiyekuwa
muislam yeye anamlea wake kwa kueleweshwa “reason” yaani kila
jambo lazima mtoto aeleweshwe .Hivyo panahitaji msingi imara katika malezi ya
kitaqwa kinadharia na kivitendo ili yamsaidie mtoto asije kuyumbayumba na
kuchanganyikiwa(confused). Katika mada ya wosia wa Mtume Muhammad(Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam) tunapata mafundisho muhimu jinsi ya kumfundisha
mtoto malezi ya kitaqwa
5 MALEZI
YA KITABIA
Ni wajibu wa kila mzazi kuwaandalia watoto msingi
wa tabia nzuri na njema kwa hasa kuhusiana
na mola wao na Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na pia kuwafundisha
adabu wakiwa na jamaa na ndugu zao na kwa kila mtu. Pia
kuwaelimisha adabu za kula, kunywa, kulala kuamka kwenda chooni
nk. Kuwatahadharisha na tabia mbaya na kuwafahamisha athari zake.
Wazazi wawe mfano kwa watoto wao, wachunge sana
wanayoyazungumza, wanayoyatazama, wanayoyasikia na wanayoyafanya kwani yote
haya watoto huyachukua kutoka kwa wazazi na walezi wao. Pia
kuhakikisha watoto wanakuwa na marafiki na masahiba wema ambao wataweza
kuchukua tabia njema na nzuri kutoka kwao.Na kuchunga na kuwaepusha watoto na
marafiki wabaya ambao pia wataweza kuwaathiri na kurithi mambo mabaya kutoka
kwao.
Kama hadithi iliyopokelewa na AbuHurayrah kutoka kwa
Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam):
"المرء على دين خليله فلينظر أحدكم من
يخالل"
الترمذي رواه
“Mtu hufuata dini ya rafiki yake, basi awe na tahadhari
mmoja wenu na anaetaka kumfanya rafiki”
Attirmidhiy
Ikiwa mzazi/mlezi atakuwa na programu madhubuti ya malezi kwa
mtoto na kuzingatia vipengele tulivyovitaja katika haki za mtoto asaa kwa
uwezo wake Allah(Subhaanahu Wata'ala) na huku tukirudi kwake kuwaombea watoto
wetu hidaaya(uongofu) ; tunaweza kujaaliwa kupata watoto wenye tabia na sifa
za kupigiwa mfano na kuja kuendeleza maadili mema na kuwa na msingi
imara kwa dini yao na katika tabia zao.Licha ya kuwa tuko katika
mazingira magumu katika kulea watoto wetu. Na kama wazazi/walezi tutakuwa
tumeshatekeleza jukumu letu la kuwaepusha watoto wetu na moto ambao kuni zake
ni mawe na watu kama anavyosema Allah (Subhanahu Wata'ala) katika suuratu
Tahreem /6
يأَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ قُواْ أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَاراً وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَـئِكَةٌ غِلاَظٌ شِدَادٌ لاَّ يَعْصُونَ اللَّهَ مَآ أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ
Enyi mlio amini! Jilindeni (jiokoeni) nafsi zenu na
ahli(familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia
Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na
wanatenda wanayo amrishwa.
Wabillahi
Tawfiq
|