Thursday, December 4, 2014

Uislamu Unasema Nini Kuhusu Siku ya Hukumu?

Kama wakristo, Waislamu wanaamini kuwa maisha ya sasa (duniani) ni maandalizi ya majaribio kwa ajili ya eneo lijalo la kuishi. Dunia hii ni mtihani kwa kila mmoja kwa minajili ya maisha baada ya kifo. Itafikia siku moja ambapo ulimwengu mzima utaangamizwa na wafu watafufuliwa kwa ajili ya kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu. Siku hii itakuwa mwanzo wa maisha yasiyo na ukomo. Hii ni Siku ya Hukumu. Katika siku hiyo, watu wote watalipwa na Mwenyezi Mungu kulingana na imani na matendo yao. Wote wanaofariki huku wakiamini kuwa, “Hapana mola wa haki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu” ilhali ni Waislamu, watalipwa katika siku hiyo na wataingizwa Peponi milele, sawa na kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na wale walioamini na wakatenda mema, hao ndio watu wa Peponi, humo watadumu.” (Qur-aan, 2:82) Lakini wale wanaofariki bila ya kuamini kuwa “Hapana mola wa haki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu” au si Waislamu, wataikosa Pepo milele na watapelekwa Motoni, sawa na kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na anayetafuta Dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.” (Qur-aan, 3:85)

Pia ni sawa na kauli Yake nyingine: “Hakika wale waliokufuru, na wakafa hali ni makafiri haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau wangeliitoa. Hao watapata adhabu kali, wala hawatakuwa na wa kuwanusuru.” (Qur-aan, 3:91)

Mmojawapo anaweza kusaili, ‘Nadhani Uislamu ni Dini nzuri, lakini ningelikuwa mwenye kusilimu, familia yangu, marafiki na watu wengine wanaweza kuniadhibu na kunikejeli. Hivyo, nisiposilimu, nitaingia Peponi na kuokoka dhidi ya Jahanamu?”
Jibu ni kile Alichokisema Mwenyezi Mungu katika Aayah iliyotangulia: “Na anayetafuta Dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.”
Baada ya kumtuma Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awalinganie watu katika Uislamu, Mwenyezi Mungu Hakubali ung’ang’anizi wa Dini yoyote isipokuwa Uislamu. Mwenyezi Mungu Ndiye Muumbaji wetu na Mwenye kuturuzuku. Alituumbia kila kilicho duniani. Neema zote na mambo yote mazuri ni kutoka Kwake. Hivyo, baada ya yote haya, pindi mtu anapokataa kumwamini Mwenyezi Mungu, Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Dini yake ya Kiislamu, ni haki kwamba aadhibiwe katika jahanamu. Kwa kweli, lengo kuu la kuumbwa kwetu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu tu na kumwabudu, sawa na kauli Yake nyingine katika Qur-aan Tukufu (51:56).
Maisha haya ya sasa ni mafupi sana. Makafiri katika Siku ya Hukumu watadhani kuwa maisha waliyoishi duniani yalikuwa ya siku moja au sehemu yake tu, kama Alivyosema: “Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanaoweka hisabu. Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua.” (Qur-aan, 23:113-114)
Pia Alisema:Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?  Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu.”
Maisha ya Akhera ni halisi. Si ya kiroho tu, bali ni ya kimwili pia. Tutaishi huko tukiwa na roho na miili yetu. Katika kuulinganisha ulimwengu huu na Akhera, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Thamani ya ulimwengu huu kulinganisha na Akhera ni kama kile kinacholetwa na kidole chako baharini pindi unapochovya humo na kukitoa.)) [85]Naam, thamani ya ulimwengu huu ikilinganishwa na ya Akhera ni sawa na matone machache ya maji yakilinganishwa na bahari.